RAIS DKT. MAGUFULI AHUTUBIA MABALOZI KATIKA SHEREHE ZA MWAKA MPYA KWA MABALOZI WANAOWAKILISHA NCHI ZAO HAPA NCHINI (DIPLOMATIC SHERRY PARTY) IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

RAIS DKT. MAGUFULI AHUTUBIA MABALOZI KATIKA SHEREHE ZA MWAKA MPYA KWA MABALOZI WANAOWAKILISHA NCHI ZAO HAPA NCHINI (DIPLOMATIC SHERRY PARTY) IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

February 09, 2018


1. 2
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mabalozi mbalimbali pamoja na Waakilishi wa Mashirika ya Kimataifa katika sherehe ya kukaribisha Mwaka mpya kwa Mabalozi hao wanaowakilisha nchi zao hapa nchini(Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
3
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Dkt. Augustine Mahiga katika picha ya pamoja na  Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini katika Hafla ya kukaribisha Mwaka mpya 2018 kwa mabalozi hao (Diplomatic Sherry Party) iliyofanyika Ikulu.
5 6 7
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na kuwakaribisha Mabalozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza kwa hafla ya kukaribisha mwaka mpya kwa Mabalozi hao.
8
Baadhi ya Mabalozi hao wakisikiliza Hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
PICHA NA IKULU

MKUTANO WA MAWAZIRI WA SEKTA YA MALIASILI NA MAZINGIRA WA JUMUIYA YA AFRIKA YA MASHARIKI WAFANYIKA LEO JIJINI ARUSHA

February 09, 2018
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) akiteta jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakati wa mkutano wa tano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Mazingira wa Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliohitimishwa leo katika ukumbi wa EAC jijini Arusha. Mkutano huo ulilenga kujadili na kusaini makubaliano mbalimbali ya namna bora ya kusimamia sekta hizo katika nchi wanachama. 
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (kulia) akisaini baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa tano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Mazingira wa Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliohitimishwa leo katika ukumbi wa EAC jijini Arusha. Mkutano huo ulilenga kujadili na kusaini makubaliano mbalimbali ya namna bora ya kusimamia sekta hizo katika nchi wanachama. Wanaoshuhudia ni Mawaziri wa Mazingira kutoka Uganda na Kenya.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba (wa pili kulia) na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Bi. Katerina Rangnitt wakiangalia baadhi ya michoro ya katuni za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira muda mfupi baada mkutano wa tano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Mazingira wa Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliohitimishwa leo katika ukumbi wa EAC jijini Arusha. Mradi huo ya katuni unafadhiliwa na Serikali ya Sweden kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kulia) na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba wakimsikiliza mmoja ya wachora katuni za kuhamasisha uhifadhi wa mazingira muda mfupi baada mkutano wa tano wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Maliasili na Mazingira wa Nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliohitimishwa leo katika ukumbi wa EAC jijini Arusha. Mkutano huo ulilenga kujadili na kusaini makubaliano mbalimbali ya namna bora ya kusimamia sekta hizo katika nchi wanachama. 
 Picha ya pamoja ya baadhi ya wajumbe wa mkutano huo.
(PICHA ZOTE NA HAMZA TEMBA-WMU)

MAELEZO YA MHE. DKT. PHILIP ISDOR MPANGO KWENYE VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MALIPO YA MADAI YA MALIMBIKIZO YA MISHAHARA KWA WATUMISHI WA UMMA

February 09, 2018
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akizungumza na waandishi wa Habari Kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari-Bunge mjini Dodoma (hawapo pichani)  kuhusu hatua ya Serikali ya kuanza kulipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa Umma, kiasi cha shilingi bilioni 43.39 kuanzia Februari 10, 2018. Kushoto ni Kamishna Msaidizi-Bajeti, Bw. Emmanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango (Utawala) Bi. Susan Mkapa (Picha-Wizara ya Fedha na Mipango)
Ndugu Wawakilishi wa vyombo vya habari, nimewaiteni leo hii ili niwape taarifa fupi kuhusu malipo ya madai ya malimbikizo ya mishahara kwa Watumimishi wa umma waliokuwa na madai ili muweze kuufikishia umma wa Watanzania.
Serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (Human Capital Management Information System – HCMIS) kufikia tarehe 01 Julai 2017 ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya shilingi 127,605,128,872.81 kwa watumishi 82,111 Wakiwemo walimu 53,925 waliokuwa wanadai shilingi 53,940,514,677.23  sawa na asilimia 42.27 ya madai yote,   na wasiokuwa walimu 28,186 waliokuwa wanadai jumla ya shilingi 73,664,614,195.58 sawa na asilimia 57.73 ya madai yote. Madai haya yalikuwa ya muda mrefu mengine yakiwa ya kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2017
Madai haya yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishiwa mishahara.

