Machinjio ya kisasa ya Ruvu lazima yakamilike ifikapo 2018 - Mpina

November 29, 2017
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akijaribu kukata nyama kwa kutumia mashine ya kisasa alipotembelea ranchi ya Ruvu hivi karibuni.
 Waziri wa Mifugo na  Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akiwa na  viongozi wa ranchi ya mifugo nchini akionyeshwa mbuzi wanaofugwa katika ranchi ya Ruvu alipotembelea ranchi hiyo hivi karibuni
 Jengo la machinjio ya kisasa lililopo katika eneo la ranchi ya Ruvu ambalo Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina amewaagiza Watendaji kuhakikisha linakamilika ifikapo Desemba 2018
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akihakiki taarifa za ununuzi wa dawa za mifugo alipotembelea ranchi ya mifugo ya Ruvu hivi karibuni.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhaga Mpina (mwenye miwani katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ranchi ya Ruvu na watumishi wa Wizara  ya Mifugo na Uvuvi alipotembelea ranchi hiyo jana
Waziri  wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga  J. Mpina ameagiza machinjio ya kisasa ya Ruvu yaliyotelekezwa kwa muda mrefu kujengwa na  kukamillika  ifikapo Desemba, 2018.

Maagizo hayo ameyatoa jana katika ranchi ya Ruvu, alipokuwa katika ziara ya kutembelea baadhi ranchi za mifugo nchini, ambapo amesema ni muhimu machinjio hayo ya ya kisasa yakamilike ili Tanzania ianze kuuza mazao yatokanayo na mifugo katika masoko ya kimataifa.

Ametoa siku tatu kwa Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kumpelekea mpango kazi unaoainisha  namna ya kukamilisha ujenzi wa machinjio hiyo ya kisasa ambayo  baada ya kukamilika itakuwa machinjio kubwa kuliko zote nchini.

Amesema kuwa Tanzania ni nchi ya tatu katika bara la Afrika kwa kuwa na uwingi wa mifugo hivyo hakuna sababu ya kushindwa kuongoza katika  soko la mazao ya mifugo katika masoko ya duniani.

Aidha, Waziri Mpina  amesema  kukamilika kwa machinjio hayo kutasaidia kupunguza  usumbufu kwa wafanyabiashara wa mifugo ambao wote nawapeleka mifugo yao Dar es Salaam   hali ambayo inaongeza uharibifu wa mazingira  kwa ujumla.

MHE MWANJELWA AWATAKA WAJUMBE WA JUMUIYA ZA CCM KUCHAGUA VIONGOZI WAADILIFU NA WACHAPA KAZI

November 29, 2017
Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Kutwa ya Mbeya, Jana Novemba 28, 2017.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa Akisakata rumba kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Kutwa ya Mbeya, Jana Novemba 28, 2017.
Makada wa CCM Mkoani Mbeya wakimlaki Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa Wakati akiondoka kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Kutwa ya Mbeya, Jana Novemba 28, 2017.
Makada wa CCM Mkoani Mbeya wakimlaki Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa Wakati akiondoka kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Kutwa ya Mbeya, Jana Novemba 28, 2017.

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

Wajumbe wa Jumuiya mbalimbali za Chama Cha Mapinduzi (CCM) wametakiwa kuchagua viongozi waadilifu, weledi na wenye maono ya kuziongoza Jumuiya hizo ila kuendana na kasi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Umoja wa Wanawake wa CCM Mkoa wa Mbeya uliokuwa na Ajenda ya uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya hiyo Mkoa na Taifa, Mhe Mwanjelwa ambaye ni mjumbe Halmashauri kuu ya CCM Taifa, Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa aliwasisitiza wajumbe hao kutochagua viongozi kwa matakwa ya urafiki na kujuana Bali kuchagua viongozi wa kazi watakaoisaidia jumuiya kuendana na mtazamo mpya wa CCM Mpya na Tanzania Mpya.

