SANJAY DUTT ATUA TANZANIA KUFANYA ROYAL TOUR

SANJAY DUTT ATUA TANZANIA KUFANYA ROYAL TOUR

September 18, 2023

 

Na John Mapepele

Msanii maarufu duniani kwenye eneo la filamu kutoka nchini ambaye ana zaidi ya wafuasi milioni mia mbili katika mitandao yake, Sanjay Dutt leo Septemba 18, 2023 ametua kuanza Royal Tour hapa nchini.

Mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na kupokewa na Mkurugenzi wa Utalii nchini Dkt. Thereza Mugobi na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Damasi Mfugale, bwana Dutt amesema ameamua kuja kutembelea vivutio vya utalii nchini kufuatia Filamu ya The Royal Tour iliyochezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuonyesha hazina ya utajiri wa vivutio vya utalii nchini.

“Naipenda sana Tanzania, naiona niifanye Tanzania kuwa nyumba yangu ya pili sasa baada ya kuitazama filamu ya The Royal Tour” amesisitiza Dutt

Aidha, amesema ameamua kuwa balozi wa kujitolea kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia mitandao yake kutokana na mapenzi yake kwa Taifa la Tanzania.

Mkurugenzi wa Utalii nchini Dkt Thereza Mugobi amefafanua kuwa Tanzania imefarijika kupata ugeni wa msanii huyo maarufu duniani kutoka India eneo ambalo lina idadi kubwa ya watu takribani bilioni 1.4 ambao ni soko la kimkakati la Tanzania.

“Ujio wa Dutt ni faraja kwetu kwa vile tunatambua itasaidia kuwa vuta wageni wengi kutoka bara la Asia ambako yeye anawafuasi wengi” ameongeza Dkt. Mugobi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Damasi Mfugale amesema Serikali itaendelea kuwakaribisha watu maarufu duniani ili wasaidie kufikia azma ya kufikisha wageni milioni tano ifikapo 2025 na kuliingizia Taifa dola bilioni Sita za kimarekani. 

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA UBUNIFU UANDISHI MATOKEO YA SENSA

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUZINGATIA UBUNIFU UANDISHI MATOKEO YA SENSA

September 18, 2023

 

Na Mwandishi Wetu – Njombe

Waandishi wa Habari nchini wameaswa kuzingatia weledi katika kuandika habari za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022.

Akifungua mafunzo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa Waandishi wa Habari wa mikoa ya Njombe na Ruvuma leo Septemba 18, 2023 mjini Njombe, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa Waandishi wa Habari wana nafasi kubwa ya kuwawezesha wananchi kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022 kujiletea maendeleo.

“Zingatieni mafunzo haya ili yawasaidie kujenga uwezo wa kufanya uchambuzi wa kina kwenye takwimu zinazotolewa baada ya Sensa ya mwaka 2022 ili zisaidie katika kukuza uchumi wa wananchi kwa kuwa watafanya maamuzi sahihi na yenye tija kwa kutumia matokeo yanayotolewa na jukumu lenu ni kuwafanya wananchi kuyaelewa,” alisisitiza Mhe. Mtaka.

Akifafanua amesema kuwa, waandishi wana nafasi kubwa ya kutumia ubunifu na mafunzo ya kuwajengea uwezo, kuwawezesha Wananchi kuongeza kasi ya kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla ikiwa watatimiza wajibu wao wa kuwahabarisha wananchi taarifa sahihi na kwa wakati.

Akiwasisitiza waandishi hao kuhusu umuhimu wa kubadilika Mhe. Mtaka amesema ulimwengu umebadilika na mahitaji yamebadilika kutokana na kukua kwa Sayansi na Teknolojia, hivyo na uandishi wa sasa unahitaji kufanya uchambuzi wa takwimu kwa usahihi ili kusaidia watakaotumia takwimu hizo kuleta matokeo chanya kwenye jamii.

Sanjari na hilo, Mhe. Mtaka amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yote watakayojifunza ili yawasaidie kuwa chachu ya kuleta mabadiliko.

Akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Mtakwimu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Israel Mwakapalala amesema kuwa mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na, uchambuzi wa takwimu za sensa kwa ajili ya habari, usambazaji wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 Kidigitali, wajibu wa Vyombo vya Habari katika kusambaza Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, majukumu ya NBS, Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 na mwongozo wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Mafunzo hayo ya siku 2 yameshirikisha waandishi wa habari takribani 70 kutoka mikoa ya Njombe na Ruvuma.

