JESHI LA POLISI LAANZA KUTOA ELIMU KWA ABIRIA NA MADEREVA ILI KUKABILIANA NA AJALI KATIKA KIPINDI CHA MWISHO WA MWAKA

JESHI LA POLISI LAANZA KUTOA ELIMU KWA ABIRIA NA MADEREVA ILI KUKABILIANA NA AJALI KATIKA KIPINDI CHA MWISHO WA MWAKA

November 10, 2015

je1
Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma, Makao Makuu ya Trafiki, Dar es Salaam, ASP Abel Swai akitoa elimu ya usalama barabarani kwa abiria, muda mfupi kabla ya kuanza safari za mikoani katika kituo Kikuu cha mabasi Ubungo, jijini Dar es Salaam, elimu ambayo inalenga kudhibiti ajali za barabarani kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka,
je2
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani, PC Asha Adam, akiwasisitiza abiria kufunga mikanda  iliyopo kwenye viti walivyoketi muda wote wa safari muda mfupi kabla ya magari  kuondoka katika kituo Kikuu cha mabasi ya abiria Ubungo, jijini Dar es Salaam, kama hatua ya kudhibiti majeraha na vifo vitokanavyo na ajali za barabarani, kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka,
je3
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Inspekta Ibrahim Omary Samwi(kushoto), na PC Elisante Bura(kulia), wakikagua moja ya magari yanayofanya safari zake mikoani, kutekeleza mkakati wa Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani kudhibiti ajali kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka.Zoezi hili limefanyika  muda mfupi kabla ya magari  kuondoka katika kituo Kikuu cha mabasi Ubungo,jijini Dar es Salaam kuelekea mikoa mbalimbali ya Tanzania .
je4
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Inspekta Ibrahim Omary Swami(aliyeko chini ya uvungu wa gari), akikagua moja ya magari yanayojiandaa kuelekea mikoani, zoezi ambalo limefanyika muda mfupi kabla ya magari kuanza kuondoka katika kituo Kikuu cha Mabasi, Ubungo jijini Dar es Salaam.aliyenyoosha kidole juu ni PC Elisante Bura. Hatua hii ya Jeshi la Polisi nchini  linalenga kudhibiti ajali kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka,.
je5
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Sajenti Jackson Mafuru (kulia), na PC Elisante Bura(kushoto), wakikagua moja ya magari yanayofanya safari zake mikoani. zoezi hili ambalo limefanyika  muda mfupi kabla ya magari  kuondoka katika kituo Kikuu cha mabasi Ubungo,jijini Dar es Salaam, ni moja ya hatua ya Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani kudhibiti ajali kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka,.
je6
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani,Koplo Abdallah Bwasi akikagua moja ya magari  yanayofanya safari zake nje ya mkoa wa Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya magari  kuondoka katika kituo Kikuu cha mabasi Ubungo,jijini Dar es Salaam.Hatua hii ya Jeshi la Polisi kupitia Kitengo cha Usalama Barabarani imekuja kwa lengo la kudhibiti ajali kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka.(Picha zote na Abubakari Akida, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi)
Kaimu Mkurugenzi Mpya Aanza Kazi, Akutana na Watendaji Muhimbili

Kaimu Mkurugenzi Mpya Aanza Kazi, Akutana na Watendaji Muhimbili

November 10, 2015

MS1
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk Hussein Kidanto (kushoto) akimtambulisha Kaimu Mkurugenzi mpya wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Mseru (kulia) ambaye ameteuliwa jana na Rais John Pombe Magufuli. Jana Rais Magufuli amemuamishia Dk Kidanto katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
MS2
Kaimu Mkurugenzi mpya wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Mseru ambaye ameteuliwa jana na Rais John Pombe Magufuli akizungumza na menejimenti ya hospitali hiyo jana.
MS3
Baadhi ya wakurugenzi wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi mpya wa Hospitali hiyo Profesa Lawrence Mseru.
MS4
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma (MNH), Aminiel Aligaesha (kushoto) na mwanasheria wa hospitali hiyo, Veronica wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi mpya wa Hospitali hiyo Profesa Lawrence Mseru.
,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,,
Kaimu  Mkurugenzi  Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence  Mseru leo ameanza kazi na kuwataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuwahi kazini kwa wakati na kufanya kazi kwa bidii.
Profesa Mseru ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam  baada ya kukutana na menejimenti ya hospitali hiyo ambayo inajumuisha Wakurugenzi 14. Mkurugenzi huyo amekutana na menejimenti hiyo majira ya saa 6:00 mchana katika ukumbi wa mikutano wa hospitali hiyo.
Pia, amekutana na kamati tendaji ya hospitali , wakurugenzi, wakuu wa idara, mameneja wa majengo ikihusisha Sewahaji, Mwaisela, jengo la watoto na jengo la wazazi saa 8: 00 mchana.
Pamoja na mambo mengine katika kikao hicho, wakurugenzi  wameeleza mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo.
Profesa Mseru ameteuliwa jana kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo baada ya Dk. Hussein Kidanto kuhamishiwa  wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine.

