ADPA WAKUTANA ARUSHA,WAKUBALIANA KUSIMAMIA MAUZO YA SOKO LA ALMASI DUNIANI.

July 28, 2022

 



Mwandishi wetu,Arusha 

Umoja wa baraza la mawaziri wa jumuiya ya nchi za Afrika zinazozalisha almasi (ADPA) umekubaliana kusimamia biashara ya madini aina ya almasi ili kuzinufaisha nchi wanachama.

Waziri wa madini nchini,Dotto Biteko amesema kwamba mkutano wa baraza la mawaziri kwa nchi zinazozalisha almasi umekutana jijini Arusha kwa lengo la kuidhinisha nyaraka muhimu za baraza hilo,kuteua sekretarieti sanjari na kuhakikisha nchi za Afrika zinakuwa na sauti moja katika kusimamia madini ya almasi.

Waziri Biteko amesisitiza kuwa wajumbe wa baraza hilo wataupitia upya mfumo wa umoja huo na kujifunza katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi barani Afrika ili yaweze kuwanufaisha waafrika.

amesema kuwa duniani kote madini ya almasi yana urasimu na mlolongo mpana hivyo mkutano huo utatoa fursa wajumbe kuchambua na kuangalia vigezo kwa baadhi ya nchi barani Afrika zilizopigwa marufuku kufanya biashara ya almasi duniani.

“Tutaupitia upya mfumo wa umoja wetu ikiwemo katiba na kuboresha miongozo mbalimbali katika eneo la usimamizi wa madini ya almasi Barani Afrika “alisisitiza Biteko 

Tanzania ni mwenyekiti na mwenyeji wa mkutano wa ADPA ambapo umoja huo unajumuisha nchi 18 barani Afrika ambapo nchi 12 wanachama na 6 ni waangalizi. 


Hata hivyo,Waziri Biteko amesema licha ya changamoto ya janga la UVIKO-19 Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika mauzo ya madini aina ya almasi katika soko la dunia.

Waziri Biteko amesema kwamba baada ya janga la UVIKO-19 bei ya almasi duniani ilianguka  lakini kwa sasa almasi imepanda juu na kuifanya Tanzania kuendelea kufanya vizuri duniani.

Waziri Biteko amesema kuwa hivi karibuni kupitia mgodi wa almasi wa Mwadui uliopo mkoani Shinyanga serikal imeuza jiwe moja la almasi lenye kareti sita kwa thamani ya dola milioni 12 katika soko la dunia jambo ambalo linaashiria mafanikio makubwa kwa nchi.

“Huu uzalishaji haujawahi kutokea katika mgodi wetu wa Mwadui kwani tumeuza jiwe moja la almasi ya pink kwa thamani ya dola milioni kumi na mbili haya ni mafanikio makubwa sana kwa nchi yetu “alisema Biteko 

Waziri Biteko amesema kwamba pamoja na mgodi wa Mwadui kusimamisha uzalishaji kwa muda kutokana na ukarabati lakini kwa sasa serikali imeongeza hisa kutoka asilimia 25 mpaka 35 kama juhudi za kuongeza uzalishaji wa almasi hapa nchini.

Mwisho

.TUTAISHANGAZA DUNIA -TIMU YA JUMUIYA YA MADOLA

July 28, 2022


Na John Mapepele, Birmingham - Uingereza

Kocha Mkuu Timothy Kingu wa kikosi cha ndondi kinachoiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola ambayo yanaanza rasmi leo Julai 28,2022 amemhakikishia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na watanzania wote kurejea na medali za ushindi kwenye mchezo huo kwa kuwa wamepata maandalizi ya kutosha.

Akizungumza katika kambi ya wachezaji hao jijini Birmingham, Uingereza amesema wachezaji wake wamepikwa vizuri na watapata hamasa ya kutosha tayari kwa ajili ya pambano lililopo mbele yao.

Aidha, amesema hamasa kubwa inayotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri anayesimamia Michezo nchini, Mhe Mohamed Mchengerwa na wadau mbalimbali kwa sasa zinawafanya wawe na ali na nguvu zaidi ya kushindana kufa na kupona kwenye mashindano haya.

