PSPF YAWAPIGA MSASA WATUMISHI OFISI YA RAS DAR ES SALAAM

January 03, 2017



Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Bw. Adam Mayingu, (kulia), akipeana mikono na Katibu Tawala Msaidizi (anayeshughulikia masuala ya serikali za mitaa), jijini Dar es Salaam, Bi. Merry Assey, baada ya kufungua semina ya mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam, iliyoandaliwa na Mfuko huo na kufanyika Januari 3, 2017 kwenye makao makuu ya PSPF Golden Jubilee Towers jijini.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said
MFUKO wa Pensheni wa PSPF, umeendesha semina ya mafunzo kwa watumishi wa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, ili kuwajengea uwezo wa kushughulikia matatizo ya wananchi ambao ni wanachama wa Mfuko huo.
Mafunzo hayo ya siku mbili, yameanza leo Januari 3, 2017, na kufunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi (sehemu ya serikali za mitaa), Bi. Merry Assey kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa ea Dar es Salaam, Paul Makonda.
“Niipongeze PSPF kwa kuandaa semina hii ambayo inatoa fursa ya watumishi hawa waliohudhuria katika mafunzo haya kuelewa huduma na shughuli zinazofanywa na Mfuko huu na kwa maana hiyo iwe rahisi kwenu kutatua kero za wananchi wanaofika pale Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kutafuta ufumbuzi hususan kwa wanachama wa Mfuko huu,.” Alisema Bi. Assey, wakati akifungua semina hiyo.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Bw. Adam Mayingu, alisema, PSPF ilifikia uamuzi wa kuandaa semina hiyo kufuatia wazo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye alitaka kujengewa uwezo kwa watumishi wa Ofisi yake ili waweze kuwahudumia vema wananchi wakiwemo wanachama wa PSPF.
“Nililipokea wazo hilo na sisi PSPF tukaona ni fursa nzuri kwa kuwaelimisha watumishi hawa ambao, ninahakika baada ya mafunzo haya, watakuwa mabalozi wetu wazuri lakini pia na wao watajiunga na Mfuko huu.” Alisema Bw. Mayingu.
Mada mbalimbali zilitolewa kwa wanasemina hao ikiwa ni pamoja na ile ya shughuli za Mfuko iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma wa Mfuko huo, Bi. Neema Muro, Kaimu Meneja Mafao, Bw. Haji Moshi na Maafisa wengine wa Mfujko huo.
 Bi. Merry Assey, akifungua semina hiyo
 Baadhi ya washiriki wa semina wakifuatilia kwa makini

RIDHIWANI ATEMBELEA WAFANYABIASHARA, AWATAKA WAHUDHURIE MIKUTANO

January 03, 2017


 Mbunge wa jimbo la Chalinze, Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani Mwanasheria Ridhiwani Kikwete akizungumza na baadhi ya wakaazi wa kijiji cha Ruvu Darajani alipokwenda kwa ajili kusikiliza mkutano wa kusomwa mwa mapato na matumizi ya kijiji ikiwa ni utekelezji wa agizo lililotolewa na Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Alhaj Hemed Majid la kuwataka viongozi wote wa vijiji vinavyounda wilaya hiyo kuitumia siku ya Jan 3 kuwasomea mapato na matumizi wannchi wao, hata hivyo mkutano huo umesogezwa mpaka Alhamisi ya Jan 5.
  Mbunge wa jimbo la Chalinze, Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani Mwanasheria Ridhiwani Kikwete akiwaunga mkono wafanyabiashara wa samaki wa kukaanga wanaofanya biashara zao katika eneo la Ruvu Darajani pembezoni kidogo mwa barabara Kuu ya Dar es Salaam- Chalinze, Morogoro- Segera, alipowatembelea kushuhudia wanavyofanya shughuli zao hizo. 
Mbunge Ridhiwani Kikwete akiwasikiliza wafanyabiashara waaouza bidhaa mbalimbali hapa wauza bidhaa jamiyambogamboga wakizungumza na mbunge wao.

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO ZINGATIENI SHERIA, KANUNI NA MAADILI, MSIKUBALI KUYUMBISHWA NA MTU.

January 03, 2017


 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw.kailima Ramadhani akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma. 
Baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao wakati wa Uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017 leo mjini Dodoma. Picha na Aron Msigwa - NEC


Na. Aron Msigwa - NEC
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI imewataka Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi mdogo wa Udiwani utakaofanyika katika Kata 20 za Tanzania Bara na Ubunge katika jimbo la Dimani Visiwani Zanzibar Januari 22, 2017 kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ili Uchaguzi huo uwe Huru na wa Haki.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhan wakati akifungua mafunzo ya siku 3 ya Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa wa Uchaguzi leo mjini Dodoma.

