Maktaba ya kijamii ya Martha Onesmo yafunguliwa wilayani Mwanga

January 04, 2024

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda akiongea katika hafla hiyo.

Mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Abdala Mwaipaya, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,akizungumza katika hafla hiyo.

Mwanzilishi wa Maktaba jamii ya Martha Onesmo, Jennifer Dickson, (kushoto mwenye Tshirt nyeupe) akitoa maelezo jinsi maktaba hiyo itakavyohudumia wananchi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (katikati) na viongozi wengine wa Serikali na Dini wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika viwanja vya usharika wa Kisangeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Mwanzilishi wa Maktaba jamii ya Martha Onesmo, Jennifer Dickson, (kulia mwenye Tshirt nyeupe), akitoa maelezo jinsi maktaba hiyo itakavyohudumia wananchi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, (wa pili kutoka kulia) wakati wa uzinduzi wa maktaba hiyo uliofanyika katika viwanja vya usharika wa Kisangeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.wengine pichani ni Askofu wa Dayosisi ya Mwanga Chediel Sendoro na Mbunge wa Jimbo la Mwanga Joseph Tadayo (kushoto).
Baadhi ya wageni waliohudhuria katika hafla hiyo wakifuatilia matukio .

Na Mwandishi Wetu

Maktaba mpya ya kijamii inayojulikana kwa jina la Martha Onesmo, iliyoanzishwa kwa ajili ya kuwahudumia wakazi wa wilaya ya Mwanga, imezinduliwa katika kata ya Msangeni, ambapo hafla ya uzinduzi ilifanyika katika katika viwanja vya kanisa la KKKT usharika wa Kisangeni na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali na wananchi wa eneo hilo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda. Maktaba hiyo imeanzishwa na kijana wa kitanzania anayesoma Chuo Kikuu nchini Rwanda, Jennifer Dickson.

Akiongea katika hafla hiyo,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, alimpongeza mwanzilishi wa mradi huo Bi. Jennifer Dickson, ambapo alisema maono yake, (ya Jennifer) yatachangia maendeleo ya watu wengi watakaotumia maktaba hiyo.

“Maktaba hii imekuja wakati muafaka ambapo Serikali imekuja na mabadiliko ya mfumo wa elimu yenye lengo la kuboresha elimu ya Watanzania kwa kuwa maktaba itatumiwa na wanafunzi, walimu na wakazi wengine kujiongezea maarifa”. alisema.

Aliongeza, "Jennifer maono yako yametupa matumaini kwa serikali kuwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu ni salama kwa sababu ina vijana wabunifu kama wewe; nikuhakikishie wewe na waliohudhuria hafla hii kuwa serikali itafanya kila linalowezekana ili kuhakikisha maktaba hii inakuwa endelevu".
Alisema Serikali imeanza kutekeleza mpango unaolenga kuboresha maktaba zote nchini ili kutoa fursa kwa wanafunzi, walimu na wakazi wengine wa ndani na wanaoishi nje ya nchi kupata ujuzi wa ziada na tayari imetenga takribani shilingi bilioni 2 kutekeleza suala hilo sambamba na kuboresha maktaba 22 katika maeneo mbalimbali nchini lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wanapata maarifa zaidi kupitia maktaba hizo.

Naye Mwanzilishi wa maktaba hiyo, Bi. Jennifer Dickson, alisema ameanzisha maktaba hiyo ili kutimiza ndoto yake ya muda mrefu aliyokuwa nayo kwa miaka mingi ya kuhakikisha wakazi wa vijijini wanafikiwa huduma za maktaba ili waweze kupata maarifa.

"Maktaba hii inayoitwa Martha Onesmo, ni kwa ajili ya kumuenzi bibi yangu, ni ndoto niliyoota tangu nasoma kidato cha sita, ninafuraha kuwa ndoto hiyo imetimia. Maktaba hii pia ni mchango wangu na wale walioniunga mkono, katika kuunga mkono juhudi za serikali zinazolenga kuboresha sekta ya elimu nchini".alisisitiza.

