HATI YA KIWANDA CHA NYAMA SHINYANGA YAREJESHWA SERIKALINI

April 21, 2018


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (mwenye miwani) akishuhudia utiaji saini wa hati ya makabidhiano ya Kiwanda cha nyama cha Shinyanga. Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba(aliyekaa upande wa kushoto) kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa (aliyeinama upande wa kulia) kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.

Hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga iliyorejeshwa Serikalini na Kampuni ya Albwardy Investment Group baada ya kuuziwa kinyemela na kampuni ya Tripple S Beef kinyume na mkataba iliyoingia na Serikali, baada ya kampuni hiyo kushindwa kukiendesha kiwanda kwa miaka 11 tangu kilipokabidhiwa.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina (aliyekaa mwenye miwani) akishuhudia ubadilishanaji wa hati ya makabidhiano ya Kiwanda cha nyama cha Shinyanga.Kushoto ni Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina aliyeiwakilisha Serikali na kulia ni Balozi Fouad Mustafa aliyewakilisha upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group

-Ni baada ya Waziri Mpina kutoa siku saba tu kuirejesha

Na John Mapepele, Dar es Salaam

Kampuni ya Albwardy Investment Group imerejesha Serikalini hati ya kiwanda cha nyama cha Shinyanga na eneo la kupumzishia mifugo la kiwanda hicho iliyouziwa kinyemela na kampuni ya Triple S Beef Limited kutokana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kutoa siku saba kwa wawekezaji Triple S Beef kusalimisha hati hizo kwa kushindwa kukiendeleza kwa miaka 11.

Akizungumza mara baada ya kusaini hati za makabidhiano ya hati hizo ofisini kwake jana, Waziri Mpina alitoa siku 14 kwa Salim Said Seif ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Tripple S Beef kujisalimisha Serikalini kwa kuvunja mkataba na serikali ambao ulimtaka kutommilikisha mwekezaji mwingine.

Hati hiyo zilisainiwa na Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina kwa upande wa Serikali na Balozi Fouad Mustafa kwa upande wa Kampuni ya Albwardy Investment Group aliyemwakilisha mmiliki wa Kampuni hiyo bwana Ali Saeed Juma Albwardy.

Waziri Mpina alisema Kampuni ya Tripple S Beef ilinunua kiwanda hicho kwa shilingi milioni 63 tu mwaka 2007 na kukiza kinyemela kwa shilingi bilioni 8 kwa Kampuni ya Albwardy Investment Group mwaka 2015 kwa mujibu wa maelezo ya mwakilishi wa kampuni hiyo, balozi Fouad Mustafa.

Aidha alisema kiwanda hicho kilijengwa kwa bilioni 8.2 na kina ukubwa wa eneo la hekta 32 huku likiwa na ziada ya eneo lenye hekta 444 zakuhifadhia mifugo.

Aidha Mpina alisema mkakati wa Serikali kwa sasa ni kuvifufua viwanda vyote vya nyama nchini na kuvitangaza kwa wawekezaji makini ili waweze kuwekeza ili mifugo iliyopo iweze kupata soko la uhakika na viwanda vilipe kodi za serikali hatimaye kuliingizia taifa mapato.

“Tunaposema Serikali ya awamu hii ni ya viwanda tuna maanisha kwa vitendo na kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi katika kiwango kinachositahili ili kujenga uchumi wa nchi yetu” alisistiza Mpina

Aliongeza kuwakwa kuwa hati za kiwanda cha Shinyanga zimekabidhiwa leo zabuni itatangazwa hivi karibuni ya kumpata mwekezaji mahiri, pamoja na kiwanda hicho viwanda vingine vitakavyotangazwa kupata mwekezaji mahiri ni pamoja na kiwanda cha nyama Mbeya na kiwanda cha Ngozi cha Mwanza.

Alisema Serikali itavitangaza viwanda hivyo pamoja kuvitengea maeneo makubwa ya kuhifadhia mifugo kabla ya kuichinjwa ili kuinua ubora na thamani ya nyama katika masoko ya kimataifa.

