WIZARA YAAHIDI KUBORESHA,KUIMARISHA MICHEZO

February 26, 2024

 Ikiwa ni saa kadhaa baada ya kumalizika kwa mashindano ya mbio zilizojipatia umaarufu kuliko mbio za nyikani, "Kili Marathon 2024", Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ukiongozwa na Katibu Mkuu wake Balozi Dkt. Samwel Shelukindo umewapongeza wanariadha wa Wizara walioshiriki mbio hizo na kuahidi kuboresha mazingira ya michezo wizarani.


Akiongea na wanamichezo hao mjini Moshi, baada ya kumalizika kwa mashindano ya Kili Marathon 2024, Dkt. Shelukindo alisema kuwa michezo ni afya, hivyo watumishi wanapaswa kujituma kufanya mazoezi mara kwa mara siyo tu kwa ajili ya kuimarisha afya zao bali kuwawezesha pia kushiriki michezo mbalimbali ndani na Nje ya nchi.

"Natambua kuwa ndani ya Wizara yetu kuna watumishi wenye vipaji tofauti, nawasihi pamoja na ufinyu wa muda mlionao mjitahidi kufanya mazoezi ili muweze kumudu ushindani wa michezo mbalimbali na kuipaisha Wizara yetu ndani na Nje," alisema Dkt. Shelukindo

Kwa upande wake, Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen Mbundi aliwapa hamasa wanamichezo ya kuongeza idadi ya michezo wizarani ili kupanua wigo wa watumish kushiriki na kuitaja michezo hiyo kuwa ni pamoja na mpira wa kikapu, mpira wa tenesi, michezo ya Jadi na ndondi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Said Shaibu Mussa aliwataka wanamichezo wa Wizara kuendelea kujituma kwa bidii na kuwa na nidhamu ya mazoezi ili kuwawezesha kushinda michezo wanayoshiriki na kuipeperusha bendera ya Wizara vizuri kwenye kila mashindano wanayoshiriki ikiwa pamoja na kuwahimiza kuandaa bonanza za michezo yatakayoshirikisha wadau tofauti ili kuimarisha mahusiano, kukuza diplomasia ya michezo hatimaye kutangaza Wizara.

Awali akiongea katika kikao cha Viongozi na wanamichezo, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo Wizarani (Nje sports Club), Bw. Ismail Hamidu Abdallah aliushukuru Uongozi wa Wizara kwa kuwawezesha na kuwapa motisha wakati wote wanaposhiriki katika michezo mbalimbali.

"Tunawashukuru Viongozi wetu kwa kutuwezesha wanamichezo, kwa kweli kwa ushirikiano tunaoupata kutoka kwenu tunaahidi kuendelea kujituma kwa bidii katika michezo na kuipaisha vyema bendera ya Wizara," amesema Bw. Ismail

Wanamichezo wa Wizara wamegawanyika katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete kwa wanawake, volleyball, mchezo wa kuvuta kamba pamoja na riadha.



SERIKALI YABORESHA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI

February 26, 2024

 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida, amasema serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa ya Kisera na Kisheria ili kujenga mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji nchini.


Dkt. Kida, amesema hayo leo Februari 26, jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na Bi. Joy Basu, Makamu Msaidizi wa Shughuli za Serikali ya Marekani, Ofisi ya Ustawi wa Biashara Afrika, kwa niaba ya Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji.

“Tunafanya maboresho ya kisera na sheria zetu, na tunatunga mpya nyingine ili kuondoa vikwazo kwa wawekezaji” alisema Dkt. Kida.

Maboresho hayo, yanakwenda sambamba na kuhamisha mfumo wa analojia ambao awali ulimtaka mwekezaji kutembelea taasisi zaidi 10 ili kukamilisha taratibu za kuwekeza nchini.

“Tumetengeneza mfumo wa kidigitali wa Dirisha la Mahali Pamoja (TeIW), mfumo huo unajumuisha taasisi saba (7) na tunafanyia kazi taasisi nyingine tano(5), ili kumwezesha mwekezaji kukamilisha taratibu mbalimbali za uwekezaji kwa njia ya kidigitali, kwa kuwa mifumo hiyo inasomana”.