Hadi sasa, tayari Mabondia wawili wa Tanzania Yusuf Changarawe na Kassim Mbundwike wameingia robo fainali za mchezo ya Jumuiya ya Madola inayoanza rasmi leo jijini Birmingham, Uingereza.

Bondia wa tatu wa Tanzania, Alex Isinde sio tu ataanzia mzunguko wa kwanza bali pia atakuwa ndiye Mtanzania wa kwanza kutupa kete kwenye mashindano haya ya 48 ya nchi zilizopata kutawaliwa na Uingereza kesho Julai 29, 2022. 

Isinde atapambana na bondia kutoka Antigua & Barbuda aitwaye Alston Ryan. 

Endapo Isinde atashinda ataungana na wenzie katika robo fainali ambapo mshindi anabeba medali ya shaba.

Endapo wakishinda robo fainali wataingia nusu fainali ambako watawania kunyakua angalau medali za fedha.

Michezo ya Jumuiya ya Madola 2022 inazinduliwa rasmi leo saa mbili usiku kwa saa za huku (Tanzania iko mbele kwa saa mbili).

Tanzania itatupa tena kete zingine siku ya Jumamosi Julai 30, 2022 wakati wanariadha wanne wa mbio ndefu (Marathon) wanawake na wanaume wataingia kuchuana.

Wanariadha hao wa marathon ni Alphonce Simbu, Hamisi Misai, Jakline Sakilu na Failuna Matanga.

Kwenye michezo hiyo Tanzania inawakilishwa na wanariadha tisa, mabondia watatu, wacheza judo wawili, waogeleaji wawili na mnyanyua vitu vizito kwa walemavu (Para-Powerlifting) mmoja.

TANGA UWASA YATENGA MILIONI 900 KUPUNGUZA UPOTEVU WA MAJI

July 28, 2022
Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Maji Cup yanayofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kombezi Jijini Tanga kushoto ni Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shilloo kulia ni  Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia usambazaji maji (ATAWAS) Constantine Chiwalo
Mstahiki Meya wa Jiji la Tanga Abdurhaman Shiloo  akizungumza kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani

 

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi inayosimamia usambazaji maji (ATAWAS) Constantine Chiwalo akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo ya Maji Cup





Na Oscar Assenga,TANGA.



MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (Tanga Uwasa) katika mwaka wa fedha 2022/2023 wametenga milioni 990 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha wanapambana na upotevu wa maji.

Hayo yalisemwa  na Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Mhandisi Rashid Shabani wakati wa ufunguzi wa Mashindano ya Maji Cup yanayofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kombezi Jijini Tanga.

Alisema fedha hiyo imetengwa kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali zikazopelekea kupunguza upotevu wa maji ambapo mwaka jana ulikuwa wastani wa asilimi 30 kwa kutekeleza hayo hiyo miradi wanaimani watapunguza upotevu huo hadi kufikia asilimia 26 June 2023.

Alisema kazi ambazo wanazilenga kuzifanya ni kuboresha miundombinu kwa ajili ya kuzibiti na kupunguza upotevu wa maji kutoka kwenye mabomba na watanunua na kufunga mita za malipo kabla hizo mita ni za aina yake na hivyo itakuwa mamlaka ya maji ya kwanza kuonyesha aina hiyo ya mita.



“Mita hizi tunatarajia tutaanza kuzifunga mwezi huu uzuri mita hizi kama kuna uvujaji mbele ya mita mteja anapata ujumbe kuna matumizi yanafanyika hebu fuatilia agizo hilo ni la wizara na sisi tunatekeleza kwa sababu tunataka kufunga mita ambazo ni rafiki kwa mtumiaji hiyo ni aina rafiki kwa sababu ina mjali mteja”Alisema



Kaimu Mkurugenzi huyo alisema wamekuwa wakipokea malalamiko bili kubwa na moja ya chanzo ni maji kuvunja mbele ya mita hivyo hilo litakwenda kutatua hilo tatizo ikiwemo kuendelea kuelimisha jamii juu ya udhibiti wa upotevu wa maji na utoaji wa taarifa kwa mamlaka.



