Polisi Tanga wakamata Kete 46 na misokoto 40 ya Madawa ya kulevya aina ya bangi na Kokan.

July 12, 2013
(KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Tanga,Constatine Massawe akizungumza na waandishi wa habari mapema leo ofisini kwake) 
 
Na Oscar Assenga,Pangani.
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga limefanikiwa kukamata kete 46 na misokoto 40 ya madawa ya kulevya aina ya Kokain na bangi baada ya kufanya msako maeneo ambayo yalikuwa yakisadikiwa wanakaa watumiaji wa madawa hayo wilayani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga,Constatine Massawe alithibitisha kukamatwa madawa hayo ni kueleza tukio hilo lilitokea Julai 10 mwaka huu baada ya polisi kuvamia eneo hilo na kuwatuka watumiaji wanne ambapo walikuwa wakiyatumia huku

Amesema kukamatwa kwa madawa hayo kumetokana taarifa ambazo jeshi zililipata kutoka kwa wananchi wa maeneo hayo na kuitaka jamii kuwa inatoa taarifa pindi wanapoona vitendo viovu kwenye jamii zao vinafanyika.

Massawe aliwataja waliokamatwa katika tukio hilo ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani ni Shabani Ramadhani (20)mvuvi na mkazi wa Malindi wilayani Pangani,Mohamed Kijiba mvuvi na mkazi wa Fungoni  na Iddi Hamdani (21)mvuvi mkazi wa Fungoni mjini Pangani.

Wakati huo huo,Kamanda Massawe alisema watu wawili walikamatwa na misokoto ya madawa ya kulevya aina ya bangi katika tukio hilo na kuwataja waliokamatwa ni Mohamed Kijiba ambaye alikutwa na bangi licha ya kukutwa pia na kokain na Rajabu Madaraka (28)wote wakazi wa Fungoni wilayani Pangani.

Kamanda Massawe ametoa wito kwa vijana kuacha kujihusisha na utumiaji na uuzaji wa madawa ya kulevya badala yake watafute kazi nyengine halali za kufanya ambazo zinaweza kuwaingizia kipato ili wapate maendeleo.


Mwisho. 

POULSEN, MICHO WATABIRI MECHI KALI

July 12, 2013
 
Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam.
Makocha wa timu hizo Kim Poulsen wa Taifa Stars na Sredojvic Micho wa The Cranes wamesema mechi ya kesho itakuwa ngumu kwa vile kila mmoja amejiandaa kuhakikisha anafanya vizuri.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari leo, makocha wote waliezea ubora wa wapinzani wao, lakini wakasisitiza kuwa wanaingia uwanjani kuhakikisha wanashinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kwa ajili ya mechi ya marudiano itakayochezwa Kampala wiki mbili zijazo.
 
Kim alisema Uganda ndiyo inayoongoza kwa ubora wa viwango vya FIFA katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo ni changamoto kwao ingawa wachezaji wake tayari wamejipanga vizuri kwa ajili ya mechi hiyo.
Naye Micho aliyefuatana na nahodha wake Hassan Wasswa alisema Taifa Stars imekuwa ikifanya vizuri tangu iwe chini ya Kim, na itakuwa na wachezaji tisa wa kikosi cha kwanza kinachocheza mechi za mchujo za Kombe la Dunia wakati kwa upande wake atakuwa na wachezaji wawili tu.
 
 

TAIFA STARS SASA MMEIVA KUPAMBANA- TENGA

July 12, 2013
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kikosi cha Taifa Stars sasa kina uwezo wa kushindana katika mashindano yoyote, kwani tayari kimeiva.
Akizungumza na wachezaji wa timu hiyo kambini kwao hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam, Rais Tenga aliwaambia kuwa kiwango walichoonesha kwenye mechi zilizopita za mchujo za Kombe la Dunia dhidi ya Morocco na Ivory Coast kimethibitisha hilo.
“Kiwango mlichoonyesha katika mechi hizo kila Mtanzania anayewafuatilia amekiona, hivyo hatuna shaka kuwa mtatuwakilisha vizuri kwenye mechi ya kesho dhidi ya Uganda,” amesema Rais Tenga na kuwataka kupigana kwa ajili ya Tanzania.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kesho (Julai 13 mwaka huu) saa 9 kamili alasiri Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itacheza na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Rais Tenga amesema TFF, mdhamini Kilimanjaro Premium Lager, Kamati ya Ushindi na Watanzania kwa ujumla wanawaunga mkono kwani wamekuwa wakiboresha kiwango chao kila wanavyozidi kucheza mechi tangu wake chini ya Kocha Kim Poulsen, Mei mwaka jana.
Wakati huo huo, Rais Tenga ameahidi kumpatia tiketi ya kwenda Uganda kwenye mechi ya marudiano mshabiki Wiseman Mwakyusa Luvanda anayetembea kwa miguu kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kesho.
“Kama ni kweli anakuja kwa kutembea, huyu ameonyesha kiwango kikubwa cha uzalendo kwa timu ya Taifa, nitampatia tiketi ya kwenda Kampala kuishangilia Taifa Stars kwenye mechi ya marudiano,” amesema Rais Tenga.