RAIS MSTAAFU MKAPA AONGOZA HARAMBEE YA KUCHANGIA MFUKO WA UDHAMINI WA KUDHIBITI UKIMWI

February 13, 2018
Rais Mstaafu Benjamin Mkapa akihutubia wakati akiongoza harambee ya kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) katika hafla iliyofanyika Hoteli ya Serena Dar es Salaam jana usiku.
Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama akihutubia katika harambee hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi,Bw.  Godfrey Simbeye akihutubia.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko akihutubia.
Wasanii wakitoa Burudani katika harambee hiyo
Wadau wakiwa kwenye harambee hiyo.
Makofi yakipigwa meza kuu. Kutoka kushoto ni Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi,  Bw. Godfrey Simbeye na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM), Bw. Tenga B. Tenga.
Wadau wakiwa kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa akitoa zawadi ya picha iliyonunuliwa kwa sh. milioni moja katika harambee hiyo.
Rais Mkapa akimkabidhi picha  Salama Mussa kutoka Benki ya NBC baada ya kuinunua katika harambee hiyo. Kulia ni Waziri Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama na wa pili kushoto ni Mdau Teddy Mapunda mratibu wa harambee hiyo.
Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akimkabidhi picha Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Alvaro Rodriguez baada ya kuinunua katika harambee hiyo.
Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa akimkabidhi picha ya simba Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko wa Hoteli ya Serena, Bw. Seraphin Lusala baada ya kuinunua kwenye harambee hiyo.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM),  Bw. Tenga B. Tenga akimkabidhi Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa mfano wa hundi yenye thamani ya sh.milioni 100 zilizo tolewa na mgodi huo kuchangia mfuko huo.


Na Dotto Mwaibale

RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa amewataka wadau mbalimbali na wananchi kuendelea kuchangia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF) kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo nchini ambapo zaidi ya sh.milioni 200 zilipatikana.

Mkapa alitoa ombi hilo wakati akiongoza harambee ya kuchangia mfuko huo iliyofanyika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya nje na ndani pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini.

"Ni wajibu kwa kila mwananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuchangia mfuko huu ili kusaidia mapambano ya Ukimwi hapa nchini na kuwa mapmbano hayo si ya mtu mmoja" alisema Mkapa. 

Katika hatua nyingine Rais Mstaafu Mkapa ameiomba Serikali kuendelea kutenga fedha za Ukimwi katika bajeti zake.

Akizungumza katika harambee hiyo Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Mheshimiwa Jenista Mhagama alisema kwamba Serikali itaendelea kusimamia Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) katika matumizi ya  fedha hizo.

Mhagama alisema asilimia 60 ya fedha hizo zitatumika kununulia madawa, asilimia 25 itatumika katika kutoa huduma za kinga pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi mapya ya Ukimwi na asilimia 15 zitatumika  kwa ajili ya uwezeshaji na ufuatiliaji wa programu za Ukimwi.

Mhagama aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kufubaza VVU kwa wanawake ni asilimia 92.9 wakati wanaume ni 86.1 na kuwa katika tisini ya tatu kati ya watu wanaoishi na VVU wenye umri wa miaka 15-64 ambao wametoa taarifa kuwa wanatumia dawa za kufubaza VVU asilimia 87.7 ya watu hao inaonyesha kiasi cha VVU kimefubazwa wanawake ni asilimia 89.2 na wanaume ni asilimia 84.

Alisema utafiti huo pia umeonyesha kuwa maambukizo mapya ya VVU (HIV incidence) kwa mwaka kwa watu wenye umri wa miaka 15-64 Tanzania Bara ni asilimia 0.29 ambayo ni sawa na watu 81,000.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko huo, Bw. Godfrey Simbeye alisema sekta binafsi imeunga mkono kwa kiasi kikubwa katika kuchangia mfuko huo na kuwa hakutakuwa na matumizi mabaya ya fedha hizo na zitakwenda kutumika kwa kile kilichokusudiwa.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko alimshukuru Rais Mstaafu Mkapa kwa kukubali kushiriki kuongoza harambee hiyo na kueleza kuwa Tacaids imekuwa ikiendesha harambee mbalimbali pamoja na kuandaa mashindano ya michezo na viingilio vyake vimekuwa vikiingia katika mfuko huo.


