WAZIRI MAKAMBA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA 26 WA KAMATI YA MAWAZIRI WA ASASI YA SIASA, ULINZI NA USALAMA YA SADC

July 12, 2024

 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai, 2024.


Mkutano huo ambao ulitanguliwa na Mkutano wa Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC uliofanyika kuanzia tarehe 08 hadi 09 Julai 2024, pamoja na mambo mengine umepokea na kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa ikiwemo Mapitio ya Utekelezaji wa Maamuzi ya Mkutano wa 25 wa MCO na Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC; Hali ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Kanda; na Uimarishaji wa Demokrasia katika Kanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. Dkt. Mulambo Haimbe amewakaribisha nchini Zambia wajumbe wa mkutano huo ambao agenda yake kuu ni kutathmini hali ya siasa, ulinzi na usalama katika nchi wanachama wa SADC na kuandaa mikakati ya pamoja ya kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana kwenye maeneo ya changamoto.

Aidha, akizungumzia hali ya amani na usalama kwenye maeneo yenye changamoto hususan eneo la Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho na eneo la Kaskazini mwa Msumbiji, Mhe. Haimbe amesema hali sasa inatia moyo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuendelea kujitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha amani, usalama na utulivu wa kudumu vinapatikana kwenye maeneo hayo ili kuwa na maendeleo endelevu ya kiuchumi katika kanda.

Kadhalika amezipongeza misheni za ulinzi wa amani za SADC iliyopo DRC na ile iliyopo Kaskazini mwa Msumbiji kwa kujitoa kikamilifu katika kuhakikisha amani na usalama kwenye maeneo hayo vinarejea mbali na changamoto kadhaa wanazopitia.

Kuhusu misheni ya ulinzi wa amani ya SADC iliyopo Msumbiji (SAMIM) ambayo inamaliza muda wake wa operesheni mwezi Julai 2024, Mhe. Haimbe ameipongeza kwa kazi kubwa iliyofanyika ya kupambana na vitendo vya ugaidi na kurejesha hali ya amani kwa wananchi wa Jimbo la Cabo Delgado lililopo Kaskazini mwa Msumbiji.

“Napongeza misheni ya SAMIM kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika. Japo wanamaliza operesheni huko Kaskazini mwa Msumbiji, bado mapambano dhidi ya ugaidi na uhalifu wa kuvuka mipaka katika Nchi zote wanachama wa SADC yataendelea. Hivyo naziomba nchi zote wanachana kuendelea kushirikiana na kuandaa mikakati ya pamoja kukabiliana na vitisho hivi” alisisitiza Mhe. Haimbe.

Awali akizungumza, Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Mpedi Magosi amesema kuwa Sekretarieti ya SADC itaendelea kushirikiana na Nchi Wanachama hususan katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda zikiwemo za kiusalama, kijamii na kiuchumi ili hatimaye kuwa na Kanda tulivu kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Pia aliongeza kusema bado jitihada za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika kanda ikiwemo ugaidi, vitendo vya uhalifu wa kuvuka mipaka na rushwa. Kadhalika, Mhe. Makosi alitumia fursa hiyo kumpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri anayemaliza muda wake Mhe. Haimbe kwa kazi nzuri aliyofanya katika kipindi chote na kumkaribisha na kumwahidi ushirikiano Mwenyekiti mpya ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Mhe. January Makamba.

Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ilianzishwa mwaka 1996 kwa lengo la kukuza na kulinda amani na usalama katika kanda ya SADC. Tanzania inachukua uenyekiti wa asasi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Agosti 2024.

Mbali na Mhe. Makamba, ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Daniel Sillo, Katibu Mkuu wa Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda, Balozi wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Lt. Jen. Mathew Mkingule, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Talha Waziri na Maafisa Waandamizi wa Wizara na Vyombo vya ulinzi na Usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba akiongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo (kulia) akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Faraji Mnyepe wakishiriki Mkutano wa 26 wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Ushirikiano katika masuala ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC-MCO) unaofanyika jijini Lusaka, Zambia tarehe 11 na 12 Julai 2024.

MSIGWA ASIFU ‘ZOGO MCHONGO ’ YA BENKI YA CRDB KUTOA ELIMU YA FEDHA KWA UMMA

July 12, 2024

 

Dar es Salaam. Tarehe 11 Julai 2024: Akizindua msimu wa pili wa kipindi maalum cha televisheni cha elimu ya fedha kwa umma cha zogo mchongo kinachoandaliwa na Benki ya CRDB, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa  na Michezo, Gerson Msigwa amesifu jitihada hizo zinazolenga kuwakomboa wananchi kiuchumi hali itakayowasaidia kuondokana na umasikini.

