WANANCHI: MRADI WA LTIP UTAPUNGUZA MIGOGORO YA ARDHI DAR ES SALAAM.

April 25, 2024

 




MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM 


Baadhi ya Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es salaam wameipongeza Serikali kwa utekelezaji wa Mradi waUboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaoendelea nchini chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.


Mradi huo ambao unalenga kuboresha usalama wa milki za ardhi nchini, utatekelezwa katika Halmashauri zaidi ya 60 nchini, na umeelezwa kuwa suluhu ya migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiripotiwa katika mikoa mbalimbali.


Wakizungumza wakati wa kikao cha kamati za urasimishaji Ardhi kilichofanyika eneo la Kipunguni Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam April 24, 2024 wananchi hao wamesema serikali imefanya jambo sahihi kwa wakati muafaka.


Mjumbe wa mtaa wa Kipunguni Bw. John Malima Nunda, amesema mradi huo utazirahisishia serikali za mitaa kazi ya kutambua maeneo na mipaka, pamoja na shughuli zinazotakiwa kufanyika.


Kwa upande wake Bi. Sofia Mwalukuta Mkazi wa Kipunguni, ameeleza kufurahishwa kwake na mradi huo ambao amesema ndio suluhu ya migogoro ya ardhi iliyoendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es salaam. 


"Hii sasa itaenda kutatua matatizo mengi ambayo tulikuwa tunakutana nayo, lakini pia itaondoa ujanja uliokuwa unafanywa na wachache kujimilikisha maeneo au kubadilisha matumizi halisi ya ardhi" amesema Sofia.


Awali akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa Mradi wa LTIP Mijini Bw. Leons Mwenda alisema Serikali itaendelea kushirikiana na kamati za urasimshaji ardhi, kwa ajili ya kuhakilisha kuwa zinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.


"Tupo hapa kuwahakikishia kuwa serikali imedhamiria kuona kwamba maeneo yenu yanakuwa rasmi, hivyo kamati hizi zitakuwa bega kwa bega na Serikali katika kila hatu ili kufanikisha mpango huu wenye maslahi makubwa kwa wananchi na Taifa" alisema Mwena.


Kwa upande wake Mratibu wa Ukwamuaji wa Urasimishaji Mkoa wa Dar es salaam Bw. Paul Mbembela, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kwa kamati na kujitokeza kutoa na kupokea mawazo mbalimbali wakati wote wa mradi.


" Upangaji huu wa maeneo ni shirikishi, jumuishi na wa makubaliano, hivyo wananchi wasisite kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima kwani unawahusu wote" amesisitiza Mbembela.


Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi unatekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ukiwa na lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuzingatia makundi maalumu kama wanawake, walemavu, wafugaji, wakulima, wazee na vijana.

AIRTEL TANZANIA YAINGIA UBIA NA TADB KUENDELEZA SEKTA YA KILIMO

April 25, 2024

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Dinesh Balsingh wakibadilishana mkataba wa kuendeleza sekta ya kilimo na kuwa ya Kidijitali.
Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege na Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Dinesh Balsingh wakisaini Mkataba wa kuendeleza sekta ya kilimo na kuwa ya Kidijitali.

AIRTEL TANZANIA imeingia makubalino na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kusaini makubaliano (MoU) ya miaka mitatu ikiwa na lengo la kuinua na kuleta maendeleo katika sekta ya kilimo kwa njia ya mtandao yaani kidijitali.

Makubaliano ya ushirikiano huu kati ya Airtel Tanzania na TADB yanadhamira ya kufanikisha kupanua ushirikiano wa sekta ya kifedha kwa wadau mbalimbali ndani ya sekta kilimo, wakiwemo wakulima, wajasiriamali wadogo vijijini, hasa wanawake na vijana. Ushirikiano wa Airtel na TADB ni moja kati ya juhudi za Airtel Tanzania kuunga mkono serikali katika kuleta matokeo chanya katika maisha ya Watanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuweka saini makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Dinesh Balsingh, alisema “Airtel kwa kushirikiana na TADB tunadhamira ya dhati ya kusaidia Watanzania kupitia ubunifu katika sekta ya mawasiliano. Hii ni kwakuwa tunaamini wakulima wanastahili kuwa miongoni mwa vikundi vinatakiwa kunufaika na ukuaji wa teknolojia nchini. Hivyo, Ushirikiano wetu na TADB unalenga katika kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kwa kutumia bidhaa mbalimbali za kidijitali ambazo zitaibua masoko mapya kwa wakulima mijini na vijijini. Bidhaa hizo zitawezesha uzalishaji wa wakulima na kuongeza mapato yao”.

Balsingh alieleza kuwa ushirikiano wa Airtel na TADB unaungana moja kwa moja na maono ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ukuaji wa sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. (Chanzo World Economic Forum). " Na hii inaonesha jinsi kilimo kilivyo muhimu katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watu wamejiajiri katika sekta ya Kilimo.".

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege alitoa shukrani zake kwa Airtel Tanzania akisema, ushirikiano wa Airtel na TADB utafungua milango ya fursa katika sekta ya kilimo. Ushirikiano huu utatoa fursa kwa wakulima kujipatia masuluhisho kwenye mahitaji na changamoto wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku.

“Ubia wa Airtel na TADB unalenga kukuza ukuaji sekta ya kilimo. Ushirikiano huu ni mwanzo wa mabadiliko makubwa yatakayowagusa wakulima wote nchini Tanzania,” alisema Bw. Frank Nyabundege – Mkurugenzi Mkuu wa TADB.

