SERIKALI YAFURAHISHWA KUANZISHWA KWA KAMPUNI AYA BIMA YA "CRDB INSURANCE COMPANY"

June 19, 2024

  

 Kamishna wa Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamaja (katikati) akifurahia uzinduzi rasmi wa kampuni tanzu ya Benki ya CRDB inayotoa huduma za bima ‘CRDB Insurance Company (CIC) Ltd’ katika hafla iliyofanyika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam 18 Juni 2024. Wengine pichani Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware (wapili kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CIC, Omary Mwaimu (wakwanza kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa CIC, Wilson Mnzava.
 
==========     ==========   =========
 
Dar es Salaam. Tarehe 18 Juni 2024: Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini, Dkt. Charles Mwamaja ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha kampuni tanzu ya bima ya ‘CRDB Insurance Company (CIC)’ ambapo amesema itasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia ufikiaji wa malengo ya serikali ya kuongeza ujumuishi wa bima kufikia asilimia 50 kwa Watanzania weny eumri wa kuanzia miaka 18 ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Mwamaja ameyasema hayo alipoizindua kampuni hiyo jijini hapa ukiwa umepita mwaka mmoja tangu ipate leseni ya kutoa huduma za bima zisizo za maisha kwa Watanzania ili kuwalinda dhidi ya majanga yanayoweza kujitokeza. Dkt. Mwamaja ameitaka CIC kutumia uzoefu na wigo mpana wa Benki ya CRDB kuwafikia wananchi hasa kwa kuzingatia kuwa Benki hiyo imeenea katika halmashauri zote nchini.

Dkt. Mwamaja ambaye amemwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba  amesema sekta ya bima nchini bado ni changa lakini ina fursa kubwa sana za kuwahudumia Watanzania iwapo elimu itatolewa na makampuni ya bima kuwekeza katika ubunifu wa bidhaa zitakazogusa makundi mbalimbali ya wateja, Taifa litafikia lengo lake la kuongeza ujumuishi wa bima ifikapo mwaka 2030.
“Niwapongeze kwa ubunifu ambao mmeanza nao kwa kuja na bima ya kilimo kwa kushirikiana na ACRE Africa. Kilimo ni sekta muhimu katika uchumi wetu inayoajiri watu wengi zaidi. Iwapo mtafika mpaka vijijini mtatoa nafuu kwa wakulima wengi kulinda mazao na mifugo yao jambo ambalo litasaidia kuwapa utulivu wa nafsi a wakulima kupitia bima hii. Tunapaswa kujua kuwa huduma bora bima ni msingi wa ustawi wa uchumi na kichocheo cha uwekezaji,” amesema Dkt. Mwamaja.

Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa taasisi ya kwanza fedha nchini kuanzisha kampuni tanzu ya bima. Dkt. Saqware amesema CIC inakwenda kuitanua sekta ya bima nchini jambo litakaloongeza ushiriki wa Watanzania katika kutumia huduma za bima. 
Akieleza ujumuishi wa huduma za bima nchini, Dkt. Saqware amesema hadi mwishoni mwa mwaka 2023 kulikuwa na watumiaji wa bima milioni 12 kutoka watu milioni 6 waliokuwa wanatumia bidhaa hizo mwaka 2022. Dkt. Saqware amesema kupitia jitihada zinazotekelezwa na Serikali ikiwamo kuanzishwa kwa kanuni ya bima za lazima kunatarajiwa kuongeza ujumuishi mara dufu kila mwaka kufikia lengo lililowekwa. 