MATOKEO YA UHAKIKI WA MADAI YA SHILINGI BILIONI 127,605,128,872.81 KWA WATUMISHI 82,111
  1. Madai ya watumishi 27,389 kati 82,111 yenye jumla ya shilingi 43,393,976,807.23 ikiwa ni asilimia 34 ya madai yote ya shilingi bilioni 127,605,128,872.81 yaliyohakikiwa yameonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho.

  1. Madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha shilingi bilioni 16.25 kwa walimu 15,919 na shilingi bilioni 27.15 kwa watumishi wasiokuwa walimu  11,470

  1. Madai yote yaliyoonekana kuwa sahihi ya shilingi bilioni 43.39 yatalipwa pamoja na mshahara wa mwezi Februari 2018 kwa mkupuo mmoja. Malipo ya Madai haya ambayo mengine yana zaidi ya miaka kumi majina ya walipwaji wote yatatangazwa kwenye magazeti kuanzia kesho tarehe 10 Februari, 2018.


Kwa matokeo hayo ya uhakiki, mazoezi yaliyofanyika likiwemo  zoezi la kuwaondoa kwenye Mfumo wa malipo ya mshahara (“payroll”) watumishi hewa, vyeti feki na wasio kuwa na sifa na  uhakiki wa madai ya malimbikizo ya mishahara uliofanyika limeweza kuokoa jumla ya shilingi bilioni 84.22 ambazo ni sawa na asilimia 66 ya madai yote ya malimbikizo ya awali ya shilingi bilioni 127.61 yaliyokuwa kwenye mfumo ambazo bila zoezi la uhakiki kufanyika zingelipwa wakati zilikuwa hazistahili kulipwa.
Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kuisababishia Serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili.

Asanteni kwa kunisikiliza

REGROW KICHOCHEO CHA KUFUNGUA UTALII WA KANDA YA KUSINI

February 09, 2018

Na Hamza Temba - Dodoma
..........................................................
Serikali imeanza utekelezaji wa mkakati wa kupanua wigo wa vivutio vya utalii nchini unaohusisha upanuzi wa maeneo ya kijeografia yenye vivutio pamoja na mazao ya utalii ili sekta hiyo ichangie zaidi kwenye pato la taifa na kuondoa umaskini katika jamii.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma.

Alisema kwa upande wa mkakati wa kupanua jeografia ya vivutio vya utalii nchini Serikali itafungua utalii wa ukanda wa kusini kwa kuboresha vivutio na miundombinu ambapo tayari imesaini mkataba wa mkopo nafuu kutoka benki ya dunia wa milioni 150 za kimarekani sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 340 za kitanzania kwa ajili ya mradi wa REGROW ambao utasimamia maliasili na kuendeleza utalii wa ukanda wa kusini.

Alisema kupitia mradi huo jumla ya viwanja vya ndege 15 vitaboreshwa ndani ya Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na uwanja wa ndege wa Nduli uliopo mjini Iringa. Maeneo mengine yatakayoboreshwa katika hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo ni Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na Mikumi.

"Mradi huo utaboresha pia usafiri wa reli kwa kuimarisha kituo cha Matambwe ambacho ni kitovu cha utalii katika Pori la Akiba la Selous",. Alisema Dk. Kigwangalla.

Akizungumzia upanuzi wa mazao ya utalii, alisema sekta hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea zaidi utalii wa wanyamapori huku ukiegemea zaidi katika ukanda wa kaskazini kwa zaidi ya asilimia 90.

Alisema kwa sasa Serikali itapanua wigo wa mazao hayo ya utalii ambapo mwezi Septemba kila mwaka utakuwa mwezi maalum wa maadhimisho ya urithi wa Tanzania (Urithi Festival) kwa ajili kuimarisha utalii wa kiutamaduni na kuhamasisha utalii wa ndani.

Alisema Serikali kupitia Wizara yake itaimarisha pia utalii wa fukwe na utalii wa mikutano.

Awali Dk. Kigwangalla alisema sekta ya Utalii ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa ambapo huchangia asilimia 17.6 ya pato la taifa, asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni na asilimia 12 ya ajira zote nchini.

Alisema pamoja na mafanikio hayo sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi na kuegemea zaidi kwenye vivutio vya ukanda wa kaskazini huku vivutio vya kanda nyingine vikiwa havichangii ipasavyo kwenye pato la taifa.

UMEPANGA KUMFANYIA NINI UMPENDAYE MSIMU HUU WA 'VALENTINE?

February 09, 2018


Na Jumia Food Tanzania


Mbali na mwezi Februari kuwa mfupi, kitu kingine kinachoupa umaarufu mwezi huu ni kujawa na shamrasharma za sikukuu ya wapendanao au ‘Valentine’s Day.’ Sikukuu hii huadhimishwa kila ifikapo Februari 14 ya kila mwaka, ambapo shughuli na matukio mbalimbali ambayo huonyesha ishara ya upendo hutawala.  

