UTUNZAJI KUMBUKUMBU KURAHISISHA MALIPO YA BIMA

January 31, 2024

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo, kuhusu Sheria ya Bima na swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Mohamed Said Issa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato ya biashara zinazofanyika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, bungeni Jijini Dodoma.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)


 Na. Khadija Ibrahim, WF, Dodoma

 

Serikali imewataka wananchi kutunza kumbukumbu na nyaraka muhimu za rejea ili kuondoa usumbufu na kurahisisha zoezi la ulipaji fidia hususan kwa wasimamizi wa mirathi kupitia bima walizokata.

 

Wito huo umetolewa bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini, Mhe. Dkt. Oscar Kikoyo, aliyetaka kufahamu wakati ambao Serikali itarekebisha Sheria ya Bima ya Tanzania ili kuweka kima cha chini cha malipo ya fidia kwa waathirika wa ajali za barabarani.

 

Alisema kuwa Septemba 2022, Mamlaka ya Bima Tanzania ilitoa Mwongozo unaotambulika kama Mwongozo wa Viwango Elekezi vya Fidia ya Bima kwa Madai ya Majeraha ya Mwili na Vifo kwa Mtu wa Tatu Kutokana na Ajali za Vyombo vya Moto.

 

“Mwongozo huo wa Viwango vya Fidia ya Bima ulitolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 na 11 cha Sheria ya Bima Sura Na. 394, lengo likiwa ni kuweka usawa na ubora katika ulipaji fidia zitokanazo na madai ya bima”, alisema Dkt. Nchemba.

 

Alisema kuwa utekelezaji wa mwongozo huo umepunguza kwa sehemu kubwa malalamiko kutoka kwa waathirika wa ajali za vyombo vya moto kwa kuwa kuna usawa katika suala la viwango vya fidia vinavyotolewa na kampuni za bima.

 

Aidha alieleza kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kujenga uelewa kwa wadau wa tasnia ya bima na wananchi kwa ujumla ili kutimiza matakwa ya Sheria ya Bima, Sura 394, ikiwemo kuboresha huduma za bima na kumlinda mteja.

 

Kwa upande mwingine, akijibu swali la Mbunge wa Konde, Mhe. Mohamed Said Issa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato ya biashara zinazofanyika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali za pande mbili zimeendelea kuboresha na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uwekezaji na biashara.

 

Alieleza kuwa baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni pamoja na kuboresha na kuunganisha mifumo ya kodi ya EFDMS na VFMS ili kusomana na kurahisisha utozaji kodi, ada na tozo, kuboresha mifumo ya urejeshaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kurahisisha mifumo ya utoaji vibali, leseni na ukaguzi wa mizigo.

 

Aidha Mhe. Dkt. Nchemba alibainisha kuwa katika kuongeza uwazi, Serikali kupitia Mamlaka za Usimamizi wa Mapato zimeweka bango linaloonesha bidhaa ambazo hazipaswi kulipiwa ushuru au kodi na bidhaa zinazopaswa kulipiwa, pamoja na viwango vinavyopaswa kulipwa.

 

Alisema kuwa pande zote zimekubaliana kuwa ushuru wa forodha unaokusanywa kwa upande wa Zanzibar, uwasilishwe kwenye mfumo wa Hazina wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato na ufanisi katika udhibiti wa biashara za magendo

 

WAZIRI MAKAMBA ANADI FURSA ZA BIASHARA, UWEKEZAJI ITALIA

January 31, 2024


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akiteta jambo na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari katika ofisi za chama hicho, Jijini Roma Italia


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba akizungumza na wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia



Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) amenadi fursa za biashara na uwekezaji zinazopatikana nchini katika mkutano wa wafanyabiashara, viongozi wa siasa na wa kijamii nchini Italia.

Katika mkutano huo, Waziri Makamba amewaeleza wafanyabiashara na wawekezaji wa Italia fursa mbalimbali za biashara zinazopatikana nchini pamoja na mageuzi makubwa ya kuboresha mazingira ya uwekezaji yanayofanyika chini ya Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Makamba amesema mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ni salama na rafiki kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kuhakikisha wafanyabiashara wanatekeleza majukumu yao katika mazingira rafiki na salama.

