RAIS DKT. MAGUFULI AHUTUBIA KATIKA SHEREHE ZA MWAKA MPYA KWA MABALOZI (NEW DIPLOMATIC SHERRY PARTY) IKULU JIJINI DAR ES SALAAM

February 10, 2017
Picha ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akihutubia Mabalozi mbalimbali  wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini katika Sherehe za Mwaka mpya kwa Mabalozi(New Diplomatic Sherry Party) Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga katika picha ya pamoja na Mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini mara baada ya kuwahutubia katika Sherehe za Mwaka mpya kwa Mabalozi(New Diplomatic Sherry Party) Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

DC ARUMERU ALEXZENDER MNYETI ATOA POLE KWA FAMILIA YA MAREHEMU MZEE KAYOMBO

February 10, 2017
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha Mhe Alexzender Mnyeti akisaini kitabu cha maombolezo kijijini Misasi
 Dc Mnyeti, MD Kayombo na familia nzima ya Mzee Kayombo walipotembelea kaburi la Mzee Kayombo
 Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe Alexzender Mnyeti (Kushoto), na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakiwa katika mazungumzo
 Dc Mnyeti akitoa salamu za pole kwa familia ya Marehemu Mzee Kayombo
 Wakati wa sala kwenye kaburi la Marehemu Mzee Kayombo
 Maombi ni muhimu katika kila jambo

Mazungumzo na Ndegu, jamaa na rafiki

Na Mathias Canal, Mwanza

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha Mhe Alexzender Pastory Mnyeti amezuru kijiji cha Misasi, Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza kutoa pole kwa familia ya Marehemu Mzee Kayombo aliyefariki Dunia siku ya saa mbili usiku katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mkoani Mwanza.

Mhe Mnyeti ametoa salamu za pole kwa wakazi wa Kijiji cha Misasi kwa kumpoteza mshauri katika kijiji hicho ambaye amekuwa nguzo kwa maendeleo ya kijiji sawia na utaratibu wake wa kuhamasisha wananchi kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mnyeti ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Misungwi kabla ya uteuzi wake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ameeleza jinsi alivyomfahamu Mzee Kayombo katika kuhakikisha jamii inasonga mbele katika maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Mnyeti alisema kuwa Mkoa wa Mwanza umepoteza mtu muhimu ambaye pia atakumbukwa kwa kazi njema alizozifanya wakati wa uhai wake.

Dc Mnyeti ametoa pole kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndugu John Lipesi Kayombo kwa kuondokewa na Mzee wake ambaye ni Mlezi wake tangu akiwa mdogo sambamba na kuisihi familia ya Marehemu Mzee Kayombo kuendeleza mshikamano na kupendana.

Marehemu Mzee Kayombo atakumbukwa kwa mambo mbalimbali aliyoyafanya wakati wa uhai wake pindi alipokuwa kazini ikiwa ni pamoja na kupanda miti katika shule zote alizofundisha, Ujenzi wa shule wakati huo, pia atakumbukwa kwa kuhamasisha ujenzi wa Zahanati ya Misasi.

Marehemu Mzee Antony Raphael Kayombo alifariki saa mbili usiku, siku ya Jumamosi ambapo hadi mauti inamkuta alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kibofu cha mkojo ambao ulianza ghafla tarehe 29/1/2017 na kupelekwa katika hospitali ya Misasi, Baadae hospitaliti ya Sekou Ture na mwishowe Hospitali ya Bugando ambapo alifanyiwa upasuaji ambapo hata hivyo hali yake iliendelea kudhoofika mpaka mauti ilipomkuta.