Umaarufu wa sikukuu hii umeendelea kushika kasi kote duniani kutokana na uzito wa maana halisi ya neno ‘upendo’ ambalo ndilo hutawala miongoni mwa washerehekeaji.  


Miongoni mwa matukio maarufu yanayofanyika katika kipindi hiki ni pamoja na watu kuwatumia wapendwa wao kadi zenye jumbe za upendo au mapenzi, kutuma zawadi kama vile maua au chokoleti kwa wapenzi wao, pamoja na kuandaa mitoko kwenye sehemu ambazo zimeandaliwa kwa mandhari ya wapendanao. 

Ukiachana na shughuli hizo, Jumia Food wamekuandalia orodha ya mambo ambayo unaweza kuyafanya kwa mpendwa/wapendwa wako katika msimu huu. 


Andika ujumbe mfupi. Unaweza ukaandika ujumbe mfupi wa upendo na kisha ukauweka kwenye mkoba au begi la mpendwa wako ambao ataupata pindi akifika kazini. Hakuna jambo zuri kama kuanza shughuli za asubuhi kama kukutana na ujumbe utakaoufanya moyo wako kujisikia vizuri, kupendwa na kuthaminiwa. 

Tuma kadi, maua au chakula. Ingawa unaweza kuwa sio utamaduni wa watanzania wengi au dhana hii kuonekana kupitwa na wakati, lakini unaweza ukamtumia mpenzi wako kadi nzuri yenye ujumbe wa mapenzi na maua ya kuvutia, au chakula anachokipenda mpaka mahali alipo. 


Mtembelee ofisini mpenzi/mpendwa wako ofisini. Unaweza ukamshangaza mpendwa wako kwa kumtembelea muda wa mchana, ukiwa na chakula anachokipendelea sana.  

Panga mtoko kwa kushtukiza. Ili kunogesha siku hii unaweza ukaamua kwenda kwenye hoteli au mgahawa na kuutumia muda wenu vizuri bila ya kumuambia kabla. Inaweza kuwa baada ya kumaliza shughuli zenu za siku nzima.


Endesha gari mkiwa pamoja. Inawezekana kila mtu hutumia gari lake kwenda na kurudi kazini, lakini unaweza kuitumia siku hii kwa kuamua kumpeleka na kumrudisha. Hii itawapatia fursa ya kutumia muda mwingi mkiwa pamoja.

Mjazie mafuta gari lake. Kama huwa haufanyi hivi mara kwa mara basi kipindi hiki unaweza ukamshangaza mpenzi wako kwa kumjazia mafuta gari lake ‘full tank.’  


Fanya jambo zuri kwa mama yake, baba, kaka au dada. Unaweza kwenda mbali zaidi kwa kuwafanyia matendo ya upendo ndugu na jamaa wa mpenzi wako. Kama vile kujumuika kwa pamoja kwa chakula, kulipa karo ya shule au hata kuwanunulia kitu ambacho wazazi wake wanakipendelea.


Mpikie chakula cha usiku. Ni mara chache wanaume huingia jikoni kuipikia familia au wapenzi wao. Utumie msimu huu kwa kumshangaza mpenzi wako kwa kupika chakula cha jioni ili naye aonje mapishi yako.

Itumie siku hiyo kwa kuzungumza kuhusiana na mipango ya maisha yenu. Inawezakana huwa mnapata muda mchache wa kuzungumza mustakabali wa maisha yenu au hampati kabisa. Itumie siku hiyo kwa kutulia sehemu tulivu pamoja na kujadili au kutafakari kwa pamoja mwenendo wa maisha yenu.


Mfulie nguo zake, kama huwa hufanyi hivyo. Hakuna shughuli ambayo watu wengi hawaipendi (hususani wanaume) kama kufua. Endapo mpenzi wako huwa anakufulia mara zote, basi mshangaze siku hiyo kwa kumfulia nguo zake.


Itenge siku maalum kwa ajili yake, panga kufanya vitu anavyovipendelea. Kuna vitu vingi ambavyo wapenzi huvifanya ambavyo siyo lazima hupendelewa na wote. Unaweza ukaitenga siku hiyo kwa kufanya vitu ambavyo mpenzi wako anavipendelea sana.


Mchumbie. Inawezekana mmekuwa kwenye mahusiano kwa muda mrefu lakini hamkupata fursa ya kufanya jambo hilo kuwa rasmi. Itumie siku hiyo kumchumbia mpenzi wako na kumjulisha kwamba unataka kuishi naye milele.