Kadhalika Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania inazingatia misingi ya utawala bora pamoja na kuzungukwa na nchi saba ambazo hazina bandari na hivyo kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma kwenda katika nchi hizo.

Waziri Makamba ameongeza kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ya Tanzania ni salama kwa sababu Tanzania imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda mitaji na uwekezaji wa kigeni pamoja na Serikali kutambua sekta binafsi kama injini ya maendeleo ya kiuchumi.

“Napenda kuwasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuja kuwekeza Tanzania kwani licha ya kuwa na mzingira salama, pia kuna fursa za kuwekeza katika sekta mbalimbali kama nishati, utalii, kilimo, afya na elimu,” alisema Waziri Makamba.

Kadhalika, Waziri Makamba ameongeza kuwa kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Soko Huru la pamoja la Afrika (AfCFTA) ambalo linahusisha watu zaidi ya bilioni 1.5 hali ambayo itawezesha wafanyabiashara wa Italia kuwafikia watu hao kupitia soko hilo.

Waziri Makamba amesema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Italia katika kutekeleza Mpango wa Mattei kwa maslahi ya pande zote mbili, na kuwasisitiza kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania na visiwani Zanzibar.

Akiongea awali katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari amesema kuwa utekelezaji wa mpango wa Mattei utakapoanza utazingatia maoni na mapendekezo yote yaliyotolewa na wadau ambapo miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika ikiwemo Tanzania.

Tanzania ni moja kati ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan) ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
WATUMIAJI WA BARABARA WASHAURIWA KUTOTUMIA VIVUKO VILIVYOZUILIWA

WATUMIAJI WA BARABARA WASHAURIWA KUTOTUMIA VIVUKO VILIVYOZUILIWA

January 31, 2024




Dar es Salaam

Watumiaji wa barabara mkoani Dar es Salaam wameshauriwa kutotumia barabara au vivuko ambavyo vimewekwa vizuizi katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha nchini.

Wito huo umetolewa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga wakati wa ukaguzi wa madaraja ya Luhufi na Tanganyika katika Wilaya ya Kinondoni.

Mhandisi Mkinga amesema katika kipindi cha mvua barabara nyingi huharibika zaidi na usalama kuwa mdogo hivyo wanaweka vibao watu wasipite au wapite kwa tahadhari kwa maana barabara ni nyembamba

“Kwa kipindi hiki cha mvua, barabara nyingi zinakuwa zimeharibika hivyo tunapoona usalama ni mdogo huwa tunaweka alama za tahadhali, kwa hiyo tunaomba watumiaji wa barabara wazingatie hizo alama” Alisisitiza Mhandisi Mkinga.

Ameongeza kusema kwamba kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu kutaka kupita kwa ngazi au magogo vitendo ambavyo ni hatarishi.

“Tunafahamu hali ilivyo kwenye daraja hadi kufikia hayo maamuzi hivyo vile tulivyoweka alama wasijaribu kupita kwani sio salama”. Amesisitiza.

Akitolea mfano wa daraja la Msumi-Madale ambalo kwa sasa hivi halipitiki kabisa na limefungwa ila bado kuna majaribio ya watu kutaka kupita kwa magogo kitu ambacho ni hatarishi.

Ameongeza kusema kwamba TARURA inaenda kujenga kivuko cha kutembea kwa miguu daraja la Msumi-Madale na litawasadia kuvuka ila wasijaribu kutumia njia zingine za kupanga mawe au miti kwani ni hatari kwa kuwa mvua zinaweza kunyesha na kusababisha kingo kuanguka na hivyo kuhatarisha maisha yao.

SERIKALI YAANZA KUFANYA TATHIMINI KUBAINI MAENEO YATAKAYOBORESHWA KUKABILIANA NA ATHARI ZA MAZINGIRA

January 31, 2024

 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wizara za kisekta imeanza kufanya tathmini nchi nzima kubainisha maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho kukabiliana na athari za kimazingira.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe Mhe. Khalifa Mohammed Issa aliyetaka kujua lini Serikali itafanya utafiti kuyabaini maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.

