Na Oscar Assenga, Tanga.
MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), unaandaa utaratibu wa kuwakopesha wanachama wake sehemu ya michango yao
wanayolipa kila mwezi ili kuwasaidia kuboresha maisha na kupambana na
umasikini.
Sanjari na hilo, mfuko huo umewataka
wananchi nchini kubadili mitizamo yao ya kuchangia harusi na sherehe mbalimbali
za kijamii na badala yake wawekeze sehemu ya fedha wanazozipata, katika mifuko
ya hifadhi ya jamii.
Akizungumza katika semina ya siku
tatu kwa Jumuiya ya Wanawake nchini (UWT) inayofanyika Jijini Tanga, Meneja wa
NSSF mkoa wa Tanga, Frank Maduga, alisema kuwa mfuko huo unaandaa utaratibu
utawawezesha wananchama kukopeshwa fedha kukidhi mahitaji yao.
“Wadhamini wa mfuko wanaandaa
utaratibu ambao utawawezesha kukopa kile wanachochangia kila mwezi,hii
itawasaidia wanachama wetu kuona ni namna gani wanaweza kupambana na
umasikini,” alisema Maduga.
Alisema wananchi hapa nchini lazima
wafahamu maisha yamekuwa na changamoto nyingi hivyo suala la kuhifadhi fedha
katika mifuko ya jamii ni suala la kisheria ambalo wanatakiwa walipe kipaumbele
kwa ajili ya kuwasaidia hapo baadae.
“Wananchi lazima waweke kipaumbe
katika suala la akiba kwa maisha ya baadaye…Hii michango ya harusi wanayojali
zaidi haina faida faida wajue maisha yamekuwa na changamoto
nyingi kwa sasa ni bora wakajali na kuwekeza katika mifuko ya jamii,” alisema
Maduga.
Hata hivyo, alikemea tabia ya jamii
ya watu wa mkoa wa Tanga, kila inapofika wakati wa sikukuu na mwanzoni mwa
mwaka, wanajitoa kuchangia katika mfuko huo na kuchukua fedha zao kwa ajili ya
matuminzi ya wakati huo akieleza kwamba hayana faida.
Alisema ni vema wananchi wakaendelea
kuchangia kwa faida ya baadaye kuliko kuchangia kisha kuchukua fedha hizo kwa
lengo la kujitoa akieleza kwamba matokeo yake, hawawezi kujiwekea akiba ya
mbeleni.
Miongoni mwa wajumbe katika semina
hiyo Mbunge Viti maalum Singida,Martha Mlata aalisema mafunzo hayo yametolewa
muda muafaka kwani yameweza kuwajenga kisiasa.
Alisema kuwa watahakikisha
wanakwenda kuhamasisha wanachama ili waone umuhimu wa kujiunga na mfuko huo
kuweza kupata mafao ya uzeeni sambamba na matibabu pindi wanapougua.
MWISHO