Wakulima waimwagia sifa Benki ya CRDB mbele ya Rais Samia

August 08, 2023

 

Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo mafupi kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya CRDB, Ndugu Maregesi Shaaban alipotembelea Banda la Benki ya CRDB katika kilele cha maadhimisho ya Nanenane yaliyofanyika kitaifa Jijini Mbeya. Wakishuhudia ni Spika wa Mbunge Mh. Dkt. Tulia Ackson na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Ndungu Fredrick Nshekanabo.
BAADHI ya wakukima mkoani Mbeya wameishukuru Benki ya CRDB mbele ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa imewasaidia kupata mikopo ya fedha na nyenzo ikiwemo trekta aina ya Power Tiller, kuwa vitawasaidia kuinua kilimo na kupata kipato.

Mmoja wa wakulima hao kutoka Wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya Halima Ally, ametoa ushuhuda huo leo mbele ya Rais Dkt. Samia alipotembelea Banda la Benki ya CRDB kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) yaliyofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

"Sisi wakulima wa Mbarali tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kutuwezesha kupata mikopo ya fedha na zana za kufanyia kazi kama ilivyotukopesha Power Tiller. Kwa kupata Power Tiller hii itaniwezesha kuendeleza kilimo changu cha mpunga na mahindi" alisema Ally.
Wakulima zaidi ya 600 kutoka Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wanatarajiwa kukopeshwa na Benki ya CRDB trekta, power tiller, zana za kuvunia, fEdha za mikopo ya kulimia na pembejeo za kilimo ikiwemo mbegu, mbolea na madawa, na mikopo ya Stakabadhi Ghalani.

Rais Dkt. Samia, aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuweza kukopesha wakulima kwa riba ya asilimia tisa, huku akiitaka benki hiyo kuendelea kufuatilia l zana za kilimo wanazowakopeaha wakulima ili ziendelee kufanya kazi, na ikibidi kuwasaidia kutengeneza pindi zinapoharibika, kwani baadhi yao zana hizo zikiharibika, wanazitelekeza.

"Nawapongeza CRDB kwa kuweza kutoa mikopo ya riba ya asilimia tisa. Itawasaidia wakulima kuweza kukopa kwa wingi na kulima kwa tija.

"Na mikopo ya Power Tiller mnayotoa kwa wakulima muweze kuifuatlia na muwasaidie au kuweza kuwasaidiia waweze kutengeneza. Wakati mwingine power tiller linaharibika na kulitelekeza hivyo kushindwa kuleta tija" alisema Rais Dkt. Samia.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki ya CRDB Maregesi Shaaban alisema Benki ya CRDB imeendelea kutoa mikopo inayofikia sh. trilioni 3.9 kwa misimu mitano iliyopita hadi kufikia Julai, 2023, sawa na asilimia 43 ya mikopo yote itolewayo na mabenki kwenye Sekta ya Kilimo na Mifugo hapa nchini.

"Tunatoa mafunzo kwenye vituo atamizi chini ya mpango maalum wa BBT kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Tunaendelea kutoa elimu ya fedha na usimamizi wa miradi kwenye vituo vilivyoko kote nchini. Uwezeshaji vijana na wanawake kwenye kilimo, uvuvi, mifugo, viwanda na biashara Bara na Visiwani.

"Benki ya CRDB kupitia kampuni yetu tanzu ya CRDB Bank Foundation, inawekeza kwa vijana na wanawake ili waweze kutimiza ndoto zao ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo na kuwapatia mitaji kwa ajili ya uanzishaji wa miradi mipya (startup capital). 

Mitaji hii hutolewa kwa vijana na wanawake wenye mawazo bunifu kibiashara, na Benki ya CRDB inatoa mitaji ya awali ikiwa ni mbegu itakayoleta matunda na kuwafungulia kesho yao yenye tija zaidi kiuchumi, chini ya program ya kipekee ijulikanayo kama IMBEJU".alisema Shaaban.

Shaaban alisema Benki ya CRDB imefanikiwa kufufua matumaini ya wana ushirika kwa kuongezea mtaji inayofikia sh. bilioni 10.2, ambapo sh. bilioni 3.2 kwa TACOBA na sh. bilioni 7.0 kwa KCBL. Taasisi hizo zilikuwa zikijiendesha kwa hasara na baada ya kupata mtaji na usimamizi madhubuti kutoka Benki ya CRDB, zimeanza kujiendesha kwa faida kubwa na kutokana na mikakati madhubuti ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia, wanaendelea kutekeleza ndoto nzuri ya kiuchumi ya uanzishwaji wa Benki ya Ushirika ya Taifa. 