Akitoa taarifa ya Umilikishwaji wa kiwanda hicho, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji na Ufuatiliaji Jones Mwalemba kutoka Hazina alisema kiwanda kilianza ujenzi wake mwaka 1975 na kwamba kimegharimu dola za kimarekani milioni 3.5 na kilijengwa na Serikali kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Alisema mwaka 2007 kiwanda hicho kilibinafsishwa kwa mwekezaji Tripple S Beef Limited lakini kutoka na matatizo ya uendeshaji kiwanda hicho kilifungwa mwaka 2017 na kukabidhiwa kwa Serikali.

Awali Waziri Mpina alipofanya ziara ya kushitukiza hivi karibuni katika kiwanda cha nyama cha Shinyanga aliagiza kwamba ifikapo Juni 30 mwaka huu kiwanda hicho kiwe kimempata mwekezaji ambaye ataanza kazi mara moja ya uchinjaji ili kutoa ajira na kuliingizia taifa mapato.

Alitoa siku saba kwa wawekezaji waliokuwa wanaendesha kiwanda hicho kusalimilisha hati za kiwanda na eneo mara mmoja ili Serikali iweze kufanya taratibu za kufufua kiwanda hicho.

Aidha amemuagiza Msajili wa Hazina kuanza uhakiki wa mali zote za kiwanda hicho baada ya kubainika wizi uliokithiri katika kiwanda hicho.

Pia Mpina ameamuru mmliki wa Kampuni inayolinda kiwanda hicho kukamatwa mara moja na kufikishwa katika mikono ya sheria kwa ajili ya kujibu mashitaka wa wizi wa mali za kiwanda hicho ambapo alimtaka Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kuanzia sasa kiwanda hicho kilindwe na vyombo vya Serikali badala ya makampuni binafsi.

KIGWANGALA ATUMIA NGORONGORO MARATHON KUWATUMIA SALAMU MAJANGILI

April 21, 2018
PICHANI: Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (fulana nyekundu) akiwa na uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) pamoja na baadhi ya washiriki wa mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila (namba 002), Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dkt. Fred Manongi (namba 003) na Meneja Mahusiano wa NCAA Joyce Mgaya (kulia waliosimama). (Picha na Yusuph Mussa Immamatukio Blog).


Na Yusuph Mussa, KaratuImmamatukio Blog

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala ametuma salamu kwa majangilli wanaojihusisha na uwindaji haramu wa wanyama kwenye Hifadhi za Taifa ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Amesema Serikali na wadau wengine wamejipanga kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa kudhibiti ujangili wa wanyama na viumbe hai vyote vinavyotokana na maliasili yetu ya asili kwenye hifadhi za Taifa.

Dkt. Kigwangala alituma salamu hizo kupitia Mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018 kwa kuanzia Lango Kuu la kuingilia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuishia Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.

Pamoja na kuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo, Dkt. Kigwangala pia alikimbia kilomita 21 kuanzia saa 3.30 asubuhi na kumaliza saa 6.20 mchana, na kusema hiyo ni ishara tosha ya kujipanga na kukabiliana na majangili. Dkt. Kigwangala alisema kwa kumaliza mbio hizo, sio tu anawatishia majangili kuwa yupo vizuri kukabiliana nao, bali anataka askari wote wa wanyama pole wawe wakakamavu na asimuone askari yeyote mwenye kitambi.

"Moja ya malengo ya mbio za Ngorongoro Marathon kwa mwaka huu ni kupambana na ujangili na majangili. Na sikumaliza mbio hizi za kilomita 21 kwa bahati mbaya, bali ni kuwadhihirishia majangili na watu wote wenye nia mbaya na rasilimali zetu kuwa nipo fiti.

"Lakini sio kwa majangili, hata kwa askari wetu, nataka kuwaeleza kuwa kuanzia sasa sitaki kuona askari anakuwa na kitambi. Hatuwezi kupambana na majangili kama askari wetu wana vitambi na wapo legelege... Na nataka kuwaeleza askari kama wanataka twende nao pamoja kwenye hili basi wajipange" alisema Kigwangala.

