MVUA ZA EL NINO NI SABABU YA ONGEZEKO LA MAMBA KASAHUNGA NA MAYOLO : DC BUNDA

MVUA ZA EL NINO NI SABABU YA ONGEZEKO LA MAMBA KASAHUNGA NA MAYOLO : DC BUNDA

January 18, 2024


Na. Beatus Maganja

Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Anney amesema mvua za El Nino zimekuwa sababu kubwa ya ongezeko la wanyamapori aina ya mamba ambao wamekuwa wakitoka maeneo yao ya asili na kwenda maeneo ya wananchi na kuleta madhara kwa maisha na mali zao katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo Wilayani Bunda.

Dkt. Vicent ameyasema hayo leo Januari 18, 2024 katika ziara ya Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, Mabula Misungwi Nyanda iliyofanyika wilayani humo kwa lengo la kuwatembelea waathirika wa mamba na kutoa pole.

“Na mwaka huu, Kamishna hali hii imeongezeka sana baada ya kuwepo kwa mvua ya El Nino ambayo imesababisha mamba kutoka katika maeneo yao ya asili kwenda kusogea kwenye maeneo ya wananchi” amesema.



Akifafanua zaidi suala hilo, Dkt. Vicent amesema mamba wamekuwa wakisafirishwa na mikondo ya maji ya mito kuelekea ziwani jambo ambalo limesababisha wanyamapori hao kuonekana kwa wingi katika kingo za Ziwa Victoria nyakati za jioni na alfajiri na hivyo kusababisha madhara kwa baadhi ya wananchi wanaokwenda kuchota maji au kuoga kando ya Ziwa hilo.

Hata hivyo pamoja na changamoto hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amepongeza jitihada za dhati zinazofanywa na timu ya Maafisa na Askari wa TAWA Kanda ya Ziwa akithibitisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana katika harakati za kuwadhibiti mamba hao na kutoa rai waongeze kasi ya kutoa elimu ya kujikinga na kuwadhibiti wanyamapori hao kwa wananchi wa maeneo yenye changamoto hiyo.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda amesema kutokana na kuongezeka kwa vilio vya wananchi vinavyotokana na matukio ya mamba katika vijiji vya Kasahunga na Mayolo Wilayani humo, imemlazimu kufanya ziara mahsusi katika vijiji hivyo ili kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kuwatembelea na kuwapa pole familia za ndugu walioathiriwa na wanyamapori hao na kufikisha salamu za rambirambi kutoka Serikalini.

Kamishna Mabula amesema Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii inayoongozwa na Waziri Angellah Kairuki wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya changamoto ya mamba inayowakabili wananchi hao na kuahidi kuongeza ulinzi kwakuwa kipaumbele cha kwanza kwa Serikali ni uhai wa wananchi wake na siyo wanyamapori.

Kwa minajiri hiyo, Kamishna Mabula ametoa maelekezo kwa Maafisa na Askari wa TAWA kwa kushirikiana na wananchi kuwasaka mamba wote walioleta madhara kwa wananchi au wenye viashiria vya kuhatarisha maisha ya binadamu katika maeneo hayo na kuwaua kwa mujibu wa Sheria.

Pia amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuchukua tahadhari wanapofanya kazi zao pembezoni mwa Ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kuweka makazi yao umbali wa Mita 60 kutoka ziwani.

Naye Diwani wa Kata ya Kasahunga Mhe.Fortunatus Maiga ameipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi wa Kata hizo na hivyo ameiomba kujenga miundombinu ya maji katika Kata yake ili kuokoa maisha ya wananchi wanaokwenda kuchota maji ziwani pamoja na kuwavuna mamba hao ambao wanahatarisha maisha ya binadamu.

SERIKALI KUPITIA BOHARI YA DAWA YAANZA USAMBAZAJI VIFAA TIBA MAJIMBONI VYENYE THAMANI ZAIDI YA BILIONI 14.7/=

January 18, 2024

 BOHARI ya Dawa (MSD) imeanza usambazaji majimboni vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 14.7 kwa ajili ya hospitali, vituo vya afya na zahanati lengo ni kupunguza vifo vya mama na mtoto.


Meneja wa MSD, Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ,Morogoro na Visiwani Zanzibar, Betia Kaema alisema hayo wakati wa makabidhiano wa vifaa hivyo na mkuu wa mkoa wa Morogoro , Adam Malima kwa ajili ya majimbo 11 ya mkoa huo.

Kaema alisema , mkoa wa Morogoro umepatiwa vifaa aina tisa vyenye thamani ya sh milioni 759 na kuanza kusambazwa katika majimbo yote 11 na kila jimbo litapokea vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 69.

