GAMBO CUP yaonesha njia ya soka Korogwe.

July 13, 2013
Na Oscar Assenga,Korogwe.
WILAYA ya Korogwe mkoani Tanga imeongeza mdau mwengine wa soka hali ambayo inaifanya wilayani hiyo kuwa miongoni mwa wilaya ambazo vijana wake wanapata fuksa ya kushiriki mashindano mbalimbali ambayo huwaweka vijana pamoja kwa kuinua vipaji vyao na  kuhamasishana kupenda soka.

 



 (Picha ya juu ,MKUU wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa akikagua timu zilizoingia fainali ya Mashindano ya Gambo Cup kabla ya kuanza hatua hiyo)

Upozungumzia soka wilayani hapa huwezi kuacha kuzungumzia Korogwe United,Nyota Fc ,Manundu Fc na Biashara  timu ambazo ziliwahi kuwika kwenye miaka ya nyumaa na kuufanya mji huo kuwa tishio katika medani ya soka hapa nchini lakini timu hizo licha ya kuvuma hivi sasa zimeishia kucheza Ligi za mikoa na wilaya.

 



(Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa akipiga mpira kwenye hatua ya fainali ya Mashindano ya Gambo Cup ikiwa ni kiashirio cha kuanza hatua hiyo)

Sio kwamba hapo ndio mahali ambapo timu hizo zinasema zimekwisha kuridhika na soka hilo bali wanamipango madhubuti ya kuanza huko ili kwa siku zijazo ziweze kucheza Ligi kubw nchini ikiwemo Ligi daraja la kwanza na Ligi Kuu.

 



Ndoto za vilabu hivyo kufikia hatua hiyo inaonekana itafanikiwa kutokana na uongozi imara wa chama cha soka wilayani humo wakishirikiana na Mkuu wa wilaya hiyo,Mrisho Gambo ambaye malengo yake makubwa ni kutaka siku zijazo wananchi wake kushuhudia mechi za Ligi kuu ikichezwa.

Ili ndoto hiyo iweze kukamilika,Mkuu huyo wa wilaya alianzisha Mashindano ya soka kwa Vijana maarufu " Gambo Cup"ambayo yalizinduliwa Machi 16 mwaka huu yalichezwa kwa mfumo wa Ligi na kuchezwa katika tarafa nne yakishirikisha timu 82 huku yakichezwa kwenye vituo 9 ambapo yalifunguliwa rasmi na Mjumbe wa NEC wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Bagamoyo Ridhiwani Kikwete.




Mashindano hayo yalidhaminiwa na Benki ya NMB kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani humo na kuchezwa katika vituo vya Kerenge,Old Korogwe, Makuyuni,Mombo,Korogwe, Mswaha,Bungu,Hale na Kwamndolwa ambapo yalikuwa na msisimuko wa hali ya juu kutokana na upinzani uliokuwa ukionyeshwa na timu zilizokuwa zikishiriki.

Kwenye vituo hivyo timu zilikuwa zikicheza kwa mtindo wa Ligi tukianzia katika tarafa ya Mombo ambapo timu zilicheza kwenye vituo vyake na kupata washindi kila kwenye kituo na kupata timu nane ambapo kituo cha Mombo kilikuwa na timu tatu na Makuyuni huku kituo cha Mswaha kikitoa timu mbili na baadae timu hizo zilimenyana kwa kucheza mtoano.

 




Baada ya kumalizika hatua hiyo zikapatikana timu mbili zilizoingia hatua ya robo fainali ambazo ni Reli Fc ya Mombo na Kosovo Fc ya Mswaha zote zikiwa zinatoka  tarafa ya Mombo huku Tarafa ya Korogwe ambayo ilikuwa na vituo vinne ambavyo ni Korogwe,Old Korogwe,Hale na Kwamndolwa.