Dkt. Kigwangala alisema nia nyingine ya NCAA kudhamini mbio hizo ni kutangaza shughuli za utalii ndani na nje ya nchi, kwani anaamini kupitia waandishi wa habari na washiriki wa mashindano hayo kutokea ndani na nje ya nchi, itawezesha kuongeza watalii na hifadhi hiyo kujulikana zaidi.

Naye Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) Anthony Mtaka, alisema moja ya mambo yanayotushinda nchini ni kujitangaza, lakini hapo hapo kushindwa kupenda vya kwetu, kwani pamoja na kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania, lakini matangazo yake mengi yapo Kenya.

Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alisema amefurahishwa na uongozi wa NCAA kudhamini mashindano hayo, kwani yatawezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufahamika duniani kote.

"Kwenye Serikali ukiwa na mtu kama Dkt. Fred Manongi (Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) mambo yatakwenda vizuri. Tumempa taarifa wiki mbili kabla ya mashindano kumuomba atudhamini, lakini akawa amekubali na mambo yamekwenda vizuri.

"Hiki cha kukubali kudhamini mashindano haya ni kikubwa sana. Sasa anatufanya Watanzania tuanze kujitangaza na kupenda vya kwetu. Hili tatizo la kushindwa kujitangaza ni kubwa ndiyo maana kila siku kuna malalamiko kuwa Kenya wanajitangaza Mlima Kilimanjaro ni wa kwao. Sisi sasa tujitoe na kuonesha rasilimali hizi za utalii ni za kwetu" alisema Mtaka.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akionesha medali yake kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mbio za Ngorongoro Marathon (kilomita 21). Alimaliza mbio hizo saa 6.20 mchana. Mbio hizo zilizoanza leo Aprili 21, 2018 saa 3.30 asubuhi kwenye lango kuu la kuingia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), zimehitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. NCAA ndiyo wadhamini wakuu wa mbio hizo. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akihutubia wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha mara baada ya kumalizika mbio za Ngorongoro Marathon leo Aprili 21, 2018 na kuhitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. Wa pili kulia ni Rais wa Chama cha Riadha (RT) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Fred Manongi (kulia), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Jubilate Mnyenye (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha Cecilia Pareso (katikati) wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (hayupo pichani) kwenye kilele cha mbio za Ngorongoro Marathon zilizohitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu leo Aprili 21, 2018. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

BREAKING NEWS…! WAZIRI TIZEBA AAGIZA MKURUGENZI WA BODI YA KOROSHO KUSIMAMISHWA KAZI

April 21, 2018


Waziri wa wizara ya kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma, Jumamosi 21 Aprili 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-WK
Waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini taarifa ya Waziri wa wizara ya kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba ofisini kwake mjini Dodoma, Jumamosi 21 Aprili 2018.
Katibu Mkuu wa wizara ya kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe akisikiliza maagizo ya kusitisha mkatanba wa kazi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Leo Jumamosi 21 Aprili 2018.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Waziri wa wizara ya kilimo Mhe. Dkt Charles Tizeba amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya kilimo Mhandisi Methew Mtigumwe kusitisha mkataba wa kazi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania Ndg Hassan Jarufo.

Waziri Tizeba ametoa agizo hilo kwa katibu mkuu wa wizara hiyo leo Jumamosi 21 Aprili 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Dodoma ikiwa ni muda mchache mara baada ya kumalizika kwa dhifa ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa.

Akielezea sababu za kuagiza kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi huyo, Mhe. Dkt Tizeba alisema kuwa hayo yamejili baada ya kuangalia mwenendo wa Ndg Jarufo na kutafakari jinsi zao la korosho linavyoendeshwa, ikiwa ni pamoja na kutoridhishwa na upatikanaji wa viuwatilifu kwa wakati.

Aidha, Mkataba huo umesitishwa kuanzia leo tarehe 21 Aprili 2018 hivyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo atapaswa kufanya taratibu zote za kiutumishi ikiwa ni pamoja na kumpatia taarifa haraka muhusika na utekelezaji wake kuanza haraka.

Alisema ndani ya muda mfupi Wizara ya kilimo itamtangaza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi hiyo ili kuchukua nafasi hiyo kuendeleza kusimamia sekta hiyo.

