RAIS KARIA AUNDA KAMATI YA TUZO

RAIS KARIA AUNDA KAMATI YA TUZO

September 06, 2017
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ameunda Kamati ya Tuzo za Ligi Kuu ya Vodacom  Tanzania Bara msimu wa 2017/18.
Kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Ahmed Mgoyi wakati Makamu Mwenyekiti ni Almas Kasongo ilihali  Amiri Mhando ameteuliwa kuwa Katibu wa kamati hiyo ya tuzo.

Mhando ni Mhariri wa Gazeti la Spotileo linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Serikali - Tanzania Standard Newspaper (TSN).

Wajumbe ambao wameteuliwa ni Ibrahim Kaude; Mkuu wa Kitengo cha Michezo katika Kampuni ya Azam Media, Patrick Kahemele na Kocha mkongwe wa soka, Kenny ‘Mzazi’ Mwaisabula.

Kadhaika Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Uchapishaji ya Global (Global Publisher inayochapisha magazeti kadhaa likiwamo Championi), Saleh Ally; Mtangazaji mahiri wa michezo kutoka Kituo cha Redio cha EFM, Ibrahim Masoud na Mtangazaji wa Vipindi katika Kituo cha Radio ya Watu, Fatma Likwata.

Pia wamo Mwandishi Mwandamizi wa Michezo wa Gazeti la Mwanaspoti linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communication (MCL), Gift Macha; Katibu Mkuu wa Chama cha Wachezaji wa Mpira wa Miguu, Said George na Mhariri wa Michezo wa Gazeti la HabariLeo linalotolewa na TSN, Zena Chande.
VIINGILIO MCHEZO WA AZAM FC v SIMBA SC

VIINGILIO MCHEZO WA AZAM FC v SIMBA SC

September 06, 2017
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kuwatangazia wananchi kuwa viingilio katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Azam na Simba.
Mchezo huo utafanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam na viingilio vitakuwa shilingi elfu kumi (Sh 10,000) kwa Jukwaa Kuu ambalo lina uwezo wa kubeba mashabiki 1,000 tu walioketi, wakati mzunguko (popular) kiingilio kitakuwa ni shilingi elfu saba tu (Sh 7,000).

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania linapenda kuwatangazia wanafamilia ya mpira wa miguu kukata tiketi kuanzia leo Jumatano Septemba 6, mwaka huu ili kujiepusha na usumbufu wa aina yoyote.

Kadhalika tunapenda kuwatangazia wananchi kwamba kwa ye yote ambaye hana tiketi ni vema wasiende uwanjani kwani ujio wake hautakuwa na tafasiri nyingine zaidi ya kuonekana kuwa ni mleta fujo.

Vyombo vya usalama vitakuwa makini kudhibniti kila aina ya vurugu uwanjani hapo hasa ikizingatiwa kuwa mchezo huo utafanyika wakati jua limezama. Mchezo utakuwa Septemba 9, 2017 saa 1.00 (19h00).

RC MASENZA AUPONGEZA MPANGO KABAMBE WA HALMASHAURI YA MJI WA MAFINGA

September 06, 2017
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akizungumza wakati wa mkutano wa utambuzi wa mpango kabambe wa halmashauri ya mji wa mafinga wilayani mufindi mkoani Iringa
Prof Aldo Lupala akitambulisha na kuelezea jinsi gani walifanikiwa kuundaa mpango huu kwa tija na maendeleo ya halmashauri ya mji wa mafinga
Mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa mafinga Charles Makoga akiwa na mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza sambamba na mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri williamu wakati mkutano wa utambulisho wa mpango kabambe wa halmashauri ya mji wa mafinga

Na Fredy Mgunda,Iringa
Halmashauri ya mji wa mafinga wilayani mufindi mkoani Iringa yajipanga kuwa manispa kwa kuanza kuupanga mji kuwa wa kisasa na wakibiashara kwa kutumia wataalamu kutoka chuo cha SUA na wataalamu kutoka halmashauri hivyo.