INNALILAH WAINNAH ILAIHI RAJIUN

HABARI ZINAZOTANGAZWA NA VYOMBO VYA HABARI NCHINI HAZICHANGII JUHUDI ZA TAIFA KATIKA KUTOKOMEZA UMASKINI HASA VIJIJINI

February 10, 2017

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk.Helen Kijo-Bisimba (kulia), akizungumza na wanahabari Dar es Salaam leo, wakati akimkaribisha Mwanachama wa Kituo hicho, Ananilea Nkya (katikati) kuzungumzia utafiti wake alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari vya Tanzania vinavyojishughulisha na maendeleo. Kushoto ni .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga. 
 Mwanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi Dar es Salaam leo, juu ya utafiti alioufanya kuhusu namna vyombo vya habari Tanzania vinavyojishughulisha na maendeleo. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk.Helen Kijo-Bisimba na .Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga 
Taarifa ya utafiti huo ikiendelea kutolewa.
Mwanahabari Hilda wa gazeti la Daily News akiwa mzigoni.
Maofisa wa LHRC wakifuatilia mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale

UTAFITI uliofanywa na Mwanachama wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ananilea Nkya, kama sehemu ya masomo yake ya  Shahada ya Uzamivu (PhD), umebaini kuwa  habari zinazotangazwa na vyombo vya habari hapa nchini  hazichangii  ipasavyo juhudi za  taifa katika  kutokomeza umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi ambao wanaishi vijijini.

Utafiti huu umabainisha kuwa sababu kubwa ni kwamba habari  zinazotangazwa na vyombo vya habari zinajikita zaidi katika matukio yanayotokea mijini, na wanaopatiwa fursa kubwa  ya  kutoa maoni  ni wanaume ambao ni watumishi wa umma na wanasiasa.

Utafiti huu umehusisha  habari 10,371 zilizotangazwa  katika vyombo vya habari 15  katika muda wa mwezi mzima Febuari  2014.

Habari hizo zilitangazwa kwenye taarifa ya habari ya saa mbili usiku kwenye televisheni mbili  na radio mbili   za  kitaifa  na  zilizochapishwa  katika magazeti 11  ya kila siku. Utafiti ulilenga kupata majibu ya swali:  Vyombo  vya habari Tanzania vinaripoti masula gani ya maendeleo  na kwa mtazamo  wa  watu gani?  Kati  ya habari 10,371 zilizofanyiwa utafiti   9,607  zilichapishwa  magazetini.

Utafiti huu unaonesha kuwa kati ya habari 10,371 zilizochapishwa 4,750 (45.8%) zilitokea Dar es Salaam na  5,621 (54.2%)  zilitoka mikoani na Zanzibar.  

Matokeo ya utafiti huu yanaonyesha kuwa kkoa wa Dar es Salaam ulinufaika zaidi  kimaendeleo kwa sababu kama habari hizo  10,371  zingegawanywa kwa usawa  kwa mikoa yote,  kila mkoa ungepata fursa ya kutoa habari  368 kuhusu mambo mbali mbali yanayohusu  maendeleo  ya wananchi  wake.

Habari hizo zingekuwa ni fursa ya mikoa kutangaza, ili kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha  wananchi kujadili changamoto na mafanikio ya  maendeleo  yao katika nyanja ya kijamii, kiuchumi na kisiasa 

Kwa kufanya hivyo wadau wa maendeleo ikiwa ni pamoja na wanachi wenyewe, serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa, mashirika ya kijamii (NGOs), taasisi za dini, taasisi za elimu, taasisi za fedha na wafadhili wa  nje wanaochangia maendeleo ya nchi yetu wangechukua hatua  sahihi na kwa wakati husika kushughulikia matatizo  yanayosababisha wananchi wengi  kuishi maisha ya kimaskini.

Hata hivyo badala ya  vyombo vya habari vya kitaifa kuwa chachu ya maendeleo  kwa kutangaza habari zinazoweza  kuinua maendeleo kila mkoa, kila wilaya na kila kijiji,   habari nyingi tena za kimatukio tu zisizofanyiwa uchunguzi  zinaufanya mkoa wa Dar es Salaam  kuchukua  fursa 15 za maendeleo  kupitia habari  ambazo  kila mkoa hapa nchini ungepata kila mwezi  kujadili masuala ya maendeleo yanayohusu watu wake.

Masuala  ya maendeleo  yayosumbua wananchi   wengi katika mikoa mingi hapa nchini  ni pamoja na ukosefu wa ajira/kipato, ukosefu wa maji safi na salama, elimu bora, huduma bora ya afya, ukosefu wa umeme na barabara.  

Aidha utafiti huu umebaini kuwa habari zinazotangazwa na vyombo vya habari vya kitaifa  ziko zaidi katika  mtazamo wa watumishi wa  umma kwa sababu  ndio wanaonukuliwa zaidi kwenye habari hizo.