VAZI LA KHANGA LAFANA KATIKA TAMASHA LA KITCHEN PARTY GALA.

November 10, 2015
Jumapili iliyoisha ya tarehe 08.11. 2015, wanawake mbali mbali jijini Dar es salaam walikutana katika tamasha la kitchen party gala likiwa limebeba ujumbe wa mwanamke simama na timiza ndoto zako.

Wanawake wakiwa wamevalia khanga ambayo ndio ilikuwa dress code ya tamasha walikusanyika kwa wingi kwa ajili ya kupata mafunzo na ushauri bila kusahau burudani.

Pia  Ilichezeshwa droo ya kushinda safari ya Afrika Kusini kwa siku mbili  alishinda, iliyodhaminiwa na kinyago tours. Pamoja na droo ya kumtafuta Mshindi wa safari ya Mikumi national park nae alipatikana akapokea certificate toka kwa mkurugenzi wa kinyago tours bi Diana.


Pichani juu ni washiriki wa kitchen party gala wakifuatilia mafunzo kwa umakini.
 Washiriki wa kiwa na cake maalum ya sikukuu yakuzaliwa Bi Rosemary ambayohaikuweza kutambulika kwa haraka kuwa ilikuwa keki maalumu yanani katika   kitchen party gala.

Msemaji Bi  Mariam Mbewa Mkurugenzi  wa green investment akielezea safari yake ya mafanikio na kuwafundisha kinamama umuhimu wa kuweka akiba.
Pichani juu ni washiriki wa kitchen party gala wakifuatilia mafunzo kwa umakini huku wakiwa na furaha tele juu ya kile kinachoelezewa kutoka kwa Msemaji.
Msemaji Bi Maida Waziri mkurugenzi wa Ibra Contractors nae alishirikisha wanawake safari yake ya mafanikio toka akiwa fundi cherehani mpaka sasa anamiliki kampuni kubwa ya ujenzi wa majengo na bara bara.Aliwasisitiza wanawake kujiamini na kutokuogopa kuthubutu ukijiamini popote unapenya lakini lazima uwe na malengo na mikakati.
Mwalimu wa masuala ya biashara na ujasiriamali Bryson Makena nae alitema cheche zake na kuwafundisha kina mama kujitambua na ujue kusudio lao hapa duniani ni lipi.
Mkurugenzi wa kinyago tours bi Diana nae alitoa funzo la kufanya kazi kwa malengo hata kama umeajiriwa malengo yako ni yapi?leo ukiachishwa kazi ghafla umejipangaje?ana miaka 27 tu lakini anamiliki kampuni yake ya Tours and safariz
Waandaaji wa women in balance kitchen party gala Mtangazaji wa E fm Dina Marios na Vida Mndolwa wakigonga chears kufungua shughuli.
                                                              Wadada wakifurahi
                                   Muongoza shughuli Dina Marios akisisitiza jambo
Ilichezeshwa droo ya kushinda safari ya Afrika Kusini kwa siku mbili na huyu dada ndio alishinda.Atasafiri na mumewe mtarajiwa na imedhaminiwa na kinyago tours.
Mshindi wa safari ya Mikumi national park nae alipatikana bi Edna Haki Ngowi akipokea certificate toka kwa mkurugenzi wa kinyago tours bi Diana
    Washiriki wakiwa katika nyuso za furaha wakati wa kitchen paty huku wakiendelea kufuatilia yanajiri katika droo za bahati nasibu
Mchungaji debora akifundisha kina mama kuwa wao ni wasababishaji wanaweza kufanya mambo yasiyowezekana yakawezekana.
                                     Dina marios akipiga selfie na mashabiki wake
                                                   PICHA NA DINA MARIOS

JIJI LA MBEYA LAJIPANGA KUKUSANYA KODI KATIKA MRADI WA SOKO JIPYA LA MWANJELWA

November 10, 2015
Kaimu Mkurugenzi jiji la Mbeya Dkt,Samuel Razalo


 Na EmanuelMadafa,Mbeya
HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, imesema imejipanga vyema katika  kuhakikisha  mradi mkubwa wa soko jipya la mwanjelwa unasimamiwa kikamilifu kwa kufuata  taratibu za serikali sanjali na mikataba  iliyoingia na benki ya CRDB  kwa kipindi cha miaka 15.

