WATANZANIA WATAKIWA KUCHANGAMKIA UNUNUZI HISA ZA AWALI ZA VODACOM

April 14, 2017
Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma

Serikali imewataka watanzania kuchangamkia fursa ya ununuzi wa asilimia 25 ya hisa za awali za kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom zinazouzwa kwa watanzania pekee ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya fedha ya mwaka 2016 kwa lengo la kuwawezesha watanzania kuwa wamiliki makampuni ya simu za mikononi hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma leo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bi Beng’i Issa amesema hi ni fursa kubwa na muhimu kwa watanzania kuwa sehemu ya wamiliki wa makampuni ya simu za mikononi kupitia ununuzi wa hisa hizi za awali.

‘’Ni uwekezaji ambao ni salama sana na hauna hasara, kwa kuwa ukiwa hutaki kuendelea kuwa mwanahisa unauza hisa zako na kurudisha pesa zako na unaweza kupata faida’’.

Ununuzi wa hisa hizi utawawezesha Watanzania kuwa wamiliki wa kampuni, watapata gawio la faida, wanaweza kutumia hisa kama dhamana za mikopo benki na wanaweza kuziuza hisa wanapokuwa na shida ya fedha.

Hisa hizi zinauzwa kwa mtanzania mmoja mmoja, watumishi walioajiriwa, wastaafu, makampuni yanayomilikiwa na watanzania, mashirika ya kitanzania, VICOBA, SACCOS, vikundi vya kijamii, wanawake na vijana. Aidha hisa moja inauzwa kwa shilling 850 na kiwango cha chini cha ununuzi ni hisa 100 na hakuna kikomo cha juu cha ununuzi wa hisa.

Baraza linatoa rai kwa Mashirika ya Hifadhi ya Jamii Nchini, Taasisi za fedha, Vikundi vya fedha vya kijamii kuwezesha wanachama na wateja wao kununua hisa hizi za awali.

Ununuzi wa Hisa hizi unapatikana kupitia matawi ya benki ya NBC, NMB, CRDB nchi nzima, mawakala wa soko la Hisa la Dar es Salaam, M-PESA na matawi mbali mbali ya benki za biashara nchini.

Baraza linawahamasisha watanzania wote kuchangamkia fursa hii muhimu ili kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wao na kufikia ndoto ya kuwa Taifa la uchumi wa kati kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Mwaka 2025.

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi linashirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari kama radio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii kuhamasisha watanzania kunua hisa hizi za awali.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani)kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’i Issa akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bw. Edward Kessy, akitoa ufafanuzi wa namna ya kununua hisa hizo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I Issa (hayupo pichani) alipokuwa anatolea ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifatilia kwa makini maelezo ya Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bi. Beng’I Issa (hayupo pichani) alipokuwa anatolea ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kununua hisa kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango mkoani Dodoma.(Piha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).

CHUO CHA SHENYANG CHA CHINA CHATOA UFADHILI KWA AIR TANZANIA NA NIT

April 14, 2017
Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii

Chuo kikuu cha shenyang kutoka nchini China kimeahidi kutoa ushirikiano na Shirika la ndege la Air  Tanzania kwa kutoa msaada wa kuwasomesha wafanyakazi wa kampuni hiyo,ili waweze kumudu ushindani wa soko la kimataifa.

Hayo yamesemwa na mwalimu wa malezi wa chuo cha Shenyang, Shi Guangda katika mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Global Education Link kwa wazazi ambao watoto wao wanasoma urubani na Masuala ya anga katika chuo hicho.

“Tangu Rais wetu wa China alipofika hapa tumekuwa na mahusiano makubwa na nchi hizi mbili, hivyo kwa kuanza kama chuo chetu tutatoa ufadhili kwa wafanyakazi wa shirika la ndege la Air Tanzania na kubadilishana mafunzo katika chuo cha usafirishaji cha NIT na Shenyang” Amesema Guangda .

Kwa upande wa Mkurugenzi mkuu wa shirika la ndege la Air Tanzania,Ladislaus Matindi ameishukuru tasisi ya Global Education Link kwa  kuwaunganisha na chuo hicho ambacho kwa sasa kimekuwa msaada mkubwa kwa kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa shirika hilo.