Mtambulishe mpenzi wako kwa familia, ndugu, jamaa na rafiki zako. Huchukua muda kidogo mpaka wapenzi wakaamua kutambulishana kwa ndugu zao au watu wa karibu. Kama mmetumia muda wa kutosha na mnapendana kwa dhati, itumieni siku hiyo kutambulishana kwa wazazi, ndugu, jamaa na marafiki.

Jumia Food kwa upande wao katika kuutambua umuhimu wa msimu huu wa wapendao, wanaendesha kampeni ambayo inawapatia fursa wateja wao kujishindia mtoko uliogharamiwa kwenye mgahawa wa Thai Kani pamoja na fursa ya kulala usiku mmoja bure kwenye hoteli ya Slipway. Ili kuweza kushinda fursa hiyo wewe pamoja na mpenzi wako, agiza chakula kupitia mtandao wao kwa kutumia nenosiri ‘LOVE.’ Mshindi atatangazwa siku moja kabla ya sikukuu ya wapendao, yaani Februari 13. 

BULYANHULU YAKABIDHI HUNDI YA SHILINGI MILIONI 75,649,524 KWA HALMASHAURI YA NYANG’HWALE

February 09, 2018
Meneja Mkuu wa Migodi wa  Bulyanhulu Benedict Busunzu akikabidhi hundi ya milioni 75,649,524  kwa Mkuu wa wilaya ya   Nyangh’hwale  Hamim Gweyama  kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa halmashauri ya wilaya ya hiyo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2017.


Meneja Mkuu wa Migodi  wa Bulyanhulu Benedict Busunzu akizungumza na madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale  ambapo alisema Acacia itaendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi .

Meneja Mkuu wa Migodi wa Bulyanhulu Benedict Busunzu akifurahia pamoja na wafanyakazi wa Bulyanhulu baada ya kukabidhi hundi kwa halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale.




Na,Joel Maduka ,Nyang'hwale





Kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu Acacia kupitia mgodi  wake  wa Bulyanhulu imekabidhi hundi ya shilingi milioni  75,649,524 kwa halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale Mkoani Geita kwa ajili ya malipo ya ushuru wa huduma kwa kipindi cha Mwezi Julai hadi Disemba mwaka 2017.

Akikabidhi mfano wa hundi hiyo  mbele ya madiwani wa halmashauri hiyo Meneja  wa  Mgodi  huo,  Benedict  Busunzu,  alisema  kawaida  mgodi  huo hutoa  ushuru  kwa  Wilaya  mbili  ya   Msalala  na  Nyangh’hwale  kwa  ajili  ya  miradi  ya  maendeleo.

Aidha  alitaja  moja  ya miradi  mingine  ambayo  mgodi  huo  umesaidia  Wilayani  humo  ni  pamoja  na  mradi  wa  mkubwa  wa  kusambaza   maji kwa  wakazi  150,000 wilayani  humo,   wenye  gharama  ya  Shilingi  Bilioni 4.5  ambao  unatarajiwa  kukamilika  mwishoni  mwa  mwaka  huu.

Aidha kwa upande wake Katibu tawala wa Mkoa wa Geita, Celestine Gesimba amewataka madiwani    na watendaji  wa  halmashauri ya hiyo    kuepuka   kutumia  fedha  zinazotolewa  na wadau  mbali mbali    kwa ajili  ya  miradi ya maendeleo  kwa  kulipana  posho  za  vikao,   badala  yake  zote  zitumike  katika miradi  kwa  manufaa  ya  ustawi  wa wakazi  wa Wilaya  hiyo.

“Ninapenda  kuwaonya  viongozi  na watendaji    ambao mpo hapa Nyangh’wale  kuwa  tusitumie hizi  fedha  kwa  ajili  ya kulipana  posho  za  vikao  badala  yake  zote  zietumike  katika  miradi  ya  maendeleo  kwa  jinsi  mtakavyoainisha,”alisema Gesimba.

  Aidha Mkurugenzi  wa  Wilaya  ya  hiyo,  Carlos  Gwamagobe,  pamoja na kushukuru mgodi  mgodi  huo  kwa kuwapatia  fedha  hizo alisema ushuru wa huduma ambayo walikuwa wakipata hapo awali  umeshuka kwani kwa  kiasi kikubwa kwani walikuwa wakipokea milioni mia nne kwa miezi sita .


“Tuna  imani  kuwa  mgodi  huu ukianza  shughuli  zake  kama  ilivyokuwa  awali   hata  ushuru  wa  huduma  utaongezeka  kwani awali  tulikuwa  tukipatiwa  kiasi  cha  Shilingi  Milioni  225   lakini  tangu  kuibuka  kwa  sakata  la  Makinikia,  ushuru  nao  umepungua  mara  mbili  ya  zile  za  awali,”alisema Gwamagobe.