Akizungumza wakati wa kikao cha mpango kabambe wa mji wa mafinga mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema kuwa mji wa mafinga unatakiwa kukuwa kwa mpangilio unao stahili hivyo kuanza na mpango huu itakuwa njia mbadala ya kutatua changamoto mbalimbali za miundo mbinu ambazpo mikoa mingine kuna migogoro mingi.

“Niwashukuru wataalamu na viongozi wa halmashauri hii kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kubuni na kuanzisha mpango kabambe ambao utakuwa mfano kwa halmashauri nyingine zinazokuwa kwa kasi  na  hazina mpango kama huu” alisema Masenza 

Masenza aliwataka viongozi na wadau wa maendeleo katika halmashauri hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya mpango huo kabambe ambao utasaidia kukuza mji kwa kasi na kuwa na mpangilio unaotakiwa hapa nchi.

“Sasa naona tuliopo hapa tunatosha kufikisha ujumbe huu kwa wananchi na wadau wengine ambao hawajahudhuria mkutano huu ili jamii kuwa na elimu na kuondoa migogoro na minong’ono iliyopo kwa wananchiwasiojua chochote kuhusu mpango huu” alisema Masenza

Aidha masenza aliwashukuru wataalamu kutoka chuo SUA kwa kufanikisha mpango kabambe huo kwa gharama nafuu tofauti wangepewa makampuni binafsi ambao mara nyingi gharama zao huwa juu sana tofauti na taasisi za kiserikali na kuitaka halmashauri ya mji wa mafinga kuendelea kuzitumia taasisi za kiserikali zenye uwezo na vigezo stahili kweli miradi mbalimbali ya mji wa mafinga.

Kwa upande wake mwenyekiti ya halmashauri ya mji wa mafinga Charles Makoga alisema kuwa mpango kabambe huu utadumu kwa takribani miaka hamsini ijayo hivyo wakazi wa halmashauri hiyo watanufaika kwa kuwa na mji ambao utakuwa umepangiliwa kwa kila kitu.

“Mkuu wa mkoa nikuahidi kuwa mpango huu utakuwa wa miaka mingi na tutafuata mambo mazuri yote kutoka kwa wataalamu ili kuufanya mji wa mafinga kuwa kivutio cha miji mingine na kuwafanya watu wenngine kuiga mfano kutoka kwetu” alisema Makoga

Makoga aliwapongeza wanafunzi, wataalamu wa chuo cha SUA pamoja na wataalamu kutoka halmashauri kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya  kuhakikisha mpango huo kukamilika kwa wakati pasipo kuwa na changamoto zozote zile.

Halmshauri ya mji wa mafinga tunategemea hivi karibuni kuwa manispaa kwa kuwa vigezo karibia vyote tunavyo hivyo tunaomba kuendelea kushirikiana na kushauriwa katika mikakati ya kuukuza mji huu unakabiliwa na ongezeko la watu kila siku alisema Makoga.

Naye Prof. Aldo Lupala alisema kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na wataalamu wengi hivyo ni vyema wakatumiwa katika miradi mingi ya kimaendeleo ili kungeza ajira na kukuza ujuzi wao pindi wawapo kazini.

“Unajua ukiwa mtaalamu halafu huna kazi kwa kiasi fulani utaalamu au ujuzi wake utapungua toafuti kila wakati mtaalamu akiwa kazini huongeza ubunifu na kukuza utaalamu wake hivyo mgeni rasmi naomba tufikishie ujumbe huu serikali kuu” alisema Lupala

Prof Lupala aliupongeza uongozi wa halmauri ya mji wa mafinga kwa kufanya kazi na wataalamu kutoka chuo kikuu cha SUA kwa ushirikiano mkubwa ambao umefanikisha kupata mpango kabambe ambao utaisaidia halmashauri kwenye mipango ya kuukuza miji huo wa mafinga kuwa manispaa.
MATOKEO YA USAILI KWA WANAOGOMBEA TPLB

