Tume yatoa Ufafanuzi kuhusu ucheleweshwaji wa matokeo ya Urais

Tume yatoa Ufafanuzi kuhusu ucheleweshwaji wa matokeo ya Urais

October 28, 2015

index 
Na Beatrice Lyimo-Maelezo Dar es salaam.
………………………………………..
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji mstaafu Damian Lubuva ametoa ufafanuzi juu ya ucheleweshaji wa matokeo ya  awali ya ngazi Rais kutoka majimbo mbalimbali nchini.
Akitangaza matokeo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 27, 2015  jijini Dar es salaam Jaji Lubuva amesema kuwa Tume inasubiri matokeo hayo kutoka kwa wasimamizi wa uchaguzi kutoka katika majimbo yote nchini.
“waandishi wa habari mnatakiwa kuwa wavumilivu na kutangaza kile ambacho mnakisikia  na si kupotosha umma kwani Tume inatoa matokeo bila kupendelea chama chochote” aliongeza Jaji Lubuva.
Mbali na hayo jumla ya majimbo 87 yameshaleta majibu ya awali ya matokeo ya urais yakiwemo Mkoa wa Kusini Pemba Jimbo la Nchonga ambapo jumla ya wananchi 8,018 walijiandikisha, 5949 walipiga kura na kura halali zilikuwa 5771 ambayo ni asilimia 97.01 na 178.29 zilikataliwa.
Vilevile katika Jimbo la Chunguni waliojiandikisha walikuwa 13,416 ambapo wananchi 10,108 sawa na asilimia 75.34 walipiga kura, kura halali zilikuwa 9,792 sawa na asilimia 96.92 pamoja na kura 311 zilikataliwa ambayo ni sawa na asilimia 3.08.
Halikadhalika katika   Mkoa wa Mbeya Jimbo la Ileje jumla ya wananchi 56,002 walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ambapo asilimia 78.56 sawa na 43,997 walipiga kura, kati ya idadi hiyo kura 43,098 zilikuwa halali na kura 896 sawa na asalimia 2.04 zilikataliwa.
Jaji Lubuva aliongeza kuwa katika Jimbo la Ileje mkoani Mbeya ACT ilipata kura 501, ADC kura 347, CCM kura 26,368, CHADEMA kura 15, 651, CHAUMA walipata kura 155, NRA kura 26,TLP kura 36, pamoja na kura 20 kutoka chama cha UPDP.
Mbali na hayo majimbo mengine yaliyowakilisha matokeo hayo ni pamoja an Jimbo la Mtama kutoka Mkoa wa Lindi, Jimbo la Tunguu Mkoa wa kusini Unguja, Jimbo la kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, Jimbo la Nachingwea, Jimbo la mtama kutoka  mkoani Lindi, Jimbo la Mafia mkoani Pwani pamoja  Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani.
Pia Mkoa wa Katavi Jimbo la Mpanda vijijini, Mkoa wa Magharibi Mjini Jimbo la Fuoni, Jimbo la Kikwajuni, Jimbo la Mwera, Jimbo la Amani na Jimbo la Magomeni Mkoa wa Unguja Jimbo la Nungwi, Kaskazini Unguja Jimbo la Bumbwini, mkoa wa Rukwa Jimbo la nkasi kusini, Mkoa wa Kagera Jimbo la Nkenge na  Jimbo la Byalamuro, kutoka Mkoani Arusha Jimbo la Arusha Mjini yaliwakilisha matokeo yao.
Kwa upande wake Msaidizi wa  Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema Bwa. Matson Chizi  amesema kuwa mchakato mzima wa Uchaguzi ni mzuri wa wapo tayari kupokea matokeo hayo kwa jinsi yatakavyokuwa.
MATUKIO KUTOKA KATIKA UKUMBI WA MWALIMU NYERERE JIJINI DAR ES SALAAM

MATUKIO KUTOKA KATIKA UKUMBI WA MWALIMU NYERERE JIJINI DAR ES SALAAM

October 28, 2015

1
Makamu Mwenyekiti Tume ya Taifa ya Uchaguzi  Bw.Hamid M. Hamid (wapili kushoto) akisoma matokeo ya wagombea nafasi ya Urais leo jijini Dar es Salaam katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,anayemfuata kulia ni Mwenyekiti  wa Tume Jaji  Mstaafu Damian Lubuva.
2
Baadhi ya waandishi wa Habari wa Ndani na  Nje ya nchi wakifuatilia zoezi la kutangazwa kwa matokeo ya wagombea Urais  katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu  leo katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Dar es Salaam.
3
Msaidizi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi Chadema Bw. Matson Chizi akihojiwa na mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya  Ujerumani (DW) Bi.Hawa Bihoga  kuhusu namna gani analiona zoezi la utangazaji wa matokeo linafanyika.
4
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi  Jaji Mstaafu Damian Lubuva  wanne kushoto kwa waliyokaa katika picha ya pamoja kwa baadhi na waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi za  Jumuiya ya SADC walipotembea ukumbi unaotumika kutangazia matokeo ya wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu leo jijini Dar es Salaam.
5
Mwandishi wa habari kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Bw.Edward Kondela akimhoji mmoja wa waangalizi wa uchaguzi ambaye ni  Mwenyekiti wa SADC  nchini Malawi Bw.Justice Mbendera  alipotembelea ukumbi wa kutangazia matokeo ya urais leo jijini Dar es Salaam.
Picha na  Anitha Jonas – MAELEZO.