“Serikali pia imeanzisha konsotia ya bima ya mafuta na gesi, pamoja ya ile ya kilimo na mifugo. Ni imani yangu kuwepo kwa makampuni kama CIC kutasaidia kufanikisha malengo kwa kuwekeza mitaji ili sehemu kubwa ya ada za bima ziwe zinabaki nchini,” alisema Kamishna Saqware huku akiitaka kampuni hiyo kuwekeza katika weledi kwa wafanyakazi na kusimamia sera na misingi iliyowekwa kisheria ili kuepukana na udanganyifu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Omary Mwaimu amemwambia Dkt. Mwamaja kuwa lengo walilonalo ni kuifanya CIC kuwa kampuni ya bima chaguo nambari moja kwa Watanzania wote kupitia huduma bunifu na nafuu ambazo zitatoa fursa kwa makundi mbalimbali ya wananchi kujiunga na hivyo kuchochea ujumuishi wa bima nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuanzishwa kwa CIC ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Benki ya CRDB kutanua wigo wake wa kufikisha huduma za fedha ikiwamo bima kwa Watanzania. 
Nsekela amebainisha kuwa uamuzi huo umetokana na hali ya ufikiaji mdogo wa huduma za bima nchini huku akieleza kuwa mkazo mkubwa wa kampuni hiyo ya CIC umeelekezwa vijijini ambapo wengi wapo nje ya mfumo rasmi wa bima.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa CIC, Wilson Mnzava amewakaribisha mawakala na madalali wa bima, wateja, pamoja na wadau wengine kuzitumia huduma za CIC akiahidi kuwa watapata utulivu wa maisha, utulivu wa nafsi, utulivu wa biashara, na utulivu wa uchumi wao kipindi majanga yanapojitokeza.
CRDB Insurance Company (CIC) inakuwa kampuni tanzu ya nne ya Benki ya CRDB baada ya zile za CRDB Bank Burundi, CRDB Bank DR Congo, na CRDB Bank Foundation. CIC inatoa huduma za bima zisizo za maisha ikiwamo bima ya magari, bima ya nyumba, bima ya vyombo vya moto, bima ya biashara, bima ya usafirishaji, bima ya safari, bima ya ukandarasi, na bima ya mitambo.









KIGOMA WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI UBORESHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA

June 19, 2024

 Na. Mwandishi Wetu, Kigoma


Wananchi mkoani Kigoma wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao wakati wa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura linalotarajiwa kuzinduliwa mkoani humo tarehe 01 Julai, 2024.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Kigoma uliofanyika leo tarehe 19 Juni, 2024 katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji.

Jaji Mwambegele amewapongeza wadau wa uchagizi na wananchi kwa ujumla kwenye mkoa wa Kigoma kwa mkoa wao kuteuliwa kuwa sehemu ya uzinduzi wa uboreshaji huo ambao utafanyika kwenye uwanja wa Kawawa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB).

“Uboreshaji wa daftari utazinduliwa hapa mkoani Kigoma tarehe 01 Julai, 2024 na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Tayari Tume imeamua kwamba uzinduzi huo ufanyike katika uwanja wa Kawawa uliopo hapa kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji,” amesema Mhe. Mwambegele.

Ameongeza kuwa Tume ilifikia uamuzi wa kufanya uzinduzi huo kwenye mkoa wa Kigoma baada ya kuzingatia mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mwamko mkubwa wa wananchi kujitokeza kwenye uboreshaji wa Daftari uliofanyika mwaka 2019/20.

“Ni matarajio ya Tume kuwa mtakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza taarifa na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao ili kuendeleza sifa hii ya mwamko wa wananchi kujitokeza kwa wingi,” amewaambia wadau hao.

Amesema, uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari utatanguliwa na shughuli mbalimbali za uhamasishaji ikiwa ni pamoja na matangazo na tamasha la uborshaji wa Daftari ambalo litafanyika siku ya Ijumaa tarehe 28 Juni, 2024 kwenye uwanja wa Kawawa.

Wakati akiwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K amesema uboreshaji kwa awamu hii ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 na kuongeza kwamba baada ya mkoa wa Kigoma uboreshaji utaendelea kwenye mikoa ya Katavi na Tabora.

“Zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Tunatarajia zoezi litakamilika Machi, 2025,” amesema Bw. Kailima.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Kigoma uliofanyika leo tarehe 19 Juni, 2024 katika Halmashauri ya Kigoma Ujiji. Tume inataraji kufanya uzinduzi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura tarehe 01 Julai, 2024. (Picha na INEC). 

Sehemu ya wadau wa uchaguzi kutoka Mkoanbi Kigoma wakishiriki katika kikao cha siku moja baina ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na wadau hao ikiwa ni maandalizi kuelekea uzinduzi wa Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utakaofanyika Julai 1, 2024 mkoani Kigoma. (Picha na INEC). 

ACHENI MATUMIZI HOLELA YA DAWA - WAZIRI UMMY

June 19, 2024

 


Na WAF - Arusha

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Watanzania kuacha matumizi holela holela ya Dawa ili kuepuka usugu wa vimelea dhidi ya dawa hususani za antibaotik kushindwa kufanya kazi ipasavyo na kugharimu maisha na nguvu kazi ya Taifa.

Waziri Ummy amesema hayo leo Juni 19, 2024 Jijini Arusha wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya nchi zacMashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) ambapo mgeni Rasmi alikuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.