“Hizi hatua tunazochukua ni kuhakikisha kuwa wadau wakubwa wa korosho ambao ni wakulima wanaendelea kunufaika na zao lao, hivyo wakulima wasiwe na wasiwasi kwani pamoja na kuondolewa Mkurugenzi huyo lakini shughuli za serikali zitaendelea kama kawaida na maslahi yao yatasimamiwa ipasavyo” Alikaririwa Mhe. Dkt Tizeba

“COASTAL UNION KUANZA NA U-20”

April 21, 2018
UONGOZI wa Klabu ya Coastal Union “Wagosi wa Kaya”umesema utaanza na usajili wa timu ya vijana chini ya miaka ishirini U-20 wiki ijayo huku wakiendelea kusaka wachezaji watakaokitumikia kikosi hicho msimu mpya
wa Ligi kuu soka Tanzania bara.

Coastal Union ambayo imepanda msimu huu kucheza Ligi kuu baada ya kusota kwenye michuano ya Ligi Daraja kwanza kwa kipindi kirefu inakusudia kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha kucheza mashindano hayo kwa mafanikio.

Akizungumza jana,Mwenyekiti wa timu hiyo Steven Mguto alisema lengo la kuanza na kikosi hicho ni kuona namna ya kukiimarisha ili baadae watakaposaka hitajika kupandishwa kucheza kwenye timu ya wakubwa waweze kuchagua.

“Kama unavyojua timu zinazoshiriki michuano ya Ligi kuu zinapaswa pia kuwa na U-20 hivyo kwa kuliona hilo tunakusudia kuanza mchakato huu wiki ijayo kwani tunapokuwa na kikosi hicho baadae tutaekeleza nguvu
kwenye usajili wa watakaocheza timu ya wakubwa “Alisema.

Hata hivyo alisema hivi sasa wanasaka wafadhili ambao watawasaidia kwenye harakati zao za usajili na ushiriki wao kwenye michuano hiyo ya Ligi kuu kutokana na kikosi kutokuwa na fedha za kuwawezesha kufanya
mambo hayo.

WAZIRI DKT. KALEMANI AWASHA UMEME KWA MARA YA KWANZA KATIKA KIJIJI CHA LUMWAGO

April 21, 2018


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri Wiliam,Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi pamoja na mwenyekiti wa chama cha mapinduzi wilaya ya Mufindi wakiwa nafungua na kuwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Lumwago kata ya Upendo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani na Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi wakishangilia baada ya kuona kweli umeme umewaka katika kijiji cha Lumwago

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akiwa Kwenye furaha ya ajabu baada ya kuona wananchi wake wamefanikiwa kupata umeme katika eneo hilo ambazo minasekana linakuwa kwa kasi kubwa

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi akiongea mbele ya wapiga kura wake wa jimbo hilo

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwaonyesha wananchi wa jimbo la Mafinga Mjini kifaa cha Umeme Tayari (UMETA).


NA FREDY MGUNDA,IRINGA.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewasha umeme kwa mara ya kwanza katika Kata ya Upendo mtaa wa Lumwago uliyopo wilayani Mufindi, Mkoa wa Iringa.

Uzinduzi huo uliofanyika mbele ya mamia ya wananchi wa mtaa wa Lumwago ambao walikuwa na furaha baada ya kuona umeme huo umewaka kwa mara ya kwanza

Waziri Kalemani alifanya uzinduzi huo akiwa katika ziara ya kazi mkoani Iringa wakati wa kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na REA awamu ya tatu.

Awali, akiongea na wananchi Dkt. Kalemani alisema kuwa wananchi zaidi ya 200 wataanza kupata umeme kufuatia tukio la kurasimishwa kuwashwa kwa nishati hiyo Lumwago.

“Tunatoa kipaumbele chetu kwa sasa kwani ni kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata umeme na huduma hiyo inakuwa ya uhakika,” alisema Dkt. Kalemani.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha harakati za kufanya ukaguzi kwenye utekelezaji wa Miradi yote ya umeme mkoani humo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali za vijiji kote nchini, kuhakikisha wanajiandaa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme katika taasisi zote za umma zikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Miradi ya Maji, Masoko na nyinginezo.

