WAZIRI KIJAJI AHIMIZA WATENDAJI KUFANYA KAZI KWA BIDII

WAZIRI KIJAJI AHIMIZA WATENDAJI KUFANYA KAZI KWA BIDII

July 06, 2024

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kupokewa katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam leo tarehe 06 Julai, 2024.

…..

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amehimiza watendaji wa Ofisi hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa katika hifadhi endelevu ya mazingira.

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais ni pana na inagusa moja kwa moja maisha ya kila siku ya wananchi hivyo wanahitaji kuelimishwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa mazingira.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo wakati akizungumza na viongozi wa Ofisi ya Makamu wa Rais mara baada ya kupokewa katika Ofisi ndogo jijini Dar es Salaam leo tarehe 06 Julai, 2024.

Ametolea mfano wa biashara ya kaboni ni baadhi ya masuala ambayo ni mapya katika jamii hivyo, ni vyema wananchi wakapata uelewa ili kuhusu fursa zinazopatikana katika ili wananchi washiriki kwa kupanda miti ambayo mwisho wa siku pamoja na kusaidia katika hifadhi ya mazingira lakini pia huingiza fedha.

“Katibu Mkuu na timu yako naomba niwahakikishie ushirikiano na ntakuwa mwanafunzi kwenu nikiendelea kujifunza ili kazi iwe rahisi na nawashukuru kwa kunipoka tangu kule Zanzibar hadi hapa (Dar es Salaam), tuchape kazi,” amesisitiza Dkt. Kijaji.

Mhe. Dkt. Kijaji amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua katika nafasi hiyo na kumuahidi kuchapa kazi na kuahidi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema lipo jukumu la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kufikia maono ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara katika nishati safi na kushirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wengi wanaachana matumizi ya kuni na mkaa ili kuokoa misitu.

Halikadhalika, amesema anafarijika kufanya kazi katika Ofisi hiyo chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ambapo amemtaja kama mlezi na mchapakazi.

Dkt. Kijaji amewapongeza watendaji kwa kuandaa Mpango kazi wa Utendaji wa Utekelezaji wa Shughuli za Ofisi ya Makamu wa Rais (2024-2025) ambao utawezesha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi na hasa kumsaidia Mhe. Makamu wa Rais katika majukumu yake kazi ya kumsaidia Mhe. Rais.

Amemshukuru Mhe. Dkt. Selemani Jafo ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na kuahidi kuendeleza pale alipoishia ili kuyafikia matamanio ya wananchi katika hifadhi ya mazingira.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amempongeza Waziri Dkt. Kijaji na kumuahidia yeye na timu yake kumpa ushirikiano katika majukumu yake.

Kikao hicho cha mapokezi Waziri Dkt. Kijaji kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bi. Christina Mndeme, Naibu Mkuu (Muungano) Bw. Abdallah Hassan Mitawi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Profesa Eliakimu Zahabu.

Mhe. Dkt. Kijaji aliteuliwa hivi karibuni kushika wadhifa huo na kuapishwa katika Ikulu ndogo ya Tunguu, Zanzibar tarehe 05 Julai, 2024

UDSM YABUNI MFUMO JOTO WA KUHIFADHI VYAKULA NA KUKUZIA KUKU BROILA

July 06, 2024

 NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV


CHUO Kikuu Cha Dar Es Salaam, Ndaki ya TEHAMA wamebuni mfumo joto unaojiendesha kwa kujiongeza na kujipunguza joto kulingana na uhitaji wa wakati husika kwenye uhifadhi vyakula pamoja na kufuga kuku wa kisasa (broila).

Akizungumza leo Julai 5,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa Sabasaba Jijini Dar es salaam Mhandisi wa Maabara, Ndaki ya Tehama Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Adriano Kamoye amesema kuku wa kisasa (broila) katika ukuaji wake wanahitaji joto kulingana na ukuaji wake.

"Katika ukuaji wa kuku wa kisasa, joto ni kitu cha muhimu sana, wafugaji wengi hutumia taa pamoja na mkaa, njia ambayo si salama katka ukuaji wa kuku hao, ndo maana tukaamua kuja na mfumo huu wa kisasa ambao ni bora na ni salama kwenye ufugaji" amesema

Aidha amesema kuwa Mfumo huo pia unaweza kutumika katika kuhifadhi mazao wakati wa usafirishaji na utunzaji kwa lengo la kuhifadhi ubora wa matunda au mbogamboga.

"Mbogamboga zinahitaji unyevunyevu wa kiasi fulani ili kuhifadhi ubora wake kwa muda mrefu, kwahiyo unyevunyevu ukiwa mkubwa au mdogo unaweza poteza ubora wake, kwahiyo mfumo huu unaweza kutuma katika mazingira hayo kutunza ubora wa matunda au mbogamboga"amesema.