"Usugu wa vimelea vya magonjwa Dhidi ya Dawa ni janga kubwa ambalo jamii ya Watanzania inapaswa kupambana nalo kwa dhati kwa kuwa madhara yake ni Mkubwa na yanagharimu fedha nyingi." Amesema Waziri Ummy

Amesema, ikiwa umeandikiwa dawa unywe kwa siku Tano basi maliza siku zote Tano, zingatia matumizi sahihi ya dawa hususani za antibaiotik na usitumie dawa bila ya kuandikiwa na daktari au mtaalam wa mifugo, unakuta dawa za mifugo anapewa binaadamu tuepuke kutengeneza janga kubwa ambalo litakwenda kugharimu Sekta ya Afya kwa siku za usoni kwa kuendelea na matumizi holela ya dawa." Amesema Waziri Ummy

Waziri Ummy ameongeza kuwa madhara ya matumizi holela ya dawa hupelekea mgonjwa kukaa hospitalini ama kuugua kwa muda mrefu bila kupona lakini pia mgonjwa kutumia gharama kubwa kwa ajili ya kujiuguza na hata kupoteza maisha kutokana na changamoto hiyo ya usugu wa vimelea dhidi ya Dawa

"kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa Yasiyoambukiza katika ukanda huu, Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) imejipanga kuja na Tafiti zitakazo saidia kuja na ushahidi wa kisayansi utakao saidia mbinu sahihi za kupambana na magonjwa hayo na kuweka sera nzuri zitakazosaidia kufikia suala la Afya kwa wote.

Aidha, Waziri Ummy amesema katika miaka 50 ya Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) ku
na mengi makubwa ya kujivunia kwa kuwa Taasisi hiyo imekuwa ikitoa msaada wa kiufundi katika masuala ya afya na nchi za ukanda wa mashariki, kati na kusini mwa Afrika wataendelea kuongeza mashrikiano baina ya nchi wanachama ili kubuni na kuendeleza afua zaidi za Afya ambazo zitasaidia kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta hiyo barani Afrika

”Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) wametusaidia sana sisi kama Tanzania katika kufanya tafiti za kisayansi kuhusu magonjwa ya kuambukiza lakini kubwa ni kuweza kutusaidia tukatengeneza mpango mkakati wa kupambana na magonjwa sugu pamoja na majanga kwa kujitathimini katika kupambana na magonjwa makubwa ya kuambukiza kama Ebola, Covid na homa ya bonde la ufa na kudhamini masomo kwa wataalamu wa Afya." Amesema Waziri Ummy.





VIJANA, WAKINA MAMA TANGA WATANGAZIWA FURSA YA KUJIKWAMUA KIUCHUMI

June 19, 2024



Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organazation (TOIO) Shaukatali Hussein akiwaonyesha wanahabari ambao hawapo pichani bajaji inayotumia umeme walioyoitengeneza

Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organazation (TOIO) Shaukatali Hussein akikagua moja ya bajaji ambazo zinatarajiwa kuunganishwa na baadae kutengenezwa kwa ajli ya kutumia umeme

Na Oscar Assenga, TANGA

VIJANA na Wakima mama waliopo katika Jiji la Tanga wametangaziwa fursa za kuchangamkia mafunzo ya namna ya kuviunga, kuvirekebisha na kutengeneza Bajaji za Umeme, Pikipiki, na Baiskeli hatua itakayowawezesha kujikwamuaa kiuchumi.

Hayo yalisemwa leo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Open Innovation Organazation (TOIO) Shaukatali Hussein wakati akizungumza kuhusu namna walivyojipanga kuendelea kuiwezesha jamii ya wakazi wa Jiji hilo.

Alisema kwamba ili kufikia lengo hilo wameona waanze kutoa mafunzo ya kuunga vitu vya umeme na mafunzo hayo yatatolewa June 26 na 27 mwaka huu jinsi ya kuunga bajaji za umeme na kuanzia saa 4 asubuh hadi saa nane mchana .

“Kwa sasa tumeona njia nzuri ya kuweza kuwakwamua kiuchumi wakina mama na vijana ni kuwapa mafunzo hayo na tunaamini watakapomaliza watapata mwanga mzuri wa kuona namna ya kuzichangamkia fursa hizo”Alisema

Aidha alisema mafunzo ya vijana na wakina mama jinsi ya kuviunga na kuvitengeneza na kuvirekebisha na namba ya kuviendesha kwani hiyo ni fursa mpya ambazo zinaweza kuinua uchumi wao.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka vijana waliopo mtaani kutumia fursa za kidigitali mpya wanapoelekea pikipiki za umeme na bajaji za umeme,baiskeli zinaingia mtaani.