YANGA, SIMBA VIWANJANI VPL J5

October 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi tatu; ambapo Yanga itaikaribisha Rhino Rangers katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Coastal Union inaikaribisha Simba katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.

Tanzania Prisons ambayo imepoteza mechi mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United na Simba inarejea uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha Kagera Sugar.

Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi moja ya kundi A itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam.

SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA

October 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Serengeti Boys) imealikwa kushiriki Olimpiki ya Afrika itakayofanyika Mei mwakani.

Mpira wa miguu ni kati ya michezo 22 itakayoshindaniwa katika mashindano yatakayofanyika Gaborone, Botswana chini ya Kamati za Olimpiki za Afrika (ANOCA).

Kwa mujibu wa Kamati ya Olimpiki ya Tanzania (TOC), Tanzania imepewa nafasi ya kushiriki katika michezo hiyo ya Olimpiki kwa Afrika kutokana na kuwa na programu nzuri za vijana hasa chini ya umri wa miaka 17.

Hiyo itakuwa ni michezo ya Pili ya Afrika kwa Olimpiki ambapo ya Kwanza ilifanyika mwaka 2010 jijini Rabat, Morocco.

KIINGILIO MECHI YA U20 WANAWAKE 1000/-

October 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya wanawake chini ya miaka 20 katika ya Tanzania na Msumbiji itakayochezwa Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa sh. 1,000.

Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 10 kamili jioni, na kiingilio hicho ni kwa ajili ya viti vya rangi ya kijani, bluu na chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh. 5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.

Timu ya Msumbiji inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Oktoba 23 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya LAM. Msumbiji yenye msafara wa watu 25 itafikia kwenye hoteli ya Sapphire

UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA

October 22, 2013
Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower.

Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).

Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti) wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi na Kazimoto Muzo.

RAMBIRAMBI MSIBA WA JIMMY MHANGO

October 22, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka huu).

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi.

Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma, Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa Kocha Mkuu wa Ashanti United.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Maziko yamefanyika leo mchana katika makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina

NASSIB AWAZAWADIA MAREFA SIMBA, YANGA

October 22, 2013
Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi hiyo akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza waamuzi hao kwa kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya mabao 3-3.

“Waamuzi wanapofanya vibaya tunawaadhibu, hivyo wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia. Vilevile kuwapongeza ni kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,” amesema.

Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo hilo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati namba mbili alikuwa Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden Mbaga.

Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na watoka Dar es Salaam ukiondoa Chacha ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.

30 WAITWA ZANZIBAR HERROES

October 22, 2013
Na Masanja Mabula .Zanzibar .
Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar Salim Nassor Bausi ametangaza majina ya wachezaji 30 ambao wataunda timu ya Zanzibar Herroes kitachakashiriki michuano ya challange .

Katika kikosi hicho Majina yaNahodha wa timu hiyo na msaidizi wake  Nadri Haroub Kanavaro na Agrey Morris yakiwa  hayamo huku pia kukiwa na mchezaji mmoja pekee kutoka timu za Pemba zinazoshiriki ligi kuu ya Zanzibar .

Makipa walioitwa kuunda timu hiyo ni Mwadin Ali kutoka Azam ,Abdalla Rashid Ruvu Shooting pamoja na Ali  Suleiman  kutoka timu ya Miembeni .

kwa upande wa walinzi ni Mohammed Azan kutoka Polisi  , Waziri Salum Azam , Shafi Hassan Malindi , Mohammed Faki Zimamoto , Salum Haji Miembeni , Said Yussuf Mtende Rangers , Mohamed Othaman kutoka Jamhuri ya Pemba , Mussa Said Chwaka Stars pamoja na Nassor Massoud Cholo Simba .

Viungo ambao wameitwa na kocha Bausi ni Abduhalim Humud ,Simba ,  Sabri Ali, JKT Oljoro , Adeyoum Saleh , Simba ,Is-haka Othaman JKU , Ali Kani JKT Oljoro , Hamad Mshamata Chuoni , Salum Hamad Miembeni , Awadh Juma , Mtibwa Sugar , na Masoud Ali Mtibwa Sugar .

Washambuliaji ambao wamepewa jukumu la kuhakikisha kwamba n yvu za timu pinzani zinapata hujuma kila wakati ni Seif Abdalla ,Azam Suleiman Kassim Serembe Coastal Union ,Khamis Mcha Azam , Amour Omar Miembeni , na Amir Hamad JKT Oljoro .

Wengine ni Jaku Joma Mafunzo , Faki Nahoda Kimbuga , Hassan Seif  Mtibwa Sugar pamoja na Juma Ali kutoka klabu ya New Geeration .

Kwa mujibu wa kocha bausi ni kwamba timu hiyo itaingia kambini Novemba 15 huku pia akiitaka ZAF kuandaa michezo mingi ya kirafiki kabla ya kuielekea Kenye kwa ajili ya michuano hiyo .