Bi Jennifer, aliendelea kusema kuwa maktaba hiyo ambayo alisema pia ina baadhi ya michango kutoka kwa wanajumuiya wa Msangeni itakuwa kituo cha mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya aina nyingine kwa ujumla itakayochangia maendeleo ya taifa na kutoa wito kwa Watanzania wote kujenga tabia ya kutumia huduma za maktaba kujisomea ili waweze kupata maarifa na kuachana na dhana potofu kuwa maktaba ni za wanafunzi, walimu na wasomi pekee.

Alitoa shukrani kwa wafadhili mbalimbali waliomwezesha kutimiza ndoto yake baadhi yake akiwataja kuwa ni pamoja na Bayport Tanzania, Barick Gold Tanzania, Dayosisi ya Mwanga ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT-MD).
Akizungumza katika hafla hiyo Askofu wa KKKT wa Dayosisi ya Mwanga Askofu Chediel Sendoro, alimpongeza Bi Jennifer, kwa ubunifu wake ambao alisema utachangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Maktaba hii ijapokuwa ipo kwenye jengo la Kanisa itatumika kwa watu wote bila kujali imani zao za kidini, lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kujiendeleza na kupata maarifa ya ziada kwa ajili ya maendeleo yake binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema.

Aidha aliwapongeza wazazi wa Bi Jennifer Dickson na Dk. Linda Ezekiel, kwa malezi mazuri ya wazazi waliyompa binti yao ambayo yalimwezesha yeye (Jennifer) kuja na maono yenye lengo la kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

"Nichukue fursa hii kuwataka wazazi wengine kuiga mfano wa wazazi wa Jennifer; pia niwasihi watoto wengine kuiga mfano wa Jennifer ili taifa liendelee kupiga hatua kupitia vijana wetu", alisema.

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof Bonaventure Rutinwa, amesema kuwa maktaba hiyo ni miundombinu ya kielimu inayomwezesha mtu wakiwemo watoto wadogo kupata elimu ya ziada kupitia usomaji wa vitabu, ambapo alisema ni vyema watoto wakaanza kusoma. kufahamishwa kuhusu umuhimu wa kutumia maktaba mapema katika hatua za utotoni.

"Tunasoma sio kupata elimu ya shule pekee bali kuboresha maisha yetu kwa ujumla na hii ni moja ya maana halisi ya kuwepo kwa maktaba kuwa;maktaba zimekusudiwa kwa ajili ya watu wote na si kwa ajili ya wanafunzi na walimu pekee",alisisitiza.

WAFANYAKAZI WA SHIRIKA LA UMOJA WA MATAIFA LA KUHUDUMIA WAKIMBIZI WAPANDA MLIMAA MREFU ZAIDI BARANI AFRIKA KUSAIDIA WATOTO WAKIMBIZI NCHINI TANZANIA

January 04, 2024

 Wafanyakazi watatu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi - UNHCR nchini Tanzania wamepanda Mlima Kilimanjaro, ambao ni mlima mrefu zaidi barani Afrika, kwa lengo la kuchangisha fedha ili kusaidia uwekaji wa vifaa vya kuzuia radi katika shule zilizopo katika kambi za wakimbizi nchini Tanzania.


Safari yao ilichukua siku sita huku hatua ya mwisho ya kufikia mita 5,895 juu ya usawa wa Bahari ikianza usiku wa manane na kumalizika majira ya mapambazuko. Mvua kubwa na radi zimeleta madhara nchini Tanzania, hasa wakimbizi.

Katika mwezi mmoja pekee mwaka wa 2023, radi ilipiga shule moja katika kambi ya wakimbizi ya Nduta na kuua papo hapo watoto 5 na kuwajeruhi watoto wengine 15. Mtoto mkimbizi mwenye umri wa miezi tisa alilazimika kupatiwa matibabu ili kuokoa maisha yake baada ya kupigwa na radi katika tukio tofauti, huku mtoto mwingine mkimbizi akiachwa na majeraha ya moto mara baada ya kupigwa na radi mwezi wa Disemba.

 "Wazo la kuchangisha fedha kwa ajili ya Watoto wakimbizi limetokana na sisi wapanda mlima kwa kuangazia mahitaji ya wakimbizi nchini Tanzania kwa kuzingatia umuhimu wa usalama wa wale ambao UNHCR inwahudumia hususani watoto.