(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712727062)






REDIO ZATAKIWA KUWA TARISHI WA MAENDELEO

REDIO ZATAKIWA KUWA TARISHI WA MAENDELEO

February 13, 2018
 Wafanyakazi wa taasisi za redio wamekumbushwa wajibu wao kama ilivyo chombo chochote cha habari kuwa matarishi wa amani, upendo, mshikamano na kuhuisha maendeleo. Aidha wameambiwa kwamba kwa kuwa Redio ina nguvu kuliko chombo chochote kingine duniani kwa kuwafikia watu wengi zaidi hivyo basi wanatakiwa kuwa makini wanapowafikishia wananchi taarifa. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Juliana Shonza katika maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Dodoma ambaye alitaka taarifa kwa wananchi kufikishwa bila ushabiki, chuki au kupiga chuku (kuongeza chumvi). Alisema tasnia ya uandishi wa Habari ni tasinia adhimu sana, hivyo Waandishi wote wa Habari wanalo jukumu kubwa la kuzingatia misingi ya uandishi ambayo ni mizania (balancing), kutofungamana na upande wowote (impartiality), kutenda haki (fairness), Utu (humanity), na mwisho kabisa kuzingatia ukweli (truthness). Siku ya Redio Duniani huadhimishwa kila mwaka duniani kote Tarehe 13 mwezi Februari ili kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Redio mahali pote duniani. Aliwakumbusha waandishi na wageni historia ngumu na mbaya ya namna redio zilivyotumika vibaya katika baadhi ya nchi duniani na kuleta machafuko hadi umwagaji damu. “Hivyo niwaase tena kutumia redio hizo na vipaza sauti kwa ajili ya kutoa taarifa muhimu juu ya masuala ya kilimo na ufugaji, majanga mbalimbali, elimu juu ya sera na sheria mbalimbali za nchi, masuala ya afya kwa jamii na elimu. Na kwa kufanya hivyo tu, ndipo tutakuwa tumeitendea haki tasnia hii.” alisema Dk. Shonza.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza akisoma hotuba kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani zilizofanyika Mjini Dodoma.
Aidha alipongeza kauli mbiu ya mwaka huu Redio na Michezo na kutoa rai kwa waandishi wote wa habari kudumisha mila na desturi za Kitanzania na kuongea Kiswahili fasaha bila kuchanganya na lugha zingine kama Kiingereza maarufu kama Kiswanglish. Aidha Waziri Mwakyembe alishukuru Shirika la UNESCO na Mtandao wa Redio Jamii Tanzania (TADIO) kwa kuwezesha siku ya redio na kusema atatafakari hoja zote zilizowasilsihwa kwake. Naye Katibu wa Mtadao wa Radio Jamii (TADIO), Marco Mipawa akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa mtandao huo, Prosper Kwigize alitaka serikali kuhakikisha kwamba urasimu unaondolewa kwenye utoaji wa taarifa kwa umma ili kuwezesha kufanyika kwa vipindi mbalimbali vya habari.
Katibu wa Mtandao wa Radio za Jamii nchini (TADIO), Marco Mipawa akisoma hotuba kwa niaba ya Mwenyekiti wa Mtandao huo, Prosper Kwigize wakati maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma kwa ufadhili wa UNESCO.
Alitaka Tamisemi kuweka utaratibu wa utoaji habari katika mfumo rahisi ili wananchi wafahamu kinachotekelezwa na serikali yao. Aidha maafisa habari walioajiriwa wapewe mamlaka na wawezeshwe kufahamu kinachofanywa na serikali na wawe na ruhusa ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari katika maeneo yao. Aidha alisema kutokana kutokuwa na vyanzo vya mapato ya uhakika serikali ingeangalia suala la kodi na ushuru mbalimbali ili kusaidia Redio za Jamii kutolipia huduma za Radio. Pia amesema sheria zilizopo ukilinganisha na mazingira halisi ya kazi ya mwanahabari, mfano sheria ya Takwimu, sheria ya huduma za habari, sheria ya makosa ya mtandao kumeshabibisha tasnia ya habari na utangazaji kuwa katika mashaka zaidi kuliko kipindi kilichopita. Pia ameitaka Serikali kutoa Ruzuku ya elimu au mafunzo ya kitaaluma kwa wanahabari ili kuwawezesha kukidhi vigezo vya kisheria ifikapo 2021 Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo amewataka waandishi na watangazaji kutumia redio kwa manufaa ya taifa kuleta mshikamano na pia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo (wa pili kushoto) akitoa salamu za UNESCO wakati maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambapo huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Februari yaliyofanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini. Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza (wa pili kulia) pamoja na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche (wa kwanza kushoto).