Mbali na kuwashukuru makada hao kwa kumchagua kuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya jambo lililopelekea Mhe Rais John Pombe Magufuli kumteua kuhudumu nafasi muhimu ya Kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe Mwanjelwa alisema kuwa serikali ya awamu ya tano ni ya kazi hivyo uchaguzi huo ni vyema kumalizika kwa kuwapata viongozi wachapakazi.

"Tunaelekea kwenye Mbeya Mpya, CCM Mpya, UWT Mpya na Tanzania Mpya hivyo msichague viongozi kutokana na makundi au watakaoendeleza makundi baada ya uchaguzi Bali chagueni viongozi shupavu na wachapakazi" Alikaririwa Mhe Mwanjelwa
Mhe Mwanjelwa (MNEC), alisema kuwa atafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuangalia jinsi utekelezaji wa ilani ya CCM inavyotekelezwa.

Mkutano huo Maalumu ulimalizika kwa salama hapo Jana Novemba 28, 2017 katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbeya ambapo viongozi mbalimbali walichaguliwa katika ngazi ya Mkoa na Taifa.

MAMBO 10 UNAYOTAKIWA KUYAFAHAMU KUHUSU UKIMWI

November 29, 2017
Na Jumia Travel Tanzania

Wakati dunia ikielekea kuadhimisha siku ya UKIMWI kila ifikapo Desemba mosi ya kila mwaka, bado Virusi Vya UKIMWI (VVU) na ugonjwa huo unabaki kuwa ni changamoto muhimu ya kiafya ndani ya jamii hususani kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati.

Kutokana na maendeleo yaliyofikiwa sasa katika upatikanaji wa tiba ya mchanganyiko wa dawa zinazotumika kuzuia VVU kuongezeka mwilini (antiretroviral therapy - ART), watu waliogundulika kuwa na VVU wanaishi kwa muda mrefu na maisha yenye afya. Kwa kuongezea, imethibitishwa kwamba dawa hizo zinazuia kuendelea kuongezeka kwa VVU.

Katika kukupatia elimu zaidi juu ya ugonjwa huu, Jumia Travel ingependa kukufahamisha juu ya mambo yafuatayo ambayo yamebainishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), ambalo huunga mkono nchi mbalimbali katika kuunda na kutekeleza sera na programu ili kuboresha na kuongeza jitihada za kuzuia VVU, matibabu, huduma na kutoa msaada kwa watu wote wanaohitaji msaada.

Taafirifa hizi zinatoa takwimu zilizopo sasa kuhusu ugonjwa huu pamoja na njia za kuuzia na kuutibu:

VVU huambukiza seli za kwenye mfumo wa kinga za mwili. Maambukizi husababisha kuendelea kuzorota kwa mfumo wa kinga ya mwili, huvunja uwezo wa mwili kuweza kuepuka baadhi ya maambukizi na magonjwa. UKIMWI hujulikana kuwa ni hatua ya juu kabisa ya VVU ambapo hujipambanua kwa kujitokeza kwa maambukizi kati ya zaidi ya 20 au saratani zinahusiana na virusi hivyo.   