Vilevile, alikumbushia umuhimu wa kila mmoja kuhakikisha baada ya kuunganishiwa umeme katika eneo lake anakumbuka kulipa bili za huduma hiyo muhimu.

“Usipolipa,Serikali itakukatia umeme hivyo kurudisha nyuma maendeleo yako,” alisisitiza.

Jambo jingine ambalo Waziri Kalemani alisisitiza ni kwa wakandarasi kuhakikisha wanawagawia bure wateja 200 wa kwanza watakaojitokeza kuunganishiwa umeme wa REA, kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kama ilivyoelekezwa na Serikali na siyo vinginevyo.

Hapo awali,mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini Cosato Chumi pamoja na kupongeza jitihada ambazo Wizara ya nishati imekuwa ikifanya nchi nzima katika kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana katika maeneo mbalimbali, pia alimwomba Waziri Kalemani kulipa upendeleo jimbo hilo kwa kuwa ndio kitovu cha uchimi wa viwanda mkoani Iringa.

“Mheshimiwa nikuombe utusaidia kwenye vijiji vilivyobaki katika jimbo langu kwasasababu wananchi wangu niwachapakazi na wapenda maendeleo” alisema Chumi

Chumi aliwamwambia waziri kuwa jimbo la Mafinga Mjini ni moja kati ya maeneo ambayo yanaviwanda vingi ambavyo vinasaidia kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuongeza ajira kwa watanzania wanaoishi katika jimbo hilo.

“Hapa tunazaidi ya viwanda arobain vya mazao ya miti na tunaviwanda vingine vingi na viwanda vyote hivi vinatumia nisharti ya umeme hivyo naomba nitoe rai kuwa mji wa mafinga unahitaji sana huduma ya nishati hii kwa kiasi kikubwa” alisema Chumi

BENKI YA DUNIA YAONESHA NIA KUSHIRIKI UJENZI RELI YA ISAKA-KIGALI

April 21, 2018


Ujumbe wa Tanzania (kulia) na ujumbe wa Benki ya Dunia (kushoto) wakiwa katika majadiliano ya miradi ya maendelea inayotarajiwa kuanza kutekelezwa mwaka ujao wa fedha.

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika Bw. Makhtar Diop akitoa ufafanuzi wa miradi ambayo itatekelezwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kulia ni Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi Bi. Bella Bird na Kushoto ni Mkurugenzi wa Mipango Benki ya Dunia ukanda wa Afrika Bi. Mamta Murthi .


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akielezea miradi ambayo itatekelezwa kwa mwaka ujao wa fedha. Kulia ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, Prof. Florens Luoga.Picha na Kitengo cha Mawasilano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango Washington D.C

Na. WFM- Washington DC

Benki ya Dunia imeonesha dhamira ya kuisaidia Tanzania katika ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) kutoka Isaka kwenda Rusumo na baadae Kigali pamoja na miundombinu mingine ya usafirishaji kama barabara ili kusaidia kuendeleza biashara na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) wakati wa majadiliano na wataalamu wa Benki ya Dunia yaliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia kanda ya Afrika Bw. Makhtar Diop, kwenye mikutano ya mwaka ya kipupwe inayoendelea mjini Washington DC Marekani.

Dkt. Mpango amesema kuwa miradi ya Kikanda ambayo Benki hiyo imeonesha nia ya kuitekeleza ni ile ya uboreshaji wa mazingira na bandari katika ziwa Victoria zikiwemo za mikoa ya Mwanza, Musoma na Kigoma na Bandari zilizoko katika Ziwa Tanganyika ambazo zitarahisisha usafiri wa kwenda Burundi na Congo.

‘Miradi hii ya Kikanda na Kitaifa ambayo Benki ya Dunia imepanga kuitekeleza kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa mwaka ujao wa fedha itahakikisha kunakuwa na mazingira endelevu na tija kwa kuwa inagusa nchi zote zinazozunguka maziwa hayo mawili’, alieleza Dkt. Mpango.