Kati ya watu 14,637 walionukuliwa kwenye habari 10,371 zilizohusishwa kwenye utafiti, watu  8,398 (57.4%) walionukuliwa  walikuwa  ni  watumishi wa umma, 1,945 (13.3%) ni wanasiasa 2,757 (18.8%) wawakilishi wa taasisi za kiraia na mashirika binafsi (CSOs) na  wananchi wa kawaida walionukuliwa walikuwa 1,199  (10.5%). 

Hata hivyo  kwa vile kuzungumza kwenye vyombo vya habari ni fursa inayoweza kudidimiza au kuharakisha maendeleo,   fursa hizo 14,637 zingegawanywa sawa  kwa makundi yote--- wananchi,  watumishi wa umma, wanasiasa,  taasisi za kiraia na mashirika binafsi, kila  kundi lingepata fursa 3,659  kuzungumza kupitia vyombo vya habari kuhusu masuala  ya maendeleo.

Hivyo kwa mujibu wa utafiti huu maafisa wa umma  walipata fursa  mara tano zaidi  kuliko wananchi wa kawaida kuzungunza kupitia   habari zilizotangazwa na vyombo vya habari vya kitaifa. 

Aidha  walipata fursa mara nne  zaidi kuliko wanasiasa na  mara tatu kuliko wawakilishi wa taasisi za kiraia na mashirika  binafsi.

Katika utafiti huu  maafisa wa umma  ni viongozi na watumishi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji/mtaa hadi taifa, mashirika ya umma, mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye ofisi zake hapa nchini  na  maafisa katika balozi zenye ofisi zake  Tanzania.  

Wanasiasa ni  wawakilishi  kutoka vyama vya siasa.  Taasisi za kiraia na mashirika binafsi   inajumuisha vyama vya kitaaluma, vyama vya wafanyakazi, taasiasi  za  dini, mashirika binafsi, shule na vyuo binafsi  na  kundi la wananchi  linajumuisha wanachi wa kawaida wanaume na wanawake.

Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa  habari zilizochapishwa  na  magazeti, kila habari kwa wastani ilinukuu mtu  (chanzo cha habari) mmoja wakati  kwa redio na  televisheni, kwa wastani, kila habari  ilinukuu  si chini ya  watu wawili.


Utafiti huo unaonyesha  kuwa  habari zinazotanganwa  na vyombo vya habari vya kitaifa  zinajihusisha zaidi  na maendeleo  ya wanasiasa kwa sababu habari  zinazonukuu wanasiasa ndizo zinapewa umuhimu mkubwa zaidi  katika  vyombo vya habari.

Kati ya habari  411  zilizotangazwa  kama habari Kuu (lead stories)  katika vyombo hivyo 15  habari 234 (57%)  zilikuwa  za kisiasa, 121 (29%)  zilijadili masuala ya kijamii na 56 (14%)  uchumi. Hii ina maana kuwa vyombo vya habari haviyapi umuhimu  masuala ya  uchumi ambayo ndiyo  yanafanya wananchi wengi kuwa maskini.

Kwa mfano utafiti unaonyesha  kuwa kati ya habari kuu 411, habari  307 (74.7%) zilichapishwa  kwenye magazeti magazetini 11 kama habari kuu. Hata hivyo kati ya habari hizo  307,   habari zilizojadili masuala ya kijami mfano shule afya na umeme zilikuwa 67 (22%), uchumi ni 39 (12.5%) na 201 (65.5%) zilikuwa ni siasa. 

Habari  za siasa  ziliandikwa kutokana na  mikutano ya kisiasa, mahojiano na wanasiasa, kampeni za uchaguzi, taarifa za vyama vya siasa kwenye vyombo vya habari, makongamamo na washa za kisiasa.

Habari za uchumi  ni zile zilizohusu masuala ya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ukusanyaji kodi kupitia mashine za kieletroniki (EFD), kilimo, matatizo ya wakulima katika kupata pembejeo na  masoko ya mazao yao, uchimbaji madini, utalii, viwanda, uwekezaji, matatizo ya ajira, mabadilisho ya fedha, biashara na ujasiriamali, uvuvi  na  misitu ikiwepo ukataji miti kupata magogo kwa ajili ya biashara ya mbao.