VVU vinaweza kuambukizwa kwa njia kadhaa. VVU vinaweza kuambukizwa kupitia: kujihusisha na ngono isiyo salama; kuhamishiwa damu au bidhaa inayohusiana na damu au kufanyiwa upandikizaji ambao sio salama; kushirikiana kutumia vifaa vya kutobolea mwili (sindano) na vimiminika au vya kuchorea michoro mwilini (tattoo); kutumia vifaa vya upasuaji na vinginevyo vyenye ncha kali; na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto mchanga wakati wa ujauzito, kujifungua na kunyonyesha.   
Zipo njia kadhaa za kuzuia maambukizi ya VVU. Njia muhimu za kuzuia maambukizi ya VVU ni: kufanya ngono salama kama vile kutumia kondomu; kupima na kupatiwa matibabu kwa magonjwa yaliyoambukizwa kupitia ngono, ikiwemo VVU ili kuzuia maambukizi kuendelea; hakikisha kwamba damu au bidhaa yoyote inayohusiana na damu unayotaka kuitumia imepimwa VVU; chagua njia salama ya kimatibabu wakati wa tohara endapo unatoka katika nchi ambazo huchangia vifaa; kama una VVU anza mara moja kutumia dawa za kusaidia kupunguza virusi kuongezeka mwilini kwa manufaa yako na pia kuzuia kuambukiza VVU kwa mwenza au mtoto wako (kama ni mjamzito au unanyonyesha).  
Watu milioni 36.7 duniani wanaishi na VVU. Duniani kote, inakadiriwa kuwa watu milioni 36.7 (milioni 34.0 - 39.8) walikuwa wanaishi na VVU mwaka 2015, na kati ya hawa milioni 1.8 (milioni 1.5 - 2.0) walikuwa ni watoto. Idadi kubwa ya watu wanaoishi na VVU wanapatikana kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Inakadiriwa watu milioni 2.1 (milioni 1.8 - 2.4) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015. Inakadiriwa watu milioni 35 mpaka sasa wamefariki kutokana na VVU, wakiwemo milioni 1.1 (940,000 mpaka milioni 1.3) mwaka 2015.    
Mchanganyiko wa dawa za ART huzuia virusi hivyo kuongezeka mwilini. Endapo kuzaliana kwa VVU kukikoma, basi seli za kinga za mwili zitaweza kuishi kwa muda mrefu na kuupatia mwili kinga dhidi ya maambukizi. Ufanisi wa dawa za ART hupelekea kupungua kwa virusi, kiasi cha virusi mwilini, kwa kiasi kikubwa hupunguza kuambukiza virusi kwa watu walio kwenye mahusiano ya kimapenzi. Endapo mmojawapo wa wapenzi kwenye mahusiano anatumia dawa za ART ipasavyo, kuna uwezekano wa maambukizi ya njia ya ngono kwa mwenza ambaye hana VVU kupungua kwa kiasi cha takribani 96%. Kupanua wigo wa matibabu ya VVU kunachangia katika jitihada za kuzuia VVU.   
Katikati ya mwaka 2016, watu milioni 18.2 duniani walipokea dawa za kusaidia kuzuia VVU kuongezeka mwilini. Kati ya hawa zaidi ya milioni 16 wanaishi kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Mwaka 2016, WHO ilitoa toleo la pili la “Miongozo juu ya matumizi ya dawa za kusaidia kuzuia kuongezeka VVU mwilini ili kutibu na kuzuia maambukizi ya VVU.” miongozo hii imetoa mapendekezo kadhaa, ikiwemo pendekezo la kutoa dawa za kusaidia kuzuia VVU kuongezeka mwilini kwa watoto kwa kipindi chote cha maisha yao, vijana na watu wazima, wakiwemo wanawake wajawazito na wanaonyonyesha waishio na VVU, licha ya idadi ya CD4 walizonazo mara baada tu baada ya kugundulika.          

