KIINGILIO MECHI YA SERENGETI BOYS 2,000/-

July 13, 2014
Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Afrika Kusini (Amajimbos) itachezwa kwa kiingilio cha sh. 2,000.

Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam ndiyo utakaokuwa mwenyeji wa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 9 kamili alasiri.

Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Shelisheli. Mwamuzi wa kati ni Allister Barra wakati wasaidizi wake ni Gerard Pool na Jean Joseph Felix Ernest wakati mezani atakuwa Nelson Emile Fred.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Andriamiasasoa Doda Nirimboavonjy kutoka Madagascar.

Kikosi cha Serengeti Boys chini ya kocha Hababuu Ali Omari kipo kambini kwa zaidi ya wiki mbili sasa kikijiandaa kwa mechi hiyo. Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 nchini Afrika Kusini.

Wakati huo huo, Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya michuano hiyo ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Rwanda na Uganda.

Mechi hiyo itachezwa nchini Rwanda kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu. Waamuzi wa mechi hiyo watatoka Burundi wakiongozwa na Pacifique Ndabihawenimana.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

SERIKALI IMETENGA BILION 2.8 KUKAMILISH MIRADI YA MAJI VIJIJI KUMI KATA YA KWEDIBOMA WILAYANI KILINDI.

July 13, 2014
Rais Jakaya Kikwete akifungua bomba la maji mara
baada ya kuzindua mradi wa maji  kijiji cha Kwediboma kata ya
Kwediboma wilayani Kilindi Mkoani Tanga wenye thamani ya shilingi
milioni 571,361,391 ambapo mpaka kufikia hatua hiyo ya kuzinduliwa
ulikuwa umegharimu kiasi cha sh.milioni 316,197,327, Rais Kikwete yupo
mkoani Tanga katika ziara ya kikazi ya siku tano aliyoanzia wilaya ya
Kilindi
KILINDI.
KATIKA kukabiliana na tatizo la maji katika kata ya Kwediboma iliyopo  wilayani Kilindi serikali imetenga kiasi cha sh. Bilion 2.8 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa maji safi kwenye vijiji kumi vinavyounda kata hiyo.

Rais Kikwete amebainisha hayo jana wakati akihutubia wananchi wa kata
  ya Kwediboma kabla ya kuzindua ujenzi wa mradi wa Maji ya Bomba wa kijiji cha Kwediboma unatekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza sekta ya maji kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.

Alisema fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao wa
  2014/2015 ili kusaidia kupunguza ukubwa wa tatzio la upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi hasa waishio maeneo ya vijijini.

"Ndugu zangu pamoja na serikali kuwekeza fedha hizi tambueni kwamba
  kama jamii mnalo jukumu kubwa la kuhakikisha mradi huu unatunzwa ili uwe endelevu kwa ajili ya kutoa huduma kwenu na vizazi vijavyo...naomba wananchi waote washiriki kutimiza jukumu hili ili kutoa huduma endelevu", alisema rais.

Vijiji vitakavyonufaika na huduma ya maji kupitia fedha hizo ni

Mpalahala, Kwedigole,Kileguru,Mzinga ambavyo kwa sasa havina huduma ya maji hasa baada ya ya chanzo chao tegemezi ambacho kilikuwa ni Malambo mawili yaliyojengwa na halmashauri kupitia mradi wa DADPS kubomolewa na mvua msimu uliopita.
Rais Jakaya Kikwete kushoto akimtwisha ndoo ya maji
mkazi wa kijiji cha Kwediboma kata ya Kwediboma wilayani Kilindi
Mkoani Tanga mara baada ya kuzindua mradi wa maji ya bomba kwenye
kijiji hicho wenye thamani ya kiasi cha sh.milioni 571,361,391 ambapo
mpaka kufikia hatua ya uzinduzi huo zilikuwa zimekwisha kutumika kiasi
cha sh.milioni 316,197,327,Rais Kikwete yupo mkoani Tanga katika ziara
ya kikazi ya siku tano aliyoanzia wilaya ya Kilindi
Awali akisoma taarifa kuhusu mradi huo, Katibu wa Kamati ya Mradi huo
  Ibrahim Abdallah alisema hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh. 517,364,391 na kwamba mpaka sasa zimetumika sh. 316,197,327 kwa ajili ya kukamilisha kazi za awamu ya kwanza ya mradi.

