RAIS DKT. MAGUFULI AWAAPISHA WAKUU WA WATATU WA MIKOA NA KUZUNGUMZA NA WAKUU WAPYA WA WILAYA IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

June 29, 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Juni, 2016 amewaapisha wakuu wa Mikoa watatu aliowateua Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Wakuu wa Mikoa walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es salaam ni Dkt. Binilith Satano Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Charles Ogesa Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara na Bi. Zainab Rajab Telack ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Mikoa imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya wateule ambao waliteuliwa na Rais Magufuli Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Aidha, miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika wilaya tatu ambapo ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Rais Magufuli pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato ya serikali na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma, kuhakikisha wananchi wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji mali.

"Katika kazi hizi wapo watakaowakejeli, katika kazi hizi wapo watakaowadhihaki, nyinyi kavumilieni na mmuweke Mungu mbele na mkawaweke watanzania mbele, mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyokuwa amewaongoza.

"Nataka kuwahakikishia tunawaunga mkono kwa nguvu zote, mkafanye kazi bila uwoga wowote, katembeeni kifua mbele, kwa sababu tumewaamini wala msiwe na wasiwasi, ukifanya kitu kizuri kwa dhamira yako iliyo njema kitazaa matunda mazuri, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa" Amesema Rais Magufuli

Katika hafla hiyo, wakuu wa mikoa walioapishwa na wakuu wa wilaya wateule wamekula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates ambapo Rais Magufuli amemuhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa serikali ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Afya, Uongozi na Kilimo.

Kwa upande wake Bi. Melinda Gate amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania na ameahidi kuwa taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
29 Juni, 2016 .

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Charles Mlingwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mara Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Zainab Telack kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Binilith Satano Mahenge kuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wakuu wa mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya wateule mara baada ya kumaliza kuwaapisha wakuu wa mikoa ya Shinyanga, Mara na Ruvuma Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha na IKULU
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Mhe George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe wakiwa na sehemu ya Wakuu wapya wa Wilaya waliofika Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 29, 2016 kula kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa Mikoa katika vituo vyao vya kazi
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Mhe George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe wakiwa na sehemu ya Wakuu wapya wa Wilaya waliofika Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 29, 2016 kula kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa Mikoa katika vituo vyao vya kazi
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Mhe George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe wakiwa na sehemu ya Wakuu wapya wa Wilaya waliofika Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 29, 2016 kula kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa Mikoa katika vituo vyao vya kazi
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI, Mhe George Simbachawene, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora Mhe. Angela Kairuki na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhandisi Mussa Iyombe wakiwa na sehemu ya Wakuu wapya wa Wilaya waliofika Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 29, 2016 kula kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa Mikoa katika vituo vyao vya kazi
Kamishna wa maadili ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania Jaji Mstaafu Salome Kaganda akitoa somo kwa wakuu wa wilaya wapya waliofika Ikulu jijini Dar es salaam leo Juni 29, 2016 kula kiapo cha maadili ya viongozi kabla ya kwenda kuapishwa na wakuu wa Mikoa katika vituo vyao vya kazi.
DKT. NDUGULILE ATAKA MABUNGE KUSHIRIKISHWA KWENYE MPANGO WA “AFYA MOJA” (ONE HEALTH)

DKT. NDUGULILE ATAKA MABUNGE KUSHIRIKISHWA KWENYE MPANGO WA “AFYA MOJA” (ONE HEALTH)

June 29, 2016
Mbunge wa Jimbo la Kigamboni (CCM) Dkt Faustine Ndugulile(Mb) ameyataka Mataifa kushirikisha Mabunge katika kufanikisha mpango wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security Agenda).

Akizungumza kwenye mkutano wa masuala ya Usalama wa Afya ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanyika Jijini Bali, Indonesia,, Dkt Ndugulile alisema, “Mabunge yanaweza kutoa mchango mkubwa sana kwenye utekelezaji wa Mpango wa Usalama wa Afya Duniani kwa kusimamia Serikali na kuhakikisha hatua zote muhimu zinatekelezwa; kutunga Sheria zitakazosimamia utekelezaji wa mpango huu pamoja na kuhakikisha mpango huu unapata fedha za kutosha kutoka kwenye Bajeti ya Serikali”.

