POLISI TABORA YANASA MAJAMBAZI WATANO NA BUNDUKI MOJA ,JAMBAZI MMOJA AUAWA KWA KUPIGWA NA WANANCHI.

July 01, 2014


Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora ACP Suzan Kaganda akiwaonesha waandishi wa habari silaha aina ya SMG iliyokamatwa ikiwa na risasi mbili pamoja na watuhumiwa watano ambapo mmoja kati ya watuhumiwa hao aliyefahamika kwa jina moja la Rajab anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30-36 alifariki dunia baada ya kushambuliwa na wananchi huko katika kijiji cha Tura wilayani Uyui. Aidha majambazi hayo yalikamatwa baada ya kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha ambapo yalifanikiwa kupora zaidi ya shilingi milioni mbili na laki tatu na ndipo makachero wa Jeshi la Polisi kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi walifanikiwa kuyakamata yakiwa na silaha hiyo ambayo imedaiwa ilitumika katika tukio la uporaji pamoja na Pikipiki mbili aina ya Sanlg
Kamanda Suzan akionesha magunia  mawili na nusu ya bhangi yaliyopatikana katika msako mkali wa Jeshi la Polisi huko eneo la Wilaya ya Nzega ambapo watu watatu wanashikiliwa kuhusiana na tukio la kuwa wauzaji na watumiaji wa bhangi.


PINDA AKUTANA NA MAMEYA NA WENYEVITI WA HALMASHAURI MJINI TANGA

PINDA AKUTANA NA MAMEYA NA WENYEVITI WA HALMASHAURI MJINI TANGA

July 01, 2014



PG4A4469
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akizungumza na baadahi ya washiriki wa mkutanono kati yake na Mameya ya Majijiji Miji na manispaa pamoja na wenyeviti wa halmashauri za miji na wilaya mjini Tanga Juni 30, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU: OMBEENI TAIFA NA UCHAGUZI MKUU UJAO

WAZIRI MKUU: OMBEENI TAIFA NA UCHAGUZI MKUU UJAO

July 01, 2014

1(5)
*Askofu Niwemugizi ataka UKAWA warudi bungeni mwezi ujao, asema siyo ombi
……………………………………………………………
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaomba viongozi wa dini kote nchini na wananchi waungane pamoja ili kuombea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumanne, Julai mosi, 2014) wakati akizungumza na maelfu ya waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya Jubilei ya miaka 25 ya Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarsicius Ngalalekumtwa katika uwanja wa Kichangani wa Kanisa Kuu la Kihesa.
“Maaskofu wote mliopo hapa, najua mnavyoipenda Tanzania… kila kanisa lina sala maalum ya kuliombea Taifa na viongozi wake, ninawaomba viongozi wetu mliombee Taifa letu ili mambo yaende salama na hasa uchaguzi wa mwakani,” alisema.
Akirejea mahubiri yaliyotolewa kwenye ibada hiyo na Mhashamu Askofu Mkuu Paulo Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Tabora ambaye alitoa mfano wa Daudi na Goliathi, Waziri Mkuu alimfananisha Goliathi na masuala ya rushwa, ubinafsi na tabia ya viongozi kutojali wananchi wa hali ya chini.
“Viongozi tusipokuwa waadilifu, tukawa wala rushwa na hatujali wananchi wa hali ya chini tutakuwa sawa na Goliathi. Nawasihi sana ombeeni Taifa hili na uchaguzi mkuu ujao ili Mungu atupe Daudi atakayeweza kuliongoza Taifa hili na kulipeleka kunakostahili,” alisema huku akishangiliwa.

MMILIKI WA MICHUZI BLOG, MUHIDIN ISSA MICHUZI AFURAHISHWA NA HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA MFUKO WA PPF KATIKA MAONYESHO YA SABASABA

July 01, 2014

Afisa Kanda Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bi Monica Mbogoni akimuhudumia mmiliki wa Mtandao wa Michuzi Blog, Ndg Muhidin Issa Michuzi wakati alipotembelea banda la PPF katika maonyesho ya Sabasaba. 
Afisa Kanda Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bi Monica Mbogoni akimuhudumia mmiliki wa Mtandao wa Michuzi Blog, Ndg Muhidin Issa Michuzi wakati alipotembelea banda la PPF katika maonyesho ya Sabasaba. 
Afisa Kanda Uendeshaji wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bi Monica Mbogoni akimkabidhi taarifa ya michango mmiliki wa Mtandao wa Michuzi Blog, Muhidin Issa Michuzi wakati alipotembelea banda la PPF kwenye maonyesho ya  38 ya Sabasaba. Pembeni wanaoshuhudia ni wafanyakazi wa mfuko wa Pensheni wa PPF.
 Meneja Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, Bi Lulu Mengele (Kulia) akimkabidhi zawadi Mmiliki wa Mtandao wa Michuzi, Ndg Muhidin Issa Michuzi wakati alipotembelea banda la PPF katika Viwanja vya maonyesho ya 38 ya biashara yanayoendelea kufanyika Jijini Dar Es Salaam.Picha Zote na Josephat Lukaza- Lukaza Blog