JAJI MKUU AITAKA BRELA KUUNGANISHA KANZIDATA YAKE YA USAJILI WA MAKAMPUNI NA MAHAKAMA

JAJI MKUU AITAKA BRELA KUUNGANISHA KANZIDATA YAKE YA USAJILI WA MAKAMPUNI NA MAHAKAMA

July 06, 2024

 


John Bukuku
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameitaka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuiwezesha Mahakama nchini kuunganishwa kwenye Kanzidata ya Wakala ili kuweza kuhakiki taarifa za kampuni kwa uharaka pindi inapokuwa inashughulikia mashauri yahusuyo kampuni hizo

Rai hiyo ameitoa leo tarehe 5 Juni, 2024 alipotembelea banda la BRELA lilipo ndani ya jengo la Wizara ya Viwanda na Biashara katika maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Ibrahim Juma amesema kuwa uunganishwaji katika kanzi data itaiwezesha Mahakama kujua uhai wa kampuni na endapo imehuisha taaifa zake kwa Msajili hii itasaidia kuamua kuendelea na kesi au kusitisha endapo kampuni haijahuisha taarifa zake kwa Msajili

Aidha, Jaji Mkuu ameipongeza BRELA kwa kazi kubwa inayofanya katika kuboresha utoaji wa huduma zake kwa njia ya mtandao

BRELA inashiriki katika kutoa huduma za papo kwa hapo kwenye maonesho ya 48 ya kimataifa ya biashara ya Dar es Salaam ndani ya banda la Wizara ya Viwanda na Biashara na banda karibu na Wizara ya Fedha na Mipango

KAMISAA MAKINDA AWATAKA WANANCHI KUTUMIA TAKWIMU SAHIHI KWA MAENDELEO

July 06, 2024

 Na. Peter Haule, WF, Dar es Salaam


Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, ametoa rai kwa wananchi kuanzia ngazi ya chini kutumia takwimu sahihi zilizopatikana kutokana na Sensa iliyofanyika katika shughuli mbalimbali za Maendeleo.

Mhe. Makinda ametoa rai hiyo alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza matumizi ya Takwimu sahihi kwa maendeleo.

Amesema Takwimu zilizotokana na sensa zina kila kitu hivyo ni vyema zikatumika kikamilifu katika mipango ya maendeleo lakini pia kutumiwa na watafiti wakiwemo wa vyuo mbalimbali katika kupata majibu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Amewataka wananchi kutembelea Banda la Wizara ya Fedha ili kupata elimu ya zianda kuhusu Sensa na takwimu kwa kuwa sasa Ofisi ya Takwimu inafanyakazi ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matokeo ya Sensa iliyofanyika.
Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akohojiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja (kushoto) katika kipindi maalumu cha Sabasaba cha Hazina TV baada ya kutembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere, Temeke, jijini Dar es Salaam.

Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akiagana na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, baada ya mahojiano ya kipindi maalumu cha Sabasaba cha Hazina TV baada ya kutembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam, ambapo alisisitiza matumizi ya takwimu sahihi.

Afisa Habari Mwandamizi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Ramadhani Kissimba, akimuongoza Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam, ambapo amesisitiza matumizi ya Takwimu sahihi kwa maendeleo.

Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akizungumza na vyombo vya Habari kuhusu umuhimu wa sensa iliyofanyika ambayo inasaidia katika kupanga mipango ya maendeleo, alipotembelea Banda la Wizara hiyo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.

Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akisaini kitabu cha wageni alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam, katikati ni Afisa Habari Mwandamizi kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Ramadhani Kissimba na kushoto ni Mwandishi Mwendesha Ofisi wa Kitengo hicho, Bi. Masia Msuya.

Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akipewa maelezo ya Mfumo wa Kielektroniki wa Malipo ya Serikali (GePG) na Afisa Usimamizi wa Mifumo ya Fedha kutoka Idara ya Usimamizi wa Mifumo ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Emmanuel Maendaenda, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.


Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akipewa maelezo ya elimu ya fedha kwa wananchi hususani vijijini na Maafisa waandamizi kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.

Kamisaa wa Sensa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Anne Semamba Makinda, akipewa maelezo kuhusu usimamizi wa madeni kutoka kwa Mchumi Mwandamizi, Idara ya Usimamizi wa Madeni Wizara ya Fedha, Bw. Sepo Seni, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), jijini Dar es Salaam.

 

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)


RAIS SAMIA,NYUSI WALIPOTEMBELEA BANDA LA VODACOM MAONESHO YA SABA SABA JIJINI DARA

July 06, 2024

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia S. Hassan, na mgeni wake, Mhe. Filipe J. Nyusi, Rais wa Msumbiji (wa pili kutoka kushoto), wakimsikiliza Philip Besiimire, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, wakati marais hao walipotembelea banda la kampuni hiyo. 