Kupima VVU kunasaidia kuhakikisha matibabu kwa watu wenye uhitaji. Upatikanaji wa huduma ya kupima VVU na madawa unatakiwa kuongezeka kwa kasi ili kufikia lengo la kutokuwa na ugonjwa wa UKIMWI kufikia mwaka 2030. Upimaji wa VVU bado ni mdogo, ambapo inakadiriwa kwamba 40% ya watu wenye VVU au zaidi ya watu milioni 14 bado hawajatambulika na hawafahamu hali ya maambukizi yao. WHO inapendekeza ubunifu kwenye mbinu za kujipima wenyewe VVU na wenza wao ili kuongeza huduma za kupima VVU kwa watu ambao hawajagundulika.    
Inakadiriwa watoto milioni 1.8 duniani wanaishi na VVU. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015, wengi wa watoto hawa wanaishi katika nchi zilizopo kusini mwa jangwa la Sahara na waliambukizwa kutoka kwa mama zao wenye VVU wakati wa ujauzito, wakati wa kuzaliwa au kunyonyeshwa. Karibu watoto 150,000 (110,000 - 190,000) walipata maambukizi mapya ya VVU mwaka 2015.
Kuondoa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto inawezekana. Ufikiwaji wa hatua za kuzuia maambukizi ya VVU umekuwa ni mdogo kwenye nchi zenye kipato cha chini na kati. Lakini jitihada zimeendelea kufanyika kwenye baadhi ya maeneo tofauti kama vile kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto pamoja na kuokoa maisha ya akina mama. Mwaka 2015, karibu wajawazito 8 kati ya 10 wanaoishi na VVU au sawa na wanawake milioni 1.1 walipokea dawa za kuzuia VVU kuongezeka mwilini. Mwaka 2015, Cuba ilikuwa ni nchi ya kwanza kutangazwa na WHO kufanikiwa kuzuia maambukizi ya VVU na Kaswende kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mwaka 2016, nchi zingine tatu: Armenia, Belarus na Thailand nazo zilithibitishwa kulifanikisha hilo.        
VVU ni sababu kubwa inayopelekea kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB). Katika mwaka 2015, inakadiriwa kuwa watu milioni 1.2 (11%) kati ya watu milioni 10.4 duniani waliopata TB walikuwa ni waathirika wa VVU pia. Mwaka huohuo takribani vifo 390,000 vilivyotokana na TB vilitokea miongoni mwa watu waliokuwa wanaishi na VVU. Nchi za Kiafrika ambazo zilizo chini ya WHO zilizidi karibu 75% ya idadi ya vifo vilivyokuwa vinahusiana kati ya TB na VVU.

WAZIRI MHAGAMA AZINDUA HUDUMA MPYA YA WCF YA WAAJIRI KUJISAJILI KWENYE MTANDAO WA INTERNET

November 29, 2017

Mkuu wa kitengo cha Tehama cha WCF, Bw. Stephen Goyayi, akielezea jinsi huduma hiyo iyakavyofanya kazi.
 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID. ARUSHA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, amezindua huduma mpya itakayowawezesha waajiri kujisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), kwa kutumia mtandao wa Internet.
Mhe. Mhagama amezindua huduma hiyo leo Novemba 29, 2017, wakati wa Mkutano wa Kwanza wa Mwaka wa Wadau wa Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), kwenye ukumbi wa Simba wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, AICC, Arusha.
“Huduma hii itawawezesha waajiri kujisajili na Mfuko kupitia mtandao wa internet na hawalazimiki kujaza fomu na kuja ofisini kwetu au kwa maafuisa kazi” Mkuu wa kitengo cha Tehama cha WCF, Bw. Stephen Goyayi, alisema wakati akitambulisha huduma hiyo kwa Mhe. Waziri.
Katika hatua nyingine, Benki ya NMB Bank plc  imenyakua tuzo baada ya kuwa mwajiri bora katika uwasilishaji michngo miongoni mwa waajiri wenye wafanyakazi wengi.
Kampuni zingine zilizonyakua tuzo kundi la waajiri ni Steel Master Ltd kwa kuwa mwajiri bora katika uwasilishaji nyaraka za madai ya fidia kwa wafanyakazi na kampuni nyingine ni KPMG  Advisory Ltd kwa kuwa mwajiri bora katika uwasilishaji michango miongoni mwa kundi la waajiri wenye wafanyakazi wengi.
WCF iliwatunukia tuzo wadau wa Mfuko huo ambapo Waziri Jenista kwa niaba ya Serikali alipokea tuzo hiyo, kwa kutambua mchango wa Serikali katika kuanzisha na kufanikisha utendaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Wadau wengine ni Shirika la Vyama vya Wafanyakazi, (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, (TUCTA), Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii, (SSRA), kwa kutambua ushiriki wake katika uanzishwaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF)
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, (wapili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Masha Mshjomba, wakishuhudia Mwenyekiyti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Bw. Emmanuel Humba, (kushoto), akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilinhi milioni 15, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo, ikiwa ni mchango wa Mfuko kusaidia mpango wa elimu mkoani humo. Makabidhiano haya yamekwenda sambamba na ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wadau wa WCF jijini Arusha

