Na Twahiru Mdimu,Dodoma.
TIMU ya Mpira wa Miguu ya
Halmashauri ya Jiji la Tanga leo Imefanikiwa kukata tiketi ya kucheza hatua ya
nusu fainali ya mashindano ya Serikali za Mitaa nchini (Shimisemita)baada ya
kuibamiza Mtwara Mikindani mabao 2-0,kwenye mchezo wa robo fainali uliochezwa
dimba la Jamhuri mkoani Dodoma.
Mchezo huo ambao ulikuwa
wa aina yake huku timu ya Halmashauri ya Jiji la Tanga ikionekana kuutawala
kipindi cha kwanza na cha pili kwa kucheza kwa umakini mkubwa na kufanikiwa
kuandika bao lao la kwanza ambalo lilifungwa na Ibrahim Mustapha katika dakika
ya 8.
Mpaka timu zote
zinakwenda mapumziko,Halmashauri ya Jiji la Tanga ilikuwa ikiongoza katika
mchezo huo ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikionekana
kujipanga vema .
Wakionekana kucheza kwa
umakini na umahiri mkubwa Halmashauri ya Jiji la Tanga waliweza kupeleka
mashambulizi mara kwa mara langoni mwa Mtwara Mikindani na kufanikiwa kupata
bao lao la pili kwenye dakika ya 80 ambalo lilifungwa nyota wa mchezo huo
Ibrahim Mustapha.
Akizungumza na Tanga Raha
mara baada ya kumalizika mchezo huo,Mweka Hazina wa timu ya Jiji la
Tanga,Twahiru Mdimu aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo kwa kuendelea kulipa
heshima jiji hili kwa kufanya vizuri kwenye michezo yao wanayokuwa wakicheza.
Licha ya kuwapongeza
wachezaji hao ,aliwataka kuhakikisha wanaendelea kuilinda heshima ya jiji la
Tanga kwa kufanya vizuri kwenye mechi yao ya
nusu fainali ambayo itachezwa kesho kati yao
na timu ya Kyela.
Akizungumzia hali za
wachezaji wa timu ya Tanga,Mdimu alisema wanaendelea vizuri isipokuwa wachezaji
wawili ambao wamepata majeraha katika mechi yao ya leo ambapo ni Daudi Kiweri.