Naibu Katibu Mkuu CCM, Mpogolo aipongeza NMB kuanzisha Fanikiwa Account

July 05, 2017
Mkuu wa Kitengo cha 'Trade Finance' wa Benki ya NMB, Linda Teggisa akimweleza Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo kuhusu huduma mbalimbali ambazo zinatolewa na Benki ya NMB alipotembelea banda la banki hiyo kwenye maonesho ya 41 ya Saba Saba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo (kulia) akiuliza jambo kwa Mkuu wa Kitengo cha Trade Finance wa Benki ya NMB, Linda Teggisa (kushoto) wakati alipotembelea banda la Benki ya NMB kwenye maonesho ya 41 ya Saba Saba.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo ameipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha akaunti ya Fanikiwa kwani ina lengo la kuwagusa watu wa kipato cha chini ambao ndiyo sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania. Mpogolo ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la benki ya NMB kwenye maonesho ya Saba Saba ambapo alipata fursa ya kupata elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinatolewa na benki hiyo kubwa nchini.
Aidha, alisema kuwa akaunti hiyo ni nzuri kwa sababu ni mahususi kwa ajili ya wafanya biashara wadogo wadogo wakiwemo mama lishe, wakaanga chips, wauza magenge n.k ambao ni sehemu kubwa ya Watanzania. Akaunti hii pia inamwezesha mfanyabishara kutambulika kama mteja mfanya biashara, atakua mwanachama kweye klabu za biashara za NMB (NMB Business Club), itamwezesha kupata mkopo mpaka milioni thelathini, ina gharama nafuu za uendeshaji na ni rahisi kuifungua kwani haihitaji nyaraka nyingi. Lakini pia mteja anaweza kupata huduma katika matawi zaidi ya 200 ya NMB yaliyoenea nchi nzima.
“Akaunti ya Fanikiwa inalenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili waweze kukuza mitaji na kuendeleza kipato chao; mtu anapopata nafasi ya kupata mkopo ni njia ya kuongeza kipato cha familia na ndivyo uchumi wa taifa unavyoweza kujengwa, Mimi niwapongeze benki ya NMB kwa kuanzisha akaunti hii na niwahamasishe Watanzania watumie fursa hii kuweza kuongeza kipato kwa ajili ya maisha yao na waweze kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Mpogolo.
Vilevile, Mpogolo aliwaasa wananchi wasiogope kuchukua mikopo kwenye mabenki ili waweze kuongeza kipato, “Ni jukumu la kila mtu kumuhamasisha mwenzake aone benki ni mahali anapoweza kupata fursa za kujikomboa kiuchumi, kuendeleza ustawi wake kwani mambo kama haya zamani hayakuwepo ambayo yanagusa watu wa hali ya chini.”
“Binafsi jambo lililonigusa ni kuanzishwa kwa akaunti ambayo inagusa watu wa kipato cha chini, naona kwamba Benki ya NMB inakwenda kuwa mkombozi wa watu wanyonge kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais na serikali yake ya kuona wananchi wa kawaida na wao wanaboresha uchumi wao.”
___________________________________________________________________________________
Joachim Mushi, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN) na Mhariri Mkuu wa Thehabari.com.
Mail address:- mushi@thehabari.com/ jomushi79@yahoo.com/ info@thehabari.com
Mobile:- 0717 030066 / 0756 469470
Web:- www.thehabari.com  
         
http://joemushi.blogspot.com

KAMPUNI YA PUMA YAKABIDHI GAWIO KWA SERIKALI SH. BILIONI 7

July 05, 2017
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto), akipokea kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania Limited, Dk. Ben Moshi mfano wa hundi yenye thamani ya sh. bilioni 7 ikiwa ni gawio la  serikali yenye hisa ya asilimia 50 katika hafla iliyofanyika mjini Dodoma. Anayeshuhudia katikati ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Philippe Corsalettti.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto), akimshukuru Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania Limited, Philippe Corsalettti, alipokuwa akikabidhiwa mfano wa hundi yenye thamani ya sh. bilioni 7 ikiwa ni gawio la serikali yenye hisa ya asilimia 50 katika hafla iliyofanyika  mjini Dodoma. Kulia ni Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Dk. Ben Moshi. 
 Dk. Philip akizungumza wakati wa hafla hiyo
 Shughuli ya kukabidhi  hundi ikiendelea