DAWA ZA SARATANI ZAPATIKANA KWA ASILIMIA 80 % KUTOKA ASILIMIA 4%

November 29, 2017
  Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (kulia), akizungumza na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Dar es Salaam leo ya kujua changamoto za upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Meshack Shimwela.
 Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Meshack Shimwela, akisisitiza jambo katika mkutano huo.
 Maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa MSD,Laurean Bwanakunu.
 Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam , Celestine Haule akichangia jambo wakaz8i akizungumza na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana.
 Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Anna Kajiru (kulia), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (wa sita kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana. 
 Mkutano ukiendelea.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage akizungumza katika mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu akisisitiza jambo wakati akizungumza na maofisa wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika ziara hiyo ya siku moja.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage ( kulia), akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu wakati wa ziara hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (wa tano kulia), akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Taasisi ya Saratani Ocean. 

Na Dotto Mwaibale

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road wameipongeza Bohari ya Dawa (MSD), kwa usambazaji wa dawa katika taasisi hiyo na maeneo mengine nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage wakati akizungumza na watendaji wa MSD ambao walifanya ziara ya kikazi ya kujua changamoto mbalimbali za usambazaji dawa katika taasisi hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu.

Katika hatua nyingine  upatikanaji wa dawa za saratani,vifaa tiba na vitendanishi  vya maabara katika taasisi hiyo ni asilimia 80  kutoka asilimia nne mwaka 2015.

Kutokana na hatua hiyo taasisi hiyo imesema ipo haja jamii kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Bohari ya Dawa MSD katika kupunguza changamoto za huduma za saratani ambapo ilikuwa kero miaka miwili iliyopita.

 Mwaiselage alisema hapo awali  upatikanaji wa dawa vifaa tiba na vitendanishi ilikuwa ni changamoto kubwa katika utendaji.

"2015 taasisi hiyo ilikuwa ikipata dawa,vifaa tiba na vitendanishi asilimia nne sasa ni asilimia 80 haya ni matokeo mazuri ya utendaji wa kazi wa MSD," alisema.

Taasisi ya The Voice of the voiceless yamteua Selembe kuwa balozi wa ‘Tunza funguo yako’

November 29, 2017
Taasisi ya the voice of the voiceless Jumapili hii ili pata balozi wao mpaya ambaye atakuwa anahiwakilisha taasisi na kuwa balozi wa mradi wao wa TUNZA FUNGUO YAKO.
Balozi huyo anafamika kwa Jina la SELEMBE ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar
Awali wakati wa tukio la ukabizishaji wa jezi ya taasisi hiyo Bwana Selembe alishukuru taasisi hiyo na  kuonyesha furaha yake ya kuchaguliwa na kupewa cheo icho kwakuwa yeye pia ni mzanzibar amefarijika kuona kuwa balozi ambaye atasimania kuongoza mradi wa TUNZA FUNGUO YAKO.
Taasisi ya VOV foundation katika kuboresha mradi wao na kuweza kufika mbali nakupata wadau ambao watachangia kwa mwaka 2018.
Kwa upande wake Omary A. Mdogwa ambaye ni mwanzilishi wa taasisi hiyo alikuwa alibainisha kuwa waliamua kumchagua Selembe kutokana na ushawishi wake kwa mchezaji huyo visiwani humo pamoja na kuangalia mambo mengine mbalimbali kama vigezo tosha kwa kuwa balozi wao.
"Tume mchagua bwana Selembe kwa nia moja tu ya kufanya utofauti na kuangalia upenzi wa mpira kwa upande wa Zanzibar. Pia tutatumia mchezo wa mpira kuweza kufanya 'donation' mbali mbali ili kuweza kusaidia vijana walio mashuleni "Alieleza Mdogwa.
Balozi mpya wa Taasisi ya the voice of the voiceless ambaye atakuwa anahiwakilisha taasisi na kuwa balozi wa mradi wao wa 'TUNZA FUNGUO YAKO' Selembe ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar
Balozi mpya wa Taasisi ya the voice of the voiceless ambaye atakuwa anahiwakilisha taasisi na kuwa balozi wa mradi wao wa 'TUNZA FUNGUO YAKO' Selembe ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Zanzibar
Viongozi wa Taasisi ya the voice of the voiceless wakimkabidhi jezi maalum Selembe  ambaye atakuwa anahiwakilisha taasisi hiyo kama Balozi wa mradi wao wa 'TUNZA FUNGUO YAKO'. Viongozi hao kulia ni Mwanzilishi wa Taasisi hiyo Omary Mdogwa na kulia ni  Mkurugenzi Mkuu wa vov foundation, Bi Anatolia Kasira