MATOKEO YA USAILI KWA WANAOGOMBEA TPLB

September 06, 2017
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imepitisha majina ya wagombea wafuatao kuwania uongozi katika  nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Kamati ya Uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu.
Majina hayo yamepitishwa mara baada ya kuwafanyia usaili uliofanyika Jumapili Septemba 3, mwaka huu kwenye Ukumbi wa TFF, Dar es Salaam. Uchaguzi Mkuu wa Kamati ya Uongozi wa Bodi ya Ligi utafanyika Oktoba 15, mwaka huu. 

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi inayotokana na kanuni za uchaguzi za TFF, majina hayo yanapaswa kutangazwa sasa.

Waliopita na majina yao kutangazwa ni Clement Sanga na Hamad Yahya wanaowania uenyekiti wakati Shani Christoms amepitishwa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti.

Wanaowania nafasi ya ujumbe wako Hamisi Madaki na Ramadhani Mahano. Hawa wamepitishwa kuwania nafasi hizo kutoka Klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Pia wamo Almasi Kasongo ambaye anawania nafasi hiyo  kupitia Klabu za Ligi Daraja la Kwanza wakati Edgar Chibura anawania nafasi ya ujumbe kupitia Klabu za Ligi Daraja la Pili. James Bwire yeye hakupitishwa kwa sababu hakufika kwenye usaili.
LIGI YA WANAWAKE KUANZA NA LIGI NDOGO

LIGI YA WANAWAKE KUANZA NA LIGI NDOGO

September 06, 2017
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeagiza Makatibu wa Vyama vya Mikoa kutuma haraka majina ya timu mabingwa wa mikoa wa soka la wanawake wa msimu wa 2016/17.

Viongozi wa mikoa wamekumbushwa kutuma timu ili kufanya maandilizi ya haraka ya Ligi Ndogo itakayofanyika Septemba 22 hadi 29, mwaka huu.

Ligi Hiyo ndogo inachezwa kutafuta timu mbili zitakazopanda daraja kucheza Ligi Kuu soka ya wanawake msimu wa 2017/2018.

Huu ni msimu wa pili wa ligi ya wanawake kwani msimu uliopita, timu shiriki zilikuwa 12 na Mlandizi Queens ya Pwani iliibuka bingwa wa kwanza katika historia ya soka hapa nchini.
Mara baada ya kumalizika kwa Ligi Ndogo, TFF itaanza taratibu za kupanga kuanza kwa Ligi Kuu kwani wakati huo tayari tutafahamu timu ambazo zimepanda. Ligi Ndogo haitahusisha timu ambazo zimecheza Ligi Kuu msimu wa 2016/17.

WAZIRI TZEBA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKURUGENZI MKUU WA (FAO) JOSÉ GRAZIANO DA SILVA JIJINI DAR ES SALAAM

September 06, 2017

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, leo Jumanne Septemba 5, 2017 amefanya mazungumzo na waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kikazi nchini Tanzania. 

Katika ziara hiyo Bw. Graziano da Silva atafanya mazungumzo na viongozi waandamizi wa Serikali, wadau na anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein sambamba na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed.

Ziara hii ya Mkurugenzi Mkuu inajili wakati FAO ikiadhimisha miaka 40 toka kuanza shughuli zake hapa Tanzania Hafla ambayo itahudhuriwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu Hassan. 

Katika mazungumzo na Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mkurugenzi Mkuu wa FAO anabadilishana mawazo na Serikali ya Muungano wa Tanzania kwenye masuala makuu yanayohusiana na uhakika wa chakula na maendeleo ya kilimo, ikijumuisha juhudi za FAO kitaifa na kikanda.