Hivyo kituo cha Korogwe ilitoa timu nne ambazo ni Old Korogwe,Korogwe mbili,Hale mmoja na Kwamndolwa  ambapo timu hizo zilimenyana kwa mtindo wa mtoano hatimaye zikabaki timu mbili ambazo ni Korogwe United na Mtonga Fc.

Katika Tarafa mbili zilizobaki kwa kuwa walikuwa na kituo kimoja kikubwa zilichukuliwa kila kituo timu mbili ambapo kituo cha Bungu zilitoka timu mbili ambazo ni Bungu Kibaoni na Soya FC huku kituo cha Magoma zilitoka timu mbili  ambazo ni Kerenge Makaburuni na Muungano FC.

Timu hizo nane ndizo ambazo zilizoingia hatua ya mwisho ambapo timu hizi zilicheza kwa mtoano kuanzia robo fainali mpaka kufikia hatua ya mtoano iliyoanza June 23 mwaka huu ambapo kila timu iliweza kuchukua na mwenzie na kubaki timu nne ambazo ziliingia hatua ya nusu fainali.

Kosovo Fc,Korogwe United,Bungu Kibaoni na Mtonga Fc ndio timu zilizofanikiwa kuingia hatua ya mwisho ya mashindano hayo na hatimaye Mtonga Fc ikaweza kuibuka na ubingwa wa michuano hiyo ambayo ilikuwa na msisimuko wa hali ya juu.

 



Akizungumza baada ya kutoa zawadi kwa washindi,Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu,Chiku Gallawa alimpongeza mkuu wa wilaya hiyo kwa kuanzisha mashindano hayo pamoja na Benki ya NMB kwa kufadhili kwa kushirikiana na wadau wengine na kueleza mashindano hayo yanafaida nyingi sana kwa vijana.

Gallawa anasema mashindano hayo yampa hamasa kubwa ambapo naye amepanga kuanzisha Kombe la Gallawa Cup ambalo itashirikisha timu kutoka wilaya zote za mkoa wa

Tanga lengo likiwa ni kuinua kiwango cha soka mkoani hapa.

Aidha pia aliwapongeza NMB kuwa kudhamini mashindano hayo na kuwataka wadau wa soka wilayani humo umoja waliouonyesha katika mashindano hayo wauendeleze  mpaka kwenye shughuli za maendeleo.
 

Kwa upande wake,Mkuu huyo wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo alizipongeza timu shiriki kwa ushindani waliuonyesha kuanza ngazi ya vituo mpaka hatua hiyo ya fainali na kuwataka wadau wa soka wilayani humo kuendelee kuunga mkono michezo.

Katika taarifa yake katika ufungaji wa mashindano iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Chama cha soka wilaya ya Korogwe,Zaina Hassani alisema mashindano hayo yalikuwa ni ya aina yake na kumpongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa hatua yake ya kuanzisha michuano hiyo na kuwataka wadu wengine waige mfano huo nao wajitokeze kudhamini mashindano ya mpira .

 


Hassani alisema endapo mashindano hayo yakiwepo mara kwa mara wilayani humo yatawafanya vijana kukosa muda wa kuzurura na kujihusisha na vitendo viovu badala yake watakuwa wakitumia muda huo kwenda uwanjani kuangalia mpira.

Mashindano hayo yaligharimu sh.milioni 21,400,000 katika vituo vyote na matayarisho yake yakiwa ni 9,580,000 huku zawadi zikigharimu jumla ya sh.milioni 5,780,000 na kutoa shukrani kwa mdhamini wa mashindano waliofanikisha mashindano hayo ambao ni benki ya NMB pamoja na wadau wengine wote waliomuungana mkono.


(Zawadi za washindi katika Michuano ya Gambo Cup zikiwa uwanjani hapo)

Anasema kuwa licha ya kumalizika mashindano hayo lakini zipo changamoto mbalimbali ambazo walikutana nazo ni vilabu vilikuwa vinalalamika kupitia waamuzi hasa kwenye vituo vya vijijini kwa maana vilabu vyengine vinakuwa havifahamu sheria hivyo basi chama hicho kiliwaomba wadau wa soka hapa nchini kupitia mashindano  hayo wadau wajitoe ili kuwasaidia waweze kufanya semina za viongozi wa vijiji ili wafahamu sheria za michezo.

