NAPE ASEMA WANAOHAMA CCM NI SAWA NA MAFUTA MACHAFU...AMTAKIA KILA LA HERI EDWARD LOWASA

August 04, 2015
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema wanachama waliokihama chama hicho wamejivua nguo mbele za watu na kwamba wapinzani wanaowachukua wanahangaika na mafuta machafu.
Aidha, amesema aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Mahanga, alikuwa anatafuta sababu za kuihama CCM na anamtakia kila la heri, yeye na rafiki yake, Edward Lowassa.

Nape aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es Salaam, alipotakiwa kueleza kuhusu kuhama kwa Lowassa na Dk Mahanga ambao wote kwa nyakati tofauti wamekimbilia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Lowassa alijitoa CCM wiki moja iliyopita baada ya kukwama uteuzi wa CCM wa kuwa mgombea wake wa urais na kukimbilia Chadema ambako anatarajiwa kuwa mgombea wake wa urais na kuungwa mkono na Umoja wa Vyama vinne vya Upinzani (Ukawa).
Dk Mahanga naye alijitoa juzi baada ya kukwama katika kura za maoni jimboni Segerea. “Wanahangaika na oil chafu. Hawa ni wale wale kama ilivyokuwa Mrema (Augustino) mwaka 1995, akabebwa kiasi cha Mwalimu Nyerere kusema mwacheni abebwa.
"Hebu jiulizeni wanaona ubaya wanapotoka, lakini mambo yakiwanyookea hawasemi, wakitoka ndio maneno mengi,” alisema Nape.
Alisema kuondoka kwa Lowassa na wengine wachache, si jambo la kwanza kutokea CCM, na pia si la ajabu wala haliwezi kuwa la mwisho huku akimtuhumu Dk Mahanga kuwa alikuwa akitafuta sababu ya kuondoka CCM.
Akizungumzia mchakato wake Mtama, Nape alisema kulifanyika juhudi kubwa za mafisadi kuhakikisha anashindwa, lakini anashukuru ameshinda na kwamba endapo atapitishwa na chama hicho kugombea ubunge, ana hakika atashinda kwani ni mwadilifu na anayezingatia ya chama hicho ikiwamo kupiga vita rushwa.

ZUTTAH, COUTINHO WATUPIWA VIRAGO YANGA SC, BEKI MTOGO, MIDO LA ZIMBABWE MBIONI KUTUA JANGWANI

August 04, 2015

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
BEKI Mghana Joseph Tetteh Zutah na kiungo Mbrazil Andrey Coutinho wanaweza kutemwa Yanga SC kupisha wachezaji wengine kabla ya dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa wiki.
Dirisha la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa Agosti 6, mwaka huu na baada ya hapo kutakuwa na nafasi ya kusajili wa wachezaji huru tu kwa wiki moja ya mwisho kabla ya kuanza msimu mpya. 
Baada ya Yanga SC kutolewa katika Robo Fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imekitathmini kikosi chake na kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
Joseph Tetteh Zuttah (kulia) na Andrey Coutinho (kushoto) wote wapo hatarini kutemwa Yanga SC

Coutinho alijiunga na Yanga SC msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
Mbrazil huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
Zuttah amesajiliwa Juni mwaka huu kufuatia kupendekezwa na kocha Pluijm, lakini baada ya wiki mbili za Kombe la Kagame, uongozi umeona hana umuhimu.
Mbali na Sherman, Coutinho na Zuttah wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Mkongo, Mbuyu Twite, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
Yanga SC ilifungwa kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Robo Fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC wiki iliyopita na tathmini ya baada ya mashindano, inaonyesha timu inahitaji marekebisho madogo. 
Na kwa kuona uimara wa Azam FC iliyotwaa Kombe la Kagame mwishoni mwa wiki na namna wapinzani, Simba SC wanavyojiimarisha, Yanga SC imeona kuna umuhimu wa kuleta wachezaji wengine bora zaidi kuchukua nafasi za Coutinho na Zuttah.
Nahodha wa FC Platinum ya Zimbabwe kiungo, Thabani Kamusoko, tayari yuko kwenye rada za Jangwani achukue moja ya nafasi hizo mbili. 
Aidha, wakala Mganda, Gibby Kalule aliyewahi kuwauzia Yanga SC, mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman amependekeza beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou mwenye umri wa miaka 29 anayechezea Goyang Hi FC ya Korea Kusini.

TASWIRA MBALI MBALI KATIKA MKUTANO MKUU WA CHADEMA UNAOFANYIKA KWENYE UKUMBI WA MLIMANI CITY, JIJINI DAR LEO

August 04, 2015

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Freeman Mbowe (wa nne kulia) akiwa ameshikana mikono na Mgombea wa Urais alieteuliwa na chama hicho, Mh. Edward Lowassa (wa tatu kulia) pamoja na Mgombea Mwenza wake, Mh. Dkt. Juma Haji Duni (mwenye suti nyeusi) pamoja na wanachama wapya wa Chama hicho, wakati wakitambulishwa kwenye Mkutano Mkuu wa Chama hicho, unaoendelea kufanyika hivi sasa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.
Picha ya pamoja.