Aidha alikumbusha historia ya redio na kazi iliyofanya duniani na kusema kwamba umuhimu wa radio upo wazi na kutaka wahusika kuzitumia kwa manufaa ya umma unaowazunguka. Naye Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Dk Moshi Kimizi, alitaka serikali na vyombo vya habari kushirikiana katika kuhimiza michezo kwa kuwa ndicho kinachowaleta wananchi pamoja.
Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Kaimu Katibu Mtendaji wa tume hiyo Dk. Moshi Kimizi (hayupo pichani) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika Mjini Dodoma.
Alisema anadhani redio na serikali vitaona njia bora ya kutangaza michezo kwa manufaa ya taifa. Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari Mh. Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge amesema Unesco inafanya kazi nzuri sana kwa kuwekeza kwenye vyombo vya Habari na kuvitaka vyombo hivyo kuitangaza Dodoma na fursa zake kwa sababu ndio makao makuu ya nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma. Wa pili kulia ni Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza, Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo (wa pili kushoto) pamoja na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche (wa kwanza kushoto).
Aidha aliitaka Redio kutangaza fursa zote ambazo zipo Dodoma ili wafanyakazi na wafanyabiashara wanaohamia Dodoma kujua wanapata wapi mahitaji yao yakiwemo Makazi, Maji, Chakula, Elimu na kadhalika. Alitaka vyombo hivyo kuvutia wawekezaji ili mji huo uwe kweli katika karne ya 21 na makao makuu ya nchi.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza akiwasili katika hoteli ya Nashera mjini Dodoma kushiriki sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge (kulia) pamoja na Katibu wa Mtandao wa Radio za Jamii nchini (TADIO), Marco Mipawa (kushoto).
Kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge, Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza, Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo pamoja na Mkuu wa Mawasiliano na Habari wa Tume ya Taifa ya Unesco (NATCOM), Christina Musaroche wakiwa meza kuu wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani mjini Dodoma.
Mratibu wa Mtandao wa Vyombo vya Habari na Jinsia Kusini mwa Afrika (GEMSAT) , Gladness Munuo akitoa mada kuhusu usawa wa jinsia katika kuripoti michezo, changamoto na taratibu zake wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma. Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akisisitiza umuhimu wa maudhui katika vipindi vya redio ambapo aliwaasa kutangaza masuala yanayowahusu wanajamii katika maeneo yanayohusika badala ya kuwalisha wasikilizaji taarifa ambazo ziko nje na mipaka wanayoishi.
Mtaalamu wa Vyombo vya Habari na Mawasiliano, Mariagoreth Charles akiwasilisha kanuni za uandishi wa habari za mtandaoni na mitandao ya kijamii kwa waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini walioshiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
Mtangazaji Mkongwe wa Habari za Michezo nchini, Abdallah Majura amesema pamoja na kwamba waandishi wanatangaza vipindi vya michezo lakini maudhui hayakidhi na kuvutia vile inavyostahili akitoa mfano hai wakati akichangia kwa nini waandishi wengi hawaandiki habari za michezo. Majura amesema yeye mwenyewe amewahi kupata tuzo mbili kwa ajili ya vipindi vya michezo.
Pichani juu na chini ni sehemu ya waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza (wa tatu kushoto), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) pamoja na Kaimu Mkuu wa Ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) nchini, Faith Shayo (wa tano kulia) wakicheza wimbo maalum wa ngoma za asili wa Kikundi cha Kaza Roho cha mjini Dodoma ulioongozwa na Msanii Mwinamila wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mh. Juliana Shonza na meza kuu wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani pamoja na wadau wengine wa habari nchini wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika mjini Dodoma.