Mradi  huo wa soko la kimataifa la Mwanjelwa lililopo jijini Mbeya  ujenzi wake imefikia  asilimia 99 hivyo upo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake.

Akizungumza  ofisini kwake  , Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Dkt. Samweli Razalo, amesema licha ya soko hilo kukamilika lakini mchakato wake wa uendeshaji utazingatia taratibu za halmashauri na mkataba walioingia na benki ya CRDB.

Amesema  hatua  hiyo, inatokana na halmashauri ya Jiji hilo kukopa kiasi cha shilingi Bilioni 13 kutoka benki ya CRDB na kufanikisha ujenzi wa soko hilo ambao umedumu kwa  zaidi ya miaka 10 tangu lilipoteketea kwa moto.


Amesema, benki hiyo kwa kukubaliana na halmashauri imepanga kiasi cha kodi kitakachopaswa kulipwa na wafanyabiashara  kuanzia shilingi elfu moja kwa siku hadi shilingi 500,000 kwa mwezi.

Amesema Wafanyabiashara ambao watatumia meza watatakiwa kulipa ushuru wa shilingi 1000 kwa siku huku wale wa maduka watalipa kiasi cha shilingi 500,000 kwa mwezi na wauza nyama watapaswa kulipa kiasi cha shilingi 400,000 kwa mwezi,”alisema.

Amesema , awali halmashauri hiyo ilipokea maombi kutoka kwa wafanyabiashara ambao walikuwa wakiomba kupunguzwa kwa gharama za tozo hizo kwani ziko juu ukilinganisha na hali ya uhumi wa sasa.

Amesema, halmashauri iliyachukua maombi hayo na kuyawasilisha kwenye mamlaka husika ya benki ya CRDB hivyo wanasubili majibu na kuwataka wafanyabiasha kuwa wapole wakati wanasubili majibu hayo kutoka kwenye uongozi wa benki hiyo.

Soko la Mwanjelwa liliteketea kwa moto mwaka 2006 na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha kutoka kwa wafanyabiashara zaidi ya 2000 walionguliwa maduka yao na ujenzi wake kuanza mwaka 2008..

Mwisho.

Muonekano wa Mradi wa Soko la Mwanjelwa Jijini Mbeya ambapo ujenzi wake bado unaendelea.(JAMIIMOJABLOG MBEYA)

NEC YAVISHUKURU VYOMBO VYA HABARI KWA COVERAGE NZURI YA UCHAGUZI MKUU 2015

November 10, 2015
  Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Giveness Aswile, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, kuvishukuru vyombo vya habari kwa kuripoti vizuri katika kipindi chote cha uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa NEC, Emanuel Kavishe.PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA;KAMANDA WA MATUKIO BLOG
 Kavishe naye akitoa pongezi kwa wanahabari kwa kutangaza vizuri matukio ya uchaguzi mkuu
 Sehemu ya wanahabari wakiwa katika mkutano huo
Aswile na Kavishe wakifurahia jambo katika mkutano huo.
Lilian Lundo-MAELEZO
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa mafanikio ya asilimia 80 ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yametokana na ushiriki mkubwa wa vyombo vya habari vilivyotekeleza kwa ufanisi kazi ya kuelimisha na kutoa habari kuhusu uchaguzi huo.
Akiongea na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mikutano wa tume hiyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga kura Giveness Aswile, amevishukuru vyombo vya habari kutokana na kazi hiyo katika kipindi chote cha uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
Alisema amani ya Tanzania iliendelea kuimarika katika kipindi chote cha uchaguzi kwa sababu vyombo vya habari vilisimamia na kutetea haki za wananchi.
Aliongeza kuwa hata tume ilifanya kazi kwa urahisi kutokana na kazi kubwa ya uelimishaji iliyofanywa na vyombo vya habari, hivyo kuipunguzia kazi NEC ya kuwaelimisha wananchi juu ya mambo ya msingi ya uchaguzi mkuu.
 “Amani ya nchi hii ilisimama kwa sababu vyombo vya habari vilisimama kutetea wananchi na tume, ilifika mahali maswali kutoka kwa wananchi yalipungua kutokana na maswali mengi kujibiwa kupitia vyombo vya habari” Alisema Giveness.
Naye Mkurugenzi Idara ya Sheria wa tume hiyo, Emmanuel Kawishe alisema hakuwa na ufahamu sahihi kuhusu vyombo vya habari na umuhimu wake katika kutekeleza majukumu yake  kwa wananchi.
 “Zamani nilifahamu mwanahabari ni adui kumbe ni daraja kati ya mtoa habari na mpokea habari, katika zoezi zima la uchaguzi mkuu wanahabari walikuwa ni sehemu ya waliotoa elimu ya mpiga kura wameweza kutumia kalamu zao vizuri.” Alisema Bwana Kawishe
Alifafanua kuwa wanahabari walifanya kazi yao kwa kuzingazitia maadili ya kazi yao kwa kutofungamana na upande wowote na kuitangaza tume kwa mtazamo chanya kwa wananchi.
Kawishe alisema kuwa vyombo vimeweza kuitangaza vizuri tume kwani kila alipopita wananchi wamekuwa wakiipongeza NEC kwa kazi nzuri ya utoaji wa elimu ya mpiga kura katika vyombo vya habari.
Uchaguzi Mkuu wa mwak 2015, umeshuhudia ushirikishwaji mkubwa wa vyombo vya habari ambapo vyombo vya habari vilipewa nafasi kubwa ya kutoa habari kuhusu uchaguzi huo ikiwemo kutoa vitambulisho vilivyowaruhusu waandishi wa habari kuingia kwenye vituo vya kupigia kura.
KUZIONA STARS V ALGERIA 5000/=