Mkurugenzi Kailima amewataka Wasimamizi hao kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali katika kushughulikia mambo yatakayojitokeza wakati wa uchaguzi huo.

Katika kutimiza majukumu yao wawe tayari kutoa ufafanuzi juu masuala mbalimbali kwa kuzingatia sheria na kutokuwa tayari kukubali kuyumbishwa na mtu yeyote atakayekiuka miongozo, sheria na kanuni za Uchaguzi.

Amewataka Wasimamizi hao watende mambo yote kwa kuzingatia kanuni na Sheria na kutoa maamuzi sahihi kwa mustakabali wa Taifa na kuwasisitiza kuepuka kutoa upendeleo katika maamuzi wanayoyafanya na wasikubali kuyumbishwa na matakwa ya baadhi ya watu.

Amewaeleza kuwa milango ya Tume iko wazi pale watakapohitaji ufafanuzi huku akitoa wito kwa Wasimamizi hao kuwasiliana na watendaji wa Tume katika mambo yanayowatatiza ili wapate ufafanuzi.

Aidha, amewataka wawe makini na hatua ya utangazaji wa matokeo kwa kutoa taarifa kwa wananchi mara kwa mara juu ya hatua zinazoendelea vituoni wakati wa ukusanyaji wa matokea ili kuwaondolea wasiwasi pindi wanapoona matokeo yamechelewa kutolewa.

" Hili naomba nilisisitize, mnapoona baadhi ya taratibu hazijakamilika tokeni nje muwaambie wananchi nini kinaendelea ili wawe na taarifa na hii itawaongezea imani wananchi wanaosubiri matokeo na kuepusha vurugu vituoni" Amesisitiza Bw.Kailima.

Amesema kuwa mfumo wa Uchaguzi wa Tanzania ni wa uwazi kwa kuwa kila chama kinakuwa na Wakala anayesimamia maslahi ya chama chake wakati wa uchaguzi, pia uwazi katika hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa kura, uhesabuji wa Matokeo na ujumlishaji wa matokeo ambayo hulinganishwa na vishina.

Kwa upande wa Mawakala wa Vyama vya Siasa watakaoshiriki katika Uchaguzi mdogo amesisitiza kuwa wanatakiwa kuzingatia maadili ikiwemo kuepuka kutoa matokeo ambayo hawajaruhusiwa kuyasema wakati wa zoezi la upigaji wa kura na wanatakiwa kuapa kiapo cha kutunza siri na kujaza fomu kwa mujibu matakwa ya kikanuni.

" Wakala Chama cha Siasa haruhusiwi kutangaza matokeo kwa mgombea wake wakati zoezi la kuhesbu kura likiendelea kituoni, na hili nalilisisitiza Mawakala wote ni lazima waape kiapo cha kutunza Siri, ni matakwa ya kikanuni, wakala asiyeapa na kujaza fomu asipewe ridhaa ya kuwa wakala wa chama cha siasa ndani ya kituo" Amesisitiza Bw. Kailima.

Amesema kila Chama kitakuwa na Mawakala wa aina tatu kwa maana ya Wakala wa Kupiga kura, Wakala wa kuhesabu kura, Wakala wa kujumlisha kura na Kutangaza Matokeo ambao watakua na jukumu la kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea wawapo kituoni, kumsaidia msaidizi wa kituo pamoja na kuangalia taratibu zinavyokwenda kituoni.

Amesisitiza kuwa maamuzi ya kituo yatatolewa na Msimamizi wa kituo na Wakala ambaye hatakubaliana na maamuzi hayo atajaza fomu namba 16 kuonyesha kuridhika au kutokuridhika.

Kuhusu mafunzo amesema yanalenga kuwajengea uwezo Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo na Kata na Maafisa Uchaguzi kuelewa Misingi, Sheria na Wajibu wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao katika usimamizi wa hatua zote za uchaguzi ikiwemo upigaji wa kura na utangazaji wa matokeo.

Ameongeza kuwa Wasimamizi na Waratibu hao watafundishwa maadili ya kuzingatia wakati wakitekeleza majukumu yao ikiwemo maadili ya uchaguzi,maelekezo kwa wasimamizi ya Uchaguzi, wajibu wao, majukumu ya makarani , taratibu za kupiga kura, kuhesabu kura, kujumlisha kura na kutangaza matokeo, kuandaa taarifa za uchaguzi pamoja na masuala mbalimbali kuhusu uchaguzi huo.