KINANA AFIKISHA SALAMU ZA RAIS SAMIA KWA WANACHI WA MBARALI

September 18, 2023

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV -Mbarali

HATIMAYE Rais Dk. Samia Suluhu Hassam amesikia kilio cha wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kuomba waendelee kuitumia kwa kilimo sehemu ya eneo la Bonde la Mto Usangu wakati hatua za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa GN28 ukiendelea.

Wananchi hao wakiongozwa na mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bahati Ndingo, viongozi wa Chama wa wilaya na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla  waliwasilisha ombi hilo kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana alipotembelea baadhi ya maeneo yenye mgogoro.

Kinana amewaambia wananchi wa Mbarali mkoani Mbeya kuwa Rais Dk. Samia amekubali ombi la wana Mbarali na kuruhusu kuendelea na kilimo kwa muda katika eneo lililozuiwa kupitia tangazo la GN 28.

Awali Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri wanane ilitoa katazo kwa wananchi waliopo katika sehemu ya eneo la bonde la Usangu kuacha kulima kwa kuwa wanaharibu vyanzo vya maji vya Mto Ruaha Mkuu ambao unapeleka maji katika Mto Ruaha.

Hivyo tangu kutolewa kwa katazo hilo wananchi wamekuwa wakililalamikia na kuomba Serikali kuliondoa katazo hilo.

Akizungumza wakati akihitimisha kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya Makamu Mwenyekiti Kinana alisema mgombea ubunge, madiwani, viongozi wa chama na wananchi walimueleza kwa nini asimuombe Rais waendelee kulima wakati suala hilo linazungumzwa.

“Nimemuomba Rais jana jioni nikamwambia wananchi wa Mbarali wanaomba waendelee kulima kwa sababu msimu unaanza mwezi ujao na Rais akasema sawa waendelee.

“Ila tu kwa yale maeneo ambayo yanavyanzo vya maji, kwa yale maeneo yote yaliyoruhusiwa mwaka jana Rais amekubali muendelee kulima,” amesema Kinana alipokuwa akielezea changamoto hiyo ambayo imeibua malalamiko mengi ya wananchi.

Kinana akielezea zaidi amesema amepata nafasi ya kupita katika baadhi ya vijiji ambavyo vina mgogoro na amekutana na wananchi ambao walimvaa na kumpa ujumbe kwani kila mtu anajua GN 28.

“Na mimi niwaahidi mambo yafuatayo la kwanza watu wote wanaioshi katika maeneo hayo waliambiwa waache kulima, wakamuomba Rais kwa sababu serikali haikua tayari waendelee kulima.

“Rais akasema anaruhusu kwa mwaka mmoja sasa jana Bahati na madiwani wawili wakanivaa wakaniambia matatizo hayajatatuliwa bado, mchakato wa tathimini bado unaendelea, fidia haijalipwa, mawe ya alama wananchi hawajashirikishwa,” amesema.

Hivyo kutokana na maelezo hayo Kinana amesema tayari amezungumza na Rais Samia na ameruhusu wananchi waendelee na shughuli za kilimo.

Akizungumzia ombi la mgombea ubunge kuhusu ujenzi wa barabara iliyokaa muda mrefu ya kutoka Lujewa, Madibila hadi Mafinga, Kinana amesema atawasiliana na wahusika (Waziri wa Ujenzi) barabara hiyo haiwezi kuishia katika makaratasi, bali ni lazima zichukuliwe hatua.

“Nimemzikiliza Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Mkoa wa Mbeya amesema hivi; shughuli za uchumi Mkoa wa Mbeya zinategemea sana shughuli za uchumi za Wilaya ya Mbarali. Ukizungumza uzalishaji Mbarali, ukizungumza matrekta Mbarali, ukizungumza viwanda Mbarali.

“Ukizungumza bodaboda Mbarali, ukizungumza vijana kujiajiri Mbarali. Lazima tuwasikilize wananchi wa Mbarali na mkoa mzima wa Mbeya,” amesema Kinana.

Kuhusu mgombea ubunge wa jimbo hilo katika uchaguzi mdogo unaofanyika leo, ameowamba wananchi kumchagua Bahati huku akieleza kuwa kura haipatikani kwa matumaini bali kwa kupiga kura.

Awali wakati akiomba kura Bahati ametumia nafasi hiyo kuelezea masuala mbalimbali yanayoendelea katika wilaya hiyo yakiwemo maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia.

Pia, amezungumzia changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo inakwamisha shughuli za maendeleo na uchumi wa wananchi wa Mbarali.





HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE SEPTEMBA 19,2023

September 18, 2023

 





































RUANGWA WAJIVUNIA RAIS SAMIA

September 18, 2023

 

Rais Samia Suluhu Hassan akiwapungia mkono wananchi alipowasili kuanza ziara wilayani humo.
Wananchi wakiwa na furaha baada Rais Samia kuwasili wilayani humo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijadiliana jambo na Mshauri wa Rais wa Siasa na Uhusiano wa Jamii, William Lukuvi wakati wa ziara hiyo.

Na Immaculate Makilika - MAELEZO 


Wananchi  wa Wilaya ya Ruangwa, Mkoa wa Lindi wameonesha kupongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na ujio wake katika Wilaya hiyo umewapa faraja.


Wakazi hao wakizungumza katika nyakati tofauti leo wilayani hapo wamesema kuwa Serikali imeboresha maisha yao kwa kuwafikishia huduma mbalimbali.


 Mkazi wa Kilimahewa Wilaya ya Ruangwa, Bi. Rahma Hokororo amesema kuwa ziara ya Rais Samia katika  Wilaya Ruangwa inawapa matumaini kuwa miradi mingi zaidi ya  maendeleo itatekelezwa kwa manufaa yao.


Pia, amemshauri Mhe. Rais Samia kuendelea kufanya kazi na kwa kuwa wao wanaunga mkono jitihada zake za kuhakikisha miradi mbalimbali inatekelezwa nchini.


" Tunayaona  maendeleo kwa macho sio kusimuliwa kwa kweli ana jitihada sana katika kutusaidia Watanzania. Kama mwanamke  ameonesha  jitihada kubwa sana, siku za nyuma tuliambiwa  wanawake hatuwezi chochote lakini yeye ameonesha  wanawake tunaweza, Watanzania tuendelee kumuamini Mhe. Rais",  amesema Bi. Rahma.



Mkazi wa Mtaa wa Likangala na mjasiriamali, Bi. Zainab Ajibu,  amesema kuwa  Ruangwa kuna umeme wa uhakika na barabara zinaendelea kujengwa hivyo wananchi hao wanapongeza jitihada hizo za Serikali.



" Mfano kuna maji, umeme na mradi wa madini unatekelezwa katika vijiji vya Namikulo, Mihewe na Matambalale, mradi huu unasaidia vijana kupata ajira za muda mfupi na lakini na kupata fedha za kuhudumia familia zao", amebainisha Bi. Ajibu.


Aidha, amesema kuwa huduma za afya ikiwemo za uzazi zimeendelea kuimarika na kupatikana  kwa urahisi na haraka  wilayani humo.


Pia, Bw. Abubakar Mkwepu amesema kuwa waanamini ujio wa Mhe. Rais  utawapa fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wajasiriamali kuuza bidhaa zao na wengine kuona fursa za uwekezaji zilizopo wilayani humo.



" Baadhi ya miradi imekamikika, mfano Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa, pia kuna vituo vya afya ikiwemo  cha Mbuyuni vimekamilika na tayari vimeanza kutoa huduma kwa kweli tunampongeza na kumshukuru Rais Samia", ameeleza Bw. Mkwepu.


Ameongeza  kuwa katika miradi ya elimu, kuna majengo ya kisasa katika kila kijiji na  wanafunzi wasoma katika mazingira bora.


Mhe. Rais Samia ameendelea na ziara yake katika Mkoa wa Lindi ambapo ataweka mawe ya msingi na kutembelea miradi mbalimbali ikiwemo  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Shule ya Sekondari ya Wasichana Lindi,  Bandari ya Uvuvi sambamba na kuzungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.


OTHMAN MASOUD AFANYA MKUTANO MAALUM WA VIONGOZI WAPYA WA ACT-WAZALENDO

September 18, 2023

 Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman ametoa wito kwa Viongozi wa Ngazi mbalimbali kuelewa dhima waliyonayo ili kuhakikisha Watu wote wa Nchi hii wanarudisha Imani ya kuishi kwa heshima na matumaini.

Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo katika Mkutano Maalum wa Viongozi Wapya wa Chama hicho wa ngazi ya Majimbo na Matawi, kutoka Mikoa ya Chake Chake na Mkoani kichama, huko katika Ukumbi wa Samael Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema kuwa lazima Safu ya Viongozi Wapya wa Chama hicho ijipange na ijitahmini kwa udhati kwa kuzingatia haja ya kutumikia umma wa watu wa Nchi hii, kwa misingi ya Amani, umoja, utulivu, maridhiano na mshikamano, pamoja na kuzingatia dhima ya kuivusha Nchi pahala ilipo, jamii ikikabiliwa na mahitaji makubwa yakiwemo ya kuirudishia heshima na malaka yake sambamba na kukabiliana na ufukara na ugumu wa maisha.