Pia yamejadiliwa mambo mengine yanayohusiana na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na FAO, pia masuala ya umuhimu kati ya pande hizo mbili.
Mbali ya Maafisa wa Serikali, Mkurugenzi Mkuu atakutana na wadau wengine wa FAO hapa nchini wakiwa ni pamoja na asasi za kiraia, taasisi za elimu, na taasisi za utafiti. 

Baadae Mkurugenzi Mkuu ataenda Zanzibar ambapo, miongoni mwa mambo mengine, anategemewa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Mradi wa Kuzalisha vifaranga vya samaki unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa KOICA. 

Pia Bw. Graziano da Silva atapata fursa ya kutembelea mradi wa kilimo cha mwani na pia kuona maonesho ya bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na wanawake wanaojihusisha na kilimo cha mwani. 

Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi Dkt Charles Tzeba alisema kuwa ujio wa Bw. Graziano da Silva nchini unaakisi ushirikiano bora uliopo kati ya Tanzania na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO) ambapo hivi karibuni ILO walisaidia katika kuandaa mpango wa kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa fedha ya kutengeneza programu ya kutoa maarifa kwa wananchi ya namna ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi katika kilimo.

Dkt Tzeba alisema kuwa tayari jarida limeshatengenezwa la namna ambavyo wananchi hususani wakulima katika kilimo chao wataweza kukabiliana na hali ya ukame au mafuriko kutokana na mvua zilizozidi kiwango.

Sambamba na hayo Mhe Tzeba alisema pia FAO wametoa simu 50 na Kompyuta 15 kwa wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya wataalamu wake kuwa na urahisi wa kukusanya taarifa na kuzifikisha kwa jamii.

Tanzania ilijiunga na FAO mwaka 1962, na mwaka 1977  FAO ilifungua ofisi zake hapa Tanzania. Katika miaka 40 ya uwepo wake, FAO imeisadia Serikali ya Tanzania katika kupanga na kutekeleza sera, mikakati na mipango ya kilimo hapa nchini. 

Kazi ya FAO imejikita katika kuboresha usalama wa chakula na lishe pamoja na maisha ya wakulima wadogo na hivyo kuwa chachu ya kukua kwa uchumi kupitia sekta ya kilimo. 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Kulia), akimpongeza Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya kuelezea taarifa mbalimbali zihusuzo wizara hiyo. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, kuzungumzia ujio wake nchini na ushirikiano baina ya FAO na serikali ya Tanzania. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva, akizungumzia na wataalamu mbalimbali katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi juu ya ujio wake nchini na ushirikiano baina ya FAO na serikali ya Tanzania. Kulia kwake ni Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba. leo Jumanne Septemba 5, 2017.

Wataalamu mbalimbali katika Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Kushoto) akiteta jambo na mwenyeji wake Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya kutembelea ofisini kwake. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba akipokea simu 50 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silvakwa ajili ya wataalamu wa kilimo kuzitumia kukusanya taarifa mbalimbali na kuziwasilisha kwa jamii. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba akionyesha moja ya siku kati ya 15 alizokabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva kwa ajili ya wataalamu wa kilimo kuzitumia kukusanya taarifa mbalimbali na kuziwasilisha kwa jamii. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva akiteta jambo na Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya kupokea zawadi. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva akipokea zawadi ya vinyago kutoka kwa Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba mara baada ya mazungumzo ya kikazi kumalizika. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva akiwaaga watendaji wa wizra ya kilimo Mifugo na Uvuvi mara baada ya kumalizika kwa mkutano akiwa na mwenyeji wake Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba. leo Jumanne Septemba 5, 2017.
Picha ya pamoja kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, (FAO), José Graziano da Silva (Aliyeketi kwenye kiti kulia), Waziri wa kilimo Mifugo na Uvuvi Mhe Dkt Charles Tzeba, Katibu Mkuu wizara ya kilimo Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Dkt Maria mashingo na wataalamu wengine kutoka FAO na Wizara ya kilimo.