COUTINHO AJIPIGA KITANZI MIAKA MIWILI YANGA SC

July 01, 2014

Kiungo mshamabuliaji Andrey Marcel Ferreira Coutinho raia wa Brazil leo amesaini mkataba wa miwili kuitumikia timu ya Young Africans kwa ajili ya michuano mbalimbali ikiwemo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Tovuti ya Yanga imemnukuu Katibu Mkuu wa klabui hiyo, Beno Njovu akisema usajli wa mchezaji Coutinho ni sehemu ya muendelezo wa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu na kama ilivyokawaida wao mambo yao ni kimyakimya.
Coutinho akisani mbele ya Katibu wa Yanga SC, Beno Njovu

Coutinho ambaye alizaliwa tarehe 12 Januari 1990 amekulia kwenye mji wa Berem ambapo alianza kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Paysandu Sports Club kabla ya kwenda nchini Asia katika nchi ya Myanmar katika klabu ya Rukhapura United.
Mpaka anajiunga na klabu ya Young Africans Andrey Coutinho alikuwa akichezea timu ya Castanhal EC iliyopo kwenye Ligi Daraja la pili ambao aliweza kuichezea kwa michezo yote  ya mzunguko wa pili mwaka 2014.

Katika hatua nyingine kikosi cha Young Africans kinatarajia kuendelea na mazoezi kesho chini ya kocha Marcio Maximo katika ufuke wa Coco Beach ikiwa ni siku yake ya kwanza na jioni katika Uwanja wa Bandari Tandika kuanza kazi baada ya leo kuwa na mkutano wa ndani na wachezaji wake pamoja na benchi la ufundi.

STARS YAJIPIMA KWA BOTSWANA

July 01, 2014

Timu ya Taifa (Taifa Stars) inacheza mechi ya kirafiki na Botswana leo (Julai Mosi mwaka huu) kuanzia saa 9 alasiri kwa saa za huko.

Mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa jijini Gaborone ni sehemu ya maandalizi ya Taifa Stars kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji (Mambas) itakayochezwa Julai 20 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inatarajiwa kurejea nchini Julai 6 mwaka huu kuendelea na programu nyingine kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji.

Wakati huo huo, kutakuwa na utaratibu maalumu kwa waandishi wa habari za michezo kwa ajili ya kuripoti mechi ya Stars dhidi ya Msumbiji. Hivyo, vyombo vya habari vinatakiwa kutuma majina mawili ya waandishi watakaoripoti mechi hiyo. Mwisho wa kupokea majina hayo ni Julai 8 mwaka huu.

WACHEZAJI WATANO WAOMBEWA ITC
Wachezaji watano wameombewa Hati ya Uhamisho ya Kimataifa (ITC) ili waweze kucheza mpira wa miguu nchini na nje ya Tanzania.

Abdulhalim Humoud kutoka Simba, Crispine Odulla (Coastal Union) na Haji Ugando (Mbagala Market FC) wameombewa ITC na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ili wakacheze nchini humo katika klabu za Sofapaka, Bandari FC na Nakuru All Stars.

Vilevile TFF imemuombea ITC mchezaji Ismaila Diarra kutoka nchini Mali ili aweze kujiunga na timu ya Azam FC. TFF inafanyia kazi maombi hayo, na mara taratibu zote zitakapokamilika itatoa ITC hizo kwa wachezaji wanaokwenda nje ya Tanzania.

SERENGETI BOYS YAJINOA KUIKABILI AFRIKA KUSINI
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na mazoezi kujiandaa kwa mechi ya mashindano dhidi ya Afrika Kusini (Amajimbos).

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili itachezwa Ijumaa ya Julai 18 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Hababuu Ali Omari ameshafanya mchujo wa awali wa wachezaji wa timu hiyo kutoka 39 na kubaki na 31. Timu hiyo imepiga kambi kwenye hosteli ya TFF iliyopo Uwanja wa Karume.

MBEYA CITY, PRISONS KUJARIBU TIKETI ZA ELEKTRONIKI
Timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) za Mbeya City na Tanzania Prisons zinacheza mechi ya kirafiki Jumamosi (Julai 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza kuchezwa jijini Mbeya katika mfumo wa matumizi ya tiketi za elektroniki kwa washabiki wanaoingia uwanjani itaanza saa 10 kamili jioni.

Kiingilio ni sh. 3,000 kwa majukwaa yote ambapo tiketi zimeanza kuuzwa leo (Julai Mosi mwaka huu).

Wakati huo huo, keshokutwa (Julai 3 mwaka huu) kutakuwa na mafunzo ya matumizi ya tiketi za elektroniki yatakayofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuanzia saa 3 asubuhi.

Washiriki wa mafunzo hayo ni wasimamizi wa mechi katika uwanja huo, viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), meneja wa Uwanja wa Sokoine na msaidizi wake, makatibu wa Tanzania Prisons na Mbeya City, maofisa habari wa Mbeya City na Tanzania Prisons, Ofisa Usalama wa MREFA na wasimamizi wa milangoni (stewards).

BONIFACE WAMBURA MGOYO
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)