 



MLINDA Mlango wa timu ya Mtonga Fc akiwa amebebwa juu ikiwa ni ishara ya kumpongeza baada ya timu yao kunyakua ubingwa wa Kombe la Gambo Cup)

Katibu huyo anasema walimu wengi wanaofundisha timu za mpira wa miguu wilayani hum hawajapata mafunzo ya ualimu hivyo sheria nyengine wanakuwa hawazifahamu lakini chama hicho kimejitahidi kutafuta wakufunzi wa kuja kufundisha walimu ambapo gharama hizo ni 754,000 ambapo fedha hizo ni pamoja na malazi,chakula kwa muda wa wiki mbili wakufunzi wawili huku chama hicho kikiwa hakina pesa hivyo aliwaomba wadau hao kujitokeza kufadhili mafunzo hayo.

Mwisho.

MKUTANO TFF WAPITISHA MAREKEBISHO YA KATIBA

July 13, 2013

Na Boniface Wambura,Dar es Salaam.
Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) uliofanyika leo (Julai 13 mwaka huu) umepitisha marekebisho ya Katiba yake, hivyo mchakato wa uchaguzi unatarajia kuanza wakati wowote.

Wajumbe zaidi ya 100 walihudhuria Mkutano huo uliofanyika ukumbi wa NSSF Waterfron, Dar es Salaam na kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera aliyewataka wajumbe kuhakikisha kiwango cha mpira wa miguu nchini kinakuwa.

Mkutano huo uliokuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga umefanya marekebisho ya Katiba kutokana na maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA). James Johnson kutoka Idara ya Wanachama ndiye aliyeiwakilisha FIFA katika mkutano huo.

Aprili mwaka huu FIFA ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa TFF, na kuagiza kwanza yafanyike marekebisho ya Katiba ili kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili ambavyo ndivyo watashughulikia matatizo ya kimaadili kwa familia ya mpira wa miguu nchini.

Mbali ya kamati hizo, mabadiliko hayo pia yametengeneza ngazi mbili za kushughulikia masuala ya kinidhamu ambazo ni; Kamati ya Nidhamu na Kamati ya Rufani ya Nidhamu.

Kamati ya Utendaji ya TFF chini ya Rais Tenga itakutana leo kwa ajili ya kuteua wajumbe watakaounda Kamati hizo ili kuruhusu kuanza mchakato wa uchaguzi ambao FIFA iliusimamisha hadi vitakapoundwa vyombo hivyo.

 

TAIFA STARS YAPOTEZA MECHI NYUMBANI

July 13, 2013
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.

Taifa Stars imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya leo (Julai 13 mwaka huu) kufungwa bao 1-0 na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.

Denis Iguma ndiye aliyefunga bao hilo pekee kwa Uganda dakika moja baada ya mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi kupuliza filimbi kuanzisha kipindi cha pili cha mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

 Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema mpira wa miguu ni mchezo wa kufunga mabao ambapo timu ilipata nafasi nzuri katika dakika ya kwanza tu lakini ilishindwa kuibadili kuwa bao.

“Uganda walitengeneza nafasi moja tu katika kipindi cha kwanza wakati sisi tulikuwa nazo kadhaa. Kipindi cha pili tuliwapa nafasi wakafunga bao lao. Lakini kwa kifupi kama wao wameweza kufunga hapa (Dar es Salaam), hata sisi tunaweza kufunga Kampala,” amesema Kim akizungumzia nafasi ya timu yake kusonga mbele.

Timu hizo zitarudiana jijini Kampala kati ya Julai 26 na 27 mwaka huu ambapo mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kwenda kwenye fainali za tatu za CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini. Stars ilicheza fainali za kwanza za CHAN zilizofanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast.