AWESO ATAKA MIRADI YA MAJI IKAMILIKE KWA WAKATI

February 13, 2018
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akikagua bomba la DAWASCO linalosambaza Maji ya Ruvu Juu iliyopo maeneo ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso akikagua Mradi wa visima 20 eneo la Kisarawe II katika mji wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso aendelea na ziara ya kukagua maendeleo ya Miradi ya Maji Mji wa Kigamboni Jijini Dar es salaam.

GOFU LUGALO YATEKELEZA AGIZO LA MKUU WA MAJESHI YASHINDA NIGERIA

February 13, 2018
Mchezaji wa Lugalo Golf Club Angel Eaton akishangilia mara baada ya kucheza mpira mzuri katika shimo namba Tisa katika mashindano ya wazi ya wanawake ya IBB ladies Championship yaliyomalizika Jumapili nchini Nigeria
Mchezaji wa Lugalo Golf Club Angel Eaton akishangilia akiwa na wechaji wenzie mara baada ya kuibuka mshindi katika mashindano ya wazi ya wanawake ya IBB ladies Championship yaliyomalizika Jumapili nchini Nigeria
Mchezaji wa Lugalo Golf Club Angel Eaton akinyenyua kikombe mara baada ya kushinda katika mashindano ya wazi ya wanawake ya IBB ladies Championship yaliyomalizika Jumapili nchini Nigeria
Mchezaji wa Lugalo Golf Club Angel Eaton akishangilia kwa kujifunika bendera ya taifa mara baada ya kucheza mpira mzuri katika shimo namba Tisa katika mashindano ya wazi ya wanawake ya IBB ladies Championship yaliyomalizika Jumapili nchini Nigeria.Picha na Luteni Selemani Semunyu

Angel Eaton Mchezaji Watimu Ya Golf Ya Wanawake Ya Klabu Ya Jeshi La Ulinzi La Wananchi Wa Tanzania Ya Lugalo Ametekeleza Agizo La Mkuu Wa Majeshi Ya Ulinzi Jenerali Mabeyo La Kulinda Heshima Ya Jeshi Katika Mashindano Nchini Nigeria

Mchezaji Huyo Nyota Wa Klabu Ya Lugalo Amefanikisha Hilo Baada Ya Kuibuka Na Ushindi Wa Jumla Baada Ya Kushinda Siku Tatu Mfululizo Kwa Mikwaju 76 Katika Siku Ya Kwanza Ya Pili Na Tatu Ya Mashindano Ya Wazi Ya Wanawake Ya Ibb Ladies Open Championship Yaliyofanyika Abuja Nchini Nigeria.

Tanzania Iliyowakilishwa Na Wachezaji Saba Kutoka Klabu Ya Lugalo Imefani9kiwa Kushika Nafasi Ya Nne Iliyonyakuliwa Na Mchezaji Wake Hawa Wanyeche Akiwa Nyuma Ya Wachezaji Kutoka Kenya Na Nigeria Huku Nafasi Ya Sita Ikinyakuliwa Na Nahodha Ayne Magombe

Hivi Karibuni Wakati Akiwaaga Wachezaji Hao Kwenda Nchini Nigeria Mkuu Wa Majeshi Ya Ulinzi Jenerali Mabeyo Aliwataka Kuhakikisha Wanalinda Heshima Ya Klabu Jeshi Na Nchi Kwa Ujumla Katika Mashindano Hayo

Mashindano Hayo Ya Siku Tatu Yaliyoshirisha Wacheza Ji 187 Kutoka Nchi 10 Zilizoshiriki Michuano Hiyo Ambapo Nahodha Wa Timu Hiyo Ayne Magombe Alisema Walikuwa Na Timu Nzuri Iliyokuwa Na Wachezaji Wazuri.

Timu Ya Lugalo Iliwakilishwa Na Wachezji Ayne Magomba,Sophia Mathias, Hawa Wanyeche,Christina William, Rehema Athumani Na Angel Eaton Ambaye Pia Alishinda Longest Drive.

KILOMBERO YAWAWEZESHA MAELFU WAZEE WASIOJIWEZA HUDUMA ZA CHF ILIYOBORESHWA

February 13, 2018
Na John Nditi, Kilombero.

HALMASHAURI ya wilaya ya Kilombero , mkoani Morogoro wamewakatia  kadi za   Mfuko wa Afya ya Jamii  (CHF ) iliyoboreshwa  wazee wasiojiweza zaidi ya 7,800 waliopo katika  kata  26  ili kuwawezesha kupata  huduma bora za matibabu katika vituo vya  Afya, Zahanati na hospitali na wategemezi wao.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri  hiyo , Dennis Londo   alisema hayo  mbele ya  Katibu tawala mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari, kabla ya zoezi la ugawaji  kadi za CHF Iliyoboreshwa  kwa baadhi ya wazee wapatao  2,100 kutoka  vijiji 23 vya kata saba za Tarafa ya Mlimba.