Dkt Ndugulile alisema kuwa muingiliano wa shughuli za kilimo, mifugo na shughuli nyingine za kibinadamu zimesababisha baadhi ya magonjwa ya wanyama kuleta athari kwa binadamu na pia usugu wa madawa ya aina ya antibiotiki. Hivyo, kuna haja ya wadau wa sekta hizi kuwa na ushirikiano wa karibu chini ya mpango wa “Afya Moja” (One Health). 
Mbunge wa Jimbo la Kigamboni (CCM) Dkt Faustine Ndugulile (Mb) (kulia), akizungumza kwenye mkutano wa masuala ya Usalama wa Afya ulioandaliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kufanyika Jijini Bali, Indonesia.
Alisema kuwaIli mpango wa “Afya Moja” ufanikiwe in lazima maboresho yafanyike kwenye uratibu wa sekta mbalimbali ndani ya nchi na pia kuandaa mpango wa pamoja wa udhibiti na kushughulikia majanga.

Dkt Ndugulile aliyasema hayo kwenye mkutano wa Mpango wa Usalama wa Afya Duniani unaofanyika mjini Bali, Indonesia. Mkutano huu ulioanza tarehe 27 Juni unatarajia kuisha tarehe 30 Juni.
Dkt Ndugulile mbali ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Mabunge Duniani (Inter Parliamentary Union) kuhusiana na masuala ya UKIMWI, Afya ya Wanawake, Vijana na Watoto.
-- Zainul A. Mzige, Operation Manager, MO BLOG, www.modewjiblog.com +255714940992.
TRA yakutanisha wadau wa kodi kujadili uanzishwaji wa chombo cha kuratibu na kusimamia wanataaluma wa kodi

TRA yakutanisha wadau wa kodi kujadili uanzishwaji wa chombo cha kuratibu na kusimamia wanataaluma wa kodi

June 29, 2016
TRA yakutanisha wadau wa kodi kujadili uanzishwaji wa chombo cha kuratibu na kusimamia wanataaluma wa kodi
Katika kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya walipa kodi na wakusanyaji wa kodi, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imefanya kongamano la pamoja na wadau wa kodi nchini likiwa na lengo la kujadili kwa pamoja kuhusu uanzishwaji wa chombo cha kuratibu na kusimamia wanataaluma wa kodi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kamishna wa Sera na Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Shogholo Msangi alisema wamekutanisha wadau hao wa kodi ili waweze kutoa maoni na kukubaliana kwa pamoja jinsi gani chombo hicho kitaweza kufanya kazi.

"Kutakuwa na chombo ambacho kitakuwa kinaratibu na kusimamia wanataaluma wa kodi na lengo ni kupitia kongamano hilo wadau wa kodi wataweza kukubaliana kwa pamoja kuona ni jinsi gani chombo hicho kitafanya kazi,
Kamishna wa Sera na Bajeti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Shogholo Msangi akitoa neno la ufunguzi katika kongamano lililoandaliwa na TRA na kukutanisha wadau mbalimbali wa kodi. (Picha zote na Rabi Hume - MO Blog)

"Unaweza kukuta kuwa mlipa kodi kwa sasa ndiyo anaumia au TRA ndiyo inaumia lakini chombo hicho kitaweza kusimamia na kuweka kila jambo sehemu sahihi kama linavyotakiwa kuwapo," alisema Msangi.

Nae Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Kodi (ITA), Prof. Isaya Jairo alisema kuwa chombo hicho kama kikianzishwa kitaweza kufanya kazi zake kwa uhuru bila kuingiliwa na TRA ili kuhakikisha kuwa kinatoa na haki kati ya mlipa kodi na wakusanyaji wa kodi (TRA) bila kuumiza upande wowote kwani jambo hilo linawahusu wote.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Kodi (ITA), Prof. Isaya Jairo akitoa neno la ukaribisho katika ufunguzi wa kongamano hilo lililofanyika Bagamoyo, Pwani.