Mshindi wa Milioni 60 za Tatumzuka aamua kuwekeza ushindi wake kwenye elimu

November 29, 2017

Catherine Triphone wiki iliyopita alitimiza ndoto yake ya kusoma baada ya kushinda milioni 60 za jackpot ya Tatumzuka. Bi Catherine ambaye anaishi na wazazi wake, siku ya jumapili alikuwa nyumbani peke yake huku akisinzia alipopigiwa simu iliyobadilisha maisha yake.

Dada huyo mwenye umri wa miaka 25, amekuwa akicheza Tatumzuka mara kwa mara kwa kutumia namba zinazoendana matukio mbalimbali yanayohusu maisha yake na ndugu zake ambapo ameshinda mara kadhaa katika droo za kila saa.

"Namba zangu daima zimekuwa 842. Hizi namba zinawakilisha siku , mwezi na mwaka wangu wa kuzaliwa. Ninaishukuru Tatu Mzuka kwa kutoa fursa hii ambapo mtu yoyote anaweza kucheza na kushinda, " aliongeza Bi Catherine

Dhamira ya Tatu Mzuka kwa sasa ni zaidi ya kubadilisha maisha ya washindi wetu; tumejizatiti pia kuunga mkono mipango mbalimbali ya serikali katika jamii ili kuboresha maisha ya Watanzania wote. Mpango huu ni sehemu ya kauli mbiu yetu ya ‘Ukishinda, Tanzania inashinda’.

"Kwa ushirikiano na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori tumeamua kununua vitabu kwa baadhi ya shule Wilayani humo. Tunatarajia kukamilisha taratibu zote na kutoa vitabu hivyo hivi karibuni. “ Alisema Sebastian Maganga, Meneja wa Mawasiliano wa Tatu Mzuka.

Kwa kuupendezesha msimu huu wa sikukuu, Tatu Mzuka imeahidi kufungua msimu huu wa furaha kwa kutoa shilingi milioni 500 kuanzia sasa mpaka Desemba 31, 2017. Utajisikiaje kama utamaliza mwaka kwa kupata ushindi mkubwa? Endelea kucheza, uendelee kushinda. Natumai Bi Catherine atafurahia sana sikukuu ambapo ni baada ya kucheza Tatumzuka kwa shilingi 500 tu.” Bwana Maganga alihitimisha

Bi Catherine anapanga kurudi shule kusoma kusoma shahada na kuwanunulia wazazi wake usafiri ili kuwaondolea adha ya usafiri wanayokumbana nayo.