“Tunamshukuru Rais kutoa fedha zilizowezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maji inayolenga kuondoa kero ya maji nchini na nyengine nga imeshaleta mabadiliko makubwa ya utapatikanaji wa huduma ya maji nchini ikiwemo Jiji la Tanga ambapo kwa sasa imefikia asiimia 97”Alisema



Hata hivyo alisema Serikali itoa bilioni 13.31kwa ajili ya kujenga miradi ya maji kuhakikisha wananchi wa Jiji la Tanga wanapata huduma ya maji safi na salama.

Alisema pia wamepenga kutanua mtambo wa kusafisha maji eneo la Mowe ambapo wametenga Bilioni 9.1 na kwa sasa unaendelea na umefikia asilimia 62.

“Lakini pia tumeendeleza mtandao wa mabomba kilimota 17.6 maeneo ya Kichangani,Pongwe,Masiwani na Neema huu ni mradi wa kukabiliana na ugonjwa wa Uviko na umekamilika asilimia 100 ulikuwa na thamani milioni 500”Alisema

Kaimu Mkurugenzi huyo alisema licha ya hivyo serikali imewezesha fedha kujenga mradi wa maji kufikisha huduma maeneo ya Kibafuta,Mleni ,ndaoya,mpirani na chongoleani na kata ya chongoleani ni eneo pekee la Jiji la Tanga ambalo lilikuwa halina mtandao wa huduma ya maji sasa miundombinu imefika na wananchi na wameanza kupata huduma hiyo ya maji.

“Mradi hu wa kupelekea maji Chongoleani una thamani ya Milioni 918 na utekelezaji mradi umefikia asilimi 90 lakini pia kuna mradi wa kulaza bomba kubwa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo ”alisema


 

Alieleza hiyo inatokana na wananchi wa eneo la Chongoleani kupata maji kwa mgawo na serikali imetoa bilioni 2.7 kwa ajili ya kulaza bomba kubwa kutoka eneo la Amboni mpaka Chongoleani ili kuhakikisha wanapata maji muda wote.

 

Mwisho.

 

WAZIRI MCHENGERWA AITEMBELEA TIMU YA JUMUIYA YA MADOLA,AIFUNDA

July 28, 2022

 


Na John Mapepele, Birmingham


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa ameitembelea timu ya wachezaji wa Tanzania inayoshiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola   Birmingham nchini Uingereza na kuitaka kupambana kufa na kupona ili kurejea na medali.

Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Julai 27, 2022 kwenye kambi ya timu hiyo huku akisisitiza kuwa watanzania wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan wana matumaini makubwa na timu hiyo hivyo hawana budi kulinda heshima kubwa waliyopewa na taifa kwa ujumla.

"Nawaomba tangulizeni uzalendo ili tuweze kushinda, hii ni vita  tunahitaji kupambana bila kujali idadi yetu wala kitu chochote. Tutashinda." Amesisitiza Mhe. Mchengerwa


Aidha,  amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuinua  na kuendeleza michezo kwa kuwa michezo ni chanzo. Ha ajira na uchumi kwa taifa

" kwa kutambua hilo ndiyo maana kwa mara ya kwanza Serikali  imeamua kutoa fedha nyingi kwa wachezaji watakaopata medali za dhahabu dola za kimarekani 10,000, shaba 7500 na fedha 5000 bado zawadi za jumla" amesisitiza  Mhe. Mchengerwa.

Pia ametumia tukio hilo kutoa pongezi kwa timu ya wanaume na wanawake ya KABBADI kwa kufuzu kuingia kwenye mashindano ya kombe la Dunia yatakayofanyika Oktoba mwaka huu nchini India.

Mhe Mchengerwa ameongozana na Mhe. Musa Sima Mjumbe wa Kamati ya Bunge inayosimamia wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na ndugu Saidi Yakubu Naibu Katibu Mkuu.