Shaaban alisema, Benki ya CRDB ikishirikiana na wauzaji wa vifaa madhubuti vya kilimo (Agricom), imeweza kuwakabidhi baadhi ya wanufaika waliopata mikopo ya kununua Power Tillers kwa ajili ya kilimo cha mpunga mkoani Mbeya.

"Benki ya CRDB itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuendeleza fursa za uwekezaji zilizopo Bara na Visiwani.

Tunawakaribisha wadau wote walipo ndani na nje ya nchi yetu ya Tanzania wafike kwenye matawi yetu yaliyoko kote nchini na kwenye nchi jirani za Burundi na Congo DRC ili tuweze kuwahudumia.

"Tunatoa Shukran za dhati kwa Business Units zote za CRDB na uongozi wa Benki yetu pendwa ya CRDB (kipekee tunatoa Shukran kwa our MD&Group CEO, CCO, COO, CFO, DCA, DCB, DRB, DC, DCA, MD-CRDB BANK FOUNDATION & the entire CRDB MARKETING TEAM) kwa kutuwezesha vilivyo hadi kufikia kilele cha maadhimisho haya ya Maonesho ya Nane Nane kitaifa mkoani Mbeya kwa mafanikio makubwa" alisema Shaaban. 

--

PROF.MKENDA ASISITIZA UWEKEZAJI KATIKA SAYANSI NA TEKNOLOJIA

August 08, 2023

 














Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amekitaka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuwekeza kwenye Sayansi na Teknolojia ili kuchangia katika kuinuia uchumi..


Prof. Mkenda ametoa rai hiyo Agosti 7, 2023 wakati akizungumza na Viongozi  na Wafanyakazi wa Chuo hicho baada ya kutembelea na kujionea Maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na MUST.

 

Prof. Mkenda ameeleza kuwa kazi ya Chuo Kikuu ni kuzalisha na kusambaza maarifa, kusaka uelewa wa mambo kupitia tafiti, hivyo amesisitiza suala la uwekezaji ili kukiwezesha Chuo hicho kujipambanua vema katika dhana ya kufanya tafiti na gunduzi za Sayansi na kufundisha masomo katika maeneo hayo.


"Tunahitaji kuwekeza lakini katika eneo hili sababu  uwezo wetu wa Teknolojia ni duni, nchi yetu na Afrika kwa ujumla zipo nyuma kwenye maeneo ya Sayansi na Teknolojia. Hivyo tunapaswa kuwekeza zaidi ili tuweze kuinua nchi  kuwa na teknolohia na zitakazo chochea uchumi" alisema Prof. Mkenda.


Ameongeza kuwa serikali itaendelea kuwasaidia wataalam na watafiti  wanaozalisha maarifa katika sayansi na teknolojia na kuchapisha matokeo ya tafiti hizo  katika majarida makubwa duniani, ili kuhamasisha na kuleta ushindani katika nyanja hizo muhimu kwa Maendeleo ya kiuchumi.


Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST)  Prof. Aloys Mvuma amesema kwa kutambua azma ya serikali katika kuboresha Elimu ya Amali, Chuo kimeanzisha Mitaala katika Elimu ya Ufundi, na sasa ina mitaala minne, inayotarajia kutoa Walimu mahiri wenye utaalam wa Uhandisi kwa ajili ya  kufundisha Vyuo vya VETA na vile vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs).

 

Aidha ameishukuru serikali na kuipongeza Wizara kupitia Idara ya Sayansi na Teknolojia kwa kuwezesha wabunifu kupata fedha zinazowasaidia kuboresha bunifu zao katika viwango vya juu.


Awali akitoa taarifa kuhusu shughuli mbalimbali za Chuo hicho Prof. Mvuma ameeleza kwamba MUST inajivunia kulea na kuatamia mawazo ya kibunifu yanayovumbuliwa na Wanafunzi, kwani mpaka sasa wanafunzi wanaomaliza hapo wameanzisha kampuni 19 ambazo zimeweza kutoa ajira kwa vijana.


Pia amebainisha kwamba "Moja ya mafanikio makubwa ni Ubunifu na utengenezaji wa mita za maji za kidijitali, zaidi ya mita 38 zimefungwa sehemu mbalimbali kwa majaribio na matokeo yake ni mazuri" alisema Prof. Mvuma.