Akizungumzia kuhusu Rufaa za mapingamizi ya wagombea amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 44 (5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, Tume ilipokea Rufaa za wagombea kutoka Kata mbalimbali ikiwemo ya Kijichi - Manispaa ya Temeke, Misugusugu- Halmashauri ya mji Kibaha, Pwani na Kata ya Ihumwa Manispaa ya Dodoma.

Amesema katika kikao cha Tume cha Desemba, 30, 2016 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitoa maamuzi ya Rufaa zote kwa haki na kwa kuzingatia kanuni, taratibu, miongozo na sheria zinazosimamia Uchaguzi ikiwemo Rufaa ya Kata ya Ihumwa, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ambayo imeondolewa kwa kuwa mkata Rufaa ameiondoa mwenyewe na amejitoa katika ugombea Udiwani kabla Rufaa yake haijasikilizwa.

Kwa Upande wa Rufaa ya jimbo la Dimani, Zanzibar Bw. Kailima ameeleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa kifungu cha 40 (6) ilipokea Rufaa ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ya kupinga maamuzi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kumthibitisha mgombea wa Chama cha Wananchi CUF kwamba ni mgombea halali katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani, Zanzibar.

Bw. Kailima ameeleza kuwa katika kikao cha Maamuzi cha Tume cha kupitia Rufaa za wagombea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikubaliana na Uamuzi wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo kuwa mgombea wa Chama cha Wananchi CUF aliyewekewa pingamizi na mgombea wa CCM amekidhi vigezo na uteuzi wake ni halali hivyo anaweza kuendelea na kampeni za kugombea nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo.




" Napenda nisisitize kuwa maamuzi yote yaliyofanywa na Tume yamezingatia Kanuni, Taratibu, Sheria na miongozo inayosimamia chaguzi, hali hii ya wagombea kukubali maamuzi ya Tume inatujengea msingi imara wa kuendelea kufanya vizuri zaidi kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 huku tukitimiza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria bila kupendelea" Amesisitiza Bw.Kailima.

CHAWABATA CHAPINGA MANISPAA YA ILALA KUKAGUA LESENI ZA WAUZA VILEO USIKU JIJINI DAR ES SALAAM

January 03, 2017
 Mwenyekiti wa Chama cha Wahudumu wa Baa Tanzania (Chawabata), Ali Hussein (kulia), akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, wakati akipinga zoezi linalofanywa na Manispaa ya Ilala la kukagua leseni za wauza vileo usiku. Kushoto ni Katibu wa chama hicho, Boniface Lameck.
LIGI KUU SOKA YA WANAWAKE TANZANIA BARA

LIGI KUU SOKA YA WANAWAKE TANZANIA BARA

January 03, 2017

Duru la Pili la Ligi Kuu soka ya Wanawake ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatarajiwa kuanza kesho Jumatano Januari 4, 2017 kwa michezo minne itakayofanyika kwenye viwanja mbalimbali.

Kwa mujibu wa ratiba, katika kundi ‘A’ pekee litakuwa na mchezo mmoja wakati kundi ‘B’ litakuwa na michezo mitatu kwa siku ya kesho Jumatano.
Mchezo pekee wa kesho wa kundi ‘A’ utakuwa kati ya Mburahati Queens ya Kinondoni, Dar es Salaam na Viva Queens ya Mtwara – mchezo utakaofanyika Uwanja wa Karume jijini katika mzunguko wa sita wa ligi hiyo.
Michezo mingine mitatu itakuwa ni ya Kundi B ambako Mejengo FC itacheza na Marsh Academy ya Mwanza kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida wakati Panama ya Iringa inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Sisterz ya Kigoma kwenye Uwanja wa Samora huku Victoria Queens ikiikaribisha Baobab ya Dodoma kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera.
Kabla ya michezo ya juma lijalo, upande wa Kundi A michezo yake miwili ya mzunguko wa sita itafanyika Alhamisi Januari 5, mwaka huu ambako Evergreen ya Temeke, Dar es Salaam itacheza na Fair Play ya Tanga kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.
Mlandizi ya Pwani inatarajiwa kuikaribisha JKT Queens ya Dar es Salaam, katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Mabatini.
..…………….…………………………………………………………………..............
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)