WALIOSAMBAZA MATOKEO YA URAIS KINYUME CHA SHERIA WAPANDISHWA KIZIMBANI MAHAKAMA YA KISUTU JIJINI DAR ES SALAAM

October 28, 2015

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (katikati), akizungumza na mmoja kati ya vijana nane waliofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam leo, kwa tuhuma za kusambaza matokeo ya kura za mgombea nafasi ya urais wa chama hicho katika mitandao ya kijamii kinyume na utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Imedaiwa vijana zaidi ya 190 walikamatwa kwa kosa hilo.
 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam leo.
Askari wa FFU wakiimarisha ulinzi mahakamani hapo.
Wafuasi wa Chadema wakionesha alama ya vidole viwili wanayoitumia.
Viongozi wa Chadema wakitoka katika mahakama hiyo baada ya kusikiliza kesi hiyo. 
Vijana waliokamatwa wakiwa katika mahakama hiyo.
………………………………………………………………..
 
Na Dotto Mwaibale
 
WATU wanane akiwemo Raia mmoja wa Korea na raia mmoja wa Kenya wamepandishwa kizimbani kwa kusambaza taarifa za matokeo ya urais katika Mtandao wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yakiwa na kichwa ‘M4C election result management system’ bila kuthibitishwa kwa lengo la kupotosha umma. 
Sanjari na hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha mahakamani hati ya kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile alichadai kuwa ni kwa sababu ya usalama na kwa maslahi ya Taifa.
Washtakiwa hao ni Mashinda Mtei (49) mkazi wa Tengeru Arusha, Julius Mwita (40) mwanasiasa na ni mkazi wa Magomeni, Frederick Fussi (25) IT, mkazi wa Mbezi, Julius Matei (45) raia wa Kenya, Meshack Mlawa (25) mchungaji na ni mkazi wa Keko, Anisa Rulanyan (41) Mhandisi, mkazi wa Kawe, Jose Nimi (51) mkazi wa Uingereza na Kim Hyunwook (42) raia wa Korea.
Wakili wa Serikali Mkuu Edwin Kakolaki alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Respicius Mwaijage wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa washtakiwa wanashtakiwa kwa mashtaka matatu.
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote, ambapo inadawa kati ya Oktoba 25 na 26 mwaka huu, wakiwa katika vituo tofauti tofauti ndani ya jiji la Dar es Salaam walitoa taarifa za uongo kwenye mitandao wakati wakijua hazijadhibitishwa.
Kakolaki alidai washtakiwa hao walisambaza taarifa hizo kwenye mtandao huo na katika mitandao mingine ya kijamii ambayo ni  Facebook na Twitter kutangaza matokeo ya urais ya mwaka huku kwa lengo la kuposha umma huku wakijua hayajadhibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika shtaka la pili linamkabili Matei, Nimi na Hyunwook, ambapo wanashtakiwa kuwa Oktoba 26 mwaka huu wakiwa katika hoteli ya King iliyopo Kinondoni , Dar es Salaam wakiwa na hati za kusafirilia zenye namba A1532119, 930879 na M 27687807 walijiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya urais ya uchaguzi wa mwaka huu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) bila kibali.
Pia, alidai katika shtaka la tatu lina mkabili Matei peke yake ambaye akiwa raia wa Kenya mwenye hati ya kusafirilia namba A1532119 akiwa ndani ya jiji  la Dar es Salaam alijihusisha na biashara katika Saccos ya Wanama bila kibali.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo, walikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo Kakolaki alidai upelelezi bado haujakamilika na pia alidai DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa sababu ya usalama na maslahi ya Serikali.
Wakili wa washtakiwa hao Peter Kibatala, alidai kuwa mashtaka yanayowakabili wateja wake yanadhaminika, kwa hiyo aliiomba mahakama iwapatie dhamana.
Pia, alidai hati hiyo ya DPP haiko mahakamani hapo kihali na kuiomba Mahakama itupilie mbali hati hiyo kwa sababu haina mashiko kisheria.
Kibatala alidai kuwa hati ya mashtaka iko tofauti na hati ya DPP kutokana na kifungu kilichokuwepo kuwa si sahihi, kwa hiyo kama ni hivyo hati hizo zote hazifai, kutokana na mapungufu hayo.
Baada ya Kibatala kudai hivyo, wakili Kakolaki alidai kuwa hati ya DPP ipo kihalali mahakamani na anayuetakiwa kuthibitisha hilo na mahakama kwa hiyo waiyachie mahakama.
Alidai kuhusu kifungu kilichotumika ni sahihi, akaiomba mahakama itupilie mbali hoja za Kibatala na washtakiwa wanyimwe dhamana kwa mujibu wa sheria, baada ya DPP kuwasilisha hati hiyo.
Hakimu Mwaijage alisema uamuzi wa hoja hizo atazitoa Oktoba 30 mwaka huu na washtakiwa aliamuru warudishwe rumande.
Nje ya mahakama
Washtakiwa hao waliondoka katika eneo hilo la mahakama wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi ambapo wakiwa ndani ya magari ya polisi walikuwa wakionesha alama za vidole viwili.
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sauti, Profesa Mwasiga Baregu na viongozi wengine wa Chadema walijitokeza mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.

