MECHI YA TWIGA STARS, ZAMBIA BURE
Washabiki
wa mpira wa miguu nchini watashuhudia bure mechi ya timu ya Taifa ya mpira wa
miguu ya wanawake (Twiga Stars) dhidi ya Zambia (Shepolopolo).
Mechi
hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC)
itachezwa Ijumaa (Februari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo
Chamazi, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili alasiri.
Twiga
Stars ambayo ilipoteza mechi ya kwanza iliyochezwa Lusaka, Februari 14 mwaka
huu kwa mabao 2-1 iko kambini chini ya Kocha Rogasian Kaijage na msaidizi wake
Nasra Juma ikijiwinda kuwakabili Wazambia wanaotarajiwa kutua nchini Alhamisi
(Februari 26 mwaka huu).
Waamuzi
wa mechi hiyo Ines Niyonsaba, Jacqueline Ndimurukundo, Axelle Shikana na Suavis
Iratunga kutoka Burundi kutoka Burundi wanatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa
(Februari 26 mwaka huu). Kamishna Fran Hilton Smith kutoka Afrika Kusini yeye
atatua nchini Februari 27 mwaka huu kwa ndege ya South Africa Airways.
RWIZA
KUSIMAMIA MECHI YA TP MAZEMBE
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Rwiza Kishongole kuwa Kamishna
wa mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya TP Mazembe na Asres De
Douala ya Cameroon.
Mechi
hiyo ya hatua ya 16 itafanyika kati ya Machi 7, 8 au 9 mwaka huu jijini
Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuchezeshwa na waamuzi
kutoka Uganda.
Mwamuzi
wa kati atakuwa Denis Batte wakati wasaidizi wake ni Mark Ssonko, Samuel
Kayondo na Mashood Ssali.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari na Mawasiliano
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)