Akibainisha maboresho mengine makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Kida ameeleza kuwa ni kuundwa kwa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji inayojumuisha taasisi nne ambazo ni; Tume ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), Kituo cha Uwekezaji (TIC), na Mamlaka ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA), hatua inayorahisisha uratibu wa shughuli za Mipango na Uwekezaji nchini .

“Tumefanya maboresho mengi na tunaendelea, nina hakika ndani ya muda mfupi vikwazo vingi vitakuwa vimeshughulikiwa kwa kiwango kikubwa, na hivyo kuwapa uhakika zaidi wawekezaji” Alisema, Dkt. Kida.

Kwa upande wake Bi. Joy Basu, amesema nia yao ni kuona namna gani Tanzania na Marekani zitaongeza ushirikiano wenye tija katika maeneo mbalimbali ya uwekezaji nchini.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amefanya wasilisho la fursa mbalimbali za kiuwekezaji, maeneo mahususi ya fursa hizo, kiwango cha mitaji, vigezo vya kuwekeza, na motisha za kuwekeza nchini.

Tangu mwaka 1997 hadi 2023, miradi zaidi ya 296 ya uwekezaji wenye ushirika wa Marekani imesajiliwa nchini, na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi ziizosajili miradi mingi nchini kupitia TIC.

TAWA IMELETA MAPINDUZI MAKUBWA KATIKA SEKTA YA UTALII KILWA - DC KILWA

February 26, 2024

 






Na. Beatus Maganja
MKUU wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Emil Ngubiagal amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ni taasisi iliyoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii na kuwa chanzo kikubwa cha mapato ya Serikali na wazawa wa wilaya hiyo kutokana na maboresho ya miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara yanayopelekea watalii wengi kutembelea Hifadhi hiyo.

Komredi Ngubiagal ameyasema hayo Februari 25, 2024 akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo ikiwa ni siku moja baada ya meli iliyobeba watalii 146 kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara.

"Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya sita kwa kuona sasa utalii katika wilaya ya Kilwa ni vyema tupeleke taasisi inayoitwa TAWA ili kusudi ikasimamie, ikaendeleze, ikaboreshe hii Sekta nzima ya utalii ya wilaya ya Kilwa" amesema Mhe. Christopher Ngubiagal

"Kwakweli kwasasa hivi unavyoona maendeleo makubwa katika Sekta hii ya utalii Kilwa yameletwa na Taasisi ya TAWA, Leo ukifika Kilwa kisiwani utaona mabadiliko makubwa katika miundombinu" ameongeza Mkuu huyo wa wilaya.

Mhe. Christopher amesema awali kabla ya ujio wa TAWA wakazi wa wilaya yake pamoja na watalii walikuwa wakipata adha ya kufika Kilwa kisiwani kutokana na uduni wa miundombinu lakini baada ya kuingia TAWA walipeleka boti za Kisasa ambazo zinawafanya watalii na wazawa hao kufika hifadhini kwa raha mstarehe.

Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza soko la utalii aliposhiriki filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kutokea.

Naye Said Amri Said mkazi wa Kilwa kisiwani amekiri kuwa ujio wa TAWA katika Hifadhi hiyo umechangia kuongeza idadi ya watalii ambapo kupitia wageni hao wakazi wa eneo hilo wananufaika kiuchumi kwa kufanya biashara ndogo ndogo ambazo zinawaingizia kipato.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya hiyo kutumia fursa ya ujio wa Meli za watalii kujiongezea kipato kwa kuuza bidhaa pendwa kwa wageni kama vile vitu mbalimbali vya asili na kiutamaduni.

MAJALIWA: RAIS SAMIA NI KINARA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CCM

February 26, 2024

 

WAZIRI MKUU na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kinara katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

“Ni ukweli usiopingika kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama chetu amekuwa kielelezo cha mafanikio makubwa yanayofikiwa na nchi yetu kwa sasa.”

Amesema tangu Dkt. Samia ashike madaraka ya Urais, ameendelea kutekeleza miradi yote ya kimkakati kama Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ilivyoelekeza.

Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo, (Jumapili 25, Februari 2024) katika Mkutano Mkuu wa CCM Jimbo la Kavuu, uliofanyika kwenye shule ya sekondari ya Mizeng…








RC GEITA AWAFUNDA WAHITIMU WAPYA WALIOJIUNGA GGML

February 26, 2024

 

Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela akizungumza katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo mbalimbali wasio na ajira ambao wamepatiwa fursa ndani ya GGML kupata mafunzo tarajali kwa muda wa mwaka mmoja sambamba na wahitimu 10 wa mafunzo huo kwa mwaka jana ambao wamepata ajira ya kudumu ndani ya kampuni hiyo.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela akisalimiana na akamu Rais Mwandamizi - Kitengo cha masuala ya Ubia/ushirika Afrika kutoka AngloGold Ashanti - GGML, Terry Strong na Meneja Mwandamizi wa masuala ya Rasilimali watu kutoka GGML, Charles Masubi.


NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela ametoa wito kwa wahitimu wa vyuo vikuu waliojiunga na program ya mafunzo tarajali katika Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), kujituma kwa bidii, kuwa wabunifu na nidhamu.

Pia ametoa wito kwa wahitimu hao, kutumia fursa zinazopatikana ndani na nje ya mgodi huo ili kujiendeleza na kuondoka wakiwa tofauti na namna walivyoingia kwenye program hiyo ya mwaka mmoja.

Shigela ametoa wito huo hivi karibuni mjini Geita katika hafla ya kuwakaribisha wahitimu 40 wa vyuo vikuu ambao wamejiunga na GGML kwa mwaka 2024/2025 kupata mafunzo tarajali sambamba na wahitimu wengine 10 wa program hiyo kwa mwaka jana ambao wameendelea na mafunzo ya juu zaidi baada ya kupata ajira ya kudumu ndani ya GGML.

Wanafunzi hao 10 waliomaliza program mwaka jana, wamechaguliwa kuendelea na program mpya inayofahamika kwa jina la African Business Unit Graduate (ABU) ambayo inawapa fursa ya kubadilishana uzoefu na wahitimu wa aina hiyo katika nchi nyingine za Ghana na Guine ambako AngloGold Ashanti kampuni mama ya GGML inamiliki migodi.

Shigela alisema nidhamu kwa wahitimu hao ni msingi muhimu katika utumishi wa aina yoyote hivyo wanapaswa kuzingatia nidhamu katika utendaji wao na hata wanapokengeuka kutekeleza majukumu yao nafsi inapaswa kuwasuta.

Alitoa mfano kuwa wapo wanafunzi ambao walienda kupata mafunzo tarajali ndani ya kampuni hiyo, na kufanikiwa kupata leseni za uchimbaji kwa ngazi mbalimbali nje ya mgodi na sasa ni matajiri.

Pia alisema kwa kuwa mzunguko wa manunuzi ya ndani ya GGML yanakaribia Sh trilioni moja kwa mwaka hasa ikizingatiwa kampuni hiyo inazingatia matakwa ya sheria ya ‘Local content’ ambayo inaitaka kufanya manunuzi ya bidhaa zake hapa nchini, nayo ni fursa nzuri kwa wahitimu hao kujifunza na kufungua kampuni za kusambaza bidhaa kwa mgodi huo.

Mbali na kuipongeza GGML kwa kuwa na mipango madhubuti inayofungua fursa kwa vijana wa kitanzania, pia aliwapongeza wahitimu hao ambao wamefanikiwa kupenya na kupata nafasi hiyo hasa ikizingatiwa walioomba nafasi hiyo walikuwa 2,800 lakini wamechaguliwa 40 pekee.

Naye Meneja Mwandamizi anayeshughulikia masuala ya rasilimali watu, Charles Masubi alisema program hiyo ya ABU ambayo inahusu wahitimu 10 wa mwaka jana itawawezesha kupata mafunzo ya juu zaidi ya ujuzi wao wa darasani.

“Kama ni mhandisi tutamfundisha namna ya kuingia makubaliano, kuandaa bajeti  lakini pia kupata ujuzi wa namna ya kuwasiliana kwa usahihi na wenzake,” alisema.

Alisema lengo la program hii ni kuwaandaa wafanyakazi wabobezi ambao wanaweza kuja kuwa viongozi wa baadae wa kampuni hiyo na hata nje ya GGML.
 