 Waziri, Dk. Mpango na CEO wa Puma,  Corsalettti. wakiwa na furaha wakati wa makabidhiano. Puma naoyo imepata gawio la sh. bil. 7
 Sehemu ya wanahabari walioshiriki kwenye hafla hiyo
 Dk. Mpango akifafanua jambo kwa kusisitiza Taasisi mbalimbali za Serikali kuboresha huduma zao na kuipatia serikali gawio kubwa.
 Wanahabari wakiwa katika hafla hiyo iliyofanyika Ofisi za Hazina mjini Dodoma
 Wakiwa na furaha baada ya hafla hiyo kufanikiwa
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mpango (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya  pamoja na viongozi wa Puma, pamoja na manaibu makatibu wakuu.. Kutoka kulia ni Katibu wa Bodi ya Puma, Gibson Mgima, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dorothy Mwanyika, CEO wa Puma, Corsaletti, Mwenyekiti wa Puma, Dk. Moshi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, D. Juliana Palangyo.
 Dk Mapango akipongezana na CEO wa Puma Corsaletti pamoja na Mwenyekiti wa Puma, Dk. Moshi
 CEO wa Puma, Corsaletti akipongezana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk.Pallangyo
 CEO wa Puma, Corsaletti akipongezana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Mwanyika
 Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy Tanzania Limited, Dk. Ben Moshi (katikati) akijadiliana jambo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto) pamoja na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Puma,  Philippe Corsalettti wakati wa hafla ya kampuni hiyo kukabidhi gawio la sh. bilioni 7 kwa serikali mjini Dodoma 
 Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Puma,  Philippe Corsalettti akiagana na Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati na Madini, Dk. Pallangyo.

Mwandishi Wetu 

SERIKALI imekubali kulifanyia kazi ombi la Kampuni ya Mafuta ya Puma Energy la kutaka taasisi za umma ziwe 
zinanunua mafuta ya kampuni hiyo yenye ubia wa asilimia 50 kwa 50 na Serikali ili faida inayopatikana itumike kwenye 
kutatua changamoto za Watanzania.

Kauli hiyo imetolewa Mjini Dodoma leo baada ya Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Puma Dk Ben Moshi kutoa ombi 
hilo kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango wakati wa tukio la kampuni hiyo kutoa gawio la Sh bilioni 7 
kwa Serikali ambayo ni faida iliyopatikana kutokana na biashara ya mafuta.

Akikubali ombi hilo Dk.Mpango alisema kuwa watalifanyia kazi ombi hilo hasa kwa kutambua hata mchango wa 
kampuni ambazo zimewekeza nchini na zina ubia na Serikali huku akitoa angalizo kuwa pamoja na ombi hilo 
kufanyiwa kazi hakuna sababu ya Puma kubweteka kwani lazima ushindani uwepo ili kupatikana kwa bidhaa bora.

"Serikali tumefurahi kwa gawio hili ambalo mmelitoa kwani fedha hizi zitakwenda kuhudumia Watanzania masikini 
ambao wanahitaji kupata huduma muhimu.Hivyo niwahakikishie Puma ombi lenu nimelisikia na tunalifanyia kazi lazima tuendelee kushirikiana ili kuwa na uwekezaji wenye tija kwa nchi yetu,"alisema Dk.Mpango.

Pia alitumia nafasi hiyo kuitaka kampuni ya Puma kuendelea kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi ili mwaka ujao wa 
fedha gawio liongezeke zaidi na kuwahakikisha Serikali inalo jicho lake ambalo linaangalia kwa kampuni zote na mashirika ambayo wana ubia nayo.


Awali kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya Sh bilioni 7 kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mwenyekiti wa Bodi ya 
Puma Dk. Mosha alisema kuwa wanatambua majukumu yao kwenye kufanyabiashara ya mafuta na ndio kampuni ambayo inaongoza kwenye soko lakini ombi lao kwa Serikali ni kwamba itoe maelekezo kwa taasisi na mashirika ya umma kununua mafuta kutoka kwao.

Alisema wanaamini ombi hilo likifanikiwa wataongeza mapato na faida kwa kampuni hiyo ambayo kwa sehemu kubwa ni kama ya Serikali na hivyo gawio litaongezeka zaidi ya lilitolewa jana huku akisisitiza jukumu lililopo mbele yao ni 
kuhakikisha wanaendelea kuwa bora katika utoaji wa huduma ya mafuta nchini.

"Kampuni yetu ina ubia na Serikali, hivyo tunaomba kama Waziri utaona inafaa mtoe maelekezo maalumu ili kuzifanya 
taasisi za umma kununua mafuta kwetu.Hii itatuwezesha kupata fedha nyingi na hivyo kuongeza gawio kwa Serikali 
Tunatamani kuona tukija tena mwakani tunatoa fedha nyingi zaidi ya hizi Sh bilioni 7,"alisisitiza.

Wakati huo huo, Meneja Mkuu wa Puma Energy Tanzania Limited Philippe Corsaletti, alisema kuwa uongozi wa 
kampuni hiyo unapongeza juhudi za Rais John Magufuli ya kuhakikisha Serikali inatekeleza mikakati yake ya kukusanya 
kodi na kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje na ndani.

Pia alisema kuwa ufanisi wa kibiashara wa kampuni hiyo kwa mwaka 2016 ulikua mzuri kwa pande zote za mauzo 
pamoja na mapato. "Ufanisi wetu mkubwa unatokana zaidi na biashara ya mafuta ya ndege ambako kwa sasa sisi ndio 
tunaongoza katika soko."

