UZINDUZI WA CHAGUA CHOCHOTE UNACHOTAKA BAYPORT ITALIPA WAFANYIKA

January 14, 2015
Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo kushoto akizungumza jambo na waandishi wa habari hawapo pichani katika uzinduzi wa huduma mpya ya Chagua chochote Bayport italipia jana jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Meneja Biashara, Thabit Mndeme.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TAASISI ya kifedha ya Bayport Financial Services, imezindua tena huduma mpya inayojulikana kama ‘Chagua chochote unachotaka Bayport italipia’, ikiwa na lengo la kuwapatia mikopo ya bidhaa mbalimbali wateja wao na Watanzania kwa ujumla.

Huduma hiyo ni mwendelezo wa ile 'Mikopo ya Bidhaa' ambapo watu wanakopeshwa bodaboda, sambamba na Bima ya Elimu iliyozinduliwa pia mapema mwaka jana kwa ajili ya kuleta urahisi katika mfumo wa maisha ya Watanzania wengi.
 Ngula Cheyo anazungumza jambo na kulia kwake ni Thabit Mndeme.
Akizungumza katika uzinduzi wa huduma hiyo mpya, Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme, alisema huduma hiyo sasa itawapatia fursa wateja wao kukopeshwa magari, nyumba, vifaa vya ujenzi, pembejeo za kilimo, ada ya shule, pikipiki, bajaj, tv, injini ya boti na nyinginezo kwa ajili ya kuwapatia mwangaza mzuri wa kimaisha na kiuchumi.

Alisema kuwa kuanzisha huduma hiyo mpya imetokana na ile ya mikopo ya bidhaa kufanya vizuri tangu ilipozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na kupatikana nchi nzima kwa kupitia matawi yaliyosambaa katika mikoa mbalimbali.
Meneja Biashara wa Bayport Financial Services, Thabit Mndeme kulia akizungumza jambo katika uzinduzi wa huduma mpya ya 'Chagua chochote Bayport italipia', ikiwa ni mwendelezo wa huduma ya mikopo ya bidhaa, ambapo wateja wa Bayport wanapata fursa ya kukopeshwa bidhaa mbalimbali, kama vile nyumba, magari, vifaa vya ujenzi na nyinginezo.
Picha zote na Mpiga Picha Wetu.
 “Bayport ilifanya mazungumzo na wateja wake mbalimbali baada ya kuzindua huduma ya Mikopo ya Bidhaa na kuona mafanikio makubwa waliyopata, hivyo mwaka huu tumeona tufike mbali zaidi kwa kuangalia namna gani Watanzania wanaweza kukopeshwa bidhaa nyingi kwa ajili ya kukuza uchumi wao.
“Ni rahisi mno kupewa mkopo wa chagua chochote unachotaka Bayport italipia kwasababu anachotakiwa kufanya mteja ni kuchagua bidhaa anayoitaka katika duka au msambazaji yoyote aliye karibu naye, kisha atapewa fomu ya malipo na kuipeleka kwenye tawi la Bayport lililo karibu yake ili apate mkopo aliyohitaji,” alisema Mndeme.

Alisema kuwa baada ya kuzinduliwa huduma hiyo ya Mikopo ya Bidhaa, wengi waliipenda na kunufaika nayo, hivyo aliwaomba wateja wao na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuiunga mkono Bayport Financial Services kwa ajili ya kuwapatia maisha bora, maana ndiyo kusudio lao.

Naye Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport Financial Services, Ngula Cheyo, alisema kwamba taasisi yao inayojihusisha na mambo ya mikopo inatambua namna bora ya matokeo mbalimbali ya kuwaendeleza kiuchumi, hivyo huduma hizi ni mwendelezo wa juhudi za kukuza uchumi wa watumishi wa umma na wafanyakazi wa kampuni zilizoidhinishwa.

“Tunajivunia kufanya kazi kwa bidii na kupanua wigo wa huduma zetu kwa matawi 80 nchi nzima, jambo linalotupa shauku ya kuona nchi yetu inapiga hatua kiuchumi kwa kuwawezesha watumishi wa umma na kampuni zilizoidhinishwa na Bayport kwa kuwapatia mikopo waipendayo, huku pia tukiwaeleza kwamba tumehamia jengo jipya la Bayport House, Morocco kwa ajili ya kuwahudumia vizuri zaidi," alisema Cheyo.

Aidha, Cheyo aliwashukuru wateja wao na Watanzania kwa ujumla kwa kuwaunga mkono miaka 9 tangu walipoanza kutoa huduma ya mikopo, huku akisema kuwa taasisi yao itaendelea kufanya kazi kwa moyo wote ili kuhakikisha kwamba pato la wananchi linakuwa kwa kuwakopesha ili wajikwamue kiuchumi.
Bayport Financial Services ni taasisi ya isiyokuwa ya kibenki inayoongoza kutoa mikopo barani Afrika na Amerika ya Kusini, huku ikianzishwa mwaka 2001 na umiliki wake ukiwa nchini Mauriritius, ambapo pia kwa Tanzania ilianzishwa rasmi mwaka 2006, huku ikiwa na matawi 80 nchi nzima.

WATU WATATU WATIWA MBARONI BAADA YA KUGUNDULIKA WAKISAFIRISHA MIRUNGI ROBA 18

January 14, 2015

 Kaimu kamanda wa polisi Tanga, Juma Ndaki akiwaonyesha waandishi wa habari viroba 18 vya mihadharati aina ya mirungi pamoja na bangi kilo 64 iliyofichwa kwenye magunia ya vitunguu maji iliyokuwa ikisafirishwa kwenda  Kilimanjaro  mapema leo.


Tanga,POLISI Mkoani Tanga inawashikilia watu watatu wakazi wa Kigamboni Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha mihadharati aina ya mirungi viroba 18 walivyovificha katika shehena ya mbao zikisafirishwa kuelekea Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kaimu kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Juma Ndaki alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 za usiku katika kizuizi cha polisi kijiji cha Chekelei barabara ielekeayo  Mombo, Segera.

Aliwataja watu hao kuwa ni Sara Mbwambo(38), Robison Sam(24) na Godfrey Machumbe (30) wote wakiwa ni wakazi wa Dar es Salaam Wilaya ya Kinondoni.

Alisema viroba hivyo vilifichwa katikati ya mbao jambo ambalo haikuwa rahisi kugundua na polisi walitilia shaka baada ya kusikia harufu ambayo si ya kawaida na kudhani kuna kitu kifananacho na madawa ya kulevya.

“Unajua sasa hivi kuna kila aina ya mbinu zinazotumika kusafirisha madawa ya kulevya----mbinu hizo nasi tunazijua na ndio maana kila wanavyofanya tunawagundua” alisema Ndaki

“Katika kila kizuizi cha polisi tumeweka wataalamu wa kubaini madawa ya kulevya na ndio tumefanikiwa hakuna anaepita hata kama ameficha ndani ya tairi na kuweka upepo tutagundua” alisema

Katika tukio jengine Ndaki alilitaja kuwa polisi inamtafuta mkazi wa Lushoto, Farid Jumaa kwa tuhuma za kusafirisha bangi kilo 64 na kuficha katika magunia ya vitunguu maji.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1 jioni katika kizuizi cha polisi cha Mombo wakati akisafirisha kuelekea  Mkoa wa Kilimanjaro na kupakia katika gari dogo ya matumizi ya nyumbani.

“Tulipoisimamisha gari jambo la kwanza tulisikia harufu kali ambayo sio ya  kawaida na kuacha hata ukaguzi wa gari----kwanza tulitaka kuteremsha magunia ambayo yalikuwa kwenye buti” alisema Ndaki

“Dereva aligoma kuyashusha na kudai ni vitunguu maji na nyanya ikiwa ni zawadi ya kupeleka kwa wazazi Machame Kilimanjaro---tuliyashusha kwa nguvu na kuyapasua na kila gunia kulikuwa na roba la bangi” alisema

Kamanda Ndaki aliwataka wadereva kuacha kuchukua mizigo ambayo hawana uhakika nayo na hivyo kuwashauri wahakikishe mzigo wanaobeba watautambua na kuwa tayari kuutolea maelezo ili kuepusha kuingia katika matatizo.