Mmoja wa wahitimu aliyepata fursa ya mafunzo tarajali kwa mwaka huu, Fakii Juma alisema GGML ina matarajio makubwa kwao katika uzalishaji hivyo watatumia vipaji vyao kuongeza ujuzi kwenye mgodi huo kutokana na elimu wanayoipata na wanajivunia kwamba wataongeza thamani ya mgodi huo.
 OFISI YA WAZIRI MKUU YASHIRIKI KILI MARATHON

OFISI YA WAZIRI MKUU YASHIRIKI KILI MARATHON

February 26, 2024



Na: Mwandishi Wetu - Kilimanjaro

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na OSHA imeshiriki mashindano ya Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro (Kilimanjaro International Marathon 2024) Moshi, Mkoani Kilimanjaro, Februari 25, 2024.


Aidha, Katika mbio hizo, wanariadha hao wameshiriki mbio za Kilometa tano (Fun run) na wengine wameshiriki mbio za umbali wa kilometa 21 (Tigo half Marathon).

Akizungumza mara baaada ya kushiriki mbio hizo, Mkurugenzi wa Msaidizi wa Utawala, Edith Semtengu amesema Ofisi hiyo imekuwa ikishiriki katika Mashindano hayo kwa lengo la kutangaza majukumu ya ofisi hiyo katika mbio hizo sambamba na kuimarisha afya za watumishi.

Vile vile, Mkurugenzi huyo amewasihi wafanyakazi kujenga utaratibu wa kufanya mazoezi ili kulinda afya zao.

Katika Mashindano hayo, Ofisi hiyo ilishiriki pamoja na Taasisi ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA).

   

KASSIM MAJALIWA APIGILIA MSUMARI: AWATAKA TANAPA KUSIMAMIA SHERIA KAMA ZILIVYOPITISHWA NA BUNGE

February 26, 2024

 Na. Jacob Kasiri - Sitalike.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewataka Makamanda wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuratibu maeneo yao vizuri na kusimamia sheria za uhifadhi kama zilivyopitishwa na Bunge ili maliasilia zilizomo ziendelee kuleta tija kwa taifa, ameyasema hayo jana Februari 25.02.2024 aliposimama kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Sitalike akiwa katika safari ya kikazi kuelekea kijiji cha Mpimbwe kilichopo Jimbo la Kavuu Mkoani Katavi.

Akiwa amesimama kusikiliza kero katika kijiji hicho cha Sitalike kilichopo mpakani mwa Hifadhi ya Taifa Katavi, wananchi walimuomba aseme neno ili wapate fursa ya kuvua samaki mto Katuma ambao unategemewa kwa zaidi ya asilimia 80 kiikolojia na uhai wa wanyama kama vile viboko na Mamba ambao maisha yao yote hutegemea maji ya mto huo.

Baada ya kusikiliza maombi hayo mhe. Majaliwa alisema, "Niwashukuru Makamanda wa TANAPA kwa kufanya maboresho katika eneo la mto Katuma, endeleeni kuratibu vizuri maeneo yenu na yale tuliyoyaweka kwenye sheria zetu yatekelezeni lakini pia fursa za wananchi nazo zipate nafasi ila si kwa kuingia katika maeneo yaliyohifadhiwa."

Vile vile Mhe. Majaliwa aliongeza, "Wakati wote TANAPA kutaneni na wananchi, sikilizeni matamanio yao, waelimisheni juu ya namna watakavyonufaika na uhifadhi lakini pia waambieni na sheria zilizopo zifuatwe ili kuepusha misuguano."

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo (CCM) Mhe. Annah Lupembe alisema kuwa suala la wananchi kuvua samaki mto Katuma lililoibuliwa hapa leo lilishapatiwa majibu katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini Sitalike - Katavi siku chache zilizopita ukiwahusisha wananchi wa Kata ya Sitalike, TANAPA na Mbunge. Ambapo TANAPA kwa kushirikiana na mbunge husika walikubaliana kuchukua hoja hiyo na kuiwasilisha ngazi za Wizara kwa hatua zaidi.

