WACHEZAJI WATATU WA TANZANITE FC MBARONI KWA KOSA LA KUMPIGA REFA

May 21, 2014

Waamuzi na washabiki wakimuamua Refa aliyekua akipokea kipigo toka kwa wachezaji wa Tanzanite Fc

Kipa wa Tanzanite akiwa ameshikwa wakati akitaka kukimbia baada ya kumshushia kipigo Refa

LEO NI KUMBUKUMBU YA MIAKA 18 YA MV BUKOBA

May 21, 2014
Leo imetimia miaka 18 tangu ndugu zetu walipopata ajali na Meli ya MV. Bukoba 21 May 1996, na wengi kupoteza maisha! Ni tukio kubwa lililoua watu wengi nchini na kuacha huzuni kubwa kwa Watanzania.
Comment R.I.P kwao ili waendelee kupumzika kwa amani!
Mei 21,1996 katika ziwa Victoria,Mwanza Tanzania meli ya Mv Bukoba ilipata ajali na zaidi ya watu 800 kupoteza maisha yao.Meli ilizama kilomita 30 kukaribia kutua nanga kwenye bandari ya mwanza ikitokea Bukoba. Meli ikuwa na uwezo wa kubeba idadi ya watu 430. 


Kwenye first and second class orodha ya abiria ilikuwa 443 na kwenye third class hakukuwepo rekodi yoyote .Takribani 1000 walifariki kwenye ajali hiyo.

Afrika ya kusini ilibidi kutoa msaada wa wanamaji wake waje kutusaidia kufanya uzamiaji wa kina kirefu kwani tulikuwa hatuna hivyo vifaa na utalaamu(sijui inagharimu kiasi gani kuvipata vifaa na utalaamu)

Meli ilikuwa na ubovu lakini iliruhusiwa kuendelea na kazi kama kawaida.(nani anajali au kuwajibishwa?)


Vifaa vya uokoaji mfano majaketi(life jacket) n.k na vitu kama hivyo vilikuwepo vya kutosha?( au hakuna uzembe wa viongozi..ni kazi ya Mungu kama walivyozoea kusema)

Hosni Mubarak ahukumiwa miaka mitatu gerezani

May 21, 2014
Mahakama moja nchini Misri imemhukumu aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa mashitaka ya wizi wa fedha za umma pamoja na wanawe wawili wa kiume ambao wameshitakiwa kwa makosa hayo hayo kifungo cha miaka minne gerezani.

Watatu hao pia wametozwa faini ya  pauni milioni 21.1 za Misri na kuagizwa kurejesha pauni nyingine milioni 125 kwenye hazina ya taifa.

Washitakiwa wengine hawakutikana na hatia .Wakati huo huo mahakama nyingine nchini humo imewahukumu vifungo mbali mbali wanachama wa udugu wa kiislamu kwa mashitaka ya kuhusika katika ghasia zilizotokea katika jimbo la Nile Delta mwezi Agosti mwaka jana. 

45 kati yao wamehukumiwa kifungo cha maisha gerezani huku wengine wakipiwa vifungo vya kati ya miaka mitatu na kumi gerezani.
 Polisi walilazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa nje ya mahakama hiyo.
HANDENI NA MAENDELEO YA KILIMO NA UFUGAJI

HANDENI NA MAENDELEO YA KILIMO NA UFUGAJI

May 21, 2014

GU4A0761  
MMoja ya wakulima wa Mahindi Wilaya ya Handeni mkoani Tanga Bw. Adalbertus Bubelwa wa pili kutoka kushoto akimwelezea Mkuu wa wilaya ya handeni Bw. Muhingo Rweyemamu, jinsi alivyoandaa shamba lake. Mkuu huyo wa wilaya alikuwa katika ziara ya kuwatembelea wakulima katika vijiji mbalimbali wilayani humo kuangalia mazao mashambani.
GU4A1133  
Mkuu wa wilaya ya Handeni Bw. Muhingo Rweyemamu, kushoto ambaye ni mwenye shamba akipata maelekezo kutoka kwa Afisa Kilimo wa Wilaya hiyo Bw. Yibarik Chiza, aliyemtembelea Mkuu huyo wa wilaya shambani kwake
Waziri Mukangara aongoza maelfu ya Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Adam Kuambiana