Ushirikiano huu wa Airtel na TADB unakwenda sambamba pia na mikakati ya serikali ya kuunga mkono juhudi za wadau wa kilimo kwa kupambaa na changamoto mbalimbali ndani ya sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima kifedha kama ilivyotajwa na Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa mkutano wa wadau wa COP28 uliofanyika Disemba 4, 2023. Alisema, “tunatakiwa kubadilika na kufanya kilimo endelevu kwa kuunga mkono ubunifu mbalimbali unaoendana na hali ya sasa.”

TAKUKURU YAFANIKISHA MAREJESHO YA SH.MILIONI 439.2 KUTOKA KWA WANUFAIKA WA MIKOPO ASILIMIA 10 KATIKA JIJI LA TANGA

April 25, 2024

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga Victor Swella akizungumza na waandshi wa habari ambao hawapo pichani wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 ambapo alisema kwamba moja ya kazi walioifanya ni ufuatiliaji wa ufanisi katika utekelezaji mkakati wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga Victor Swella akizungumza na waandshi wa habari ambao hawapo pichani wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 ambapo alisema kwamba moja ya kazi walioifanya ni ufuatiliaji wa ufanisi katika utekelezaji mkakati wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu.


Na Oscar Assenga,TANGA.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru Mkoani Tanga imefanikisha marejesho ya kiasi cha Sh. Milioni 439,279,300.00 kutoka kwa wanufaika wa mikopo asilimia 10 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga Victor Swella wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwaa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 ambapo alisema kwamba moja ya kazi walioifanya ni ufuatiliaji wa ufanisi katika utekelezaji mkakati wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vijana,wanawake na watu wenye ulemavu.

Alisema kwamba miongoni mwa changamoto waliozozibaini katika ufuatiliaji huo ni kutokuzingatiwa kwa masharti ya urejeshaji mikopo hiyo kwa wakati kutoka kwa wanufaika ambapo kabla ufuatiliaji kufanyika kiasi cha Bilioni 2,152,229,900 zilikuwa hazijarejeshwa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo na muda wa marejesho ulikuwa umeshapita.

Aidha alisema baada ya kulibaini hilo taasisi hiyo iliwakutanisha wadau na kuweka mapendekezo ya kurejesha fedha hizo na hadi kufikia mwezi Februari 2024 Jumla ya Sh.Milioni 439,279,300.00 zilikuwa zimerejeshwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na kufanya fedha ambazo hazijarejeshwa kuwa ni Bilioni 1,712,950,600.00 huku jitihada za ufuatiliaji zinaendelea.

Mkuu huyo wa Takukuru alisema pia katika kipindi hicho walifanikiwa kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 46 yenye thamani ya Bilioni 8,041,998,680.00 katika sekta za kipaumbele kama vile elimu,barabara ,maji na afya.

Alisema katika ufuatiliaji huo walibaini miradi 32 yenye thamani ya Bilioni 4,866,068,966.00 kuwa na mapungufu na ushauri ulitolewa wa kurekebisha mapungufu hayo kupitia vikao na wadau husika pamoja na kuanzisha uchunguzi wa miradi ambayo walibaini uwepo wa tuhuma za vitendo vya rushwa.

“Miongoni mwa miradi tunayoichunguza katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe ni manunuzi ya Sh. Milioni 6,400,000 ya uwekaji milango kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara wenye thamani ya Milioni 245 lakini pia ujenzi wa madarasa mawili ,matundu 18 ya vyoo na mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua wenye thamani ya Milioni 70,000,000 na uchunguzi unaofanyika ni wa ubadhirifu wa Sh.Milioni 30,000,000.00 kwenye ujenzi wa matundu hayo ya vyoo na mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua.

RAIS SAMIA AIPA TANROADS BIL 66 KUANZA UREJESHAJI MIUNDOMBINU YA BARABARA ILIYOHARIBIKA

April 25, 2024

 Na Mathias Canal


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa Bilioni 66 kwa ajili ya kuanza urejeshaji wa miundombinu ya barabara zilizoharibika nchini.

Fedha hizo tayari zimegawanywa kwa mameneja wa TANROADS mikoa yote iliyoathirika kwa ajili ya kufanya kazi kwa haraka usiku na mchana ili kurekebisha kadhia zilizozikumbumba barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Akizungumza Jijini Arusha mara baada ya kukagua Barabara ya Afrika Mashariki (Arusha bypass) iliyoharibiwa na mvua hizo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mha. Mohamed Besta amesema kuwa kutokana na udharula huo tayari Rais Samia ametoa fedha za matengenezo ya miundiombinu hiyo ambazo zimeshapelekwa katika Mikoa yote Nchini.

Mhandisi Besta amesema kuwa tayari kazi inaendelea katika maeneo yote nchini na fedha hizo zinaratibiwa na vitengo maalumu vya dharula vilivyopo TANROADS pamoja na ofisi za mikoa.

Ameongeza kuwa kutokana na tathimini iliyofanyika mpaka sasa zaidi ya Shilingi Bilioni 250 zinahitajika kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya Barabara kuu za Mikoa yote Nchini ambazo zimeharibika vibaya kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini.

Amesema kuwa kuna baadhi ya maeneo kama Kanda ya Ziwa na Nyanda za juu kusini mwa Nchi mvua zimeendelea kunyesha tangu mwezi Oktoba mwaka jana, na sasa unaelekea mwezi wa saba na mvua bado zinaendelea kunyesha.

“Tunamshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani ametupatia shilingi bilioni 66 ambazo tumezisambaza katika Mikoa yote ambapo mameneja wote wa Mikoa wamepewa kutokana na hali ya dharura ya Mkoa husika’’ ameeleza

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha Mhandisi Regnald Massawe amesema Mkoa huo umetengewa kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kazi hizo za dharura na matengenezo ya kurejesha miundombinu hiyo yanaendelea kufanyika kwa kasi.