Nundu aiomba serikali kufufua viwanda vilivyokufa Tanga

July 13, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
MBUNGE wa Jimbo la Tanga,Omari Nundu ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara
kuangalia uwezekano wa kuvirudisha viwanda vilivyokufa mkoani hapa ili viweze kurudi katika hali yake kama ilivyokuwa hapo zamani.

Kauli ya Mbunge huyo ameitoa wakati wa uzinduzi wa mradi wa Tanga Economic Corridor Limited uliofanywa hivi karibuni na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Mohamed Ghali Bilal ambapo amesema mradi huo mkubwa mkoa utabadilika kutokana na uwepo wa viwanda 17 ambavyo
vinatarajiwa kujengwa katika eneo la Pongwe jijini Tanga.

Nundu amesema  mradi huo utakapokamilika utawasaidia wananchi kuweza kupata ajira pamoja na kuzalisha  fuksa mbalimbali hali ambayo itasaidia kuwaondolea umaskini na kuinua kipato chao cha kila siku.

Amesema licha ya ajira kuongezeka kupitia viwanda hivyo pia itachangia ongezeko la kodi kwa serikali na kupelekea kuchangia pato la mkoa wa Tanga na Taifa kwa ujumla na kueleza lazima wananchi wafahamu kuwa mafanikio yoyote hayapatikani bila kuwepo kwa viwanda.

Katika mradi huo zaidi ya makampuni 20 yamejitokeza kujenga viwanda eneo hilo ambapo ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi desemba mwaka huu.

Mwisho.

Kuachwa Kaseja na Simba ni Jambo la kawaida-Msumari

July 13, 2013
Na Oscar Assenga,Tanga.
WANACHAMA wa Simba Mkoa wa Tanga wamesema kuachwa kwa mlinda mlango Juma Kaseja kwenye
kikosi hicho msimu huu ni jambo la kawaida ambalo linaweza kumkuta mchezaji yoyote katika medani ya soka hapa nchini.

Akizungumza blog hii,Mwenyekiti wa Matawi hayo Mkoa wa Tanga,Mbwana Msumari alisema anashangaa kuibuka maneno mengi baada ya mlinda mlango huyo kuachwa na klabu hiyo msimu huu.

Msumari alisema wanachama wa timu hiyo na wadau waliibuka na maneno mengi ambapo kila kundi lilikuja na mtazamo wake kuhusu kuachwa kwa mchezaji huyo wengine wakidai itakuwa ni pengo kubwa kwa wasifu ya walinda milango ndani ya klabu hiyo,wengine wakidiriki hata kuandamana.

Alisema wakumbuke kwamba Kaseja huyo huyo aliwahi kutoka akaenda Yanga na Simba walicheza Ligi Kuu bila matatizo yoyote na kufanya vizuri bila kuwepo mlinda mlango huyo sasa anashangazwa na watu hao.

Aidha alisema ni lazima watanzania waache usajili wa mazoea ambao unaleta athari mara kwa mara kwa timu kwani Athumani Chuji aliwahi kuachwa na Yanga akaenda Simba na Yanga wakafanya vizuri kwa hiyo mabadiliko yanapokuja kwenye soka yasizuiliwe yaachiwe kocha afanye maamuzi yake.

Msumari alisema ni vizuri maamuzi ya Kocha yasiingiliwe kwenye maamuzi yao waachwe hao ni kamati ya usajili wafanye kazi yao  na hata makocha wa timu za ulaya wanafanya mabadiliko kutoka timu moja kwenda timu nyengine.

Hata hivyo aliongeza kwa Simba la ajabu ni lipi hapo alihoji Mwenyekiti huyo huku akisisitiza maamuzi yaliyofanywa na kamati ya usajili pamoja na kocha ni sahihi yaheshimiwe kwa maslahi ya timu inawezekana wameamua kwa sababu zao ambazo sie hatuzijui na hatuwezi kuhoji.

Mwisho.