ZEC: MAALIM SEIF ANAPASWA KUCHULIWA HATUA ZA KISHERIA KWA KUTANGAZA MATOKEO

October 28, 2015
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imesema imesikitishwa na kitendo cha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF) kujitangazia ushindi katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili tarehe 25 Oktoba, 2015 na imevitaka vyombo vinavyosimamia utii wa sheria kumchukulia hatua kiongozi huyo wa CUF. 

“kitendo cha Maalim Seif kujitangaza mshindi amevunja kifungu cha 42 (5) cha sheria ya mwaka 1984 ambacho kinaipa mamlaka Tume ya Uchaguzi kuwa chombo pekee chenye mamlaka hayo” Mwenyekiti huyo alifafanua. 

Akijibu maswali ya waandishi wa habari leo, Mweyekiti wa ZEC Jecha Salum Jecha alisema kuwa Maalim Seif ametenda kosa la jinai hivyo mamlaka zinazohusika zinapaswa kumchukulia hatua. Kwa mujibu wa kifungu hicho, mtu akithibitika ametenda kosa hilo atahukumiwa kulipa faini ya Tzs laki tano au kwenda jela miaka mitano au adhabu zote. 

“Tume haina mamlaka ya kumkamata wala kumhoji Maalim lakini viko vyombo vyenye mamlaka hayo hivyo itakuwa ni vyema vikatimiza wajibu wao kwa kumkamata na kumhoji mhusika hasa ukizingatiwa kuwa hii ni mara ya pili kwa Maalim Seif kutenda kosa kama hilo” 

Mwenyekiti wa Tume alieleza. Alibainisha kuwa Tume yake imekijadili kitendo hicho kwa makini na uzito unaostahiki na kubainisha kuwa tangazo hilo linaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu uliopo nchini. 

Bwana Jecha alibainisha kuwa Maalim Seif, kama walivyo wagombea wengine 13 wa nafasi ya urais wa Zanzibar wanaelewa fika sheria hiyo hivyo alitoa wito kwa wagombea wengine kuwa watulivu kama walivyo wananchi. 

Kuhusu kasi ndogo ya Tumeyake kutangaza matokeo, Mwenyekiti huyo alisema hivi sasa kazi kubwa wanayoifanya ni kuhakiki kura kujua kama hakuna tofauti ya kura baina ya zile zilizoandikwa na hali halisi. 

“Wanaoandika na kuhesabu kura wote ni binadamu hivyo wanaweza kuchanganya mahesabu na ndio maana kazi yetu hivi sasa ni kulinganisha kura”alisisitiza Mwenyekiti wa Tume.

 Kuhusu kukamatwa kwa karatasi za kupigia kura huko katika jimbo la uchaguzi la Chonga, Wilaya ya Chake Chake, mkoa wa Kusini Pemba, Bwana Jecha alikiri kutokea kwa hilo na kwamba suala hilo sasa liko chini ya mikono ya Jeshi la Polisi.

 Alitahadharisha juu vitendo vya baadhi ya wagombea kuchukua vyeti bandia vinavyoonesha kuwa tayari wao wameshinda nafasi za ubunge au ujumbe wa Baraza la Wawakilishi. Bwana Jecha alitoa wito kwa wananchi kufanya subira wakati huu Tume yake ikifanya kazi ya kukusanya na kuhakiki kura na baadae kuwatangaza washindi. -- ---- Cathbert Angelo Kajuna, Founder and Mananging Director Kajunason Blog, P.O Box 6482, Dar es Salaam. Tel: +255 787 999 774 Alt: +255 765 253 445 www.kajunason.blogspot.com "Everything is Possible Through Peace & Stability''