WAKUU WA MIKOA YA KANDA YA KASKAZINI WAKUTANA NA WANAHABARI LEO JIJINI DAR ES SALAAM KULITAMBULISHA KONGANO LA UWEKEZAJI.

September 10, 2013

Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Tanga, Arusha , Kilimanjaro na Manyara wakizungumza na Waandishi wa Habari juu ya fursa za uwekezaji katika kanda hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Chiku Gallawa akisisitiza jambo katika Mkutano huo.

Picha ya pamoja ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda yaKaskazini na baadhi ya viongozi wa TIC. Kutoka kushoto ni Mhe. Elaston John Mbwilo, mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe.  Magesa .S. Mulongo , Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Leonidas E. Gama, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Mhe. Chiku Gallawa Mkuu wa Mkoa wa Tanga. Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bw. Abby Kagomba. Kwa Habari zaidi kuhusu Mkoa wa Tanga tembelea tovuti yetu www.tanga.go.tz na Blog www.mkoatanga.blogspot.com. Stori na Monica Laurent, Afisa Habari Mkoa wa Tanga.
NA MONICA LAURENT,PRO TANGA.

Kongano la Uwekezaji Kanda ya Kaskazini linatarajiwa kufanyika Septemba 26 na 27 mwaka  huu katika Hoteli ya Mkonge Jiji la Tanga. Lengo kuu likiwa ni kukuza Uchumi na Kuongeza ajira Kanda ya Kaskazini.

Umuhimu wa Kongano hili ndio ulilosukuma Wakuu wa Mikoa wa Kanda ya Kaskazini kukutana leo katika Ukumbi wa kituo cha Uwekezaji ( TIC)  na Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali  ili kuweza kuwatangazia Wananchi na Umma kwa ujumla kuhusu fursa za maendeleo zilizopo katika mikoa hii.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini, Mwenyeji wa Kongano hili Mhe. Chiku Gallawa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga amesema maandalizi ya Kongano hili yako katika hatua za mwisho.

Gallawa alisema mkoa wa Tanga uko tayari kupokea wageni/ wawekezaji"Tunategemea kupokea wageni/wawekezaji zaidi ya 600 kutoka ndani na nje ya Tanzania na ni imani yetu kwamba kupitia kongano hili hali ya Uchumi katika Kanda hii utaimarika”

Nao Wakuu wa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga ambayo inaunda Kanda ya Kazkazini wamepata nafasi ya kunadi fursa za uwekezaji zinazopatikana katika mikoa hiyo.Fursa nyingi zinapatikana kwenye Kilimo, Utalii, Viwanda, Ufugaji na Madini.

Ni wito kwa kila mwekezaji kutumia fursa hii kuwekeza katika mikoa hii ambayo imejaliwa kuwa na rutuba nzuri, hali ya hewa nzuri, madini mbalimbali, mbuga za wanyama n.k.

Kushiriki kwenye Kongano hili jiandikishe kwa fomu maalumu ambayo ipo kwenye tovuti ya Kanda www.investnorthernzone.go.tz kisha tembelea fursa za uwekezaji kwa kuchagua Mkoa husika.

TANGAZO LA KUMBUKUMBU.

September 10, 2013
Marry Aron Kakuru
Ni mwaka mmoja sasa umepita tangu ulipotutoka tarehe 12  Septemba 2012 kwa ugonjwa wa kansa ya ziwa katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam alipokuwa umelazwa.

Daima unakumbukwa na mumeo Deo Kakuru Msimu,wazazi wako,wakwe zako,kaka na dada zako,shemeji zako,wifi zako, majirani na wafanyakazi wenzio wa Tumaini hospital,marafiki ndugu na jamaa.

Sisi tulikupenda lakini Mungu alikupenda zaidi.Pumziko la Amani, Bwana ametoa,Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe.Amina.

Ibada ya Mkesha ya Kumuombea itafanyika nyumbani kwake, Chuda jijini Tanga na kufuatiwa na Ibada ya kumuombea itayofanyika Septemba 12 mwaka huu.

PONDAMALI AFUNGIWA MIEZI 3, FAINI MILIONI 1/-

September 10, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. milioni moja na kumfungia miezi mitatu kocha wa makipa wa timu ya Coastal Union kwa kuwatukana washabiki wanaominika kuwa wa Simba.

Pondamali alifanya kosa hilo katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mwamuzi Martin Saanya na mwamuzi msaidizi namba moja Jesse Erasmo waliochezesha mechi kati ya Yanga na Coastal Union nao wamefungiwa mwaka mmoja kila mmoja kwa kutoimudu mechi hiyo.

Nayo Yanga imepigwa faini ya sh. milioni moja (sh. 500,000) kwa kila kosa kutokana na washabiki wake kuwarushia waamuzi chupa za maji baada ya Coastal Union kusawazisha bao katika mechi hiyo. Pia waliwarushia chupa waamuzi hao wakati wakirejea vyumbani baada ya pambano hilo.