Habari za kijamii ni zile zilizojikita kwenye  haki za binadamu, jinsia, mimba mashuleni, kuozesha kwa nguvu watoto wa kike, ukatili majumbani, biashara ya binadamu na migogoro ya ardhi. 

Zilihusisha pia  masuala ya elimu kama vile uhaba wa walimu, vitabu na madawati katika shule  za  umma (serikali), uhaba wa chakula, ajali za barabarani, miundo mbinu, masula ya kisheria,  masuala ya  dini, na habari  za mahakamani. 

Vyombo vya habari vya umma vya utangazaji vilivyohusishwa kwenye  utafiti huu ni TBC 1 na TBC Taifa wakati vyombo vya habari vya watu binafsi ni pamoja na ITV na Radio One. Magazeti ya kila siku ya Kiswahili yalikuwa ni Nipashe, Mwananchi, Mtanzania, Majira, JamboLeo and Tanzania Daima. Na magazeti ya Kiingereza yalikuwa the Citizen na the Guardian na gazeti la serikali Daily News.

Utafiti unaonyesha pia  kwamba habari zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Tanzania zilitawaliwa na mfumo dume ambapo kati ya watu 14,655 walionukuliwa katika taarifa 10,371 kwenye vyombo vya habari 15, wanawake walikuwa 2,646 (18%) na wanaume 12,009 (82%). 

Utafiti unadhihirisha jinsi ambavyo maoni yanayohusu  maendeleo yanayowasilishwa kupitia habari yanavyotawaliwa na wanaume.

Watu 14,637 walionukuliwa kwenye taarifa za habari walinufaika na nafasi ya vyombo vya habari kama fursa ya maendeleo kwa sababu waliweza kuwasilisha maono yao ambayo yalichagiza mipango ya maendeleo ya taifa . 

Hii inadhihirisha kwamba hoja/maoni  yaliyotolewa na  watu hao 14, 637 yangehesabiwa kuwa fursa za maendeleo na kugawanywa kwa uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume kama makundi ya kijamii kila kundi lingepata fursa 7,318 ya  kuzungumzia  masuala ya maendeleo  kwa mtazamo wao.  

Hivyo basi kwa dhana kwamba idadi ya wanaume walionukuliwa katika taarifa za habari ni 82% na wanawake ni 18%, inamaanisha kwamba wanaume walikuwa na nafasi mara tano Zaidi ya wanawake katika kupata fursa kwenye vyombo vya habari kama sehemu ya kuwasilisha maoni yao ambayo yalichechemua mipango ya taifa ya maendeleo. 

Hii inaonyesha jinsi ambavyo wanawake ambao ndio sehemu kubwa ya idadi ya watu nchini Tanzania wanakosa fursa. Utafiti huu umeonye wanawake wanakosa fursa mara tano ikilinganishwa na wanaum,e katika   kuzungumza kwenye vyombo vya habari .

Utafiti huu unaonyesha kuwa  masuala ya kimaendeleo yanayowagusa wanawake kama kundi kubwa katika jamii linalojumuisha  zaidi ya 51% ya idadi ya watu nchini yameendelea kutokushughulikiwa. Kwa mfano , kutokana na hali hiyo wanawake walio katika umri wa kuzaa wameendelea kuhatarisha maisha kwa vifo ambavyo vingeweza kuzuilika wakati wa kujifungua. 

Sambamba na hilo wanawake wengi wameendelea kutumia muda mwingi kutembea umbali mrefu wakitafuta maji na kuni kwa sababu ya kutokuwepo kwa mabomba ya maji na umeme. Na hivyo kudumaza uchumi wa faimilia zao na taifa.

Kwa upande wa magazeti kati ya watu 12,822 walionukuliwa 2371 (18.5%) walikuwa wanawake na 10,451 (81.5) walikuwa wanaume. 

Hii inamaana kuwa taarifa za habari zilizochapishwa kwenye magazeti 11 ya kila siku, kwa wastani wanaume walikuwa na fursa mara nne zaidi kulinganisha na wanawake  kutoa maoni yao juu ya masuala ya maendeleo.

Hata hivyo, gazeti la Daily News lilikuwa na 24% ya wanawake ambao maoni yao juu ya maendeleo yalipenyeza kwenye uwanda wa habari. Hii inamaanisha kwamba kupitia taarifa za habari za Daily News.  Wanaume walikuwa na nafasi mara tatu Zaidi ya kujadili masuala ya kimaendeleo kuliko wanawake. 

Katika upande mwingine, gazeti la Mtanzania na the Citizen uwakilishi wa wanawake ilikua 16%, na 16.2% kwa kila moja ambapo hii inaonyesha ni jinsi gani magazeti haya mawili yalimpa mwanaume nafasi mara tano Zaidi ya mwakamke katika kujipambanua katika masuala ya kimaendeleo.

Kadhalika utafiti unaonyesha kuwa  habari zinaandikwa zaidi na wanaume . Utafiti unaonyesha kwamba wanahabari 8,094 walihusika katika ukusanyaji wa taarifa zilizotumika kuunda taarifa za habari 10,371 ambazo zilitolewa kwenye vyombo vya habari 15 vilivyofanyiwa utafiti katika utafiti huu. Miongoni mwa  walioandika bahari hizo, wanahabari  3,039 (37.6%) walikuwa wanawake na 5,053 (62.4%) walikuwa wanaume.

Hii inaonyesha jinsi ambavyo waandishi wa kiume wanapata fursa karibu mara mbili ikilinganishwa na wanahabari wa kike  katika kuandaa habari juu ya masuala ya maendeleo. Hii inatoa maana kwamba waandishi wanawake wamepoteza fursa kuandaa habari zinazohusu maendeleo ya nchi kwa mtazamo wa  wanawake   ambazo zingeweza kuibua masuala yanayoathiri wanawake katika maendeleo na kuweza kushughulikiwa. 



NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO DKT.ASHATU KIJAJI AZINDUA HUDUMA MPYA YA ‘ECOBANK MOBILE APP’

February 10, 2017




Naibu Waziri wa fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma mpya ya ‘Ecobank Mobile App’ iliyozinduliwa jana jijini Dar es salaam. Programu hii ya kidijitali kutoka Ecobank ni mahususi kwa ajili ya kurahisisha huduma za kibenki kwa njia ya haraka na usalama kupitia simu za mkononi.
Naibu Waziri wa fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akipeana mkono na Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Ecobank Bw. Peter Machunde mara baada ya kuzindua rasmi huduma mpya ya kidijitali ya ‘Ecobank Mobile App’ iliyozinduliwa jana jijini Dar es salaam. Anayeshuhudia (katikati) ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ecobank-Afrika Bw. Ade Ayeyemi na Mkurugezi Mkuu wa Ecobank Tanzania Bw. Enoch Osei-Safo.
Mkurugenzi Mkuu wa Ecobank Tanzania Bw. Enoch-Osei Safo akisoma hotuba yake wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma mpya ya ‘Ecobank Mobile App’ ambayo ilizinduliwa jana jijini Dar es salaam. Programu hii ya kidijitali kutoka Ecobank ni mahususi kwa ajili ya kurahisisha huduma za kibenki kwa njia ya haraka na usalama kupitia simu za mkononi.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Ecobank wakifuatilia kwa makini hafla ya uzinduzi wa huduma mpya ya kidijitali ya ‘Ecobank Mobile App’ iliyozinduliwa jana jijini Dar es salaam. Programu hii ya kidijitali kutoka Ecobank ni mahususi kwa ajili yakurahisisha huduma za kibenki kwa njia ya haraka na usalama kupitia simu za mkononi.
Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Ecobank Tanzania Bw. Peter Machunde akiteta jambo na Naibu Waziri wa fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma mpya ya kidijitali ya ‘Ecobank Mobile App’ iliyozinduliwa rasmi jana jijini Dar es salaam.
Naibu Waziri wa fedha na Mipango Dr. Ashatu Kijaji akipakata maelezo kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi wa Ecobank Tanzania kuhusiana huduma mbalimbali zinazopatikana kwenye programu ya kidijitali ya ‘Ecobank Mobile App’ iliyozinduliwa jana jijini Dar es salaam. Pamoja nae ni Kaimu Mwenyekiti wa bodi ya Ecobank Tanzania Bw. Peter Machunde.