“ Kama tunavyofahamu Serikali yetu inayoongozwa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan , imenunua vifaa kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto vyenye thamani ya sah bilioni 14.7 na vifaa hivyo vilizinduliwa na Waziri wetu wa Afya kwa ajili ya majimbo ya Tanzania nzima” alisema Kaema.

Kaema alivitaja vifaa vilivyokabidhiwa kwa kila jimbo la mkoa huo na idadi yake kwenye mabano ni Drip stand (330), vitanda vya kawaida vya wagonjwa (330), vitanda vya kujifungulia mama wanajawazito (220) na seti (220) za kujifungulia mama wajawazito.

Alitaja vingine ni shuka (1,320), magodoro (330), Examination table (220), meza ndogo za wagonjwa kuwekea vifaa vyao pale wanapokuwa wamelazwa (165) na Bed side Locker (330).

Kaema alisema hizo zote ni juhudi za serikali katika kuondoa kabisa ama kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua .

“ Kwa sasa serikali imetoa kipaumbele kuimarisha na kuwezesha hospitali zote mikoani ambazo zimeanishwa katika majimbo mbalimbali kuwa na vifaa hivi ili kuweza kuondokana kabisa na vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua” alisema Kaema .

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima ,alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombonu ya sekta ya afya na kwa sasa imejielekeza katika uboreshaji wa viwango vya utoaji wa huduma za afya nchini.

“ Malengo yetu sisi mkoa baada ya kupokea kwa vifaa tiba hivi ni kwenda kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na hili tumekuwa tukilihimiza nyakati zote “ Malima .

Mkuu wa mkoa huyo alisema licha ya kupokea vifaa tiba hivyo, mkakati wa mkoa ni kuendelea kutoa elimu kuhusiana na kujikunga na magonjwa mbalimbali na namna ya utumiaji wa vifaa hivyo kwa wagonjwa.

Hivi karibuni Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu alizindua usambazaji wa vifaa vya kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 14.9 ambavyo vitasambazwa katika majimbo 214 na halmashauri nchi nzima.

Ummy alisema usambazaji wa vifaa vya hivyo umelenga kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto na kuimarisha uzazi salama nchini.



















KATIBU NENELWA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MTENDAJI WA HESLB JIJINI DODOMA

January 18, 2024

 


Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru, alipomtembelea leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.
Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akikabidhiwa machapisho na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru, alipomtembelea leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.
Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akisoma machapisho aliyokabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru (kulia), alipomtembelea leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.
Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru akitoa maelezo kuhusu machapisho alipomtembelea leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.

Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru, alipomtembelea leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.

Katibu wa Bunge, Ndg. Nenelwa Mwihambi, akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Ndg. Abdul-Razaq Badru baada ya mazungumzo yaliyofanyika leo tarehe 18 Januari, 2024 ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma

(PICHA NA OFISI YA BUNGE)

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI MKUTANO WA UTAWALA BORA USWISI

January 18, 2024


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika kudhibiti rushwa unahitajika uongozi imara pamoja na kuishirikisha jamii na wadau kuanzia ngazi ya watoto shuleni.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akishiriki mjadala wa ngazi ya juu uliyohusu masuala ya Utawala Bora na kukabiliana na Rushwa uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi.

Amesema rushwa imekua changamoto kubwa inayoleta madhara zikiwemo rushwa za ndani ya mataifa na zile za kimataifa.

Akitoa uzoefu wa Tanzania katika kupambana na rushwa, Makamu wa Rais amesema serikali imeweza kuendelea kufanikiwa kupunguza kiwango cha rushwa kwa kuimarisha taasisi za utawala kama vile ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa kuhakikisha anawezeshwa kwa rasilimali fedha na rasilimaji watu, vifaa na uwezo wa kutumia teknolojia ili aweze kufutilia matumizi ya serikali.

Pia Makamu wa Rais amesema serikali imeendelea kuimarisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuwepo kwa mfumo wa uangalizi kutoka Bunge la Tanzania kupitia kamati za bunge kama vile Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambazo hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali.

Makamu wa Rais amesema kwa kuzingatia serikali hufanya manunuzi kwa asilimia kubwa, hivyo imeimarisha Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma ili kudhibiti rushwa katika michakato ya manunuzi.

Pia amesema nchini Tanzania wadau mbalimbali na watu binafsi hufanya ufuatiliaji wa matumizi ya serikali na mwenendo wa rushwa kwa kutumia taasisi binafsi.