Vilevile Coastal Union imepigwa faini ya sh. 100,000 baada ya kuchelewa kwenye kikao cha maandalizi ya mechi (pre match meeting). Timu hiyo ilichelewa kwa dakika 23. Kikao kinatakiwa kuanza saa 4 kamili asubuhi.

TEMEKE YAIZAMISHA RUKWA 5-1 COPA COCA-COLA

September 10, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Temeke imejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza robo fainali ya michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya leo (Septemba 10 mwaka huu) asubuhi kuizamisha Rukwa mabao 5-1.

Hadi mapumziko katika mechi hiyo ya kundi B hatua ya Fainali za Taifa iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume jijini Dar es Salaam, washindi walikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao ya washindi yalitiwa wavuni na Constantine Katepa aliyefunga dakika ya 28, Patrick Ambrose dakika ya 36 huku Hamisi Kajole akipiga mawili dakika ya 43 na 71. Bao la nne lilifungwa dakika ya 46 na Ramadhan Juma.

Rukwa ambayo kwa matokeo hayo imeshatolewa ilipata bao lake dakika ya 51 kupitia kwa Francisco Nkanga. Timu nyingine katika kundi hilo ni Geita na Ilala.

Robo Fainali ya michuano hiyo itaanza keshokutwa (Septemba 12 mwaka huu). Kila kundi linatoa timu mbili kucheza hatua hiyo katika mashindano hayo yanayodhaminiwa na kampuni ya Coca-Cola.

KIMONDO KUCHEZA MBOZI, KURUGENZI WAMBI FDL

September 10, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAAM.
Timu za Kimondo SC ya Mbeya na Kurugenzi ya Mafinga zitatumia viwanja vya Mbozi na Mafinga kwa ajili ya mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayoanza Jumamosi (Septemba 14 mwaka huu).

Kimondo SC sasa itatumia Uwanja wa CCM Vwava ulioko wilayani Mbozi badala ya Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine wa jijini Mbeya. Nayo Kurugenzi itatumia Uwanja wa Wambi ulioko Mafinga mkoani Iringa badala ya Uwanja wa Makambako ulioko mkoani Njombe.

Mechi za fungua dimba FDL msimu huu zitakuwa kati ya Burkina Faso na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, Mkamba Rangers na Lipuli ya Iringa kwenye Uwanja wa CCM Mkamba, Majimaji na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea na Kimondo na Kurugenzi kwenye Uwanja wa CCM Vwawa katika mechi za kundi B.

Septemba 14 mwaka huu Tessema na Green Warriors zitaoneshana kazi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. Siku inayofuata (Septemba 15 mwaka huu) Transit Camp na Polisi Dar (Mabatini mjini Mlandizi) wakati mechi nyingine za kundi hilo la A zitakuwa kati ya Villa Squad na African Lyon (Karume) na Ndanda FC na Friends Rangers (Nangwanda Sijaona, Mtwara).

Kundi C ni Polisi Mara na Polisi Dodoma (Uwanja wa Karume, Musoma), Kanembwa JKT na Polisi Tabora (Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma), Stand United na Mwadui (Kambarage, Shinyanga) wakati Pamba na Toto Africans zitamenyana Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

COASTAL UNION WAITUMIA SALAMU TANZANIA PRISON.

September 10, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
KOCHA Mkuu wa timu ya Coastal Union,Hemed Morroco amesema kikosi chake kipo imara kuweza kuwakabili wapinzani wao Tanzania Prison katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania bara ambao utachezwa Septemba 14 mwaka huu katika uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa.

Akizungumza jana,Morroco alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanaendelea vizuri kwa wachezaji wake kufanya mazoezi kila siku asubuhi na jioni ili kuweza kuwakabili maafande hao wa jeshi la magereza hapa nchini pamoja na kuchukua pointi tatu muhimu.

Morroco alisema wao msimu huu wamedhamiria kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa wanaongoza ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 14 ikiwa ni malengo yao waliyojiwekea kwa muda mrefu na kueleza hilo litawezekana kutokana na uimara wao na mshikamano uliopo.

Alisema ligi kuu msimu huu sio ya kubeza kutokana na kila timu kuonekana kujipanga na kutaka kupata pointi tatu muhimu hasa zinapokuwa zikicheza mechi zao za ugenini na nyumbani hivyo nasi tumejipanga zaidi kuhakikisha hilo kwenye timu yetu linafanikiwa.

   "Tunajua mechi yetu na Prison haitakuwa rahisi sana kutokana na kuwa kila timu imejiandaa vya kutosha hivyo tutahakikisha tunatumia uwezo watu tulionao ili kuhakikisha pointi tatu muhimu zinabakia hapa hapa nyumbani "Alisema Morroco.

Aidha aliwataka wapenzi na mashabiki wa soka mkoani hapa kuendelea kuisapoti timu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi hasa wanapocheza mechi zao ili kuipa hamasa ya kuweza kufanya vizuri kwenye michezo yao iliyosalia katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.

