MAKONDA AWATUMIA SALAMU WATUMISHI WAZEMBE TANGA

January 20, 2024

 








Na Oscar Assenga, TANGA

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Paul Makonda amewatumia salamu watumishi wa Serikali wazembe mkoani Tanga wasiowajibika kwamba hawatakubali kuwavumilia kwa sababu wao ndio wamekuwa chanzo cha kumchonganisha Rais na wananchi wake.

Alitoa kauli hiyo wakati alipozungumza na wananchi kwenye mkutano wa Hadhara kwenye viwanja vya Lamore Jijini Tanga mara akitokea wilayani Pangani akiwa kwenye ziara yake ya kichama mkoani hapa.

Alisema kwamba chama hicho hakiwezi kukubali kuwafumbia macho watumishi ambao wamekuwa wakishindwa kuwajibika huku wananchi wakiendelea kuteseka wakati wanapokwenda kupata huduma katika maeneo yao.

Makonda alisema moja kati ya maelekezo kumi aliopewa na Rais Samia baada ya kupendekezwa na hatimae kuteuliwa ni kuwa sauti ya wananchi wa hali ya chini na wasio na pesa vyeo wala elimu .

Alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kimaendeleo na wajibu wa chama ni kuhoji miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na iendane na thamani ya fedha zilizotengwa.

"Nina maelekezo kumi toka kwa Rais Samia,moja ni kuhakikisha je miradi inajengwa kwa wakati?kazi yangu na wenzangu kushughulika na wanaofanya ubadhilifu wa fedha hizo"Alisema Makonda.

Aidha alisema katika ziara yake ya siku mbili lengo la kukiimarisha chama kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu wa 2024 na uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais 2025 ili kukidhi matakwa ya katiba ya Chama hicho ya kushinda chaguzi zote,kuunda dola na kuunda Serikali.

Alisema mbali na hilo pia katika ziara hiyo ameitumia kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia majawabu yalikosekana kwa muda mrefu ambapo alitoa maelekezo mbalimbali kwa watumishi wa umma katika idara zilizolalamikiwa namna ya kumaliza kero za wananchi hao.

Makonda amekuwa na utaratibu wa kuwasimamisha watumishi wa Serikali toka idara zote mbele ya Mikutano yake ya hadhara moja wajibu maswali ya wananchi lakini pia wananchi wajionea wenyewe wanao wasababishia waichukie Serikali yao kwa kushindwa kuwahudumia.

Awali akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutoa fedha nyingi mkoani Tanga kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rajabu alitumia fursa hiyo kumuomba Makonda miradi yote inayotekelezwa mkoani humo iwanufaishe wazawa ili kuondoa malalamiko ya wananchi kutokupata hizo za ajira na kushindwa kunufaika na miradi hiyo inayotekelezwa katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Waziri Kindamba akizungumza wakati akitoa salamu za mkoa alisema mkoa uko salama na Serikali ina mahusiano mazuri na Chama na Wazee jambo ambalo limeufanya Mkoa huu kiendelea kuwa shwari na kutokuwa na matukio ya Uvunjifu wa amani.

WANANCHI FUATILIENI TARATIBU NA MAELEKEZO YA SERIKALI KUKABILIANA NA MADHARA YATOKANAYO NA MVUA-DKT. YONAZI

January 20, 2024

 

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi akizungumza na waandishi wa Habari amabao hawapo katika picha, katika eneo maarufu kwa jina  la Daraja la Masai, lililopo katika barabara ya uhuru Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza mara baada ya kumaliza ziara yake ya kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea.
Aliyesimama Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Baladya Eliakama, akizungumza kuhusiana na madhara ya mvua zinaoendelea kunyesha katika mkoa wa Mwanza kabla ya kuanza kwa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na Mvua hizo.
Kati picha (katikati) Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge n Uratibu Dkt. Jim Yonazi na wataalam kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mwanza, TARURA, TANROADS na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wakiwa katika ziara ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Mvua zinazoendela kunyesha, Mkoani Mwanza
Wataalam kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu wakiwa katika kikao kabla kuanza kwa ziara ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge n Uratibu Dkt. Jim Yonazi ya kutembelea baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na Mvua zinazoendela kunyesha mkoani Mwanza.
Katika ni sehemu ya kingo za miundombinu ya Daraja unapopita mto Nyamilongo Wilayani Nyamagana lilivyoharibiwa na mvua zinazoendela kunyesha Mkoani Mwanza.


 NA. MWANDISHI WETU – MWANZA


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amewataka wananchi kuzingatia na kufuata taratibu zinazotolewa na Serikali ili kuweza kukabiliana na madhara yatokananyo na mvua hasa za El nino kuweza kuokoa maisha na mali zao.

Ameyasema hayo Januari 20, 2024, Jijini Mwanza alipokuwa katika ziara ya kukagua hali ya Mafuriko katika Jiji la Mwanza ambapo mvua la El nino zinazoendelea zimeleta athari mbalimbali na kuharibu miundombinu pamoja na mali za watu.

Dkt. Yonazi amesema ni muhimu sana wananchi kuwa wazalendo na kufuata maelekezo ya serikali kwa sababu suala zima la uokoaji ni gharama.

“Suala hili ni gharama kwa Serikali lakini pia inaweza kugharimu maisha hivyo ni muhimu sana pale ambapo tumeelekezwa na Serikali kufuata taratibu tuweze kufuata taratibu.” Alisisitiza.

Katibu Mkuu Dkt. Yonazi amebainisha kuwa kwa wananchi ambao wameelekezwa kuhama katika maeneo hatarishi waweze kuhama ili waweze kulinda maisha yao, mali zao na maisha ya jamii kwa ujumla na ametoa wito kwa wananchi kote nchini kufuata taratibu, miongozo na maelekezo halali ya Serikali na ndiyo namna ya kujilinda dhidi ya mafuriko na majanga.

Amewataka pia wananchi kushiriki katika miradi mikubwa akitolea mfano mradi wa ujenzi wa kingo za mto Nyamilongo unaopita katika wilaya ya Nyamagana ili maji yake yasiende katika makazi ya watu na kuharibu mali nyingine na kufahamu kwamba ushiriki wao utaleta faida katika maana ya kutunza mali zao, mali za asili na kuhakikisha kwamba maisha yanaendelea vizuri.

Katika hatua nyingine,Dkt. Yonazi amewaasa watumishi wa umma kufuata utaratibu hasa katika kusimamia suala zima la ujenzi holela, kwani unapofanyika ujenzi holela ni rahisi sana kupata madhara.

“Ili kuweza kuwa na makazi bora kwa wananchi wetu ni vizuri kuhakikisha maisha hayahatarishwi na mafuriko na hata yanapotokea mafuriko inakuwa rahisi kuokoa.” Amesema Dkt. Yonazi

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amesema, mvua hizi za El nino kwa baadhi ya maeneo katika mkoa wa Mwanza zimeleta uharibifu wa baadhi ya miundombinu kama vile madaraja na Barabara.

Aidha amepongeza Wakala wa Barabara  vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Mwanza kwa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba miundombinu hiyo inarejea katika hali yake ya kawaida.

Sambamba na hilo aliongelea suala la mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mkoani humo, ambapo alisema ulianzia katika Wilaya ya Magu na kufika katika wilaya ya Ilemela na Nyamagana ambapo Serikali ya mkoa kwa kiasi kikubwa imechukua  hatua, tahadhari pamoja na Kudhibiti.