Akitolea mfano hali halisi ya maisha ilivyo katika visiwa vya Unguja na Pemba, Mheshimiwa Othman ametaja mazingira magumu yanayowakabili vijana, wazee, akinamama na watoto, pamoja na udhaifu katika mifumo ya utoaji wa huduma muhimu za kijamii, ambapo wananchi wanakosa uhakika wa mahitaji yao ya msingi ya kila siku, na hivyo kulazimika kuishi kwa kugombea sadaka.

“Haya hatukuyachagua; Nchi hii si Maskini, bali ni kutokana na kukosekana kwa Viongozi wenye maono; kukosekana kwa Viongozi walio-makini ambao ni wenye azma njema ya kuwaongoza watu kwa misingi ya haki na uadilifu pamoja na kupigania heshima na maendeleo ya watu wote”, ameongeza Mheshimiwa Othman.

“Madola mbalimbali yalipanga na yalikaa pamoja kutaka Zanzibar idhibitiwe; hayo siyo siri yapo hadharani kwani yameandikwa katika Nyaraka, na hao waliofanya hivyo sasa hawana tena haja ya kuona Zanzibar inadhibitiwa; kila zama na kitabu chake”, amefahamisha Mheshimiwa Othman akibainisha hatua mbalimbali ambazo dunia imepita pamoja na kuidhoofisha Nchi hii kiuchumi.

Akiongelea haja ya kukaa pamoja na kuwanasihi Viongozi Wapya kupitia Kikao hicho maalum, Mheshimiwa Othman amesema kuwa Chama hicho hakikuendesha Uchaguzi wa Ndani wa hivi karibuni kwa lengo la kuwapatia watu nafasi za kugombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, wala kujiwekea safu ya kuungwamkono kwa chaguzi zijazo, bali ni kutokana na kuaminiwa na umma na hivyo wajitathmini juu ya dhima ya kuwatumikia watu wote ipasavyo.

“Tuwatazameni Watu ambao walikubali kusamehe kila kitu, kwaajili kupigania maslahi ya umma na Mamlaka kamili ya Nchi; sisi kuwasaliti hata Mwenyezi Mungu hatokuwa radhi” amesisitiza Mheshimiwa Othman.

Amekaririwa akisema, “kuna waliouwawa, kuna watu waliodhulumiwa, kuna watu waliokimbilia Nje ya Nchi kwasababu ya Madhila, kuna Watu waliovunjiwa Makaazi yao; kuna Watu Waliofukuzwa kazi na Wanaodai kutokana na dhulma mbali mbali; hivyo hayo yote ndugu zangu yanaashiria tuna kazi kubwa na dhima ya kiasi gani ya kuwaongoza na kupigania heshima ya watu wote, na wala lengo siyo kujitafutia vyeo na maslahi binafsi”.

Aidha amesema, “ieleweke kwamba haya siyo ya kisiasa bali ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya watu ndani ya Nchi hii yanakoelekea hayaleti matumaini kutokana na ukosefu wa kujipanga, kushindwa kuzingatia haki na uadilifu, na pia kukosekana kwa hisia za kujali dhamana na maadili ya uongozi”.

“Na sasa kwamba tunajiandaa kwa safari lazima tufahamishane tunakotoka ni wapi, na wapi tunajipanga kuelekea”, ameongeza Mheshimiwa Othman akipongeza mwitikio wa Viongozi Wapya wa Chama sambamba na Wagombea walioshindwa kupitia zoezi la Uchaguzi huo.  

Akifahamisha juu ya mazingatio muhimu kupitia Zoezi la kuwapata Viongozi hao Wapya, baada ya Uchaguzi huo wa Ndani ya Chama hicho wa hivi karibuni, Mheshimiwa Othman amekariri ile Kaulimbiu isemayo, “tuchague mmoja tubaki wamoja”, kwa azma aliyoitaja kufuta machungu na hisia za kukata tamaa miongoni mwa Wagombea walioshindwa.

Mheshimiwa Othman amechukua fursa hiyo kuwapongeza Wanachama waliojitokeza kwa wingi kugombea Nafasi mbalimbali za Uongozi wa Chama hicho, kupitia Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani ya chama wa hivi karibuni, na pia kueleza matumaini aliyonayo kutokana na umoja, mshikamano na maridhiano ya wanachama, hali inayoashiria mwendelezo wa uimara, hasa baada ya matokeo ya kushinda na kushindwa.