CRDB yainyamazisha NMB tamasha la Simba Day

August 08, 2023
Wakati maelfu ya Watanzania kutoka kila pembe ya nchi wakiacha shughuli zao na kuelekea Lupaso kushuhudia ‘Wenye Nchi,’ Klabu ya Simba ikiukaribisha msimu mpya kwa tamasha lililofana, kikosi cha timu ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB jana kiling’ara kwenye tamasha la Simba Day baada ya kuwanyamazisha wapinzani wao, Benki ya NMB kwa ushindi wa bao 1-0.
 
Kwenye tamasha hilo ambalo Simba iliendeleza utamaduni wake wa kuujaza uwanja kwa mashabiki wenye ari kubwa ya kuishangilia, walipata burudani murua kutoka kwa maofisa wa benki hizo mbili kubwa zaidi nchini walioziacha suti zao na kutupia bukta na fulana na kukiwasha mbele ya wapenda soka 60,000 walioujaza Uwanja wa Taifa almaarufu kama Uwanja wa Benjamini Mkapa au Lupaso jijini Dar es Salaam. 
Akizungumza baada ya kupata ushindi huo, Kapteni wa Timu ya Benki ya CRDB, Nicodemus Milinga amesema ilikuwa ni lazima washinde kwani walijiandaa vilivyo.
 
“Kujituma na kufuata maelekezo ya kocha. Wote tulikuwa na ari ya juu ya kuipigania brand (nembo) kama vile tunavyotoa huduma bora kwa wateja wetu kila siku, ndani na nje ya nchi,” amesema Milinga.
 
Twaha Beimbaya, kocha aliyejifunzia Uingereza na akaja akachukua kombe la U17 na JKT Tanzania mwaka 2021 halafu akaisaidia Pan Africa isishuke daraja la kwanza mwaka jana anayeinoa timu ya Benki ya CRDB, anasema uzoefu walioupata kwa kushiriki michuano ya Sikukuu ya Mei Mosi walikomenyana na vikosi vigumu vya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,  umewaongezea kujiamini wachezaji wake.
“Tulipotoka huko, niliwaomba wachezaji kuhakikisha wanapata muda wa kufanya mazoezi ndio maana walikuwa vizuri kwenye pambano hili lililoshuhudiwa na mashabiki wengi zaidi nchini,” amesema Beimbaya.
 
Bao hilo pekee katika msimu huu wa 15 wa Simba Day, liliwekwa kimiani na mshambuliaji makini Abdallah Magohe baada ya makosa ya kipa wa Benki ya NMB kuanzisha mpira kimakosa hivyo kuwapa Benki ya CRDB ushindi ulioshangiliwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Abdulmajid Nsekela.
 
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo uliokuwa burudani tamu kwenye tamasha hilo kutokana na soka la kitabuni lililoonyeshwa na timu zote huku washindi wakifunika, kilimalizika bila milango ya timu hizo kufunguliwa.
 
Kocha wa timu ya Benki ya NMB, nyota wa zamani wa Yanga, Mohammed Hussein almaarufu kama Mmachinga alikiri kuzidiwa na wapinzani wao waliotumia nafasi waliyoipata kushinda mchezo huo.

--

WENZA WA VIONGOZI WAZINDUA HUDUMA ZA TAULO ZA KIKE MASHULENI

August 08, 2023

 

Mama Zakhia Bilal akigawa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mtoni wilayani Temeke. (Picha kwa hisani ya Manispaa ya Temeke).

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa akikata utepe kuzindua mradi wa ukarabati wa vyoo vya wasichana na uwekaji wa taulo za kike katika Shule ya Msingi Mtoni wilayani Temeke.
Wenza wa viongozi wakiongozwa na Mama Tunu Pinda (wa kwanza kushoto) na Mama Mary Majaliwa (wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele).
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Mobhare Matinyi, akimshukuru Mama Celina Retala, Afisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha HQ Psds cha taulo za kike kilichopo wilayani Temeke.

 

Na Khadija Kalili

ASASI ya wenza wa Viiongozi nchini iitwayo Ladies of New Millenium, leo Agosti 7, 2023, imezindua mradi wa choo kwa ajili ya kusaidia watoto wa kike ili waweze kujisitiri na kupata huduma zote wanazozihitaji wakiwa kwenye hedhi.

Uzinduzi huo umefanywa na mlezi wa asasi hiyo, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa, umefanyika katika Shule ya Msingi Mtoni, Wilayani Temeke, na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Mobhare Matinyi.

Mheshimiwa Matinyi ametoa shukrani za dhati kwa taasisi hiyo kwa kukikarabati choo cha watoto wa kike na kuwezesha kupata huduma hiyo muhimu.
Mheshimiwa Matinyi amewashukuru pia wadau mbalimbali akiwemo Bi Celina Godfrey Retala, Afisa Mtendaji Mkuu wa HQ Pads kwa kuchangia katoni 100 za taulo za kike kwa ajili ya watoto kujihifadhi wakati wa hedhi.