Alisema kupitia kongamano hilo wamekutanisha wataalam wa kodi, wahasibu, walipa kodi, wanasheria, washauri wa kodi na walimu wa kodi kutoka vyuoni ili kuweza kupata maoni ya pamoja na kupata maoni ya makubaliano ya pande zote ambayo yatatumika katika kuendesha chombo hicho.

Na Rabi Hume - MO Blog)
Baadhi ya wadau waliohudhuria kongamano hilo la siku moja lililofanyika Bagamoyo, Pwani.






Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja (group one).
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja (group two).
SMZ YAAHIDI KUENDELEZA MIPANGO YA UCHUMI INAYOCHAGIZWA KIMATAIFA

SMZ YAAHIDI KUENDELEZA MIPANGO YA UCHUMI INAYOCHAGIZWA KIMATAIFA

June 29, 2016
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendelea kuhakikisha mipango yote ya kimaendeleo inayochagizwa na malengo endelevu ya kimataifa inatekelezwa kwa vitendo ili wananchi waweze kunufaika.

Imesema katika malengo ya milennia ya 2015 serikali ilifanikiwa katika baadhi ya sekta zikiwemo sekta za elimu, afya na miundo mbinu hatua zinazotakiwa kuendelea kupewa kipaumbele na wadau wa maendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani humo. Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Alisema licha ya kuwepo na changamoto mbali mbali za kiutendaji katika utekelezaji wa mipango hiyo ikiwemo suala la wananchi kutokuwa na uelewa mzuri wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya dunia bado mamlaka husika zinaendelea kutoa elimu hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho katika Mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wanaojadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umeandaliwa na ESRF kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini.

Reli alieleza kwamba malengo na mipango mbalimbali ya maendeleo ni kuwasaidia wananchi wa Zanzibar waweze kuondokana na tatizo sugu la umaskini, magonjwa na changamoto za kiusalama.

“Katika MDG tumeweza kufanikiwa kwa baadhi ya malengo ikiwemo suala la elimu na afya lakini kuna mengine bado hatukuweza kufanikiwa kuyafikia na kwa sasa tunaendelea na malengo mapya ya SDG’s ambayo tunatakiwa kuyafanyia kazi ili yaende sambamba na mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar." alisema Reli.

Aidha alisema bado wanajadiliana ni kwa namna gani mipango ya kimataifa tutaiingiza katika sera na mipango yetu ya kimaendeleo ili wananchi waweze kunufaika na fursa hizo za kimaendeleo na kiuchumi kwa ufanisi zaidi.

Alisema utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ambayo ni 17 yanatakiwa kupewa kipaumbele kwani yanagusa nyanja mbalimbali za kijamii yakiwemo maisha halisi ya wananchi wanaostahiki kunufaika na fursa na mahitaji muhimu ya kibinadamu.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, Bw. Alvaro Rodriguez katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar.

Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafti, Uchumi na Kijamii nchini ( ESRF), Dkt.Tausi Kida akitoa neno la ukaribisho alisema, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika SDG’s ni vyema sera na mipango endelevu ya nchi husika iweke vipaumbele vya kukuza uchumi kuanzia ngazi za chini

Kida alieleza kwamba katika utekelezaji wa SDG’s lazima kuwepo na mpango endelevu wa ufuatiliaji kuanzia ngazi za chini hadi taifa kwa lengo la kuhakikisha malengo hayo yanatekelezwa kwa mujibu wa matakwa ya malengo ya kimataifa.

Naye Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN), Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga alisema endapo malengo ya dunia yataweza kutekelezwa ipasavyo Zanzibar itaweza kupunguza changamoto mbali mbali zinazokabili sekta za kijamii na kiuchumi.

Alisema UN itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika utekelezaji wa SDG’s kama ilivyokuwa katika utekelezaji wa malengo ya dunia MDG’s yaliyopita ili serikali iweze kufikia ngazi za chini kwa kuinua kipato cha wananchi kiendane na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli akitoa nasha wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar ambao umefanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Senga aliishauri serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kuwashirikisha wananchi wa ngazi za chini katika kupanga na kutekeleza maendeleo yao katika maeneo husika ya wananchi.

“Changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya kimataifa ili yaendane na mipango ya maendeleo ya serikali ni upungufu wa ushirikishwaji wa wananchi ama jamii husika na wengine hawafikiwi kabisa katika maeneo yao jambo linalotakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka katika kutekeleza kwa vitendo Malengo ya Maendeleo Endelevu ya SDG’s”, alifafanua Senga.

Naye Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, Rogers Dhliwayo alisema Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s yanatakiwa yawekewe vipaumbele mbalimbali vya takwimu na tafti za kiuchumi katika maeneo tofauti ya jamii ili malengo endelevu yaweze kuwafikia walengwa.

Kwa upade wa washiriki wa mkutano huo kwa nyakati tofauti walisema kwamba mipango mbalimbali ya kimaendeleo inayopangwa na serikali inatakiwa kuwekewa vipaumbele kwa wananchi badala ya utekelezaji na tathimini kubakia ngazi za serikali kuu pekee.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) na Mkurugenzi wa Kupunguza Umaskini na Kuinua Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Anna Mwasha wakinakili mambo muhimu wakati mgeni rasmi (hayupo piichani) akitoa nasaha zake.

Walisema kwamba katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ni lazima kutengeneza mpango mkakati wa mawasiliano wa masuala ya utamaduni, mila na desturi za jamii husika ambapo mipango hiyo inatakiwa kutekelezwa ili iwe rahisi wananchi kufahamu vizuri umuhimu wa mipango hiyo.

Washiriki hao walisema katika utekelezaji wa mipango hiyo ni lazima kuwepo na mikakati ya makusudi ya kuhakikisha changamoto ya umasikini uliokithiri unapungua kulingana na mikakati mbalimbali inayowekwa na vipaumbele vya kimataifa ili viweze kutekelezwa kwa vitendo na nchi husika.

Aidha wameshauri kwamba katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu SDG’s ni lazima kuzingatia suala la serikali za mitaa, kutumia lugha nyepesi katika mawasiliano, kufanya marejeo katika maandiko ya baadhi ya waasisi wa kitaifa akiwemo Mwalimu Nyerere na kufanya utafiti juu ya matumizi sahihi ya Rasilimali.
Pichani juu na chini ni wadau wa sekta za maendeleo visiwani Zanzibar walioshiriki katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani humo ambao umefanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.

Sambamba na hayo wamesema katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ni lazima kuweka kipaumbele kwa makundi maalum ya watu wenye mahitaji maalum wakiwemo Watu wenye Ulemavu.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF) ambapo imewakutanisha wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).


Mshauri wa Masuala ya Uchumi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Tanzania, Rogers Dhliwayo akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar.

Kutoka kushoto ni Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) Ofisi ya Zanzibar, Anna Senga, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, mgeni rasmi Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Kida (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Kupunguza Umaskini na Kuinua Uchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Anna Mwasha wakiwa meza kuu.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto ya visiwani Zanzibar, Mauwa Makame Rajab akitoa maoni katika mkutano wa wadau wa sekta za maendeleo nchini wa kujadili utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) visiwani Zanzibar uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto) na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Juma Reli wakisikiliza maoni ya wadau yaliyokuwa yakiwasishwa kwenye mkutano kuelekea utekelezaji wa SDGs.
Bw. Sefu Mwinyi kutoka Tume ya Mipango Zanzibar akiwasilisha maoni yake katika mkutano huo uliowakutanisha wadau wa sekta za maendeleo visiwani Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya ya Elimu na Mafunzo ya Amali visiwani Zanzibar, Khadija Juma (kushoto) akichangia hoja katika mkutano huo. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora visiwani Zanzibar, Asha Abdallah Ali.
Mgeni rasmi katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo.
-- Zainul A. Mzige, Operation Manager, MO BLOG, www.modewjiblog.com +255714940992.