MGAZA: Serikali itaendelea kuhamasisha kilimo cha Muhogo

July 11, 2013
Na Oscar Assenga, Mkinga.

MKUU wa wilaya ya Mkinga, Mboni Mgaza amesema serikali wilayani humo itaendelea kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kilimo cha Muhogo ili kiweza kuwa mkombozi wao katika maendeleo na kuinua kipato chao.

Kauli ya Mkuu huyo wa wilaya ilisomwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Mkinga Zuwani Makame hivi karibuni aliyemuwakilisha katika uzinduzi wa kampeni ya kilimo cha muhogo iliyoanzishwa na shirika la Farm Radio Internationali kwa kushirikiana na kituo cha Radio Mwambao ya Tanga.

Makame alisema Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa wakulima ikiwemo kuwapatia wakulima elimu stahiki kuhusu kilimo chenye tija wataweza kunufaika na kilimo chao, hivyo itaendelea kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kupata elimu ya kilimo bora.

Aidha alisema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali kwenye shughuli za kilimo katika maeneo mengi hasa ya wilaya ya Mkinga, na changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu ya njia bora ya kuendesha kilimo chenye tija hivyo kampeni hizi zimekuja wakati muafaka, naamini zitawanufaisha wakulima na kuweza kupata mazao mengi katika kilimo chao.

Alieleza kuwa uzinduzi wa kilimo hicho utasaidia wananchi kujiondoa kwenye umasikini kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, na ndicho ambacho wenzetu wa Farm Radio international kupitia mradi huu wanafanya kuelimisha wakulima kwa njia ya Radio.

Hata hivyo amesema licha ya kuwa na wataalamu wa ugani wachache na hivyo matumizi ya redio yatasaidia kuwafikia wakulima wengi sana kwani redio zinafika maeneo mengi ili kuweza kuongeza ujuzi kwa wakulima hao kabla ya kuanza msimu wa kilimo.

Katibu Tawala huyo amewataka wakulima wote wa vijiji vya Mzingi Mwagogo, Mapojoni, Mvunde manyinyi na vijiji vyote vya wilaya ya Mkinga na vijiji jirani vya wilaya za jirani ambapo kampeni hizi zinagusa kupitia mradi wa njia bora za uvunaji ,usindikaji na uhifadhi  wa zao la muhogo , mtumie vema fursa hii iliyoletwa na wenzetu wa Farm Radio   kwa kushiriki kwenye Kampeni hii kikamilifu.

Ameongeza kuwa kampeni hii itawanufaisha sana kwenye kilimo na itawasaidia kupata masoko na kujiongezea kipato ikiwa watazingatia vema yale yatakayokuwa yanafanyika na kuelezwa na wataalamu mbalimbali wa kilimo.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Mtaalamu wa Mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo kutoka shirika la Farm Radio International lenye makao yake makuu jijini Arusha, Terevael Aremu Nassary amesem,a shirika hilo limeona umuhimu wa kushirikiana na radio Mwambao ya Tanga katika kufikisha elimu yake juu ya njia bora za uvunaji,usindikaji na uhifadhi wa zao la muhogo ambalo lina soko na linazalishwa kwa wingi mkoani Tanga ikiwemo wilaya ya Mkinga.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa radio Mwambao FM, Mfaume Kikwato alisema vipindi vya elimu juu ya njia bora ya uvunaji, usindikaji na uhifadhi wa zao la Muhogo vitakuwa vikirushwa na kituo hicho kuanzia Julai 5 mwaka huu na kuendelea kila siku za Ijumaa saa moja hadi saa moja na nusu na marudio yake yatakuwa Jumapili saa moja na nusu mpaka saa mbili usiku.

Mwisho

MECHI YA STAND, KIMONDO NAYO KUPIGWA JUMAPILI

July 11, 2013
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya iliyokuwa ichezwe Jumamosi  imesogezwa mbele kwa siku moja.

Akizungumza na Blog hii,Ofisa habari wa shirikisho la soka hapa nchini TFF,Ipichani kulia)Boniface Wambura alisema timu hizo sasa zitacheza Jumapili  kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.


Kimondo ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
 
Mechi nyingine ya ligi hiyo itakuwa kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara, na itafanyika kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Mwamuzi wa mechi hiyo ni Hans Mabena kutoka Tanga.

TENGA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI KESHO

July 11, 2013
TENGA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI KESHO
 Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi
wa habari. Mkutano huo utafanyika kesho (Julai 12 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwenye hoteli ya Tansoma.

Kutokana na mkutano huo, sasa mkutano kati ya makocha wa Taifa Stars na The Cranes uliokuwa ufanyike saa 5 asubuhi ofisi za TFF nao umehamishiwa hoteli ya Tansoma. Mkutano huo pia utahusisha manahodha wa timu zote mbili.

Wakati huo huo ,Wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika

Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) wanawasili jijini Dar es Salaam kesho (Julai 12 mwaka huu).

Mkutano huo wa marekebisho ya Katiba utakuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga na utafanyika ukumbi wa NSSF Waterfront kuanzia saa 3 kamili asubuhi. Wajumbe wote wa mkutano huo watafikia hoteli ya Travertine.

Pia mkutano huo utahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa wakiwemo kutoka Shirikisho la Kimataifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA).

UGANDA CRANES YAWASILI KUIKABILI STARS

UGANDA CRANES YAWASILI KUIKABILI STARS

July 11, 2013
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) imewasili Dar es Salaam leo tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati yake na Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

The Cranes inayofundishwa na Mserbia Sredojvic Micho imetua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 5.30 asubuhi kwa ndege ya Air Uganda, na imefikia hoteli ya Sapphire.

Timu hiyo leo (Julai 11 mwaka huu) itafanya mazoezi saa 9 alasiri kwenye Uwanja wa Karume, wakati kesho saa 9 alasiri itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa, kabla ya kuipisha Taifa Stars itakayoanza mazoezi saa 10 kamili jioni.

Taifa Stars inayofundishwa na Mdenmark Kim Poulsen, na kudhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, leo kwa mujibu wa program yake haitakuwa na mazoezi.
 
Wachezaji wanaounda The Cranes ni makipa Ismail Watenga, Kimera Ali na Muwonge Hamza. Mabeki ni Guma Dennis, Kasaaga Richard, Kawooya Fahad, Kisalita Ayub, Magombe Hakim, Malinga Richard, Mukisa Yusuf, Savio Kabugo na Wadada Nicholas.

Viungo ni Ali Feni, Birungi Michael, Frank Kalanda, Hassan Wasswa, Kyeyune Said, Majwega Brian, Mpande Joseph, Muganga Ronald, Ntege Ivan, Owen Kasule, wakati washambuliaji ni Edema Patrick, Herman Wasswa na Tonny Odur.