SIMBA SC YADHIHIRISHIA UBABE KWA YANGA, YAWAPIGA 3-1 NA OKWI WAO

December 21, 2013

Nahodha wa Simba SC, Haruna Shamte akiwa ameinua Kombe baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe mwenye suti nyeusi kulia baada ya kuifunga Yanga SC mabao 3-1  
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
SIMBA SC ndiye Mtani Jembe 2013. Hiyo inafuatia Wekundu hao wa Msimbazi kuwafunga watani wao wa jadi, Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba yamefungwa na Amisi Tambwe mawili na Awadh Juma moja, wakati la Yanga lilifungwa na Emmanuel Okwi. 
Katika mchezo huo, Yanga ilimaliza pungufu baada ya beki wake, Kevin Yondan kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, baada ya kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’. 
Mfungaji wa mabao mawili ya Simba SC leo, Amisi Tambwe akipongezwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya'
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yote yalifugwa na Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44.

Tambwe alifunga bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya kiufundi ya Said Hamisi Ndemla na kumtungua kipa Juma Kaseja.

Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Jonas Mkude aliyeinasa pasi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kuelekea kwa Frank Domayo, akampasia Henry Joseph ambaye alimpelekea Ndemla, aliyempa mfungaji.

Tambwe alifunga bao la pili kwa penalti baada ya beki wa Yanga, David Luhende kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyeingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Ndemla. 

Kwa ujumla, Simba SC ndiyo waliocheza vizuri kipindi cha kwanza wakionana kwa pasi za uhakika, wakati wapinzani wao walikosa mbinu za kuipenya ngome ya Wekundu wa Msimbazi, iliyoongozwa na Mkenya Donald Mosoti Omwanwa.
Krosi nyingi za Mrisho Ngassa kutoka kulia ama zilidakwa na Ivo Mapunda au zilipitiliza nje.

Kipindi cha pili, Yanga SC walianza kwa mabadiliko, wakiingiza wachezaji watatu kwa mpigo, Emmanuel Okwi, Simon Msuva na Hassan Dilunga kuchukua nafasi za Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na Athumani Iddi ‘Chuji’.  

Lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia Yanga SC kwani wapinzani wao Simba walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Awadh Juma.

Bao hilo lilitokana na makosa ya beki Mbuyu Twite kumrudishia mpira mfupi kipa Juma Kaseja, ambaye alijaribu kuuweka sawa, lakini akazidiwa na Awadh aliyeupokonya na kuusukumia nyavuni.

Baada ya bao hilo, Simba walianza kucheza kwa kujiamini zaidi wakipiga pasi za kusisimua na kuwafurahisha mashabiki wao, huku Yanga wakihaha kusaka bao la kufutia machozi.

Alikuwa Okwi aliyeifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 87, akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima. 

Baada ya mchezo huo, Yanga walikabidhiwa Medali za Fedha Kombe dogo na hundi milioni 98.9, wakati wapinzani wao walivalishwa Medali za Dhahabu, Kombe kubwa na hundi ya Sh. Milioni 1 kutokana na promosheni ya Nani Mtani Jembe.

Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende/Oscar Joshua dk79, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Juma Abdul dk53, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Hassan Dilunga dk46, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu/Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete dk69 na Hamisi Kiiza/Emmanuel Okwi dk46.

Simba SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk55, Henry Joseph/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk34/Abdulhalim Humud dk72, Amisi Tambwe/Amri Kiemba dk54, Said Ndemla/Ramadhani Singano ‘Messi’dk27 na Awadh Juma.

SIMBA WAICHAPA YANGA BAO 3-1

December 21, 2013
 Wachezaji wa Simba na baadhi ya viongozi wao wakipozi na kombe lao kwa furaha baada ya kukabidhiwa kombe hilo kwa kuifunga Yanga katika mchezo wa Nani Mtani Jembe, uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Katika mchezo huo Simba wameibuka washindi kwa.kuichapa Yanga mabao 3-1, mabao ya Simba yalifungwa na Hamis Tambwe mawili na Ramadhan Singano huku la kufutia machozi la Yanga likifungwa na Emmanuel Okwi.
 Meneja wa Yanga, Afidh Ally akipokea mfano wa hundi ya zaidi  sh. 98 milioni Kwa kuibuka washindi katika shindano la Nani Mtani Jembe kwa kupata kura nyingi katika unywaji wa bia ya Kilimanjaro.
Kiongozi wa Simba Hans Pope, akimpongeza Henry Joseph, baada ya mchezo huo. Kaa na ukurasa huu kwa matukio zaidi ya mchezo huu yatakayokujia hapo baadaye.
 Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, akiruka hewani kushangilia bao la kwanza la Simba lililofungwa na Hamis Tambwe katika dakika ya 14, ya kipindi cha kwanza.
 Mshambuliaji wa Simba Hamis Tambwe, akifunga bao la pili kwa mkwaju wa penati katika dakika ya 44, baada ya beki wa Yanga, David Luhende kumkwatua Ramadhan Singano katika eneo la hatari.
Mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbagu, akijaribu kumfinya beki wa Simba, Joseph Owino wakati wa mtanange huo. Mpira sasa ni kipindi cha pili.