Kwa kuzingatia hilo ilitubidi kuweka bidii ya kupanda mlima." alielezea Murithi M'nkubitu, mmoja wa wapandaji. Kwa Damla Balaban, ambaye ameshiriki kupanda mlima ameeleza namna ambavyo timu ya UNHCR ilikumbushwa mara kwa mara juu ya hali halisi ya maisha katika kambi nyingi za wakimbizi pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo licha ya mandhari nzuri ya mlima Kilimanjaro jambo ambalo liliwapa motisha katika safari yao yote.

“Kulikuwa na giza, baridi, na hatukuwa na usingizi wala njaa. Kulikuwa na changamoto za kimwili katika kupanda hadi kileleni lakini sikutilia shaka kama ningeweza kufanya hivyo au la, ilibidi nifanye. Hakukuwa na chaguo la kuacha, kwa sababu lengo lilikuwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya usalama wa watoto wakimbizi” alisema Damla.

“Kila nilipofikiria kuhusu watoto wakimbizi ambao wameathiriwa na radi na familia zilizopoteza Watoto wao nilipata moyo na Nguvu ya pekee ya kuendelea, kusonga mbele, na kamwe sikukata tamaa. Kupanda hadi kilele cha Mlima Kilimanjaro ilikuwa changamoto kubwa kwangu – nilipokuwa nikienda juu zaidi, oksijeni ilikuwa ikipungua, na nilipata shida katika kupumua,” aliongeza Yajun Hu.

Mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kuathiri watu waliolazimika kukimbia makazi yao na jamii zinazowakaribisha na kuwahifadhi. Katika miongo ya hivi karibuni, mkoa wa Kigoma ambao uko Kaskazini - Magharibi mwa Tanzania, ambako kuna kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu - umekabiliwa na hali mbaya ya hewa kama vile joto kali, mafuriko yaliyoambatana na radi pamoja na dhoruba. Kati ya shule 56 zilizopo katika kambi za wakimbizi za Nduta na Nyarugusu nchini Tanzania, shule 46 hazina vifaa vya kuzuia radi.

Hofu ya matukio ya radi kuendelea kudhuru watoto wakimbizi ni ukweli wa kutisha kwa wakimbizi wengi na waomba hifadhi kwani Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetabiri mvua kubwa zaidi na dhoruba katika miezi ijayo. Kuweka kifaa kimoja cha kizuia radi kunagharimu takribani dola 1,700 na kinaweza kuokoa maisha ya watoto wakimbizi 1,500. "Hata hivyo, tunahitaji kuharakisha uwekaji wa vifaa vya kuzuia radi ili kulinda maisha ya Watoto wakimbizi na Jamii tunayoihudumia.

Uwepo wa vifaa vya kuzuia radi utapunguza hatari za vifo vya wakimbizi, hasa watoto. Hili ni janga linaloepukika kama kwa pamoja tutachukua hatua sasa,” amesema George Kuchio, Kaimu Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania (Uhifadhi). Kwa sasa Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 240,000, wengi wao kutoka Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku zaidi ya nusu yao wakiwa ni watoto.

Kufikia tarehe 15 Desemba 2023, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 37 pekee ya rasilimali zinazohitajika ili kuweza kuwahudumia wakimbizi nchini. UNHCR inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kuchangia huduma katika kambi za wakimbizi, na hasa kuchangisha fedha kwa ajili ya vifaa vya kuzuia radi katika shule za wakimbizi. Kupoteza mtoto mmoja kwa kupigwa na radi ni sawa na kupoteza Watoto wengi kwa mara moja.

 Maelezo zaidi kuhusu namna ya kuchangia pamoja na picha yanapatikana hapa >> https://www.launchgood.com/campaign/climbing_mt_kilimanjaro_to_keep_refugee_children_safe _from_lighting_strikes_in_schools_in_tanzania#!/






 

MBUNGE LUGANGIRA ATAKA MATUMIZI YA MITANDAO KATIKA UCHAGUZI YAINGIE KATIKA SHERIA

January 04, 2024

 



MBUNGE wa Viti Maalumu, Neema Lugangira ameshauri Mswada wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi uwe na Ibara inayoongelea masuala ya Matumizi ya Mitandao katika Uchaguzi ikiwemo (Akili Mnemba - AI).