Londo  alisema   kuwa , hadi sasa  kiasi cha Sh milioni 13.3 zimetumika  kwa ajili ya mpango wa kuwakatia wazee wasiojiweza  bima  ya  afya ya CHF Iliyoboreshwa.

Hata hivyo alisema , halmashauri hiyo imejipanga  kuhakikisha wazee wanapatiwa bima ya Afya CHF iliyoboreshwa na lengo  ni  kuwafikia  wazee wasiojiweza  zaidi ya  15,000  katika kata zote 26.

“ Halmashauri ya wilaya hii imejipanga vyema na inatekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM  na miongoni mwa mam ohayo ni kundi la wazee wasiojiweza wamenufaka na huduma ya bima  ya afya” alisema Londo.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri  hiyo , David Ligazio aliwataka watendaji wa vituo vya afya, zahanati na hospitali  ambaki madirisha ya wazee hayajaanzishwa waanzishe mara moja   ili  wazee hao wapate  unafuu wa huduma kulingana na lengo lililokusudiwa .

Kwa pande wake  mkuu wa wilaya ya Kilombero , James Ihunyo  alisema  , halmashauri hiyo inaendelea kufanya vizuri kutokana na  sehemu ya fedha zinazopatikana za   makusanyo ya ndani  kuelekezwa  kuboresha huduma za kijamii ikiwemo kuwakatia  bima  ya afya wazee wasiojiweza sambamba na kwa halmashauri ya mji Ifakara.

Awali  akisoma taarifa ya ugawaji wa kazi hizo ,  Ofisa Elimu Kata Kalengakelu,  Zainab Said  alisema,  wazee wasiojiweza walionufaika na mpango huo ni wa kutoka kwenye vijiji 23 vya  kata ya Chisano, Kalengakelu, Mlimba, Kamwene, Utengule , Masagati na Uchindile .

Akizungumza katika halfa hiyo katibu tawala wa mkoa huo, Tandari alizitaka halmashauri nyingine ndani ya mkoa huo  kuiga mfano wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero  ili kuhakikisha wazee wote wanakuwa bima ya afya.

Nao baadhi ya wanufaika na mpango huowa CHF iliyoboreshwa ,Nelasi Nyingi  na Petro Karubandika kwa nyakati tofauti waliipongeza Serikali na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero  kwa kuwawezesha kuingizwa kunufaika na huduma za afya hasa ikizingatiwa wao wanahauwezo wa kifedha na wategemezi wao.
 Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari  ( wapili  kushoto) akimkabidhi kadi ya bima ya afya ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Iliyoboreshwa mzee  Petro Karubandika mkazi wa kata ya Mlimba , halmashauri ya wilaya ya Kilombero  wakati wa zoezi la ugawaji  kadi  hizo kwa wapatao  2,100 kutoka  vijiji 23 vya kata saba za Tarafa ya Mlimba na (  kushoto) ni  mkuu wa wilaya ya Kilombero, James Ihunyo na ( watatu kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Kilombero, Dennis Londo.
 Katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari  ( wapili kushoto) akimkabidhi kadi ya bima ya afya ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Iliyoboreshwa   Nelasi Nyingi , mkazi wa kata ya Mlimba , halmashauri ya wilaya ya Kilombero  wakati wa zoezi la ugawaji  kadi  hizo kwa wapatao  2,100 kutoka  vijiji 23 vya kata saba za Tarafa ya Mlimba (  kushoto ) ni mkuu wa wilaya ya Kilombero, James Ihunyo na ( watatu kushoto) ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Kilombero, Dennis Londo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri   ya Kilombero , Dennis Londo  ( kulia) akitoa maelezo mafupi ya mapango wa kuwakatia bima ya afya wazee  wasiojiweza kwa  Katibu tawala mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari ( wapili kutoka kushoto) wakati wa  zoezi la ugawaji  kadi za CHF Iliyoboreshwa  kwa  wazee wapatao  2,100 wa  vijiji 23 vya kata saba za Tarafa ya Mlimba.
Baadhi ya wazee wa kata saba za tarafa ya Malimba , halmashauri ya wilaya ya Kilombero wakimsikiliza mgeni rasmi Katibu tawala mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari  ( hayupo pichani) wakati wa  zoezi la ugawaji  kadi za CHF Iliyoboreshwa  kwa  wazee wapatao  2,100 wa  vijiji 23 vya kata saba za Tarafa ya Mlimba.  ( Picha na John Nditi).