KUZIONA STARS V ALGERIA 5000/=

November 10, 2015
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa Jumamosi kati ya Tanzania dhidi ya Algeria utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam bei ya chini kuwa ni shilingi elfu tano (5,000) tu.
Tiketi za mchezo huo zitaanzwa kuuzwa siku ya ijumaa katika vituo mbalimbali vinavyotumiwa na TFF kuuzia tiketi, ambapo kiingilio kingine kitakua ni elfu kumi (10,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio cha elfu tano kikiwa ni kwa viti vya rangi ya Bluu, Kijani na rangi ya Machungwa.
Wakati huo huo kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhamininiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, kinatarajiwa kurejea nyumbani kesho Jumatano mchana kwa shirika la ndege la Fastjet tayari kwa maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Algeria siku ya Jumamosi.
Stars iliyoweka kambi nchini Afrika Kusini imekua ikifanya mazoezi kila siku katika uwanja wa Edenvale, ambapo mpaka sasa wachezaji wote wapo katika hali nzuri hakuna majeruhi na kila mmoja yupo tayari kwa mchezo wa Jumamosi.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Mkwasa amesema vijana wake wapo vizuri kifaya, kifikra na morali ni ya hali juu “wachezaji wamekua wakifanya mazoezi kwa nguvu na kuonyesha umakini mkubwa” alisema Mkwasa.
Aidha Mkwasa amewaomba watanzania na wadau wote wa mpira wa miguu nchini kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti ya kuwashangilia vijana katika mchezo dhidi ya Algeria Jumamosi, kwani kutawafanya wachezaji kujisikia wapo nyumbani na kucheza kwa nguvu zaidi.
Wachezaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu walioshinda kombe la Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa wiki na klabu yao ya TP Mazembe wanatarajiwa kuungana na wenzao kambini kesho jijini Dar ess alaam.

FAHAMU JINSI #RECRUITME INAVYOWEZA KUKUPA UJUZI UTAKAOKUSAIDIA KUPATA KAZI UITAKAYO

November 10, 2015
Na Jamiimojablog
Ujuzi, katika soko la ajira ni mali ambayo inahitaji matengenezo na uboreshaji. Kama mali nyingine yoyote, matumizi yake bora, hukuzalishia zaidi. Sababu nyingi zimetolewa katika kipindi cha miaka mingi kwamba kuna utofauti wa wazi baina ya mtu mwenye elimu aliyeko kazini na mwenye elimu bila kazi. Utofauti huo ni jinsi ujuzi wa watu hao wawili unavyotumika.



Vijana wengi wa Tanzania wana ujuzi waliopata kutokana na mafunzo mbalimbali, lakini baadhi yao kushindwa kutumia ujuzi walionao. Sababu pekee inayosababisha hili ni; mahitaji ya ujuzi katika soko la ajira hayako sambamba na ujuzi utolewao. Matokeo yake ni vijana kujikuta kwenye sintofahamu iliyosababishwa na mgongano wa kiujuzi. Ushindani mkubwa katika soko la ajira duniani ni kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA ambayo imechukua nafasi kubwa ya ajira za watu, na kama ajira inahitajika basi mtu ni lazima uwe na ujuzi maalumu.