Amesema kuwa ni lazima kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira kadri iwezekanavyo ili kuendelea kufaidi rasilimali za maziwa hayo makubwa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na nchi jirani zinazozunguka maziwa hayo.

Aidha amebainisha kuwa mwakani, Benki ya Dunia imeonesha nia ya kutoa fedha kwa ajili ya tekeleza mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji eneo la Ruhuji ambapo utakapokamilika unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 300.

‘Eneo hili la sekta ya umeme ni muhimu sana kwa ajili ya maendeleo ya viwanda kwa kuwa uchumi wa viwanda hauwezi kukua bila kuwepo umeme wa uhakika’ alifafanua Waziri Mpango.

Vilevile Benki ya Dunia (WB) imekubali kuisaidia Tanzania kutoa mafunzo katika uchambuzi wa miradi mbalimbali ili kusaidia Serikali ya Tanzania kutokuingia kwenye madeni makubwa zaidi ambayo hayawezi kulipika.

Waziri Mpango alieleza kuwa kutokuwa na ufanisi wa kutosha katika kuchambua miradi ambayo inagharamiwa na fedha za mikopo inasababisha nchi kubeba mzigo mkubwa wa madeni hivyo ni vyema Tanzania ikahakikisha kuwa miradi hasa ile inayogharamiwa kwa fedha za mikopo inachambuliwa vizuri ili mradi husika unapokamilika uweze kulipa deni.

Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali itakua na miradi mingi ya kutekeleza, miongoni mwa miradi hiyo ni kupambana na tatizo la utapiamlo hivyo ni vema kama nchi ikaangalia namna bora ambayo Benki ya Dunia inaweza kusaidia katika utekelezaji wake.

“Kitaalamu mpaka mwanadamu anapofikisha siku 1000 ni kipindi muhimu sana kinachoamua maisha ya mwanadamu atakapokuwa mtu mzima atakuwa na uwezo gani wa kufikiri, kutokana na hali hiyo mtu ambaye atakua na utapiamlo uwezo wake utakua ni mdogo zaidi kulinganisha na mtoto aliyepata lishe bora’” alifafanua Dkt. Mpango.

Katika kutekeleza mradi huo Serikali itafanya kazi na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Taasisi ya Chakula na Lishe ili kuhakikisha kwamba Taifa linapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la utapiamlo.

Mikutano hiyo ya mwaka ya kipupwe kati ya ujumbe wa Serikali ya Tanzania na Wataalamu wa Benki ya Dunia imekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Tanzania itanufaika kutokana programu mbalimbali ambazo zitagharamiwa na Benki ya Dunia kwa mikopo nafuu.

MAKAMBA AFUNGUA KONGAMANO LA VYUO VYA ELIMU YA JUU KUHUSU MUUNGANO

April 21, 2018



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akifungua kongamano la vijana kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo mkoani Dodoma. Jumla ya Vyuo sita vimeshiriki katika Kongamano hilo lililofanyika katika Chuo cha Mipango, Dodoma na mada kuu ikiwa ni fursa zilizopo katika Muungano.

Sehemu ya wanafunzi kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo mkoani Dodoma wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba. Kongamano hilo limefanyika katika Chuo cha Mipango Dodoma na kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka Vyuo vya Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara, St. John, Chuo cha Mipango, Chuo cha Madini na Chuo Kikuu cha Dodoma.


Sehemu ya wanafunzi kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vilivyopo mkoani Dodoma wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba. Kongamano hilo limefanyika katika Chuo cha Mipango Dodoma na kuhudhuriwa na wanafunzi kutoka Vyuo vya Hombolo, Chuo cha Elimu ya Biashara, St. John, Chuo cha Mipango, Chuo cha Madini na Chuo Kikuu cha Dodoma.



Waratibu wa kongamano hilo, kutoka kushoto ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Muungano Bi. Lupy Mwaikambo, Bw. Sifuni Msangi Kaimu Mkurugenzi Idara ya Muungano na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Joseph Malongo wakifuatilia hotuba ya ufunguzi kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba.