Naye, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara - TANAPA Herman Batiho akiambatana na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini Steria Ndaga alisema, "Licha ya suala hili kushughulikiwa na mamlaka za juu tambueni kuwa, mto huu una mamba na viboko wengi, hivyo kuvua samaki eneo lenye wanyama wengi kiasi hicho ni kuhatarisha maisha yao aidha, kuna wanyama kama mamba na baadhi ya ndege hutegemea samaki hao.

Pia kuna wavuvi wengine hutumia sumu na tumeshawakamata majangili wa hivyo. Sumu hii imekuwa na madhara makubwa kwa watumiaji wa samaki hao, viumbe vingine vinavyoishi majini na kwa wanyama wanaokunywa maji hayo".

Kamishna Batiho pia aliwataka wakazi wa Kata ya Sitalike na vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa Katavi kuachana na uvuvi wa kutegemea mto badala yake wachimbe mabwawa ya kufugia samaki TANAPA itashirikiana nao kwa kuwaletea wataalam watakaowafundisha namna bora ya kuchimba na kupata mbegu ya vifaranga.

Ikumbukwe kuwa Oktoba 10, 2019 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alipotembelea hifadhi hiyo aliiagiza TANAPA kuchimba mabwawa kunusuru uhai wa Viboko kutokana na kukauka kwa mto Katuma kulikosababishwa na matumizi yasiyoendelevu ya rasilimali maji. Hivyo kuruhusu matumizi holela ya mto huo yanaweza kuturudisha tena katika kadhia ya mwaka 2019.








WAZIRI BASHE ATAKA SERA YA FEDHA SEKTA YA KILIMO, AZINDUA OFISI ZA TADB KANDA YA MAGHARIBI

February 26, 2024

 Na Said Mwishehe, Michuzi TV- Tabora


WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amezindua Ofisi za Benki ya Meandeleo ya Kilimo(TADB) Kanda ya Magharibi huku akitumia nafasi hiyo kueleza umefika wakati wa kuwa na  sera ya fedha katika kilimo lengo likiwa kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu tofauti na ilivyosasa ambapo wanakopa katika benki zenye mlengo wa kibiashara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ofisi za Benki ya TADB Kanda ya Magharibi Mjini Tabora , Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema kanda hiyo inajumuisha Mkoa wa Tabora, Kigoma na Katavi na uwepo wa ofisi za benki hiyo katika kanda hiyo inakwenda kusogeza huduma karibu na wakulima.

Akielezea zaidi kuhusu mikakati ya Serikali katika kilimo amesema pamoja na mambo mengine iko haja ya kuwa na sera ya fedha itakayohusu sekta ya kilimo ambayo itatoa fursa ya wakulima kuwa na uwezo wa kukopesheka kwa urahisi na bila ya kuwepo kwa vikwazo ambavyo vinasababishwa na kutokuwepo kwa sera ya fedha katika kilimo.

"Jambo la pili ambalo nataka niseme na kwa kuwa mwakilishi wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT)  yuko hapa , mikopo katika sekta ya uchumi wa nchi yetu uchumi wote mikopo inayoingia ni zaidi ya Sh.trilioni 20 na inayokwenda sekta ya kilimo ni asilimia chini ya 10...

"Na bado ukienda kwenye uzalishaji katika kilimo fedha inayotolewa kama mkopo ni ndogo sana.Sasa hoja yangu na nimeshaongea na Waziri wa Fedha , Gavana wa Benki Kuu , Waziri wa Mipango  na ninawaandikia barua.

"Tunahitaji  sera ya fedha ya kilimo kwani haiwezekani kilimo kikopeshwe kwa kutumia sera za benki za biashara.Kutumia sera hiyo bado hatutoweza kutoa watu kwenye umasikini," amesema Waziri Bashe.

Ameongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa katika kuinua sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima akitolea mfano ujenzi wa miundombinu ikiwemo ya kilimo cha umwagiliaji unaofanywa na Serikali.

"Serikali ikashamaliza kuboresha miundombinu mkulima anahitaji fedha ya kununua mbolea , pembejeo na mambo mengine yanayohusu kilimo.Kwa hiyo ni muhimu tukawa na sera ya kupata mitaji kwenye sekta za uzalishaji kilimo, mifugo na uvuvi."

Amesisitiza lazima kuwe na sera inayoeleweka na yeye kama Waziri wa Kilimo atawasukuma wote wanaohusika ili  kupata sera hiyo na anaamini itafanikiwa.