Matindi ametaja kuwa upatikanaji wa nafasi hiyo itasaidia kutoa motisha kwa vijana wetu ambao wanafanya kazi katika shirika hilo na wengine ambao wako nje kuwa na hamu ya kusoma masuala ya usafirishaji .

Kwa upande wake mkurugenzi wa Global Education link , AbduMalik Molell alitumia fursa hiyo kuzungumza na wazazi hao juu ya swala la bima ya wanafunzi amabo wanasoma chuo hicho katika swala zima la matibabu na majanga mengine ambayo yatawakuta wanafunzi.


Mkurugenzi wa Global Education Link, AbdulMalik Mollel akimkabidhi hati ya ufadhili wa masomo Mkurugenzi wa shirika la ndege nchini Air Tanzania,Ladislaus Matindi kwa ajili ya wafanyakazi wa shirika hilo watakotakiwa kwenda kusoma China
Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la Air Tanzania Ladislaus Matindi akizungumza na wazazi ambao watoto wao wanasoma masuala ya Anga nchini China
Mkurugenzi wa Global Education Link, AbdulMalik Mollel akifafanua jambo kuhusu masuala ya bima ya matibabu kwa wazazi ambao wamefika katika mkutano huo

WAKAZI WA JIJI LA MWANZA KULIPOKEA TAMASHA LA "NYANZA FESTIVAL" KWA KISHINDO.

April 14, 2017
Judith Ferdinand, BMGHabari
Wakazi wa Jiji la Mwanza na viunga vyake, wanatarajia kupata burudani ya kukata na mundu kutoka kwa wasanii mbalimbali Kanda ya Ziwa katika tamasha la burudani "Nyanza Festival 2017".

Burudani hiyo ambayo itakua ya aina yake kwa kuwakutanisha wasanii kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, itafanyika Siku Kuu ya Pasaka kuanzia saa nne asubuhi mpaka majogoo kwa kiingilio cha shilingi 5,000 tu katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Mratibu wa tamasha hilo, Fabian Fanuel, amesema mbali na burudani ya mziki pia kutakua na mchezo wa mpira wa miguu kati ya  Waandish wa habari za michezo Kanda ya Ziwa LASPOJA Fc na Bongo Movie, na Madjs na Watangazaji wa vipindi vya burudani watacheza na wafanyakazi wa halmashauri ya Jiji la Mwanza.
   
Naye Afisa Habari wa tamasha hilo, George Binagi, amebainisha kwamba wanatasnia wa burudani hususani wanamuziki mastaa na chipukizi kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, wameahidi kudondosha burudani kali siku hiyo.

"Zaidi ya wasanii 30 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa tayari wamethibitisha kupanda jukwaa la Nyanza Festival 2017 hivyo niwasihi wapenzi wa burudani wakae tayari kwa burudani hiyo ambapo kiingilio itakuwa elfu tano tu". Amesema  Binagi.

Nyanza Festival ni tamasha lililoasisiwa na Wanatasnia mbalimbali kutoka Kanda ya Ziwa wakiwemo wanamuziki, watangazaji, waandishi wa habari, Madjz na wadau wengine wengi kupitia umoja wao wa Mwanza.Com chini ya kampuni ya Famara Entertainment, lengo likiwa ni kuukuza na kuuendeleza zaidi muziki wa Kanda ya Ziwa.
MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME CHA MTERA

MAKAMU WA RAIS ATEMBELEA KITUO CHA KUFUA UMEME CHA MTERA

April 14, 2017
LUI1
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea taarifa ya kina cha maji katika kituo cha kufua umeme cha Mtera kutoka kwa Meneja wa Kituo hicho Mhandisi John Sikauki wakati akiwa njiani kuelekea Dodoma baada ya kumaliza shughuli za kuzindua Kikosi Kazi  cha Taifa cha kunusuru ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu mjini Iringa. (PichA na Ofisi ya Makamu wa Rais)
LUI2
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafanyakazi wa kituo cha kufua umeme cha Mtera akiwa njiani kuelekea Dodoma baada ya kumaliza shughuli za kuzindua Kikosi Kazi  cha Taifa cha kunusuru ikolojia ya Bonde la Mto Ruaha Mkuu mjini Iringa. (PichA na Ofisi ya Makamu wa Rais)