SAGINI ATANGAZA SIKU 14 KUONDOA NAMBA ZA 3D, MADEREVA WA SERIKALI KUKIONA

SAGINI ATANGAZA SIKU 14 KUONDOA NAMBA ZA 3D, MADEREVA WA SERIKALI KUKIONA

March 05, 2024


DAR ES SALAAM - Na Mwandishi Wetu;-

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetangaza siku 14 kwa watumiaji wa Vyombo vya Moto barabarani kuondoa namba za magari zilizoongezwa ukubwa maarufu kama (3D) na Vimulimuli kwa magari yote yasiyoruhusiwa kuwekwa, namba zote zenye vibao vyeusi na zizonatumia namba za chasis, taa zozote na stika ambazo zimeongezwa kwa matakwa ya wamiliki au madereva.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Machi 04, 2024 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Jumanne Sagini (Mb) alisema kuwa namba hizo hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), bali zinatengenezwa kiholela mtaani na herufi hizo kubandikwa juu ya namba halali na kutosomeka katika umbali unaotakiwa ambapo katika viwango vya TBS namba ya chombo cha moto isomeke kwa umbali usiopunga mita 100 ambapo 3D haifiki kiwango hicho.

"Mambo yote yanayohusiana na Usalama Barabarani hufanywa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa mtu mmoja mmoja au binafsi kwa mujibu wa usalama barabarani kuhusu matumizi ya namba yamebainishwa vizuri sana na sheria kwamba Namba zinazowekwa zinatakiwa ziweje? ziwe zimeandikwa na nani? anayetambulika na nani? ziwe na ubora gani? namba hizi zote hazijawekwa kwa bahati mbaya," Alisema Sagini

Mhe. Sagini alisema kuwa, Ving'ora vinatoa ishara fulani ili magari mengine yaweza kupisha na hapa nisisitize kuwa, magari yanayotakiwa kuwekwa Ving'ora yanajulikana kama ya Polisi, Zimamoto ya Wagonjwa na yale yaliyopo katika misafara ya Viongozi kufanya hivyo bila kibali maalum ni ukiukwaji wa sheria.

Aidha, Naibu Waziri Sagini alisema kuwa, zoezi la ubanduaji wa namba zilizoongezwa ukubwa litaendeshwa hata kwenye magari ya Serikali ambapo yakibainika na makosa ya namna hiyo wanaotumia watachukuliwa hatua.

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhani Ng'anzi alisema kuwa, wanapiga marufuku namba zilizoongezeka ukubwa kwa sababu kiusalama Namba za 3D sio salama na namba za magari lazima ziwe 2D kutokana na mifumo na kamera kutotambua 3D.

"Baada ya Tarehe 15 Machi, 2024 tutaendelea kuzibandua na tukiona ile plate namba haisomeki vizuri tutakukamata na hili zoezi mnatakiwa muondoe wenyewe kwa hiyari lasivyo Jeshi la Polisi litakukamata kwa kuvunja sheria hata tukikuta namba haisomeki vizuri yaani imechubuka," Alisema.

Aidha, Kamanda Ng'anzi aliongezea kuwa, Operesheni itajumuisha na Taa/Sport light kinyume na taratibu za mtengenezaji au kibali kutoka kwa Mkaguzi wa magari na uwekaji wa stika za rangi mbalimbali kwenye taa kubwa mbele na nyuma ya gari, ambazo zinabadilisha mwanga wa taa halisi mfano stika nyeusi, blue nyekundu na tinted.
     

CHUO CHA CATC CHAENDESHA MAFUNZO YA USALAMA WA USAFIRI WA ANGA KWA TANAPA HIFADHI YA TAIFA MIKUMI

March 05, 2024

 

Chuo cha Usafiri wa Anga nchini (CATC) kinaendesha mafunzo ya Usalama wa Usafiri wa anga kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) yakilenga kutambua na kudhibiti vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza katika viwanja vya ndege vinavyoendeshwa na shirika hilo.

Akieleza juu ya mafunzo hayo ya siku 5 kuanzia Machi 04, 2024 -Machi 08, 2024 yanayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro , Mkufunzi Mkuu wa CATC Thamarat Abeid alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu inayohusiana na usalama katika viwanja vya ndege kwa kutumia sheria, kanuni na taratibu za Shirika la Usafiri wa Anga duniani - ( ICAO), pamoja na kanuni na taratibu ambazo zimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili wataalam wafanye kazi kwa ufasaha na kuleta tija kwa taifa na dunia kwa ujumla.

Aidha, mkufunzi huyo aliongeza kuwa mafunzo haya yanahusisha vihatarishi mbalimbali vilivyopo katika viwanja vya ndege, utoaji wa taarifa ambazo ni muhimu sana ili wamiliki wa ndege na marubani wapate wigo mpana wa uelewa hata kama itatokea changamoto ijadiliwe kwa pamoja na kupata mwafaka wa pamoja kati ya wamiliki wa viwanja, marubani, wamiliki wa ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa TANAPA Fredrick I. Malisa akimwakilisha kamanda wa Kanda ya Mashariki, amewashukuru wakufunzi wa mafunzo hayo na kuwadokeza kuwa usafiri wa anga kwa upande wa TANAPA ni nguzo muhimu sana katika mnyororo wa kukuza utalii nchini.

Na kuongeza kuwa kwa kutambua umuhimu huo katika kipindi cha takribani miaka minne Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 130 katika maboresho ya viwanja vya ndege vinavyoendeshwa na TANAPA pamoja na manunuzi ya mitambo na vifaa vya ujenzi ili kuendana na kasi ya utalii na usalama wa watalii na hatimaye kuweza kufikia malengo ya kitaifa ya idadi ya watalii Milioni tano na Mapato Shilingi Bilioni sita ifikapo mwaka 2025/2026.

Aidha, Kamishna msaidizi wa uhifadhi Fredrick I. Malisa alisema, TANAPA inatambua umuhimu wa kazi za usalama wa viwanja vya ndege kufanyika kwa ufanisi, hivyo ni lazima watumishi wanaofanya kazi hizo kujengewa uwezo, na ndio msingi wa mafunzo hayo ya kibobezi yanayotolewa na wakufunzi wa CATC .

Hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo ilihudhuriwa pia na Afisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia viwanja vya ndege TANAPA, Christine Bgoya pamoja na mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kamishna msaidizi wa uhifadhi Augustine Masesa

Mafunzo hayo kwa TANAPA yamehusisha maafisa na Askari kutoka Idara ya Miundombinu na wengine ambao wanahusika moja kwa moja na masuala haya ya utekelezaji wa kanuni za usalama wa viwanja vyetu vya ndege kutoka hifadhi 11 na TANAPA makao makuu.