Halikadhalika amesema ripoti mbalimbali kutoka kwa mashirika binafsi husaidia katika kutambua mwenendo wa vitendo vya rushwa na hivyo kuweka mikakati ya kukabiliana navyo.

Makamu wa Rais amesema kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia pamoja na uwazi katika michakato mbalimbali ya uwekezaji hususani katika sekta ya madini kumesaidia katika kupunguza vitendo vya rushwa.

Makamu wa Rais yupo nchini Uswisi ambapo anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati wa mjadala wa ngazi ya juu uliyohusu masuala ya Utawala Bora na kukabiliana na Rushwa uliyofanyika katika Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini Uswisi. Tarehe 18 Januari 2024.

TANZANIA YAHUDHURIA MKUTANO KIMATAIFA KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA ANGA

January 18, 2024

 


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (MB), akifuatilia mkutano wa kimataifa wa mawaziri wa Usafiri wa Anga huko Hyderabad, India.

 Mkutano huo unajadili fursa na changamoto za sekta hiyo. Waziri Mbarawa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga la Tanzania, Bw. Hamza Johari

TEF YAWAFARIJI WAATHIRIKA WA MAFURIKO KILOSA

January 18, 2024

 


 Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) leo limekabidhi msaada wa kiutu kwa waathirika wa mafuriko wilayani Kilosa mkoani Morogoro yaliyotokea hivi karibuni.

Msaada huo wa vyakula na nguo za watoto na wakubwa umewasilishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa hilo, Jane Mihanji, kwa niaba ya Mwenyekiti wake, Deodatus Balile, kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka.

Akikabidhi msaada huo, Mihanji amesema umetokana na kuguswa kwao na janga hilo lililoleta athari kubwa kwa wakazi wa Kilosa.

Amesema mbali na wao kufanya kazi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii, kiubinadamu wameguswa na majanga ya asili yaliyowakuta Watanzania wenzao, hivyo waliamua kuchangishana na kuwasilisha msaada huo kunakohusika.

Shaka, akipokea msaada huo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, ameishukuru TEF kwa kujitoa kwao.

Shaka ameomba ushirikiano kati ya TEF na Serikali udumishwe, huku akiwahakikishia wahariri hao kuwa msaada huo utafika kwa walengwa kama ilivyokusudiwa.

Shaka amesema jamii wilayani Kilosa inatoa shukrani za dhati kwa wadau waliowafariji waathirika kwani kutoa ni moyo, si utajiri.

TEF iliwakilishwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu, Anita Mendoza; Mjumbe Kamati ya Utendaji Jane Mihanji na Mjumbe Rashid Mtagaluka.

KUNDI KUBWA LA WANANCHI 515 LAHAMA NGORONGORO KWENDA MSOMERA

January 18, 2024

 


Na Mwandishi wetu, Karatu Arusha.
KUNDI lenye kaya 72 wananchi 515 na mifugo 2,206 limeagwa leo tarehe 18/01/2024 baada ya kujiandikisha na kuamua kuhama kwa hiyari kutoka katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera handeni Mkoani Tanga.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, meneja wa mradi wa kuhamisha wananchi waishio ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Fedes Mdala ameeleza kuwa baada ya kundi hili kuhama leo inafikisha jumla ya kaya 749 zenye watu 4,337 na mifugo 19,915 ambayo tayari zimehama ndani ya hifadhi kwenda maeneo yaliyopangwa na serikali pamoja na maeneo mengine ambayo wananchi wamechagua.

Kamishna wa Uhifadhi NCAA Richard Kiiza ameeleza kuwa kundi la awamu hii ndio kubwa zaidi kuondoka tangu kuanza utekelezaji wa zoezi hili na kuongeza kuwa kadri ujenzi wa Nyumba za makazi unavyoendelea Kijiji cha Msomera, kitwai na Saunyi idadi ya wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari imeendelea kuongezeka ambapo hadi sasa zaidi ya kaya 1,070 zimeshajiandikisha kuhama na zoezi la uhamasishaji na uelimishaji linaendelea.

Kamishna Kiiza ameongeza kuwa zoezi la ujenzi wa Nyumba 5,000 katika Kijiji cha Msomera, Saunyi na Kitwai linaendeela chini ya SUMA JKT na tayari zaidi ya nyumba 360 zimeshakamilika na nyumba zingine zaidi ya 2,000 na nyumba nyingine ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Kiiza amewahimiza wananchi walioagwa leo kuendelea kuwa mabalozi wa kuwahimiza wananchi waliobaki kujiandikisha kuhama kwa hiari ili wanufaike na Maisha bora yaliyoandaliwa na Serikali nje ya Hifadhi.