Pichani, Bw. Besiimire anaelezea shughuli za kampuni hiyo mnamo Julai 4, 2024, wakati wa uzinduzi rasmi wa maonesho ya 48 ya Sabasaba ambapo Vodacom pia iliibuka mshindi wa jumla huku mheshimiwa January Makamba (katikati), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akitazama.







MWANASHERIA MKUU APONGEZA USIMAMIZI WA SHERIA YA USALAMA NA AFYA KAZINI

July 06, 2024

 


Na Mwandishi Wetu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, ameupongeza Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini.

Ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la OSHA katika maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Saba Saba) yanayoendelea katika Viwanjwa vya Saba Saba vilivyopo Barabara ya Kilwa, Temeke Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Feleshi alipokelewa na mwenyeji wake, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, ambaye alimweleza jinsi Taasisi hiyo yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa inavyotekeleza majukumu yake ya msingi.

“Ili kutimiza wajibu wetu wa kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, tunaanza kwa kutambua maeneo ya kazi kwa kuyasajili na kisha kuweka utaratibu mzuri wa wataalam wetu kufika katika maeneo husika kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa mifumo ya usalama na afya na kushauri maboresho yanayohitajika,” ameeleza Mtendaji Mkuu.

Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA, ameeleza kuhusu mkakati unaotumika na OSHA kuyafikia maeneo yote ya kazi nchini ambapo amesema mifumo ya TEHAMA ndio nyenzo inayotumika kuyafikia maeneo ya kazi mengi kiurahisi.

“Tunatumia mfumo wetu wa kieletroniki wa usimamizi wa taarifa za maeneo ya kazi (Workplace Information Management System-WIMS) ambao unatuwezesha kuwasiliana na wadau wetu kwa njia rahisi na haraka ambapo kupitia mfumo huo wadau wetu wanaweza kupata huduma zetu mbali mbali ikiwemo kusajili sehemu za kazi wakiwa mahali popote, kuwasilisha taarifa za ajali, kujisajili kupata mafunzo na kuwasilisha taarifa za ajali zinazotokea mahali pa kazi,” amefafanua Bi. Mwenda.

Akimweleza Mwanasheria Mkuu changamoto ambazo Taasisi ya OSHA inakabiliana nazo, Bi. Mwenda amesema changamoto kubwa ni uelewa mdogo wa masuala ya usalama na afya miongoni mwa wananchi pamoja na kasi kubwa ya ukuaji wa teknolojia ya uzalishaji katika maeneo ya kazi ambayo huzalisha vihatarishi vipya kila mara.

Hata hivyo, Bi. Mwenda ambaye ndiye Mkaguzi Mkuu wa maeneo ya kazi nchini amesema Taasisi yake inazichukulia changamoto tajwa kuwa fursa kwa kuongeza program za kuelimisha umma pamoja na kuwekeza katika kuongeza utaalam wa wakaguzi wake ambao wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara ndani na nje ya nchi ili kuendana na teknolojia mpya.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye dhamana ya kulinda nguvukazi ya Taifa dhidi ya ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi mbali mbali katika sehemu za kazi kupitia kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake.

TBS KANDA YA MASHARIKI YATEKETEZA TANI 4.5 ZA BIDHAA HAFIFU

July 06, 2024

 


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), Kanda ya Mashariki limeteketeza bidhaa hafifu tani 4.5 zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 90 mara baada ya kufanya ukaguzi na kufanikiwa kukamata bidhaa hizo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo ambalo limefanyika leo Julai 5,2024 Pugu Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Kanda ya Mashariki, Francis Mapunda amesema kuwa walifanya oparesheni ya Ukaguzi Kanda ya Mashariki na kubaini kuwepo udanganyifu kwa baadhi ya wafanyabiashara kuuza bidhaa zilizo chini ya kiwango.

Amesema kuwa bidhaa hizo wamezikamata katika Mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro na Pwani ambapo bidhaa hizo zilikuwa hazijasajiliwa, zilizoisha muda wa matumizi pamoja na bidhaa zisizosalama kwa walaji.

Aidha amewaonya wafanyabiashara wanaouza bidhaa zilizoisha muda wake ambapo amesema wanapaswa kuwa na utamaduni wa kukagua bidhaa zao na kama zimeisha muda wake ni vyema wakaziondoa mara moja ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.

Pamoja na hayo amewaasa wananchi kuwa makini na ununuaji wa bidhaa sokoni ikiwemo chakula kuangalia tarehe ya za kutengenezwa na tarehe za kuisha muda wake lakini vilevile na kuangalia kwenye mitandao ya kijamii bidhaa ambazo zimepigwa marufuku kwamba si salama kwa matumizi ya binadamu.