 Meneja wa Mawasiliano wa Tatu Mzuka Sebastian Maganga akizungumza mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) mapema leo jijini Dar,alipokuwa akimtangaza Mshindi wa milioni 60 za jackpot ya Tatumzuka. Bi Catherine Triphone (pichani kulia).
 Mshindi wa milioni 60 za jackpot ya Tatumzuka. Bi Catherine Triphone (pichani kulia).akitoa ufafanuzi namna alivyoshinda hizo milioni 60 na namna atakavyozitumia,ambapo Catherine amesema kuwa fedha hizo atazitumia kujielimisha .
 Meneja wa Mawasiliano wa Tatu Mzuka Sebastian Maganga akimkabidhi mfano wa hundi,Mshindi wa milioni 60 za jackpot ya Tatumzuka. Bi Catherine Triphone (pichani kulia).

WAZIRI MKUU MAJALIWA AIPONGEZA WCF KWA KUPIGA HATUA KUBWA NDANI YA KIPINDI KIFUPI

November 29, 2017

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Umlemavu, Mhe. Jenista Mhagama, akifungua mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Wadau wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kwenye ukumnbi wa Simba, Kituo cga Mikutano cha Kimataifa, AICC Arusha leo Novemba 29, 2017

  
 NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, ARUSHA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), kwa mafanikio ambayo Mfuko umepayata katika kipindi cha muda mfupi tangu uanzishwe.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Wadau wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF) jijini Arusha leo Novemba 29, 2017, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama amesema, katika kipindi kifupi cha miaka miwili tangu WCF ianizshwe Mfuko umeweza kutekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kusajili wanachama na kulipa Mafao ya Fidia.
“Mfuko umeanza kufikia wanyonge kwani umeonyesha jinsi ambavyo wafanyakazi wanyonge waliokuwa hawalipwa fidia wanapopata madhara kazini, sasa kutokana na kuwepo kwa Mfuko huu wanyonge wameanza kufaidi matunda kama ambavyo serikali ilidhamiria.
“Nitoe wito kwa viongozi wa Mfuko, endeleeni kutoa elimu kwa wananchi hususan waajiri ili waweze kujisajili na hivyo kuwapunguzia mzigo wa kuwalipa fidia wafanyakazi wao pindi wanapopata madhara wawapo kazini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Bw. Masha Mshomba amesema hali ya Mfuko ni njema tangu uanzishwe, “Tunapokutana leo hii kwa mara ya kwanza kabisa, napenda kuwajulisha kuwa Mfuko umekuwa ukifanya vizuri katika kuimarika kifedha ambapo kwa mwaka wa kwanza tu, Mfuko ulifikia kiasi cha shilingi Bilioni 65.68 na katika mwaka wake wa pili ambapo ndio huu tulio nao napenda kuwafahamisha kuwa Mfuko umekuwa hadi kufikia Shilingi Bilioni 135 fedha ambazo bado hazijakaguliwa lakini sitarajii tofauti kubwa sana hata zoezi la ukaguzi litakapofanyika”. Amesema Bw. Mshomba.

Aidha Bw. Mshomba alisema, madhumuni ya Mkutano huu wa siku mbili ambao umebeba kauli mbiu ya "Mafao ya Fidia: Haki ya Mfanyakazi na chachu katika kukuza uchumi wa viwanda”.  ni kutoa taarifa ya mwaka ya Mfuko, kutathmini maendeleo na changamoto zinazoukabili Mfuko na kupokea maoni ya kuboresha huduma za Mfuko.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Bw. Emmanuel Humba amesema, tangu Mfuko uanzishwe, umetoa mafunzo mbalimbali  kwa wadau wa Mfuko ikiwa ni pamoja na Madaktari.

FULL VIDEO: SERIKALI YASISITIZA DESEMBA 31 KUWA UKOMO WA UWEKAGI WA VIGINGI (BEACONS) VYA MPAKA HIFADHIN

November 29, 2017



Na Hamza Temba - Wizara ya Maliasili
..........................................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga amesisitiza agizo la Serikali lililotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu kuhusu kukamilisha zoezi la uwekagi wa vigingi vya mpaka kwenye maeneo ya hifadhi nchini ifikapo Desemba 31 mwaka huu.