Lugangira ametoa ushauri huo leo jijini Dar es Salaam wakati akichangia kwenye mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kujadili miswada ya sheria za uchaguzi na mswada wa sheria za vyama vya siasa.

Alisema Novemba 2023, Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika (Association of African Election Authorities) ilipitisha Mwongozo wa Matumizi ya Mitandao katika Uchaguzi barani Afrika na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ni Mjumbe katika Jumuiya hiyo, hivyo itakuwa sio jambo jema kutunga Sheria ambayo inakinzana na maazimio hayo.

"Mswaada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi haijagusia kabisa suala la Matumizi katika Uchaguzi, jambo ambalo limeshathibika kuwa moja ya maeneo yenye changamoto kubwa katika chaguzi zetu," alisema

Alisema ni lazima kuangalia pia athari za teknolojia mpya kama akili mnemba “artificial intelligence” katika Uchaguzi kwa kuwa tayari dunia imekwenda huko.

"Napenda kushauri na kusisitiza Sheria hii ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi uhakikishe inaongezwa Ibara Mpya katika eneo hili la Matumizi ya Mitandao katika uchaguzi sababu Jumuiya ya Tume za Uchaguzi Afrika ambapo Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania ni Mjumbe, alisema.
MAMLAKA YA HALI YA HEWA (TMA) YATOA TATHMINI YA JOTO NCHINI

MAMLAKA YA HALI YA HEWA (TMA) YATOA TATHMINI YA JOTO NCHINI

January 04, 2024


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya tathmini ya hali ya joto na mwenendo wake katika maeneo mbalimbali nchini.

Ongezeko la joto nchini husababishwa na kusogea kwa jua la utosi sambamba na upungufu wa mvua unaojitokeza katika maeneo mbalimbali. Kwa kawaida vipindi vya jua la utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).

Aidha, wastani wa ongezeko la joto la dunia katika mwaka wa 2023 ulifikia nyuzi joto 1.40C na ulivunja rekodi na kuwa ni mwaka wenye joto zaidi katika historia ya dunia, ukichagizwa na uwepo wa El Niño na mabadiliko ya tabianchi. Kwa upande wa Tanzania, tathmini zinaonesha pia wastani wa ongezeko la joto kwa mwaka 2023 ulikuwa nyuzi joto 1.00C kwa upande wa Tanzania na pia kuufanya mwaka 2023 kuvunja rekodi na kuwa mwaka wenye joto zaidi katika historia.

Katika kipindi cha mwezi Disemba, 2023 kumekuwepo na ongezeko la joto kwa baadhi ya maeneo nchini hususan nyakati ambazo kumekuwa na vipindi vichache vya mvua. Hadi kufikia tarehe 29 Disemba, 2023 kituo cha Morogoro kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 33.9 °C ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 1.3 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Disemba. Kituo cha Tanga kiliripoti nyuzi joto 33.6 °C mnamo tarehe 01 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 1.5), Dodoma nyuzi joto 33.5 °C mnamo tarehe 19 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 2.9), Dar es Salaam nyuzi joto 33.2 °C mnamo tarehe 02 Disemba (ongezeko la nyuzi joto 1.2) na Zanzibar nyuzi joto 33.4 °C mnamo tarehe 02 Disemba, 2023 (ongezeko la nyuzi joto 1.6).

Hata hivyo, katika kipindi cha mwezi Januari, 2024 vipindi vya mvua vinatarajiwa kuendelea kujitokeza katika maeneo mengi nchini. Hali hii inatarajiwa kusababisha kupungua kwa joto katika baadhi ya maeneo hususan yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa.

MKOA WA PWANI UNALENGA YA KUANDIKISHA WANAFUNZI 51,446 DARASA LA KWANZA,NA AWALI 55,771

January 04, 2024

 Na Mwamvua Mwinyi, Pwani



Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Abubakar Kunenge amefafanua kuwa, Mkoa huo una malengo ya kuandikisha wanafunzi wa shule za awali  55,771 pamoja na wanafunzi 51,446 wa darasa la kwanza.