Katika kushughulikia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali imeanza kuyafanyia kazi maeneo hayo kwa kutekeleza miradi ya mazingira pande zote mbili za Muungano.

Amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa tuta linalozuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi na mashamba unaotekelezwa eneo la eneo la Sipwese Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini, Pemba.

Halikadhalika, amesema mradi huo unatekelezwa pia katika eneo la Mikindani, Mtwara ambako kunajengwa ukuta utakaosaidia kupunguza kasi ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya watu na kuta kwa ajili ya kurejesha fukwe katika hali yake.

“Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imetuma timu ya wataalamu ikishirikiana na wizara za kisekta kufanya tathmini ambayo itatusaidia kubaini maeneo gani yenye changamoto na kuyafanyia kazi hivyo kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama,” amesisitiza Waziri Dkt. Jafo.

Awali, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alisema Serikali inaendelea na kampeni za kuhamasisha wananchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo zoezi la upandaji wa miti katika maeneo yote nchini.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariam Nasoro Kisangi aliyeuliza mkakati ya Serikali wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, Mhe. Khamis alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inafanya kampeni hizo kwa kushirikiana na taasisi kuhamasisha ubunifu, utafiti na uendelezaji wa teknolojia za kukabiliana na changamoto hiyo.

Mhe. Khamis alibainisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) na Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi ya Mazingira (2022-2032).

Aidha, alisema kuwa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar upo Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar (2014-2030) ambao unatekelezwa kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais yenye dhamani ya mazingira.

Alisema Serikali inayo Mipango ambayo kwa pamoja imeelezea changamoto na hatua mbalimbali za kuzifuata katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Tunatambua mkakati tulionao wa kusafisha mito na tayari Mhesehimiwa Waziri (Dkt. Jafo) alishaunda Kamati na kubaini chanzo mkusanyiko wa mchanga mkoani Dar es Salaam na kuziba mifereji nasi tunaendelea kutoa elimu na kusimamia Sheria ya Mita 60 na Usafishaji wa mito kwa kutoa mchanga na takataka nyingine,” alisema Mhe. Khamis.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akijadiliana jambo na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge Jijini Dodoma leo Januari 31, 2024.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Januari 31, 2024 kuhusu mkakati wa Serikali wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwasili bungeni jijini Dodoma kushiriki kipindi cha maswali na majibu katika Kikao cha pili Mkutano wa 14 wa Bunge leo Januari 31, 2024.

WATEJA WA BENKI YA CRDB KUZAWADIWA SH.MILIONI 470 KAMPENI YA BENKI NI SIMBANKING

January 31, 2024

  

Dar es Salaam. Tarehe 31 Januari 2024:  Katika jitihada zake za kuhamasisha  matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini, Benki ya CRDB imezindua msimu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ni SimBanking’ na kutenga jumla ya zawadi zenye thamani ya Shilingi milioni 470 mamilioni kwa wateja wake mwaka huu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja wadogo na wakati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul amesema lengo la kampeni hiyo ni kujenga utamaduni wa matumizi ya kidijitali katika huduma za kifedha ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuondokana na matumizi ya fedha taslimu.
“Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaihamisha dunia kutoka kwenye miamala ya fedha taslimu kwenda ile isiyohusisha fedha taslimu yaani cashless economy. Tanzania hatupaswi kuachwa nyuma, ni lazima twende na mabadiliko hayo tena kwa kasi inayostahili,” amesema Bonaventure.

Kushiriki na kujiwekea nafasi ya ushindi katika kampeni hiyo mteja anatakiwa kutumia SimBanking kufanya miamala yake yote ya kibenki ikiwamo kulipia ankara za maji, umeme au visimbusi vya television, ada, malipo ya manunuzi, kutuma pesa, kulipia kodi, mikopo ya kidijitali, kutoa fedha kwa ATM au CRDB Wakala, kulipia bima ya vyombo vya moto, na huduma nyenginezo.
“Kwa kadri mteja atakavyokuwa akifanya miamala mingi zaidi ndivyo atakavyojiwekea nafasi ya ushindi,” amesema Bonaventure huku akibainisha kuwa katika kampeni hiyo itakayoenda hadi mwisho wa mwaka, kutakuwa na washindi wa gari aina ya Toyota Dualis watakaopatikana kila baada ya miezi mitatu, huku zawadi za  bajaj na pikipiki zikitolewa kwa mshindi wa kwanza na wa pili kila mwezi.

Aidha, katika msimu huu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ya SimBanking’, Benki ya CRDB imetenga zawadi za kompyuta mpakato kufikia 10 kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu, zawadi za simu janja, pamoja na fedha taslimu.

Pamoja na zawadi hizi Benki hiyo pia imetenga kiasi cha Shilingi milioni 200 zitakazotolewa kupitia Tembo Points ambazo mteja atakuwa akikusanya kila anapofanya muamala. Wateja wataweza kubadili Tembo Points zao kuwa fedha na kuzitumia kulipia huduma au bidhaa.
Bonaventure amewakumbusha wateja wa  Benki ya CRDB ambao hawajakamilisha usajili wa huduma za SimBanking kukamilisha mchakato huo ili wakidhi vigezo vya kujishindia moja kati ya zawadi zilizotangazwa na kuwakaribisha wananchi wengine kufungua akaunti kwa vigezo nafuu sana na kuunganishwa na SimBanking ili kufurahia huduma zilizoboreshwa zaidi.

Benki imeendelea kuiboresha huduma yake ya SimBanking ili kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa na uzoefu ulio bora zaidi kwa wateja.  Mwaka jana, tulizindua SimBanking App iliyoboreshwa ambayo inatumia akili mnemba (Artificial intelligence), ianyoiwezesha kuwa na uwezo mkubwa katika utambuzi wa tabia na mahitaji ya mteja pindi anapotumia.

Mapema mwaka huu Benki ya CRDB imeongeza huduma mbili mpya ndani ya SimBanking ikiwamo  huduma ya malipo kupitia Msimbomilia wa Taifa (TANQR) ikimuwezesha mteja kufanya malipo kwa watoa huduma wote wa Benki ya CRDB na hata mitandao ya simu. Huduma nyengine ni ile ya kujitengenezea Tembo Virtual Card mahsusi kufanikisha miamala ya kieletroniki popote pale duniani kwa kushirikiana na Union Pay.










EWURA YAENDESHA SEMINA KWA KAMATI YA BUNGE YA SHERIA NDOGO

EWURA YAENDESHA SEMINA KWA KAMATI YA BUNGE YA SHERIA NDOGO

January 31, 2024


 
Mkurugenzi wa Petroli EWURA, Bw. Gerald Maganga, akijibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria Ndogo, wakati wa semina iliyoandaliwa na EWURA, bungeni jijini Dodoma.
Ofisa Mkuu wa Uhusiano EWURA, Bw. Wilfred Mwakalosi, akiwasilisha mada kuhusu Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, wakati wa semina iliyoandaliwa na EWURA kwa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria Ndogo,iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.
 

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Sheria ya Ndogo, Mhe. Jasson Rweikiza, akitoa hoja, wakati wa semina ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, iliyoandaliwa na EWURA, iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria ndogo wakifatilia semina iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliyofanyika bungeni jijini Dodoma.

..........

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeendesha semina ya siku moja kuhusu Udhibiti kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Jasson Rweikiza.

Akiwasilisha mada kuhusu kazi na majukumu ya EWURA, Ofisa Mkuu wa Uhusiano, Bw. Wilfred Mwakalosi, alisema EWURA ina jukumu kuu la kuhakikisha huduma zinazodhibitiwa zinapatikana kwa wakati na kwa gharama sahihi.

Akijibu hoja kuhusu masuala ya petroli kwenye semina hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Petroli Bw. Gerald Maganga alisema EWURA iko mbioni kuanza kuwianisha gharama za mafuta kwa bandari zote zinazopokea mafuta nchini ili kuongeza tija.

Semina hiyo pia imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga na viongozi wengine kutoka Wizara ya Nishati na EWURA.
WAGONJWA WA RED EYE WARIPOTIWA KATIKA VITUO NA HOSPITAL MBALIMBALI ZANZIBAR

WAGONJWA WA RED EYE WARIPOTIWA KATIKA VITUO NA HOSPITAL MBALIMBALI ZANZIBAR

January 31, 2024






Naibu waziri wa afya Zanzibar Mhe.Hassan Khamis Khafidh akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.



Mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho dkt. Rajab Mohammed Hilal akitoa maelezo ya kitaalam kuhusiana na ugonjwa wa macho mekundu (red eye) huko Wizara ya Afya Mjini Unguja.
-


PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar

Jumla ya wagonjwa 4,579 wa ugonjwa wa macho (red eyes) wameripotiwa katika vituo vya afya, na hospitali Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya ugonjwa huo huko Wizara ya Afya wilaya ya mjini Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Hassan Khamis Hafidh amesema idadi ya takwimu hizo zimejumuisha wagonjwa waliofika kwenye vituo vya afya na hospitali za binafsi na serikali Unguja na Pemba.

Aidha amewataka wananchi kuacha kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza sambamba na kuchukua tahadhari za usafi ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara ili kujikinga na maradhi hayo .

amesema endapo jamii itaendelea kutumia dawa hizo kunaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hilo hivyo aliwataka wananchi kufika hospitali mara tu wanapoona dalili za ugonjwa huo ili kupata matibabu stahiki na kwa wakati sahihi.

Hatahivyo aliiasa jamii kuacha kushikana mikono na mtu mwenye maambukizi au kugusa sehemu ya kitu ambacho kimeguswa na mtu huyo, na kuwataka kutumia maji baridi kunawia uso mara kwa mara, pamoja na kujitenga wakati wa kusubiri huduma katika vituo vya afya ili kuepusha maambukizi mapya.

“ni vizuri mgojwa yeyote wa macho asisubiri eneo walilokaa wagonjwa wengine atibiwe chumba maalum kilichotengwa kwa ajili ya wagonjwa wa namna hiyo na akimaliza matibabu aende moja kwa moja nyumbani ili kupunguza hatari ya maambukizi mapya”alisema naibu Waziri.

Akitoa maelezo ya kitaalamu kuhusiana na ugonjwa huo mratibu wa huduma za afya ya msingi na matibabu ya macho Dkt. Rajab Mohammed Hilal
amesema ugonjwa wa macho mekundu husababishwa na virusi wanaoitwa Adenovirus na kupelekea maambukizi ya kirusi kwenye ngozi nyembamba inayozunguka gololi la jicho (conjunctiva) pamoja na kioo (Cornea) cha jicho.

Aliongeza kwa kusema ugonjwa huo unaambukizwa kutoka kwa mtu mmoja mwenye ugonjwa huo na kwenda kwa mwengine na kusambaza maambukizi kwa haraka sana ndani ya siku 10 hadi 12.

Alifahamisha kuwa dalili kubwa za ugonjwa huo ni pamoja na jicho kuwa jekundu, kuwasha na kuchomachoma , mifuniko ya macho kuvimba, macho kuogopa mwangaza, macho kutoa matongo matongo meupe au ya njano kuona ukungu kwa uoni wa mbali katika macho, pamoja na maumivu ya macho.

Alisema miongoni mwa athari za muda mrefu zinazoweza kujitokeza endapo jamii itaendelea kutumia dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo ni pamoja kupunguza uoni.

Itakumbukwa kuwa wiki mbili zilizopita ugonjwa wa macho mekundu (red eye) uliripotiwa katika mikoa ya Tanzania bara na kutokana na maingiliano ya wananchi ya mara kwa mara ugonjwa huo umeweza kuingia visiwani Zanzibar.