TBS yafunga kiwanda cha kuzalisha mikate Tanga

TBS yafunga kiwanda cha kuzalisha mikate Tanga

May 26, 2013
Na Amina Omari,Tanga
Kiwanda cha kutengeneza mikate cha (TANGA MODERN  BAKERY )kimekua cha pili kufungiwa shirika la viwango Tanzania TBS katika kipindi kisichozidi wiki moja mkoani Tanga baada ya kubainika kuwa kinazalisha mikate bila  kufuata taratibu za viwango bora vya uzalishaji.
 
Akizungumza katika oparesheni hiyo, Afisa Uhusiano wa TBS Rhoida  Andusamile alisema wamezuia uzalishaji katika kiwanda hicho baada ya kubaini kuwa wamiliki wakiwanda hicho wamekua wakitengeneza mikate ambayo inatengenezwa bila kufuata taratibu za shirika la viwango nchini.
 
Alisema mikate ni bidhaa ambayo ipo katika viwango vya lazima vya ubora hivyo kiwanda hicho kwa muda mrefu kimekuwa  kinazalisha bidhaa bila kuwa na nembo ya ubora ya kutoka TBS.
 
“Niwajibu wetu kuhakikisha kila mzalishaji  nchini anazalisha bidhaa zenye ubora kwa lengo la kuwakinga walaji na madhara ya kiafya hivyo tumekuwa tukiendesha ukaguzi wa mara kwa mara katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini lengo ikiwa ni kumlinda mlaji”Andusamile.
 
Nae mkaguzi washirika hilo Deusdedit Paschal alisema bakery hiyo ilitakiwa kabla haijaanza uzalishaji wapeleke  sampuli za mikate TBS kwa ajili ya kuangalia ubora pamoja na ukaguzi kufanyika lakini yote hayo hayakufanyika.
 
Alisema kwa miaka 16 kiwango hicho kimekuwa kizalisha mikate hiyo pamoja na bidhaa nyingine kama keki bila ya ya kuwa na mikataba na TBS wala nembo ya ubora pamoja na ukaguzi.
 
Kwa upande wake  Meneja wa kiwanda hicho Hilal Salim alikiri kuendesha uzalishaji bila kuwa na nembo ya kuthibitisha ubora wa bidhaa yake ,hata hivyo alliomba TBS kutokifungia kiwanda hicho kwani wananchi wengi wataathirika na ukosefu wa bidhaa zake
 
Hata hivyo baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho walisema kufungiwa kwa kiwanda hicho kutawathiri kiuchumi kwani walikuwa wanatagemea ajira hiyo kuendesha   familia zao.
 
Mei 22 mwaka huu shirika la viwango nchini TBS lilifungia kiwanda cha kutengeneza maji cha Al Hayaa kutoka na kuendeleza uzalishaji wa bidhaa hiyo bila kuwa na  leseni ya ubora.
RCL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI LEO

RCL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI LEO

May 26, 2013

Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inaendelea leo (Mei 26 mwaka huu) kwa mechi sita za kwanza zitakazochezwa katika miji sita tofauti.

Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Machava FC ya Kilimanjaro itakuwa mwenyeji wa Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Nayo Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida huku Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara ikimenyana na Biharamulo FC ya Kagera kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi wakati Njombe Mji itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

Mwisho.
TAIFA STARS KWENDA ADDIS ABABA LEO

TAIFA STARS KWENDA ADDIS ABABA LEO

May 26, 2013
Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja.

Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa.

Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.

Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko.

Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Shindano la Redd"s Miss Tanga laiva.

May 26, 2013
WAREMBO wanaowania taji la Redd"s Miss Tanga,2013 wakiwa katika pozi mara baada ya kumaliza mazoezi yao yanayoendelea katika ukumbi wa club Lavida Loca jijini Tanga.
Redd's Miss Tanga, kutembelea vivutio vya utalii June 17.

Redd's Miss Tanga, kutembelea vivutio vya utalii June 17.

May 26, 2013

Na Oscar Assenga,Tanga.
WAREMBO wanaowania umalkia wa Mkoa wa Tanga “Redd’s Miss Tanga 2013”wanatarajiwa kutembelea katika vivutio vya utalii na maeneo ya kihistori yaliyopo mkoani hapa June 17 mwaka huu lengo likiwa ni kujifunza utalii wa ndani ili kuweza kupata fuksa nzuri ya kuweza kuutangaza kwa wageni na wenyeji.

Shindano hilo linatarajiwa kufanyika 22 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa ambapo litapambwa na wasanii nguli wa muziki wa dansi hapa nchini na bongo fleva ili kuweza kuwapa burudani wakazi wa mkoa huu ambao watajitokeza kushuhudia kinyang’anyiro hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, Mkurugezi wa Kampuni ya DATK Intertaimeint, Asha Kigundula, alisema kuwa warembo hao tayari wameanza mazoezi kwenye Ukumbi wa Lavida uliopo jijini Tanga ambapo wameweza kuwateka wadau wa tasnia hiyo ambao wamekuwa wakijitokeza kila siku kushuhudia mazoezi hayo.

   “Ninachoweza kusema shindano la mwaka huu litakuwa la aina yake kutokana na kusheheni warembo bomba wenye mvuto na hivyo kuonyesha kutakuwa na mchuano mkali miongoni mwao “Alisema Kigundula 

Shindano hilo litaanza saa 2, usiku na kueleza kuwa maandalizi ya shindano hilo yanaendelea vizuri na jumla ya warembo 14 watashindania taji hilo. Kigundula alisema kuwa mpaka juzi warembo 10 wamejitokeza na kuanza mazoezi yanayosimamiwa na warembo hao ni Miss Tanga 2012 Teresia Kimolo na Mariam Bandawe.

Warembo hao ni Hawa Ramadhan (18),Hazina Mbaga (19)Like Abdulraman (19), Jack Emannuel (18),Waida Mmbwambo(20), Tatu Hussein(19), Mwanahamis Mashaka(20), Neema Abdallah (18), Winfrida Gutram (21)Lulu Mbonea (19) na Aisha Rashid (21).

"Kila kitu kinaendelea vizuri, ikiwa na warembo kuendelea kujiandikisha kushiriki shindano la mwaka huu, ambalo nina hakika litakuwa la aina yake"alisema Kigundula

Alisema kwamba shindano la mwaka huu litaandika historia mpya ya urembo mkoani humo kwa kuwa Kampuni DATK imejipanga, hivyo mashabiki wa mashindano ya urembo wa jijini hapo kwa ujumla wakae mkao wa kupata raha.

Redd's, Miss Tanga, imedhaminiwa na CXC Africa,Executive Solutions,Busta General Supply, Mkwabi Interprises,Lusindic Investment LTD, Lavida Pub,Jambo Leo,Staa Spoti,Five Brothers Cloud's Media Group,  pamoja na Blog Michuzi Media Group,Bongostaz.com, Saluti5,Kajuna, JaneJohn, na Kidevu na Assengaoscar.blogspot.com.

   Mwisho.