Amefafanua katika kipindi kisichozidi miaka miwili Rais Samia ameipatia TADB Sh.Bilioni  632."Sasa ni sheria zipi zinazoisimamia TADB kukopesha ?Kwa sasa  ni kama benki za biashara.Hatuwezi,  kwa hiyo lazima tutoe maamuzi na nimuombe Gavana , Waziri wa Fedha amenielewa, Waziri wa Mipango amenielewa tufanikishe jambo hili.

"Tutahakikisha tunasukuma tuwe na sera ya fedha katika sekta ya kilimo katika nchi hii ili tuweze kufika mahali ambako tunatakiwa kwenda, " amesema Waziri Bashe huku akitumia nafasi hiyo kuagiza jengo la ofisi za TADB kupewa jina la aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Hassan Mwakasuvi aliyefariki dunia juzi na lengo la ofisi kupewa jina lake ni kuenzi mchango wake mkubwa katika kilimo ndani na nje ya Mkoa wa Tabora.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) Frank Nyabundege  amekieleza umuhinu wa ofisi ya TADB Kanda ya Magharibi amesema toka mwaka 2018, mikoa ya  Kigoma, Katavi na Tabora ilikuwa ikihudumiwa na ofisi ndogo iliyokuwa Kigoma na baadae kuhamishiwa Tabora.

Ameongeza kwamba hadi kufikia  Februari, 2024, TADB imekwisha wezesha wakulima na wafugaji kwa kutoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Sh.bilioni 19.59 (Mkoa wa Kigoma, Sh. bilioni 7.209, Mkoa wa Katavi, Sh. bilioni 2.394, na Mkoa wa Tabora, Sh.bilioni 9.996).

"Mikopo hii imetolewa kwenye miradi ya mpunga, chikichi, maharage, mahindi, unenepeshaji wa ng’ombe, tangawizi, ufugaji wa kuku, ufugaji wa nguruwe, na ufugaji wa kondoo. Benki inaendelea kuweka mikakati thabiti ya kukopesha kwenye zao la tumbaku, pamba na asali, kwani  mazao haya yanachangia kukuza uchumi wa mkoa wa Tabora."

Aidha ameishukuru Ofisi ya Manispaa ya Tabora, kwa kutupatia jengo hilo la ofisi kwa miaka 33 bure. Hiyo ni ishara kubwa ya ushirikiano kati ya Mkoa wa Tabora na benki yao, hivyo ameahidi jengo hilo kutumika vizuri.

Ameongeza wanatamani kuendelea kusogeza huduma kwa wananchi na endapo ikimpendeza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma kutoa jengo Kigoma Mjini bure, anaahidi benki hiyo iko tayari kufungua ofisi ndani ya mwaka huu wa 2024.

 

Waziri  wa Kilimo Husen Bashe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo nchini(TADB)Frank Nyabundege mara baada ya kuwasili wakati wauzinduzi wa Tawi la benki hiyo mkoani Tabora
Waziri  wa Kilimo Husen Bashe akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Kilimo nchini(TADB)Frank Nyabundege mara baada ya kuwasili wakati wauzinduzi wa Tawi la benki hiyo mkoani Tabora
Mkurugenzi  Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB)  akomuonesha ramani ya mikoa na wilaya ambayo benki hiyo ipo nchini Waziri wa Kilimo Hussen Bashe wakati wa uzinduzi wa tawi la benki yiyo mkoani Tabora.
Waziri wa Kilimo Hussen Bashe akizungumza wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya TADB Kanda ya Magharibi inayojumuisha Mkoa wa Kigoma, Tabora na Katavi.

KAVUU YATEKELEZA MIRADI YA ELIMU YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 9.98

February 26, 2024

 Na Munir Shemweta, MLELE


Jimbo la Kavuu lililopo halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi katika kipindi cha kuanzia Novemba 2020 mpaka Februari 2024 limefanikiwa kutekeleza miradi ya elimu yenye thamani ya zaidi ya Tsh 9,986,388,189.47.


Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo hilo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu wa kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024. Mgeni rasmi kwenye mkutano huo alikuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa.