WIZARA YA FEDHA YAMLIPA MKANDARASI ANAYEJENGA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE (TERMINAL 3) FEDHA ZOTE ANAZODAI

February 10, 2017
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James akizungumza na Wanahabari kuhusu Wizara yake ilivyotekeleza Agizo la Rais Dkt. John Magufu kuhusu  kumlipa Mkandarasi ayejenga Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 3).

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Doto James, Wizara ya Fedha na Mipango imemlipa Mkandarasi anayejenga Mradi wa upanuzi wa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(Terminal 3) Kampuni ya BAM International kiasi cha Euro Milioni 9.5 sawa na zaidi ya Tsh. Bilioni 22 za Kitanzania mara baada ya kuhakiki madai hayo.

Katika Hatua nyingine Wizara ya Fedha inaandaa Malipo ya awali (Advance Payment) kiasi cha Tsh. Bilioni 300 kwa ajili ya kumlipa Mkandarasi anayejenga Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Kutumia Umeme na Mafuta(Standard Gauge) katika awamu ya kwanza itakayoanzia kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro katika awamu yake ya kwanza ya Ujenzi huo.

TADB YAANZA KUTEKELEZA MKATABA WA USHIRIKIANO KATI YA TANZANIA NA MOROCCO

February 10, 2017


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeanza kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Ushirikiano uliosainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na Morocco wakati wa Ziara ya Mfalme wa Morocco Mtukufu Mohammed VI alipotembelea Tanzania kwa mwaliko wa Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli mnamo mwezi Oktoba 2016.

Katika kutekeleza makubaliano hayo, ujumbe wa TADB ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Francis Assenga na Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha, Bw. Albert Ngusaru upo nchini Morocco, pamoja na mambo mengine kuainisha maeneo ambayo Benki hiyo itashirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM) na kuwekeana mikakati ya utekelezaji. 

Kwa mujibu wa Bw. Assenga, pamoja na kupanga mikakati hiyo, ujumbe huo ulipata fursa ya kukagua miradi kadhaa ya kilimo na ufugaji ambayo Tanzania inaweza kuianzisha kwa mafanikio.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TAD, Bw. Francis Assenga (Katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha, Bw. Albert Ngusaru (Watatu kushoto) wakiwa na wenyeji wao Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya Morocco (GCAM).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Francis Assenga (wa pili toka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kilimo ya Morocco (Credit Agricole) Bw. Jamal Eddine Wl Jamali (Katikati). Wengine ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB  Bw. Albert Ngusaru na Wakurugenzi wawili wa Benki ya Credit Agricole Bi. Dkhil Mariem (Kushoto) na Bi Leila Akhmisse (Kulia).
Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ukipatiwa maelezo juu ya miradi ya kilimo inavyoendeshwa nchini Morocco wakati Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Francis Assenga (Mwenye Kaunda Suti) na Bw. Albert Ngusaru Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha (Mwanye Daftari) walipotembelea Morocco wiki hii kuanza utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano kati ya TADB na GCAM.
Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ukipatiwa maelezo juu ya miradi ya kilimo inavyoendeshwa nchini Morocco wakati Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB Bw. Francis Assenga (Mwenye Kaunda Suti) na Bw. Albert Ngusaru Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha (Mwanye Daftari) walipotembelea Morocco wiki hii kuanza utekelezaji wa Mkataba wa Ushirikiano kati ya TADB na GCAM.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania Bw. Francis Assenga (Katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Credit Agricole na Tamwil El Fellah wakati walipokagua miradi mbalimbali ya kilimo na ufugaji katika vijiji vya mji wa Khemisset nchini Morocco jana. Kulia kabisa ni Bw. Albert Ngusaru ambaye ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) Bw. Francis Assenga (kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kilimo ya Morocco (Credit Agricole) Bw. Jamal Eddine W. Jamali (Katikati). Kulia ni Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB  Bw. Albert Ngusaru. 


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (Kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Hazina na Utafutaji Fedha wa TADB  Bw. Albert Ngusaru (Kulia) walipotembelea Benki ya Kilimo ya Morocco (Credit Agricole).