#IdrisnaUber: Kampuni ya Uber imesaini mkataba na Msanii Idris Sultan kuwa Balozi wake nchini Tanzania mwaka 2018

April 21, 2018






Dar es Salaam, Tarehe 20 Aprili 2018.... Kampuni ya Uber imemtangaza msanii Idris Sultan kuwa balozi wake mpya nchini Tanzania mwaka 2018. Idris anakuwa msanii wa kwanza nchini Tanzania kuwa balozi wa Uber, programu ya usafiri yenye umaarufu mkubwa, nchini Tanzania.

Msanii huyu wa uchekeshaji, muigizaji wa tamthlia, na mtangazaji wa vipindi vya redio ametangazwa rasmi katika hafla ya kukata na shoka iliyokwenda kwa jina la #IdrisnaUber iliyohudhuriwa na wageni wachache na wanahabari wa humu inchini. Shughuli hiyo imefanyika katika mgahawa wa kifahari wa Akemi jijini Dar es Salaam.

Tangu mwanzoni mwa zoezi hili, tulifanya juhudi kubwa kuhakikisha kwamba tunampata balozi mwenye ufuasi mkubwa na atakayeiletea Uber ufanisi nchini Tanzania,amenukuliwa Bi.Elizabeth Njeri, Meneja wa Masoko wa Uber Kanda ya Afrika Mashariki. Idris Sultan ni mcheshi na ni msanii ambaye hafanyi mambo yake kwa mazoea, pia anaheshimika katika tasnia ya uchekeshaji,tamthlia, na utangazaji wa vipindi vya redio. Tuna imani kwamba Idris atailetea Uber tija kubwa kwa sababu ni mzalendo kweli kweli - yeye ni kielelezo cha Utanzania na anawasiliana na mashabiki wake kupitia mitandao ya jamii kila wakati. Hizi ndizo sifa tunazosistiza tunapotaka kuwa na mkataba na mabalozi wa kampuni yetu kwa sababu zinasaidia sana katika kuonesha kwamba tunajali maslahi ya wasafiri na madereva wanaotumia mfumo wetu nchini Tanzania.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Bw Alfred Msemo; Meneja Msimamizi wa Uber nchini Tanzania, alisema; “Kampuni ya Uber inajituma kutumia uwezo wake kupitia oparesheni zake kimataifa ili kuwa karibu na wateja wake humu nchini. Mchango wa Idris Sultan katika muziki wa Tanzania unaendana na dhamira yetu ya kujenga kampuni ya kimataifa inayogusa maisha ya madereva na wasafiri wanaotumia mfumo wetu hapa nchini. Tutaendelea kuwahudumia wasafiri wetu sambamba na kutoa fursa za ajira kwa madereva wanaotumia mfumo wetu

Idris alifurahi sana alipotangazwa kuwa Balozi wa Uber nchini Tanzania; “Nimefurahi sana na ni heshima kubwa kwangu kupata fursa hii adimu ya kushirikiana na Uber,kwa sababu mimi nishabiki mkubwa wa mapinduzi yaliyoletwa katika sekta ya usafiri kupitia kwa mfumo wake kote duniani. Nimefurahi kuona jinsi Uber imepata umaarufu jijini Dar es Salaam, binafsi mara nyingi mimi hutumia usafiri wa uberX nikiwa na marafiki zangu kwenye mitoko yetu ya jioni na sasa wamaleta huduma nyingine ya bajaji; uberPOA ambayo nina hamu sana kuitumia - utaniona hivi karibuni. Uber inaendelea kubadilisha maisha ya maelfu ya madereva jijini Dar es Salaam sambamba na kuwapa wasafiri uhuru wa kuchagua usafiri wanaotaka. Nimefurahi sana kuwa sehemu ya kampuni ambayo inajituma kuleta mabadiliko chanya katika maisha yetu.

Baadaye kwenye hafla hiyo, Idris alipanda jukwaani na kuwatumbuiza mashabiki, wanahabari,na wafanyakazi wa Uber kwa kionjo cha kazi yake ya uchekeshaji. Msanii huyo na mshindi wa zamani wa shindano la Big Brother Africa alivunja mbavu za umati huo kwa vichekesho vyake.