Waziri Mukangara aongoza maelfu ya Watanzania kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Adam Kuambiana

May 21, 2014

APK0a  
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akitoa heshima za mwishomapema jana katika viwanja vya Leaders kwa mwili wa msanii wa Filamu nchini Marehemu Adam Philip Kuambiana aliyefariki ghafla mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
APK0c  
Mjane wa marehemu Adam Kuambiana, Bi. Janeth Rite akiwa katika wakati mgumu kutokana na kushuhudia mwili wa mme wake ukiwa katika jeneza.
APK1 
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Adam Philip Kuambiana wakati wa shughuli za kutoa heshima za mwisho kwa marehemu iliyofanyika leo katika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam, kushoto ni mjane wa marehemu Bi. Janeth Rite.
APK2  
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania Bi. Joyce Fisso akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Bodi ya Filamu kwa familia ya marehemu Adamu PhilipKuambiana aliyekuwa msanii wa Filamu na mkurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza filamu ya APK akiyefariki ghafla siku ya jumamosi kutokana na ugonjwa wa Vidonda vya Tumbo.
MB DOG AIMWAGIA SIFA VIDEO YAKE YA "MBONA UMENUNA"

MB DOG AIMWAGIA SIFA VIDEO YAKE YA "MBONA UMENUNA"

May 21, 2014
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MKALI wa muziki wa kizazi kipya, Mbwana Mohamed Mb Dog, amesifia video ya wimbo wake mpya ya Mbona Umenuna akisema imeandaliwa kwa kiwango cha juu na kudhihirisha ubora wake.
Mb Dog pichani.
Akizungumza leo asubuhi jijini Dar es Salaam, Mb Dog alisema mashabiki wote watakaopata bahati ya kuitazama video hiyo iliyotengenezwa na Abby Kazi, ataamini makali yake.
 
Alisema lengo lake ni kuwapatia mashabiki burudani kamili, hivyo wadau wote wapate muda wa kuitazama video hiyo iliyoachiwa rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita, sambamba na kuingizwa kwenye mitandao ya kijamii, youtube na blogs.
 
“Hii ni safari yangu ya kurudi katika makali yangu ya zamani, hivyo naamini wimbo wangu ulipokewa kwa shangwe na sasa nimeachia video.
“Mashabiki wote naomba waniunge mkono kwa kuiangalia kazi hii na kusubiri mambo mazuri zaidi kutoka kwangu, maana mipango yangu ni kufanya kazi nzuri zaidi ya Bongo Fleva,” alisema.
 
Katika video hiyo, msanii huyo anaonyesha ujuzi wa aina yake wa kuimba, huku mdundo ‘beat’ yake ikipigwa kisasa zaidi kulingana na mabadiliko ya kisanii kwa wakali wengi Tanzania.

MVELLA AJIUNGA SEKRETARIETI YA TFF

May 21, 2014

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA), Eliud Mvella amejiunga na Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Amejiunga na Sekretarieti ya TFF katika Idara ya Sheria na Vyama Wanachama kuanzia leo (Mei 21 mwaka huu) ambapo atashughulikia masuala ya wanachama.

Mvella alijiuzulu rasmi wadhifa wake IRFA jana (Mei 20 mwaka huu). Mwenyekiti wa IRFA, Cyprian Kwihyava amepokea barua ya kujiuzulu huko ambapo ameelezea masikitiko yake kwa uamuzi huo wa Mvella.

Ni imani ya TFF kuwa Mvella atatumia uzoefu wake wa muda mrefu katika uongozi wa mpira wa miguu kuhakikisha TFF inaimarisha uhusiano wake na wanachama wake.

TFF ina wanachama 44 ambao ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

DIT, CBE KUCHEZA FAINALI BEACH SOCCER

May 21, 2014
Fainali ya michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (beach soccer) kati ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) inachezwa Jumapili (Mei 25 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.



Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi iliyopita.



Mgeni rasmi katika fainali hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na itaanza saa 4 kamili asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3 kamili asubuhi.



Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo Kigamboni.



Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.



Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ).



Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.



BONIFACE WAMBURA

OFISA HABARI NA MAWASILIANO

SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)