Msigwa amesema elimu ya fedha itakayotolewa katika kipindi hiki cha Zogo Mchongo kupitia televisheni ya Clouds, itawafungua Watanzania wengi juu ya fursa zilizopo kwenye taasisi za fedha zikiongozwa na Benki ya CRDB. Maarifa watakayoyapata pia yatawasaidia kujikomboa kiuchumi na kuliwezesha taifa kuyafikia malengo ya kuwa na uchumi jumuishi,” amesema Msigwa.
Katibu mkuu huyo amesema kipindi hicho cha elimu ya fedha pia kinakwenda kusaidia kupambana na maadui wawili kati ya watatu waliotajwa na Mwalimu Nyerere ambao ni ujinga na umasikini na hilo likifanyika rahisi jamii kukabiliana na magonjwa. “Ukishapambana na ujinga na umasikini ni rahisi kutafuta maarifa mengine yakiwamo ya kukabiliana na maradhi,” amesema Msigwa.

“Nawapongeza Benki ya CRDB kwa jitihada zenu za kuwaelimisha Watanzania. Kila mmoja akishiriki katika hili itakuwa rahisi kufanikisha malengo ya serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Msigwa.
Aidha, Msigwa amesema kuwa fedha nyingi nchini zinazunguka kwenye sekta isiyo rasmi kwasababu wananchi wengi hawafahamu faida za matumizi ya huduma za benki. Kutokana na hivyo, Wajasiriamali wengi wamekuwa wakijinyima fursa za kunufaika na mikopo pamoja na huduma nyingine za benki.

“Ni imani yangu kipindi hiki cha Zongo Mchongo kitawafungua macho na kuwawezesha kuchangamkia fursa zitakazosaidia kukuza biashara zao na uchumi wa taifa letu,” ameongezea Msigwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kipindi hicho cha Zogo Mchongo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Elimu ya Fedha (2021/22 – 2025/26) unaolenga kuongeza ufahamu na matumizi ya huduma za fedha kwa wananchi.
Mbali na hayo, Nsekela alibainisha kuwa Zogo Mchongo imekuwa jukwaa muhimu la kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuwa na akaunti za benki, kuwekeza, na kutumia huduma za kifedha kwa usalama na ufanisi. Hii ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya kujumuisha kifedha na kuimarisha uchumi wa taifa kwa ujumla.

“Tukiwa Benki kiongozi ya kizalendo tunawajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya fedha kwani kwa kufanya hivyo sio tu tunasaidia kuchochea ujumuishi wa kifedha bali pia wa kiuchumi kwani elimu hii itasaidia watu kuchangamkia fursa za kiuchumi kutokana na maarifa waliyonayo ya huduma za fedha ambazo zinatolewa na Benki yao ya CRDB,” amesema Nsekela.
Nsekela aliongeza kuwa kupitia programu mbalimbali za elimu na uwezeshaji kwa jamii, Benki ya CRDB inaendelea kujitolea katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii kwa kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia watu wengi zaidi, hususan wale wa vijijini na maeneo yasiyo na huduma za benki.

Joseline Kamuhanda, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, amesema kuwa msimu wa kwanza wa Zogo Mchongo ulikuwa na mafanikio makubwa, na kutokana na mafanikio hayo, wamefanya maboresho makubwa ili kurahisisha uelewa kwa watazamaji wa kipindi hiki kinachorushwa na Clouds TV.
"Msimu huu mpya tumeongeza mada nyingi ambazo zinaelimisha na kuburudisha. Tunataka watazamaji wetu wapate maarifa ya kina kuhusu masuala ya kifedha na waweze kujenga uelewa mzuri zaidi wa jinsi ya kudhibiti na kuwekeza fedha zao. Maboresho haya ni sehemu ya dhamira yetu ya kuendelea kuwahudumia wateja wetu na jamii kwa ujumla." amesema Joseline.

Kipindi cha Zogo Mchongo kinalenga kuongeza ufahamu wa masuala muhimu kama vile bajeti, utunzaji akiba, na namna ya kufanya uwekezaji. Mada zilizoongezwa ni katika msimu huu wa Zogo Mchongo ni pamoja na programu ya IMBEJU ambayo imekuwa kimbilio la vijana na wanawake wajasiriamali kote nchini,  bidhaa kama Hodari kwa wajasiriamali, Huduma zinazofuta misingi ya sharia ‘Al Barakah’,  huduma za Watanzania waishio nje ya nchi ‘Diaspora’, na uwezeshaji kwa biashara.