Amesema, kati ya kiasi hicho cha fedha Tsh 6,849,553,942.86 zimetumika kujenga miundombinu ya madarasa, kukamilisha maboma, maabara na ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari huku Tsh 1,258,714,246.61 zikutumika kugharamia elimu bila malipo, mitihani na kulipa posho kwa walimu wanaojitolea wa masomo ya sayansi.

Aidha, Mhe, Pinda alisema katika kipindi hicho cha utekelezaji ilani ya CCM jimbo lake la Kavuu limeweza kuimarisha utoaji wa elimu Jumuishi kwa wanafunzi ambapo ndani ya jimbo hilo kuna shule 27 jumuishi zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kitengo kimoja kilichopo shule ya msingi Majimoto.


‘’ Jumla ya Wanafunzi wenye mahitaji maalum ni 219 yaani wavulana ni 133 Wasichana 86 na walimu 10 wakiwemo wanaume 6 na wanawake 4 na miundombinu inaendelea kuboreshwa kuhakikisha makundi yote ya watoto wanapata haki ya kupata elimu na katika mazingira wezeshi’’ alisema Mhe, Pinda.

Akizungunza katika mkutano huo, Waziri Mkuu Kasima Majaliwa Majaliwa ameeleza kuwa hatua iliyofikia kwenye sekta ya elimu ndani ya jimbo hilo kni nzuri huku akisisitiza kuwa lengo la mbunge wa jimbo hilo ni kuhakikisha wanafunzi wanaotembea umbali mrefu wanaepukana na adha hiyo.

"Wakati nilipotembelea jimbo hili siku za nyuma na kuzindua madarasa mapya nane ipo tofauti kubwa ya wakati huo na kipindi hiki ambapo sasa kuna shule nyingi na kubwa kama hii ya Mizengo Pinda Sekondari" alisema Mhe, Majaliwa.

‘’Mabadiliko ninayoyaona katika jimbo la Kavuu hususan kwenye sekta ya elimu sioni kama wana mpimbwe na kavuu kwa ujumla hamyaoni’’. alisema.

Amemuelezea mbunge wa jimbo la Kavuu kuwa, ni mahiri katika kuratibu mambo na kuwataka wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika jimbo hilo kumpa nguvu ili aweze kufanya kazi.

Aidha, Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda aligusia pia maboresho katika sekta ya afya na kueleza kuwa, wamefanikiwa kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya (Kalista) ambapo ilani ya chama chake inatoa kipaumbele kujenga na kuimarisha vituo vya kutolea huduma za afya sambamba na ukamilishaji wa maboma ili kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi ifikapo mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, kwa kipindi cha 2021 hadi 2024, Halmashauri ya Mpimbwe imeendelea na upanuzi wa hospitali ya Halmashauri kwa ujenzi wa wodi tatu za wagonjwa, Wodi ya upasuaji, wodi ya daraja la kwanza, jengo la upasuaji sambamba na ujenzi wa jengo la huduma za dharura katika hospitali ya wilaya.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa akimueleza jambo Mbunge wa Jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda alipokwenda jimboni kwake kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kavuu tarehe 25 Februari 2024.
Sehemu ya wajumbe na wageni waalikwa wakifuatilia uwasilishwaji Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kavuu halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi Mhe, Geophrey Pinda tarehe 25 Februari 2024.

 

Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Geophrey Pinda akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuanzia Novemba 2020 hadi Februari 2024 katika Mkutano Mkuu  wa jimbo la Kavuu uliofanyika Shule ya Sekondari Mizengo Pinda katika halmashauri ya Mpimbwe mkoa wa Katavi tarehe 25 Februari 2024.

MAJARIBIO YA TRENI YA UMEME YA KISASA YA (SGR)

February 26, 2024

 Treni ya Umeme ya Kisasa ya (SGR) ikipita maeneo ya Pugu Jijini Dar es Salaam katika majaribio yake ya kawaida. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza majaribio ya Treni hiyo ya SGR kutoka Mkoani Dar es Salaam hadi Mkoani Pwani na hivi karibuni itaendelea na majaribio hayo mpaka Mkoani Morogoro. Huduma rasmi za Usafiri huo zinatarajiwa kuanza Mwezi wa Julai, 2024.