KACHUMBARI:AIMWAGIA SIFA COASTAL UNION.

September 10, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
KOCHA Mkuu wa timu ya Mafunzo ya Zanzibar,Mohamed Kachumbari amekimwagia sifa kikosi cha Coastal Union ya Tanga kwa kusema uwezo walionao utawafanya kufika mbali kisoka ikiwemo kutwaa taji la Ligi kuu Tanzania bara .

Kachumbari alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika mechi yao ya kirafiki na Coastal Union ambapo mafunzo walikubali kichapo cha bao 1-0,bao ambalo lilifungwa na Yayo Lutimba aliyeingia kipindi cha pili baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mohamed Banka.

Alisema licha ya timu yao kucheza vema na kupiga mipira mara kwa mara langoni mwa Coastal Union lakini mlinda mlango wao aliweza kuwa imara kwa kuyapangua hali ambayo iliwapeleka kukosa bao na kuambulia kichapo.

Mchezo huo wa leo ulikuwa mkali wenye upinzani mkubwa kutokana na timu zote kuonekana kuukamia,huku Coastal Union wakikosa kosa mabao kwenye mechi hiyo ambapo mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoweza kuona lango la mwenzie.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo kila timu iliweza kuingia uwanjani hapo ikiwa na hari kwa timu zote kufanya mabadiliko kwa Coastal Union kuwatoa Othumani Tamim,Mbwana Bakari,Danny Lyanga,Soud Mohamed, na Atupele Green.

Ambao nafasi zao zilichukuliwa na Masumbuko Keneth,Mohamed Banka,Yayo Lutimba,Marcus Ndehele na Abdi Banda ambao walichukua chachu kwa kuleta ushindi kwenye kikosi cha Mafunzo na kuipa ushindi timu yao kutokana na kucheza vema.

Coastal Union iliwakilishwa na Gk Said Lubawa,Mbwana Bakari,Othuman Tamim,Philipo Mugenzi,Yusuph Chuma,Razack Khalfan,Danny Lyanga,Soud Mohamed,Atupile Green,Pius Kisambale na Abdallah Othuman.

Huku Mafunzo ikiwakilishwa na Gk Abdallah Swamadu,Abdul Halim,Haji Abdi,Yusuph Makame,Said Mussa,Hassan Ahmada,Hamad Haji,Haji Mwambe,Sadick Habibu,Mohamed Ally na Walid Ibrahim.

WADAU WA SOKA PEMBA WAVITAKA VILABU VYA LIGI KUU KUWA NA WASEMAJI.

September 10, 2013
Na Masanja Mabula -Pemba .
Baadhi ya wadau na mashabiki wa soka Kisiwani Pemba wamevitaka vilabu vya ligi kuu Visiwani Zanzibar , kuweka wasemaji wa Vilabu vya ili iwe ni rahisi kwa mashabiki wa Vilabu hivyo kuweza kupata taarifa za timu zao .

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi Kisiwani Humo , wamesema kwa kukosekana kwa wasemaji kunawanyima uhuru wa kuweza kupata taarifa juu wa vilabu vyao ,jambo ambalo linawafanya washindwe kufahamu usajili wa timu zao kabla ya kuanza kwa ligi hiyo .

Khamis Mohammed Kombo amesema kuwa ni tofauti na timu ya Tanzania Bara ambazo zinawasemaji wao , ambapo mashabiki na wapenzi wa vilabu hivyo hupata taarifa za usajili pamoja na maandalizi ya timu zao .

Hata hivyo uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kwamba kikwazo cha kutokuwa na wasemaji wa timu ni katiba ambazo zinaruhusu kuwa na makatibu wenenzi badala ya wasemaji wenye taaluma ya habari kama ilivyo kwa vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzani Bara .

Aidha pamoja na katiba kutoruhusu kuwa na wasemaji wenye taaluma ya habari , lakini hata hizo nafsi za uwenezi ni  bora wakapewa wanahabari ambazo wanamapenzi na vilabu hivyo , ili waweze kuitumia taaluma yao kuwapasha mashabiki juu kile kinachoendelea katika vilabu vyao.

Mmoja wa Viongozi wa moja ya klabu inayoshiriki ligi Kuu Zanzibar (jina tunalo) alisema kuwa utaratibu wa kuwa na wasemaji ni mzuri , na kushauri kufanyika kwa marekebisho katika katiba za vilabu ili kuwepo na wasemaji ambao ni wanahabari .

Alisema kuwa hata wandishi wa habari wanapohitaji kujua maandalizi pamoja na usajili katika vilabu  hivyo hushindwa kutambua ni kiongozi gani anayeweza kutoa taarifa hizo , jambo ambalo linawafanya mashabiki na wapenzi wa vilabu hivyo kusubiri ligi ianze ili wajue usajili wa wachezaji .