Alisisitiza wakati wakitoa gawio hilo la Sh bilioni 7 kwa Serikali, jambo kubwa ambalo linawapa faraja ni juhudi za 
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais ,Dk.John Magufuli ambaye pamoja na mambo mengine ya kuleta 
maendeleo ameimarisha mfumo wa kukusanya kodi na kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje na ndani kama 
ilivyooneshwa kwenye bajeti ya 2017/2018. 

"Puma imekuwa ikifuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya tano, na kuridhishwa na utendaji wake, hivyo uongozi wa Puma Energy utaendelea kutoa ushrikiano kama ambavyo wamekua wakishirikiana siku zote.

"Pia tunafurahishwa na hatua ambazo Rais wetu anachukua katika kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zinawanufaisha 
Watanzania wote, hivyo Puma tutaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano,"alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu gawio ambalo wamelitoa kwa Serikali Meneja huyo wa Puma alisema kufikia mwisho wa 
mwaka ulioishia Desemba 31 mwaka 2016 kampuni hiyo ilitengeneza faida kabla ya kodi ya jumla ya 
Sh bilioni 35.5 na kufafanua Puma Energy iliwekeza kwa nguvu katika kipindi cha mwaka 2016 ili kuboresha 
miundombinu yake ya ndani na rasilimali zake.

"Lengo letu lilikuwa ni kuimarisha uwepo wake sehemu mbalimbali na kukuza biashara yake. Hivyo kutokana na 
mazingira mazuri ya biashara bodi ya wakurugenzi imependekeza gawio la Sh.bilioni kwa mwaka ulioishia 2016 iweze kulipwa kwa Serikali kutokana na utendaji mzuri wa kampuni.Mwaka 2015 gawio lilikua Sh bilioni 4.5 bilioni na hivyo hiyo inawakilisha ongezeko la asilimia 56 ukilinganisha na mwaka jana na hii ni sambamba kabisa na mkakati wa 
kampuni,"aliongeza.

Alitumia nafasi hiyo kuelezea majukumu ya kampuni hiyo ni masoko na usambazaji wa bidhaa za petroli ndani ya 
Tanzania na kufafanua wanao uwezo wa kuhifadhi lita za mafuta milioni  94, vituo 47 vya mafuta maeneo mbalimbali 
nchini na inahudumia viwanja vinane vya ndege.


MANISPAA YA UBUNGO YAANZISHA REJESTA YA WAKAZI KWA KILA MTAA

July 05, 2017
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akionyesha kitabu cha kutunza kumbukumbu za kusikiliza malalamiko ya wananchi katika Ofisi za serikali muda mchache mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Kibamba CCM. Leo June 5, 2017
 Mfano wa Fomu ya huduma kwa mwananchi (Fomu ya malalamiko)
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza wakati wa kuelezea dhima ya kuanzisha Daftari la wakazi wa kila Mtaa katika Manispaa ya Ubungo.Leo June 5, 2017
 Kitabu cha Kutunza kumbukumbu za kusikiliza malalamiko ya wananchi katika ofisi za serikali

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akizungumza wakati wa kuelezea dhima ya kuanzisha Daftari la wakazi wa kila Mtaa katika Manispaa ya Ubungo.Leo June 5, 2017
 Mfano wa Fomu ya Rejista ya Wakazi katika kila Mtaa

Ili kupunguza uhalifu katika Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam imebainika kuwa ni vyema kuwatambua wananchi wote na mahali wanapoishi ikiwemo kubaini wageni wote wanaowasili katika Manispaa ya Ubungo ikiwa ni pamoja na mahali wanapofikia.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Kibamba Chama Jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Kayombo amesema kuwa  kumekuwa na uhalifu kwa kiasi kikubwa katika maeneo mbalimbali Katika Manispaa hiyo jambo ambalo limetafutiwa muarobaini kwa kuanzishwa daftari la wakazi litakalobainisha wakazi wote ili kukitokea uhalifu iwe rahisi kuwabaini wahalifu hao.
Kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya Wakazi wa Mtaa ni agizo lililotolewa hivi karibuni na MKUU wa Wilaya ya Temeke Mhe Felix Lyaviva kwa Wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa za Kigamboni, Ilala, Temeke, Kinondoni na Ubungo wakati akihutubia kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda katika ufunguzi wa semina ya mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ili kuwaelimisha watumiaji wa Intaneti wapatao milioni 20 sambamba na watumiaji wa simu za mikononi wapatao milioni 40 kuwa na matumizi bora ya simu za mikononi na mitandao ya kijamii.
Mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amesema kuwa pamoja na kuanzishwa kwa Daftari la Rejesta ya wakazi wa Mtaa pia kutakuwa na Fomu ya Rufaa ya Malalamiko katika kila Mtaa sambamba na kitabu cha kutunza kumbukumbu za kusikiliza malalamiko ya wananchi katika Ofisi za serikali.

Tayari vitabu hivyo vyote vimeanza kugawanywa katika kila Mtaa ili kuanza utekelezaji wa zoezi hilo haraka iwezekanavyo.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO 
HALMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO