Tamasha la Handeni Kwetu kufanyika Desemba 13 mwaka huu

September 01, 2014
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TAMASHA kubwa la umataduni linalojulikana kama 'Handeni Kwetu' limepangwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu, katika Uwanja wa Azimio, wilayani Handeni, mkoani Tanga.

Katika tamasha hilo linalofanyika kwa mara pili, burudani mbalimbali za ngoma za asili zinatarajiwa kuonekana jukwaani, ambapo pia vikundi kutoka nje ya Handeni, mkoani Tanga navyo vitaalikwa kwa ajili ya kwenda kutoa burudani wilayani humo.

Akizungumza  jijini Dar es Salaam, Mratibu Mkuu wa tamasha hilo, Kambi Mbwana, alisema kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanawekwa ili kuliweka katika kilele cha ubora na kuchangia maendeleo ya sanaa na uchumi kwa ujumla.

Alisema kuwa mwaka jana tamasha hilo lilianza kwa mafanikio makubwa, ambapo wageni mbalimbali walifika wilayani humo, jambo lililochangia pia kuitangaza Handeni na mkoa mzima wa Tanga.

“Mwaka huu tumeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa tamasha letu linaendelea kukua kwa kasi baada ya kuanzishwa kwa mafanikio makubwa mwaka jana.

“Naamini kuwa haya ni matunda ya kushirikiana kwa pamoja na wadau wote, ikiwamo serikali kwa kupitia ofisi zote za wilaya ya Handeni, hivyo watu wajiandae mmbo mazuri na makubwa kutoka kwenye tamasha hili,” alisema Mbwana.

Tamasha la utamaduni la Handeni, linalojulikana kama Handeni Kwetu, ni miongoni mwa matamasha yenye mchango mkubwa, ambapo kwa mwaka jana Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ndio waliokuwa wadhamini wakuu na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kuliweka katika mguso wa aina yake.
RAIS KIKWETE AFUNGUA RASMI NYUMBA ZA MAKAZI ZA MEDELI LEO HII

RAIS KIKWETE AFUNGUA RASMI NYUMBA ZA MAKAZI ZA MEDELI LEO HII

September 01, 2014


1Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitembelea mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma wenye nyumba 150, kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu,  Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi (wa kwanza kushoto) Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Zakhia Meghji na Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye. (Picha zote kwa hisani ya Shirika la Nyumba la Taifa)
2Rais Jakaya Kikwete akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma wengine wanaoshuhudia ni Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC, Nehemia Mchechu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Zakhia Meghji.
3 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitembelea mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma wenye nyumba 150, kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Kyando Mchechu,  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Zakhia Meghji na Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene. Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye.4 Majengo ya Nyumba za Makazi za Medeli Mjini Dodoma kama yanavyoonekana pichani.5 Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Zakhia Meghji  huku Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye na Naibu Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene wakishuhudia  wakati wa ufunguzi rasmi wa mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma. Mradi una jumla ya nyumba 150. (Picha zote kwa hisani ya Shirika la Nyumba la Taifa)6 Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Meneja wa NHC katika Ofisi ya Mkurugenzi Mkuu, Bulla Boma wakati wa ufunguzi rasmi wa mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma.7 Rais Jakaya Kikwete katika picha ya pamoja na Watendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mara baada ya ufunguzi rasmi wa mradi wa nyumba za makazi za Medeli zilizopo Mjini Dodoma.
MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA, MHE. SAMUEL SITTA AWAAHIDI WALEMAVU KUTENDEWA HAKI KATIKA KATIBA MPYA IJAYO

MWENYEKITI WA BUNGE MAALUM LA KATIBA, MHE. SAMUEL SITTA AWAAHIDI WALEMAVU KUTENDEWA HAKI KATIKA KATIBA MPYA IJAYO

September 01, 2014
PIX 1-1
Na Benedict Liwenga, Maelezo-Dodoma.
01/09/2014.
MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta amewahakikishia Watu wenye Ulemavu nchini kuwa wanatendewa haki katika Katiba Mpya itakayopatikana.
Mhe. Sitta ameyasema hayo leo Septemba Mosi, 2014 katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) ambalo lilikuja katika Bunge Maalum kwa lengo la kuwasilisha hoja zenye msisitizo kuhusu haki za watu wenye ulemavu katika mchakato Katiba Mpya.
Mhe. Sitta amesema kuwa kazi wanayoifanya ya kuyapokea makundi mbalimbali Bungeni hapo haina lengo la kuja na hoja mpya na kuziwasilisha katika Bunge hilo, bali ni mawasiliano ya kawaida yanayohusu safari kutoka Rasimu Mpya ya Katiba mpaka kufikia katika Katiba Mpya inayopendekezwa ipatikane.
“Jambo lolote lililoandikwa na binadamu halikosi kasoro, katika Rasimu hii ya Katiba tumegundua inayomapungufu kadha wa kadha, kuna baadhi ya maoni ambayo hayakuzingatiwa ndiyo maana tunayafanyia kazi ili yawemo katika Katiba Mpya itakayopatikana,”.alisema Mhe. Sitta.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Inclusive Development Promoters and Consultants kutoka Dar es Salaam, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo ambaye pia ni mwanachama wa Shirikisho hilo,amesema kuwa Kikosi cha Ushauri kuhusu masuala ya watu wenye Ulemavu kimeweka kipaumbele cha msisitizo wao ambao unajielekeza katika hoja za kuongeza masuala ya mambo ya Muungano ambapo wamependekeza kuwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano kuongezewe suala moja zaidi la Nane kwa mujibu wa Rasimu ya Pili ya Katiba ambalo ni uratibu wa masuala ya haki, usawa na fursa na uwajibikaji kwa watu wenye ulemavu kama jambo la Muungano.
Bw. Rutachwamagyo ameongeza kuwa hoja nyingine ya msisitizo inahusiana na suala la uanzishwaji wa chombo cha uratibu wa haki, usawa wa fursa na uwajibikaji wa haki za watu wenye ulemavu ambayo hii ni kwa mujibu wa Ibara ya 33 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu na Mkataba mwenza wa nyongeza iliyoridhiwa kwa pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amesema kuwa wanataka chombo hiko kijulikane kama Tume ya Kitaifa Juu ya Haki, Usawa wa Fursa na Uwajibikaji kwa Watu wenye Ulemavu.
Aidha, Bw. Rutachwamagyo amegusia pia juu ya hoja nyingine inayohusu suala la Uwakilishi wa watu wenye ulemavu kwenye Bunge la Tanzania, Baraza la Wawakilishi, Mabaraza ya Madiwani utamkwe na Katiba na ukokotolewe kwa misingi ya asilimia badala ya kuweka idadi mahsusi.
“Mathalani, tunapendekeza kifungu 113 kisomeke kuwa asilimia 5% ya Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watakuwa ni watu wenye ulemavu wakiwakilisha kundi hili na watapatikana kwa kuchaguliwa na wahusika wenyewe,” alisema .
Aliongeza kuongeza kwa kuzitaja hoja nyingine ikiwemo suala la matumizi ya lugha sanifu kwa muktadha wa watu wenye ulemavu na amesema kuwa kuna hali ya matumizi ya misamiati na islahi ambazo zinakinzana na dhana za walemavu kimataifa hivyo ni vema kukawa na tafsiri sahihi ya majina kwa watu hao ili kuepuka kukinzana huko, aidha amegusia pia suala la Hifadhi ya jamii huku akifafanua kuwa wadau wenye ulemavu nchini wanadai kuwepo kwa ibara maalum ndani ya Katiba inayoelekeza masharti ya upatikanaji wa hifadhi ya jamii kwa watu wenye Ulemavu ikiwa ni pamoja na kulipwa gharama ama kupewa unafuu ya kupunguza makali ya walemavu kwa mujibu wa ibara ya 28 ya Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu ya 2006.
Akiongea kwa niaba ya watu wenye ulemavu, Mhe. Amon Mpanjo ambaye ni mjumbe wa Bunge hilo amemuomba Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba kuunga mkono sio kupokea maoni mapya, bali kuyaboresha yale yaliyokwisha wasilishwa hapo awali.
“Tukuombe Mwenyekiti ulisisitizie Bunge letu Maalum la Katiba liweze kuzingatia haki za watu wenye Ulemavu ili nao wapate kuwa na maisha bora,” alisema Mpanjo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa SHIVYAWATA, Bi. Amina Mollel amesisitiza juu ya hitaji la wanawake la hamsini kwa hamsini na kati ya hizo, asilimia 5% wawe ni wabunge walemavu na ameitaka Tanzania kuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa nafasi nyingi za uongozi kada mbalimbali kwa walemavu.
“Hii iwe chachu katika kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanapewa nafasi kwa uwezo walionao na sio kubaguliwa,” alisema Amina.
WATANZANIA WASHAURIWA KUWEKEZA KWA KUWAJALI WATOTO

WATANZANIA WASHAURIWA KUWEKEZA KWA KUWAJALI WATOTO

September 01, 2014


Mkuu wa Kitengo cha Usuluishi na Ushauri wa Sheria (katikati) akisisitiza jambo kwa wanahabari alipokuwa akitoa tamko kwa vyombo vya habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Valerie Msoka. Kushoto ni Mwanasheria wa Tamwa, Loyce Gondwe na kulia ni Mwanachama wa TAMWA, Marie Shaba.
Mkuu wa Kitengo cha Usuluishi na Ushauri wa Sheria (katikati) akisisitiza jambo kwa wanahabari alipokuwa akitoa tamko kwa vyombo vya habari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Bi. Valerie Msoka. Kushoto ni Mwanasheria wa Tamwa, Loyce Gondwe na kulia ni Mwanachama wa TAMWA, Marie Shaba.
Mkutano wa waandishi wa habari pamoja na wawakilishi wa TAMWA wakisoma tamko lao juu ya umuhimu wa jamii kuwajali watoto.
Mkutano wa waandishi wa habari pamoja na wawakilishi wa TAMWA wakisoma tamko lao juu ya umuhimu wa jamii kuwajali watoto.
Mwanachama wa TAMWA, Marie Shaba (wa kwanza kulia) akizungumza katika semina kwa baadhi ya wanahabari juu ya uandishi wa habari za kuwatetea watoto.
Mwanachama wa TAMWA, Marie Shaba (wa kwanza kulia) akizungumza katika semina kwa baadhi ya wanahabari juu ya uandishi wa habari za kuwatetea watoto.
CHAMA cha Wanahabari Wanawake nchini Tanzania (TAMWA) kimeitaka Serikali na jamii kwa ujumla kuwekeza katika kumuandaa mtoto kwani licha ya kuwa zawadi kubwa, watoto pia ni tumaini na uhai wa taifa kuendelea. Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Valerie Msoka katika taarifa iliyosomwa kwa wanahabari jijini Dar es Salaam kuhamasisha jamii kwa ujumla kuwajali watoto hasa kwenye mchakato unaoendelea hivi sasa wa uundaji wa Katiba mpya

TUME YA UTUMISHI WA UMMA YAENDELEA KUIMARISHA UZINGATIAJI WA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU ZA MASUALA YA AJIRA

September 01, 2014


Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Neema Tawale akieleza kwa waandishi wa Habari (Hawapo pichani) kuhusu tathmini ya Tume juu ya uzingatiaji wa sheria,kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika utumishi wa uuma, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. John Mbisso.

Kaimu Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma Bw. John Mbisso  akiongea na waandishi wa (Hawapo pichani) kuhusu jitihada wanazozifanya katika kuwaongezea uelewa wadau juu ya haki na wajibu wao katika masuala ya ajira katika utumishi wa umma, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kulia ni Naibu Katibu wa Tume hiyo Bi. Neema Tawale.

Baadhi ya waandishi wa habari waliwasikiliza wawasilishaji toka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
(Picha na Hassan Silayo)
Na Fatma Salum
Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma imeendelea kuimarisha Kiwango cha uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu wa Ofisi ya Rais Tume ya Utumishi wa Umma  Bi Neema Tawale katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Bi Tawale alisema kuwa tathmini kuhusu uzingatiaji wa sheria, kanuni na taratibu za  masuala ya ajira iliyofanywa na Tume hiyo mwaka 2010/2011 katika Wizara, Idara zinazojitegemea, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekretarieti za Mikoa imebainisha kuwa kiwango cha uzingatiaji kimeongezeka hadi kufikia asilimia 64 kwenye vipengele  vya Uajiri, Upimaji wa Utendaji Kazi wa Wazi (OPRAS), Likizo ya Mwaka na Likizo ya Ugonjwa.
Akifafanua zaidi Bi Tawale aliongeza kuwa ukilinganisha na utafiti wa kwanza uliofanyika mwaka 2005/2006 ambapo kiwango kilikuwa ni asilimia 50 ongezeko hilo limetokana na elimu inayotolewa na Tume kwa wadau kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Na.8 ya mwaka 2002 na Marekebisho yake Na.18 ya mwaka 2007.
“Tume ya Utumishi wa Umma inajitahidi kuweka mikakati ili kuhakikisha inakabiliana na changamoto za masuala ya ajira katika kuongeza uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu kwa kuendelea kutoa elimu kupitia miongozo, vipindi kwenye vyombo vya habari na maonyesho mbalimbali ya kitaifa”. Alisema Bi Tawale.
Aidha Bi Tawale alisema kuwa Mwongozo uliotolewa na Tume hiyo kuhusu masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma unawawezesha Waajiri na Mamlaka za Ajira kufuata taratibu wanaposhughulikia masuala ya ajira kwenye mamlaka zao.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za ajira zinatekelezwa ipasavyo Tume huagiza Waajiri au Mamlaka za Ajira kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwaita mbele ya Tume kujieleza ikithibitika wamekiuka sheria au wameshindwa kutekeleza majukumu yao.
Naye Kaimu Katibu Msaidizi wa Tume hiyo Bw. John Mbisso alitoa msisitizo kwa waajiri kushughulikia masuala ya ajira ya watumishi wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuepuka migogoro na kupunguza malalamiko kuhusu masuala ya ajira kwenye utumishi wa umma.