Amesema lengo la kukamilisha zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa mwisho wa kumaliza migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu baina ya vijiji na maeneo ya hifadhi nchini.

Mhe. Hasunga ametoa kauli hiyo jana wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi ya msitu wa Isalalo Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe ambapo aliziagiza taasisi zilizo chini ya Wizara yake kukamilisha zoezi hilo kabla ya tarehe hiyo ili kuiwezesha Serikali kubaini maeneo yenye mapungufu na kuyatolea uamuzi.

“Ifikapo tarehe 31 tuwe tumemaliza kuweka hizo beacon (vigingi) za mipaka, baada ya hapo hatua itakayofuata, Serikali tutakaa na kuangaliza ni vijiji vingapi au maeneo gani yameingia ndani ya hifadhi, tuangalie je tuwaachie hayo maeneo wananchi au tuwahamishe tuwapeleke maeneo mengine, maamuzi hayo yatakuja baada ya kufanya tathmini na kubaini penye mapungufu.

“Sasa ikitokea kwamba imefika tarehe 31 hatujatekeleza hili mimi kama Naibu Waziri nitakuwa sina kazi, maana sijatekeleza agizo la Serikali, kwahiyo lazima tulisimamie, na mimi sasa kabla halijanipasukia nitakupasukia bwana Meneja (Meneja TFS Wilaya ya Mbozi), nitakuja kukagua mipaka, na kabla ya tarehe 31 nitakuja kukagua tena,”alisema Naibu Waziri Hasunga.

Wakati huo huo amekemea vitendo vya baadhi ya wananchi wanaoingiza mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini na kuwataka kufugia majumbani kwao au maeneo yaliyotengwa kwa ajili hiyo, amewatahadharisha pia juu ya ukali wa sheria za uhifadhi na kwamba endapo mifugo itakamatwa hifadhini sheria zilizopo zinaruhusu utaifishaji.

Aidha aliwataka wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo ya msitu wa Isalalo kuacha vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti hovyo kwa ajili ya mkaa na uanzishaji wa maeneo ya kilimo. Pia alitoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo vya maji na kuacha vitendo vya uchomaji moto misitu.

Katika hatua nyingine ameuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Nyanda za Juu Kusini kuwashirikisha wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo ya msitu kwenye ulinzi wa hifadhi ikiwa ni pamoja na kuwawezesha miche ya miti ya kutosha kwa ajili ya kupanda  kwenye maeneo yao yanayozunguka hifadhi hiyo.

Aidha ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kupima maeneo yao na kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa kuanisha maeneo kwa ajili ya kilimo, ufugaji na maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima ya wananchi

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni alisema katika kuimarisha mpaka wa hifadhi ya msitu huo wa Isalalo ambao una ukubwa wa hekta 11,552, jumla ya vigingi 30 vimewekwa kuzunguka hifadhi hiyo.

Alizitaja baadhi ya  changamoto katika hifadhi hiyo kuwa ni uvamizi wa wakulima na wafugaji, uvunaji haramu wa miti, uchomaji mkaa na moto, na ung'oaji wa vigingi vya mpaka na mabango.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo alisema ili kuimarisha uhifadhi wa msitu wa Isalalo ni vema wananchi wakashirikishwa ikiwemo kuanzishwa kwa vikundi vya vijana ambao watawezeshwa bodaboda zitakazowanufaisha kiuchumi na wakati huo huo zikatumika kwenye ulinzi wa hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kushoto) akioneshwa ramani ya Hifadhi ya Msitu wa Isalalo na Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Wilaya ya Mbozi, Fred Mgeni (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua hifadhi hiyo kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani Songwe jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo wakati wa kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo Mkoani Songwe kwenye ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya Mbozi, John Palingo (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua Hifadhi ya Msitu wa Isalalo uliopo wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuimarisha uhifadhi mkoani humo.