“Tutoke na Misingi hii ya Uongozi mimi naamini tutafanikiwa;  kwa kufanya hivyo, sisi tumefanya darasa la demokrasia kwani safari hii tunataka tuonyeshe vipi viongozi wa kuwaongoza watu wanapatikana na vipi Nchi inaongozwa; nawaomba sote Viongozi tuwe na dhamira njema ya kuwatumikia watu ambao wametuamini”, amesema Mheshimiwa Othman akitangaza kuwa yeye binafsi hana Mgombea wa ‘mbeleko’ ndani ya Chama hicho huku akikemea tabia ya ‘double face (sura mbili)’.

Hivyo amesema wajibu wa kiongozi ni kuepusha na kutatua tatizo kwa umoja, Imani, mashirikiano, nia safi na kuvumiliana, wala siyo kulalamika na kufitinisha, huku akikariri ule usemi kwamba, “ukiona giza washa mshumaa kwani giza haliondoki kwa malalamiko”. 

Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani, amesema Safu Mpya ya Uongozi wa Chama hicho ni nyenzo muhimu kuelekea safari ya kutetea heshima ya Visiwa vya Unguja na Pemba, kupitia Uchaguzi hapo ifikapo Mwaka 2025, na kuunda Serikali ambayo Viongozi wake watajali thamani na maslahi ya watu wote bila ubaguzi.

Akikumbusha hatua mbambali za Historia ya Harakati za Mageuzi Nchini, na Machungu ambayo Wapinzani wameyapata, Bimani ameitumia fursa ya kuihutubia hadhira hiyo kubwa kuwakumbusha Viongozi hao Wapya na kuwataka waelewe kwamba, kama ilivyokuwa kwa Waasisi wa Siasa za Kutetea Mamlaka na Heshima ya Zanzibar, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Wenzake, dhamira siyo kupigania vyeo na nafasi za kuongoza, bali kuweka kando tamaa, fitna na ubinafsi, kwaajili ya Umoja wa Kitaifa na Maslahi ya Umma.

Mratib wa ACT-Wazalendo kisiwani Pemba, Bw. Said Ali Mbarouk akitoa Ripoti ya Kisiasa ya Chama chake amefahamisha kuwa hali ya kujitolea kwa hali na mali kwa wanachama, wapenzi na wafuasi wake, ni ishara ya kuendelea kwa uimara, uthibiti na utayari wa Wapemba katika kuipigania Mamlaka Kamili ya Zanzibar.

“Pemba tupo tayari Waheshimiwa, tunachosubiri ni maelekezo na miongozi ya viongozi wetu, na tunachongojea ni ushindi ifikapo Mwaka Elfu Mbili na Ishirini na Tano”, amesema Mbarouk.

Kwa upande wake, Katibu wa Chaguzi wa ACT-Wazalendo, Bw. Muhene Said Rashid amerudia kauli yake kwamba Zoezi la kuwapata Viongozi wa Ngazi zote wa Chama hicho, kuanzia Matawi yote takriban 678 na Majimbo 50 ya Unguja na Pemba, lililoanza mwezi wa Agosti, Mwaka huu, limeendelea vyema na kufikia asilimia 93.8, licha ya dharura ndogo ndogo za kibinaadamu zilitatuliwa hatimaye katika maeneo machache, ikiwemo Jimbo la Mkoani.

Mkutano huo maalum ulioanza kwa Dua iliyosomwa na Sheikh Mohamed Mbwana kutoka Chambani, sambamba na Burudani mbalimbali za Kisiwani hapa, zikiwemo za Wasanii Mashuhuri, akiwemo Vuale Omar Vuale ‘Walanlahoa’ na Yahya Hilal, umelenga katika Kuwakusanya baadhi ya Watendaji Wakuu wa wakiwemo Wenyekiti na Makatibu wa Matawi, Majimbo na Mikoa, Wabunge, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, pamoja na Kuwahutubia Viongozi Wapya wa Mikoa ya Chake Chake na Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, waliopatikana kupitia Mchakato wa hivi karibuni wa Uchaguzi, ndani ya Chama hicho.  

Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, yupo Kisiwani Pemba, kwa Ziara Maalum ya Siku 4 kwaajili ya Shughuli za Chama na Serikali, tangu aliopowasili mapema Ijumaa, na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa na Viongozi mbalimbali wa ACT-Wazalendo Kisiwani, katika Mkutano Maalum, ndani Ukumbi wa Samael Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba leo.