Tangazo hili linakuja siku chache tangu Uber ilipo tangaza kushirikiana na Tigo kwenye mpango
ambao wateja wa Tigo wanapata bando za bure wanapotumia programu ya Uber. Ushirikiano
huu wa kipekee nchini Tanzania umekuwa na manufaa makubwa kwa wasafiri na madereva
wanaotumia Uber na umechochea wasafiri na madereva zaidi kujiandikisha kutumia programuya Uber nchini Tanzania.

WANAFUNZI LUGALO WALIA NA MIUNDOMBINU KWA WALEMAVU

April 21, 2018

Na Mwandishi Wetu, IRINGA
WAHITIMU wa kidato cha sita wa Sekondari ya Lugalo mkoani hapa wameiomba Serikali kuisadia kuboresha miundombinu kwa ajili ya wanafunzi walemavu.

Katika Risala yao kwa mgeni Rasmi wamesema pamoja na mafanikio mengi waliyoyapata kupitia shule hiyo bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kukosekana kwa uzio, mfumo mbovu wa maji taka kukosekana kwa karatasi maalum za walemavu wasioona pamoja na kutokuwa na miundombinu rafiki kuwezesha kuwa salama katika mazingira ya shule kwa wanafunzi wenye uhitaji maalum pamoja na uhaba wa waalimu wa Sayansi.

Akijibu Risala ya wanafunzi hao, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma shuleni hapo, Nayman Chavalla, kupitia kampuni inayoitwa Lugalo Associate Company Limited wameanza kukarabati nyumba ya Mkuu wa shule pamoja na ya Makamu wa shule na kuahidi kuwa umoja huo utaendelea kusaidia shule hiyo endapo matokeo ya taaluma yataboreshwa.

Chavalla ameongeza kuwa Umoja huo unayo nia ya dhati katika kusaidia kutatua changamoto za elimu shuleni hapo na kuwataka walimu kufuta daraja sifuri na daraja la nne katika matokeo ya kitaifa ili kuleta motisha kwa wadau wanaochangia maendeleo ya shule.

Pia amesema pamoja na kuwa Serikali inahamasisha Elimu Bure lakini bado jukumu la kujibidiisha katika masomo na kuinua viwango vya ufaulu ni la Mwanafunzi na waalimu wenyewe katika kukuza taaluma yenye viwango.

Mmoja wa wahitimu mwenye ulemavu wa macho, Elizabeth Mwaisoba mwenye umri wa miaka 18 amesema kuna haja kwa Serikali kuendelea kusaidia wazazi wenye watoto wenye uhitaji maalum katika kupata elimu kwani inahitaji kipato kikubwa katika kuwahudia wanafunzi wenye uhitaji wa ziada na kuiomba Wizara husika kutillia mkazo suala la komputa zenye sauti ili nao waweze kwenda sambamba na teknolojia ya sasa.

Felista Mkesela, mwenye ualbino, amesema ipo haja ya waalimu kuona umuhimu wa kuweka vifaa vya kukuza maandishi ya ubaoni na kuongeza muda wa ziada kwa wanafunzi walio na ulemavu wawapo darasani, kwani kuwapa muda sawa na wanafunzi wa kawaida kunaathiri kufanya vizuri katika masomo yao.
Mkuu wa Shule hiyo, Benjamin Kabungo, amesema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 63 wenye ulemavu wakiwemo wasioona, albino, wenye uoni hafifu, na walemavu wa viungo na kwamba walimu 4 wa Elimu Dumishi, awali Shule hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1945 na kujulikana kama The H.H Aga Khani, pia imeanzisha ufugaji wa viumbe wakiwemo panya weupe kwa ajili ya kufanya utafiti wa Kisayansi.

Maendeleo Vijijini Blog (Kwenye Rasilimali Kulikosahaulika) Twitter: @MaendeleoVijiji Instagram: #Maendeleo_Vijijini Cell: +255 - 0656 - 331 974 Whatsapp: +255 - 656 - 331 974