Akiwaaga wananchi hao Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Kanali Wilson Sakulo ameeleza kuwa wananchi wanaohama kwa hiyari wanapewa stahiki zao zote za msingi ikiwepo nyumba yenye hati kwenye eneo la ukubwa wa ekari 2.5, shamba la kulima la ekari tano, huduma za maji, shule, afya, barabara, mabwawa, majosho, minada, umeme na huduma za mawasiliano na kupata uhuru wa kufanya shughuli za kilimo na kuishi Maisha huru tofauti na hifadhini.

Kanali Sakulo ameelekeza uongozi wa NCAA kuendelea kutoa elimu, uhamasishaji na uandikishaji kwa wananchi walio tayari kuhama kwa hiari na kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyejiandikisha kuhama anahamishwa kwa wakati, kupata stahiki zake zote na kuhakikisha wananchi wanaohama hawarudi tena maeneo ambayo wameshahama kwa kuwa Serikali yetu imeshawajengea mazingira wezeshi yenye huduma zote muhimu za kijamii.

Mmoja ya wananchi aliyehama Petro Tengesi amemshukuru Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwa wananchi wa Ngorongoro na kuendelea kuwajengea mazingira bora nje ya hifadhi ikiwemo ulipwaji wa stahiki zao za kuhama, kusafirishiwa mizigo yao pamoja naa kuboreshewa huduma za kijamii nje ya hifadhi.

NDAKI MPYA YA CHUO KIKUU MZUMBE KUJENGWA TANGA

January 18, 2024




 Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi, "Higher Education for Economic Transformation - HEET Project," Januari 8, 2024 kimekabidhi eneo la ujenzi wa Ndaki ya Tanga kwa Mshauri mwelekezi kwa Kampuni ya Mekon Arch. Consult Limited ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza usanifu wa miundombinu. 

 Hafla hiyo imefanyika katika Wilaya ya Mkinga, Kata ya Gombero, kijiji cha Pangarawe Mkoani Tanga na kushuhudiwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanali Maulid Surumbu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba.

 Awali akizungumza na wananchi wa Kitongoji hicho cha Pangarawe Kanali Surumbu amesema ni wazi kuwa ongezeko la miundombinu ya vyuo vikuu ni kukuza sekta ya elimu na kusaidia maendeleo katika nyanja ya Sayansi na Teknolojia. 

Amesema ni muda muafaka kwa wananchi wa Tanga hususan wakazi wa Wilaya ya Mkinga kuchangamkia fursa zitakazotoka na utekelezaji wa mradi huo. 

 “Licha ya kwamba lengo la msingi ni kutoa elimu, ujenzi huu utatoa ajira na fursa za kimaendeleo. Hivyo sisi wakazi wa Wilaya ya Mkinga ni vema tukachangamkia fursa hiyo na kuwa walinzi wa mradi huu”. Amesisitiza Kanali Surumbu. 

 Naye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amesema miundombinu itakayojengwa katika eneo hilo ni pamoja na Jengo la Taaluma, Hosteli mbili, Bwalo la Chakula, Jengo la Zahanati, mfumo wa majitaka, na tenki la maji lenye ujazo wa lita laki nne.

 “Katika mradi huu mkubwa Serikali imetenga kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 21 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu katika Chuo Kikuu Mzumbe. Kati ya fedha hizi kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 7 zitatumika kwenye ujenzi wa miundombinu ya Kampasi ya Tanga.” Amesema Prof. William Mwegoha 

 Amesema mradi utakapokamilika Chuo Kikuu Mzumbe kitaanzisha program mbalimbali za Sayansi na Sayansi Tumizi kama vile Uhandisi, Teknolojia na TEHAMA, usimamizi wa mifumo na katika hatua za awali program nyingi zaidi zitazidi kuongezwa kadiri ya mahitaji. 

 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Eliza Mwakasangula amefafanua hatua za maendeleo ya mradi tangu ulivyoanza na kuelezea malengo yake na kuishukuru jamii ya Pangarawe kwa uongozi imara na ushirikiano na moyo wa kujitolea wakati wote wa utekelezaji wa mradi.

 “Tunajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizi za kuleta mageuzi katika elimu na tunaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha mafanikio ya mradi huu kwa maendeleo ya elimu nchini Tanzania” Amesisitiza Prof. Mwakasangula. 

 Kwa upande wake Mhe. Danstan Kitandula Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mkinga amesema atahakikisha miundombinu wezeshi ikiwa ni pamoja na Barabara, Umeme na Maji vinafika katika eneo la Mradi ili shughuli zikamilike kwa wakati. 

 Nae Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Mekon Arch. Consult Limited amewahakikishia wana Mkinga, kukamilika kwa michoro ya eneo hilo ndani ya miezi mitatu hadi minne. 

 “Niwahakikishie baada ya miezi mitatu hadi minne Mkandarasi atakuwa amewasili eneo husika na kuanza ujenzi utaanza. 

Badala ya kuwa ndoto kwenye vitabu, sasa ni halisia, wanamkinga mtafaidi, majengo yatakayokidhi viwango vya ubora” Amesisitiza Dkt. Moses Mkonyi Mshauri Elekezi - Mekon Arch. Consult Limited.

SERIKALI- WAWEKEZAJI RUKSA MSOMERA

January 18, 2024

 Na John Mapepele 


Serikali imesema  wawekezaji wa ndani na nje wanaruhusiwa kuwekeza katika eneo la Msomera ili kuleta maendeleo na  kusaidia kuboresha maisha ya wananchi walioamua kwa hiari kuhamia  eneo hili.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi ametoa kauli hiyo leo Januari 17, 2024 Kijijini Msomera kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari zaidi ya 60 waliokuwa kwenye ziara maalum ya siku nne  kwenye Hifadhi ya Ngorongoro na Msomera kushuhudia zoezi  linalofanywa na Serikali la kuwahamisha wananchi kwa hiari kupisha uhifadhi na kuwaboreshea maisha yao.

Waandishi wamepomgeza jitihada zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan za kuwaboreshea wananchi maisha.

Matinyi amewahakikishia wawekezaji kuwa wanaruhisiwa  kuwekeza  kama ambavyo wanafanya katika maeneo mengine kwa kuzingatia sheria za nchi huku pia akiwataka  wananchi kuchangamkia fursa  hizo baada ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali za kukamilisha huduma za kijamii na miundombinu yote muhimu.

Amesema sasa tayari ujenzi wa  nyumba 1000 upo katika hatua mbalimbali kwenye eneo la Msomera na kwamba huduma  za ujenzi wa shule za msingi na sekindari, zahanati,  eneo la mnada, mabwawa ya kunyweshea mifugo, majosho barabara na umeme unafanyika kwa kasi kubwa.


Amesisitiza kwamba malengo makubwa ya zoezi hili ni kuboresha maisha ya wananchi waliokuwa wakiishi Ngorongoro kwa dhiki na kuboresha uhifadhi wa Ngorongoro kwa faida ya  vizazi vya sasa  na baadaye.

Wakati huo huo amesema tayari kaya 72 zenye jumla ya watu 500 waliojiandikisha kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro kuja Msomera wanatarajiwa kuagwa kesho katika ofisi za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na  viongozi mbalimbali wa Serikali.

Katika ziara hiyo waandishi wa Habari iliyoratibiwa na Wizara ya Maliasili kupitia  Ngorongoro kwa kushirikiana na  Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali waandishi walipata fursa ya kutembelelea  eneo la makazi ya watu  Ngorongoro Kisha Msomera.



RC Sendiga asisitiza ukamilishwaji ujenzi wa shule ya Wasichana

January 18, 2024

 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendinga ameagiza ukamilishwa wa haraka shule ya wasichana mkoani humo inayojengwa katika Kijiji cha Kiongozi Halmashauri ya Mji wa Babati na huku akisisitiza kuongezwa kwa idadi ya mafundi ujenzi ili kuongeza kasi ya ujenzi.

Maagizo hayo yametolewa na Mhe. Sendinga Jan 17, 2024 mara baada ya kufanya ziara kwenye mradi huo wenye thamani ya shilingi Bil. 3 ili kujionea mwenendo wa ujenzi na ukamilishwaji wa shule hiyo itakayochukua wanafunzi wasichana wa kuanzia kidato cha Kwanza hadi cha Sita kutoka Mkoani Manyara na Mikoa Mingine.
Mhe. Sendiga ameiagiza Ofisi ya Divisheni ya Elimu ya Sekondari katika Halmashauri ya Mji Babati kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa kufuatilia na kukamilisha usajili wa shule mapema pale mradi unapokaribia kukamilika.
Aidha, Mhe. Queen Sendiga ametoa pongezi kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati  Mhe. Lazaeo Twange pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mji kwa utekelezaji vizuri wa maelekezo yake na kuridhishwa na kasi ya ujenzi ilivyo sasa.