Ameeeleza, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2023 Jumla ya wanafunzi 25,136 wameandikishwa ikiwa ni sawa na asilimia 45.1 .

Akitoa taarifa hiyo katika kikao cha mtandao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI ambapo alisema mkoa huo, una malengo wa kuandikisha wanafunzi wa darasa la kwanza 51,446 ambapo hadi sasa wanafunzi 37,694 wameshaandikishwa, sawa na asilimia 73.3 .

Alieleza, uandikishaji wa shule za awali na darasa la kwanza unaendelea hadi kufikia mwezi Machi mwaka 2024.

Vilevile akibainisha kuhusu wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2024, alisema kwa shule za kutwa na shule Teule ya Mkoa ni 40,796 na ufaulu ukiwa ni asilimia 83.7.

Kunenge alieleza, wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza wataendelelea na masomo yao bila ya kikwazo chochote.

Kwa upande wa Miundombinu, Kunenge alieleza, mkoa umepokea jumla ya sh. Bilioni 29.7 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu.

"Ujenzi wa shule mpya 36 ,Vyumba vya madarasa 198,nyumba za walimu 13 matundu ya vyoo 269 ,mabweni 21 vituo vya walimu TRC 13 zitajengwa" Fedha hizi zimekuja kupitia miradi ya Boost, Sequip one na two kutoka Serikali Kuu, Barrick na wadau wengine"

Kuhusu miradi ya Boost ,Kunenge  alisema mkoa ulitakiwa kujenga shule 13 ambapo baadhi ya shule zimekamilika .

Kwa upande wa miradi ya Sequip shule zipo 23 na shule 19 kati ya hizo zimesajiliwa na shule nne zinatarajiwa kusajiliwa mwishoni mwa Januari 2024.


NGOTA AHIMIZA UMUHIMU WA VITEGA UCHUMI KILA WILAYA

January 04, 2024

Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Tanga Hamis Ngota akizungumza wakati wa mkutano wake na wajumbe wa umoja huo uliofanyika Jijini Tanga








Oscar Assenga,TANGA

Mwenyekiti wa Smaujata Mkoa wa Tanga Hamis Ngota amehimiza umuhimu wa ushirikiano utakaokwenda sambamba na vitega uchumi kila wilaya ambavyo vitakuwa ni chachu ya kuweza kuukwamua Jumuiya hiyo.


Mbota aliyasema hayo wakati wa mkutano wake na wajumbe wanaounda Jumuiya hiyo uliofanyika Jijini Tanga ambapo alisema hatua hiyo ni utekelezaji kwa vitendo maono ya viongozi wao wa Taifa.

Alisema viongozi wao umoja huo Taifa wameelekeza lazima kila mkoa uweze kuwa na kitega uchumi chake ambapo tayari kwa mkoa huo wameanza mchakato wa kufanikisha suala hilo.

“Viongozi wa Sumaujata Mkoa wa Tanga tujiathimini na tuhakikishe tunaunga mkono kauli mbiu ya Mwenyekiti wetu Taifa kwamba kila shujaa awe na kadi ya bima ya afya na kitega uchumi chake“Alisema

Aidha alisema kuwa wanataka kuwa na mradi katika mkoa ambao utasimamiwa na wilaya ambao utasimama ili kuweza kuwa rahisi kutekeleza miradi yao.

“Lakini kikubwa naombeni ndugu zangu mnipe ushirikiano kwa maana tuna mipango mingi mizuri ya kuukwamua umoja wetu huu kwa mkoa wa Tanga na tayati tuna mpango kazi ambao utawasaidia wanataka kwenda wapi na wanataka kufanya nini”Alisema Mwenyekiti huyo.

Hata hivyo aliwaomba ushirikiana ikiwemo kuhakikisha wanajitoa kwa nguvu zao kuhakikisha wanapata mafanikio makubwa kwani miradi itakapoanza kunahitajika usimamizi mzuri.