DC  Matinyi ametoa wito kwa watu na wadau wengine kuunga mkono juhudi hizi ili kumuwezesha mtoto wa kike kupata elimu bora bila usumbufu na kuleta mafanikio hapo baadaye kwa jamii.

 Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, ndugu Victor Kangati, ameipongeza asasi hiyo kwa kuleta mradi huo kwani ni miongoni mwa mbinu kubwa zinazosaidia kupunguza utoro kwa watoto wa kike.

Taasisi hiyo yenye lengo la kuwawezesha vijana na watoto kupitia elimu yenye ufanisi na ujumuishwaji katika ngazi zote za maamuzi, imeendesha hafla hiyo na kuhudhuriwa na wake wa viongozi  akiwemo mlezi wa taasisi, Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa, Mwenyekiti wa taasisi Mama Tunu Pinda na wenza wengine wa viongozi wakiwemo Mama Zakhia Bilal, Mama Asha Bilal, Mama Asina Kawawa na Mama Asha Balozi na Mama Mwantumu Mahiza.

Wadau wa maendeleo Aga Khan Foundation, HQ Pads, na Tosh Cargo .

WASIMAIZI WA UCHAGUZI WATAKIWAKUTEKELEZA MAJUKUMU KWA UFANISI

August 08, 2023

 

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi Mkoani Morogoro leo tarehe 08 Agosti, 2023. Mafunzo hayo ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mabarali na kata sita za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 19 Septemba, 2023. 
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi Mkoani Morogoro leo tarehe 08 Agosti, 2023. Mafunzo hayo ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mabarali na kata sita za Tanzania Bara unaotarajiwa kufanyika tarehe 19 Septemba, 2023. 
Sehemu ya Wasimamizi wa Uchaguzi wakiwa kwenye mafunzo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akizungumza ambapo aliwataka watendaji hao wa uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuwasiliana na Tume wakati wowote wanapopata changamoto ya kiutendaji.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (Rufaa) Mhe. Jacobs Mwambegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi nchini kufanya kazi kwa weledi ili chaguzi ziwe nzuri, zenye ufanisi na amani.

Jaji Mwambegele ameyasema hayo leo tarehe 08 Agosti, 2023 Mkoani Morogoro, wakati akifungua mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya na kata sita za Tanzania Bara.

Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa, hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na hivyo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, amesema Jaji Mwambegele. 

Amewaasa watendaji hao kuwa pamoja na uzoefu ambao baadhi yao wanao katika uendeshaji wa  uchaguzi, wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea.

“Wakati wote wa mchakato wa uchaguzi huu, ni vema mkavishirikisha kwa karibu vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi katika  maeneo yenu kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikishwa kwani jambo hilo litawarahisishia  utekelezaji wa majukumu yenu, Jaji Mwambegele amewaeleza  watendaji hao.

Amewasisitiza juu ya umuhimu wa kuhakikisha kuwa wanayatambua  na kuyajua  vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika jimbo, kata na vituo vya kupigia kura.

Aidha, aliwataka watendaji hao kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema ili kubaini mahitaji maalum ya vituo husika kwa lengo la  kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.

Jaji Mwambegele pia amewakumbusha watendaji hao kuhakikisha siku ya uchaguzi wanaweka utaratibu utakaowezesha kila kituo cha kupigia kura kufunguliwa saa 1:00 asubuhi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima aliwataka watendaji hao wa uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuwasiliana na Tume wakati wowote wanapopata changamoto ya kiutendaji.

Kailima amewaasa watendaji hao kuhakikisha kwamba wanazingatia viapo vyao ikiwa ni pamoja na kutopendelea upande wowote wakati wote wa uchaguzi.

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali na kata sita za Tanzania Bara utafanyika tarehe 19 Septemba, 2023, wagombea watachukua fomu kuanzia tarehe 13 hadi 19 Agosti, 2023, siku ya uteuzi itakuwa tarehe 19 Agosti, 2023 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 20 Agosti, 2023 hadi tarehe 18 Septemba, 2023. 

Kata zitakazofanya uchaguzi mdogo ni; Nala iliyopo Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mkoani Dodoma, Mwaniko iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Old Moshi Magharibi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi na Marangu Kitowo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, Mtyangimbole iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na Mfaranyaki iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma. 

CCM TANGA YATOA MAELEKEZO KWA MKUU WA WILAYA YA KOROGWE MWEGELO

August 08, 2023

 








NA MASHAKA MHANDO, Korogwe 


CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga, kimetoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya Korogwe Jokate Mwegelo kupitia Katibu Tawala wake (DAS) Mwanaid Rajabu, wahakikishe vituo vya afya vya Kerenge na Mnyuzi vinamalizika haraka ili vianze kutoa matibabu kwa wananchi.



Akizungumza katika siku yake ya kwanza katika mwendelezo wa ziara zake kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa ilani ya chama, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajabu Abdallah ambaye alitoa maelekezo hayo baada ya kutofurahishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi hiyo.


Aidha aliiomba Ofisi hiyo ya DC kufuatilia kwa makini taarifa za kibank ili kuweza kujiridhisha na matuminzi ya fedha za miradi hiyo baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Korogwe Vijijini kueleza kwamba kipo kiasi cha fedha kimebaki ingawa mradi huo umesimama kwa sasa.


Rajabu alisema Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo vya afya kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaoteseka kwa kutembea umbali mrefu zaidi ya km 40 kufuata huduma Korogwe Mjini jambo ambalo ni hatari kwa maisha ya wananchi hao.


"Mna DC makini sana katika wilaya hii na naomba nitoe maelekezo yafuatayo, DAS hakikasha unamwambia DC mfuatilie majengo haya na yaishe mapema wananchi wetu wapate huduma, lakini pia fatilieni fedha kama ipo kweli kwenye akaunti" alisema na kuongeza,


"Haiwezekani Rais Dkt Samia Suluhu Hassan atafute fedha kwa kuzunguka huko na huko halafu watu washindwe kuzisimamia, watumishi mliopewa dhamana fanyeni kazi kwa weledi wenu na maelekezo haya tunayoyatoa kama hamtayafanyia kazi mtajua chama hiki ni kikubwa kuliko mtu yeyote yule,".


Alisema kinachofanywa na watendaji na Viongozi Wilayani hapo kwa kutokukamilisha ujenzi wa vituo hivyo ni kumchonganisha Rais, Mbunge na hata Diwani dhidi ya wananchi na kuonekana Serikali haiwajali wananchi wake kumbe Korogwe wameletewa fedha nyingi katika miradi mbalimbali lakini watendaji wanashindwa kuzisimamia.


Alisema vipo vituo vya afya vimejengwa kwa gharama hizo hizo za Shs Mil 400 karibu Mkoa mzima wa Tanga na majengo yote yamejengwa tofauti na Korogwe ambapo wamepokea shs Mil 500 kwa kituo kimoja na havijakamilika hali inayoonekana kuna matuminzi mabaya ya fedha.


Aidha alisema pesa nyingi zimeelekezwa Wilayani Korogwe kwa ajili ya miradi ya vituo vya afya jambo la kusikitisha vituo hivyo havijakamilika na ni dalili za wazi zinazoonyesha Wilaya ya korogwe imeonyesha kiasi gani kuna uzembe wa usimamiaji wa miradi ya maendeleo.


Rajabu aliwataka viongozi waliopewa dhama na Rais wafanye kazi kwa weledi na watambue kufanya hivyo kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa kama sio kumaliza kero za wananchi hasa katika miradi ya kimaendeleo.


Kwa upande wake Mbunge wa Korogwe Vijijini Timotheo Mzava alisema kwanza wanamshukuru Mh, Rais kwa kutoa Bil 1 kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya afya ambapo Kituo cha afya cha Kerenge Shs Mil 500 na kile cha Mnyuzi Shs Mil 500 na kushukuru maelekezo ya Mwenyekiti huyo kwamba yatasaidia wananchi.


Aidha alisema changamoto ya utekekezaji wa miradi hiyo ni ucheleweshwaji na hata majengo yaliyokuwatayari hayakuanza kutumika ingawa uhitaji wa huduma hiyo ni mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.


Alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali ijitoe kwa nguvu zote ili utekelezaji wa vituo hivyo vya afya vikamilike kwa wakati ili kuwaondolea adha wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.


Akitoa taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya Korogwe Halfan Magani alisema miradi hiyo imechelewa kutokana na taratibu za kimanunuzi kupitia mfumo wa force Account kupitia kamati ambazo zipo Kijijini.


Alisema mbali ya changamoto hiyo ya mfumo wa kimanunuzi pia  mkandarasi alishindwa kuendelea na mradi na Halmashauri ipo kwenye mchakato wa kumtafuta mkandarasi mwengine ili aweze kumalia sehemu iliyobaki.

Mwisho