Mwalimu mjini Arusha mwenye ujuzi wa TEHAMA ana nafasi kubwa ya kupata ajira kuliko yule asiye na ujuzi huo. Karani jijini Dar es Salaam mwenye ujuzi wa teknolojia ya juu ana nafasi kubwa ya ajira kuliko yule asiye na ujuzi huo. Tour guide mkoani Morogoro mwenye ujuzi wa mitandao ya kijamii na ulimwengu wa kidijitali ana uwezekano mkubwa wa kugundua fursa mpya kuliko yule asiye na ujuzi huo. Mwana masoko wa Mbeya mwenye maarifa zaidi juu ya matumizi ya mitandao ana nafasi kubwa ya kuvutia watu zaidi ya yule anayeendelea kutegemea mbinu za kizamani. Orodha ni ndefu.



Umewahi kujiuliza kwa nini Ronaldo, Messi, Rooney, Usain Bolt, Venus, Serena na wanamichezo wengine wameendela kutamba katika tasnia ya michezo kwa muda mrefu? Siri imelala katika kuboresha ujuzi wao. Ili umuhimu wa mtu uonekane katika  soko la ajira, lazima uwe na ujuzi husika na uendelee kuuongeza mara kwa mara.


Ujuzi unaweza kupatikana kupitia njia mbalimbali. Mtu anaweza kwenda shule; wengine wanaweza kufanya kazi na wazoefu. Mwingine anaweza pia kutumia muda kwenye mitandao na kupata ujuzi autakao. Miongoni mwa majukwaa ya kuaminika kwenye mtandao yanayokuja kwa kasi katika kutoa ujuzi na mafunzo bora na bure ni RecruitMe. Kupitia RecruitMe, unaweza kuokoa muda na fedha na bado ukapata kitu kilicho bora. Unaweza kuchagua mafunzo na ujuzi unaoutaka na kujifunza kwa muda mfupi sana. RecruitMe husaidia kuimarisha ujuzi wako, na kukufanya uwe yule mtu ambaye kila mwajiri angetaka kuwa naye. Anza sasa kuboresha ujuzi wako kupitia RecruitMe, ili upate kazi uitakayo bila wasiwasi. Kujiunga, tembelea: http://recruitme.co.tz/
KILIMANJARO YAPANGWA NA WENYEJI CECAFA

KILIMANJARO YAPANGWA NA WENYEJI CECAFA

November 10, 2015
Ratiba ya michuano ya Kombe la Challenji kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenger Cup) imetoka jana ambapo timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Star’ imepangwa kundi moja na wenyeji Ethiopia.
Katika taarifa ya CECAFA iliyotolewa jana, Kilimanjaro Star imepangwa kundi A pamoja na wenyeji Ethiopia, Somali na waaalikwa wa michuano hiyo timu ya Taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’.
Kundi B lina  Bingwa mtetezi timu ya Kenya, Uganda, Burundi na Djibouti, huku kundi C likiwa na timu za Rwanda, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 21 nchini Ethiopia katika mji wa Addis Ababa na kumalizika Disemba 6 mwaka huu.
AZAM CUP KUENDELEA LEO

AZAM CUP KUENDELEA LEO

November 10, 2015
Michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) inatarajiwa kuendelea leo katika viwanja vinne tofauti nchini, ambapo kila timu inahitaji kupata ushindi ili kusonga mbele katika mzunguko wa pili utakaochezwa mwezi Disemba mwaka huu.
Jijini Mbeya wenyeji Mbeya Warriors watakuwa wenyeji wa Wenda FC mchezo utakaochezwa uwanja wa Sokoine jijini humo, huku katika uwanja wa Majimaji mjini Songera timu ya Mighty Elephant watakua wenyeji wa African Wanderes.
Kariakoo ya Lindi watawakaribisha Changanyikeni FC katika uwanja wa Ilulu, huku timu ya Sabasaba ya mjini Morogoro wakiwakaribisha jirani zao Mkamba Rangers katika uwanja wa Jamhuri.
Michuano hiyo itaendelea kesho Jumatano kwa michezo miwili, Polisi Morogoro watawakaribisha Green Warriors uwanja wa Jamhuri mjini humo, huku timu ya Mshikamano FC wakiwa wenyeji wa Cosmopolitan katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Katika michezo iliyochezwa jana, Abajalo ilibuka na ushindi wa mabao 5 – 1 dhidi ya Transit Camp, huku Pamba FC ya jijini Mwanza ikiibuka na ushindi wa bao 1- 10 dhidi ya Bulyankulu FC ya mkoani Shinyanga.