MASHUJAA BENDI KUWASHA MOTO TANGA JANUARI 11

December 21, 2013


Na Oscar Assenga,Tanga.
BENDI ya Mziki wa Dansi nchini Mashujaa yenye makazi yake jijini Dar es Salaam inatarajiwa kufanya onyesho la aina yake Januari 11 mwakano mkoani hapa amblo litafanyika ukumbi wa Nyumbani Hotel.

Onyesho hilo limeandaliwa na Kampuni ya New Face kwa kushirikiana na Mashujaa Band lenye lengo la kuwapa burudani wakazi wa Tanga  na kuzitambulisha tuzo 5 walizopata wakati wa Kilimanjaro Music Award.

Akizungumzia maandalizi ya Onyesho hilo,Mkurugenzi wa Kampuni ya New Face Intertainment,Maximilian Luhanga alisema kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa na kinachosuburiwa na siku ya onyesho hilo kufanyika.

Luhanga alisema kuwa wasanii nguli wa band hiyo akiwemo Charles Baba watawakonga nyoyo mashabiki wao kwa kutoa burudani ya aina yake siku hiyo wakiwa sambamba na Furgson,

HOTUBA YA MH ZITTO Z. KABWE - KIGOMA – 21 DESEMBA 2013

December 21, 2013

Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu, uzalendo na uwajibikaji. Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. 
Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi mwaka 1994. Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. 

PPF YAELEZA MAFANIKIO YALIYOPATIKANA TOKEA KUANZISHWA KWAKE.

December 21, 2013
Na Raisa Said,Handeni.

Imewekwa Saa 05:16 Desemba 21.
 Mfuko wa Pensheni wa PPF,umeeleza mafanikio yaliyopatikana kuanzishwa kwake kuwa ni pamoja na kuwalipia ada za masomo ya juu watoto yatima walioachwa na wazazi wao ambao ni wanachama wa mfuko huo kutokana na kufanya vizuri kwenye shule mbalimbali nchini. 
Meneja wa Kanda wa PPF, Zahra Kayugwa, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa tamasha la Handeni Kwetu lililofanyika mjini hapa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

MNDOLWA:NITATOA MILIONI 5 KWA VIJANA WATAKAOANDAA EKARI TANO ZA ALIZETI

December 21, 2013
Raisa  Said,Korogwe
MJUMBE wa  Halmashauri kuu  CCM  Taifa {NEC} Kupitia  Jimbo  la  Korogwe  vijijini  Dr. Edmund  Mndolwa  ameahidi  kutoa  mil. 5  kwa vijana ambao  wataandaa ekari  tano  za  shamba  la kulimia alizeti  lengo  likiwa kuwakwamua  kiuchumi.

Akizungumza   katika  mikutano  mbalimbali wakati  wa ziara  yake  ya  siku  za saba   jimboni humo  alisema  ameahidi  kutoa  pesa  hiyo  kwa  vijana  wakata  20  ambao  wataandaa   maeneo  ya  kulimia  alizeti.

Dk  Mndolwa  ambae  pia  ni mwenyekiti  wa  Wazazi  Mkoa wa  Tanga  alisema  kuwa  mpango  huo  utaweza kuwasaidia  vijana  wengi  kujiajili  na  kuepuka  kufanya  vitendo  viovu  na  kuacha  kukaa vijiweni  bila  ajira.

MAKAMBA AMWAGA VIFAA VYA MICHEZO JIMBONI KWAKE.

December 21, 2013


Na Rais Said,Lushoto.
 
NAIBU Waziri wa Mawasiliano,Sayansi na Technologia,Januari Makamba amemwaga vifaa vya michezo jimboni kwake vyenye thamani ya sh.milioni 2 lengo likiwa ni kuhamasisha vijana kupenda mchezo wa mpira wa miguu.
 
Vifaa vilivyotolewa na Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli ni mipira 50 kwa vijana ikiwa ni harakati za kuhamasisha kuinua sekta ya michezo jimboni humo na kupata timu ambayo baadae itakuja kuwa tishio kwenye medani ya soka mkoani hapa.