""Mradi huu unaotarajiwa kunufaisha wakazi 7,139 wa kijiji cha

Kwediboma ulianza mwaka 2010 baada ya kuibuliwa na wananchi ....katika awamu ya pili iliyoanza mwaka 2013 tulijenga miundombinu pamoja na vituo 24 vya kusambazia maji kijijini, nyumba ya kuhifadhia mitambo ya kusukumia maji toka kwenye chanzo , tangi, kufunga dira", alisema.

Katibu huyo alisema kubomoka kwa malambo hayo tayari kulisababisha
  ugomvi mkubwa baina ya wakulima na wafugaji ambao wamekuwa wakihama hama kusaka malisho.

JK AKERWA NA WATENDAJI WA VIJIJI NA KATA KUPOKEA RUSHWA YA MBUZI NA KONDOO .

July 13, 2014
PANGANI.
RAIS Jakaya Kikwete amewaonya watendaji wa vijiji na kata kuacha kupokea rushwa ya Mbuzi na Kondoo ili kuwaruhusu wafugaji kuingia kwenye maeneo yao kwani kufanya hivyo kunapelekea kuibuka migogoro kati ya wakulima na wafugaji hali inayotishia usalama wa wananchi hao.

Kauli hiyo ya Mkuu wan chi alitoa wakati akiwahutubia wananchi wa
  wilaya ya Pangani kwenye uwanja wa Sakura akiwa katika ziara yake wilayani hapa iliyoambatana na uzinduzi wa miradi ya maendele.

Alisema kimsingi suala la migogoro hiyo inachagiwa na viongozi hao 
ambao wamekuwa wakishindwa kuweka mipango imara ambayo inaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo hayo kwa kugeuka kuwa chanzo chake hali inayopelekea wananchi kuichukua serikali.

      “Mimi naambieni watendaji wa vijiji na kata ambao mnachangia
kuwepo migogoro kwenye maeneo yenu acheni tabia hiyo mara moja kwani ukibainika hatutaweza kukuvumilia lazima uchukuliwe hatua zinazostahili kumaliza tatizo hilo “Alisema Rais Kikwete.

Aidha alisema kuwa sio kama viongozi hao wanashindwa kuweka mipango 
mizuri ya kulipatia ufumbuzi tatizo la migogoro ya ardhi bali miongoni mwao wamekuwa wakichangia hali hiyo kwa kuwakaribisha wageni kwenye maeneo yao bila kufuata taratibu zilizopo.

Akizungumzia suala la mifugo kwenye maeneo ambayo yameonekana kuwa na 
misuguano ya mara kwa mara Rais Kikwete alisema umefika wakati wa viongozi wake kuyatafutia ufumbuzi kwa kuweka utaratibu utakaowezesha kuondoa kero hizo.

Aliongeza kuwa katika jambo hilo Serikali imeweka mpango mkakati kwa 
mkoa mzima wa Tanga ambao utasaidia kupunguza tatizo la ardhi ili kuwapa fursa wananchi kufanya shughuli za kimaendeleo badala ya kuendelea kufikiria namna ya kutatua tatizo hilo.

Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa hapa nchini inayokabiliwa na 
migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji ambao hupelekea wakati mwengine kupelekea mapigano ikiwemo kuharibu miundombinu iliyopo kutokaa na ufinyu wa ardhi.

Aliwataka viongozi kutengeneza utaratibu mzuri ambao hautaleta

migogoro kwenye maeneo ambayo wafugaji hao wanaoishi ili waweze kuishi kwa utulivu ikiwemo kuzitaka kamati za ulinzi na usalama za wilaya ya mikoa kuhakikisha wanazipatia ufumbuzi kero hizo.