IGP MANGU APANGUA KIKOSI CHAKE, ABADILI MAKAMANDA
MKUU
wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest
Mangu ameanza kufanya mabadiliko ya baadhi ya makamanda wa mikoa, wakuu
wa upelelezi wa mikoa, wakuu wa usalama barabarani wa mikoa pamoja na
watendaji wengine wa vikosi na vitengo mbalimbali ndani ya Jeshi hilo.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi,
Advera Senso-SSP; miongoni mwa makamanda wa mikoa waliofanyiwa
mabadiliko ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Mkoa wa Ruvuma Kamishna
msaidizi mwandamizi (SACP) Deusdedit Nsimeki anayekwenda kuwa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Manyara, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara
Kamishna msaidizi (ACP) Akili Mpwapwa sasa anakuwa Kamanda wa Polisi
Ruvuma.
Taarifa hiyo imeeleza aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Lindi, Kamishna
Msaidizi (ACP) Renatha Mzinga anakuwa Kamanda wa Mkoa wa Lindi,
aliyekuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi (ACP) Suzan
Kaganda amehamishwa kuwa Kamanda Mkoa wa Tabora huku aliyekuwa Kamanda
wa Polisi Tabora (ACP), Peter Ouma amehamishiwa Polisi Makao Makuu.