RAIS DKT. MWINYI AKABIDHI ZAWADI KWA WASHINDI WA ZANZIBAR INTERNATIONAL MARATHON

October 29, 2023

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia Wanamichezo na Wananchi walioshiriki katika Mbio za Zanzibar International Marathon, katika viwanja vya Bustani ya Forodhani Jijini Zanzibar, baada ya kumaliza kwa mbio hizo za Kilomita 21,10 na 5, zilizoazia katika eneo Ngomekongwe na kumalizikia katika bustani ya forodhani Jijini Zanzibar leo 29-10-2023 na (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Waziri wa Habari.Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe.Tabia Maulid Mwita.Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi Mshindi wa Kwanza wa Kilomita 10 wa Mbio za Zanzibar Internatinal Maratho kwa Wanawake Sarah Ramadhan mfano wa hundi ya shilingi 2,000,000/- baada ya kumaliza mbio hizo.(Picha na Ikulu)
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akimkabidhi zawadi Mshindi wa Kwanza wa Kilomita 10 wa Mbio za Zanzibar Internatinal Maratho kwa Wanaume John Tulumbu mfano wa hundi ya shilingi 2,000,000/- na zawadi nyengine,baada ya kumaliza mbio hizo.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi mshindi wa Kwanza wa Kilomita 21 Wanawake Lilian Leley, baada ya kumaliza mbio za Zanzibar International Marathon, zilizofanyika leo Jijini Zanzibar 29-10-2023 na (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe.Tabia Maulid Mwita.(Picha na Ikulu)
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Washindi wa Mbio za Zanzibar International Marathon zilizofanyika leo Jijini Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Waziri wa Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita na (kulia kwa Rais) Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Tanzania Mhe.Dkt.Damas Ndumbaro.(Picha na Ikulu)

BASHUNGWA AAGIZA UJENZI WA NJIA NNE BUKOBA KAZI IFANYIKE USIKU NA MCHANA

October 29, 2023

 







WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa Kagera kumsimamia Mkandarasi M/s Abemulo Contractors Ltd afanye kazi usiku na mchana ya ujenzi wa upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye) - Bukoba Port (km 5.1), sehemu ya kwanza yenye urefu wa kilometa 1.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo tarehe 28 Oktoba 2023 Bukoba mkoani Kagera wakati akikagua kuanza kwa kazi ya Ujenzi wa upanuzi wa Barabara hiyo ya njia nne sehemu ya kwanza inayoanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi eneo la Mitaga lenye urefu wa Kilometa 1.

Bashungwa amesema kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango aliyoyatoa kwa TANROADS ya kukabiliana na ajali za mara kwa mara zinazotokea kwenye mteremko wa Nyangoye katika barabara hiyo.

“Ili kutekeleza maelekezo hayo ya Makamu wa Rais, tayari Serikali Sikivu inayoongozwa na Mheshiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa Bilioni 4.61 kuanza ujenzi wa upanuzi sehemu ya kwanza inayoanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi Mitaga yenye urefu wa kilometa 1", amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amesema atawasilisha maombi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwezesha ujenzi na upanuzi wa njia nne katika sehemu ya kwanza ifike Roundabout ya Bukoba mjini ambapo kutakuwa na ongezeko la Mita 600 ili kuwezesha magari kufika kwa urahisi katika stendi mpya ya Bukoba inayojengwa.

Bashungwa amesema kuwa upanuzi wa barabara hiyo katika Mji wa Bukoba unaenda sambamba na ujenzi wa miradi mingine ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa Stendi mpya ya Kisasa ya Bukoba kupitia mradi wa kupendezesha Miji (TACTIC) na upanuzi wa Bandari ya Bukoba.

Amesema mpango wa Serikali ni kuhakikisha barabara ya Rwamishenye kupitia Stendi ya Bukoba hadi Bandari ya Bukoba inapanuliwa kwa njia nne ili kurahisisha huduma ya Usafiri na Usafirishaji katika Mji wa Bukoba ambapo itasaidia kufungua mkoa huo kiuchumi.

Kadhalika, Bashungwa amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Stephen Byabato kwa namna anavyoendelea kusimama kidete kuhakikisha vipaumbele vya Maendeleo katika Jimbo lake Bukoba mjini vinatekelezwa bila kikwazo chochote.

Awali, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa Kagera, Eng. Ntuli Mwaikokesy amesema upanuzi wa njia nne wa barabara ya Bukoba (Rwamishenye) - Bukoba Port (kilometa 5.1) utetekelezwa kwa awamu 4.

Eng. Ntuli amesema Sehemu ya kwanza ya Upanuzi wa njia nne kuanzia Roundabout ya Rwamishenye hadi eneo la Mitaga utatekelezwa kwa miezi 12 ambapo kazi ilianza Oktoba 9, 2023 na jumla ya Wananchi 25 wamepisha upanuzi wa ujenzi ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.8 zitatengwa kulipa fidia.
WAZIRI MKUU KUWA MGENI RASMI MKUTANO WA WADAU WA ANGA

WAZIRI MKUU KUWA MGENI RASMI MKUTANO WA WADAU WA ANGA

October 29, 2023

 

Na Sophia Kingimali

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa anatarajia kuwa Mgeni rasmi kwenye mkutano mkubwa wa wadau wa Anga ambao watajadili mambo mbalimbali na
na namna walivyojipanga kuendeleza sekta ya anga na kuwa chachu ya uchumi wa Taifa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 29, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), Hamza Johari wakati akizungumzia miaka 20 ya mamlaka hiyo ambapo amesema waliamua kuandaa mbio za TCAA Fun Run 2023 katika mbio hizo ambazo wakinbiaji watashiriki katika mbio za kilomita 5 na 10.

Amesema Mamlaka hiyo ilianzishwa mwaka 2003 kufikia mwaka huu imetimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake hivyo wanaangalia miaka 20 walikotoka na 20 wanakokwenda.


“Kesho tunatarajia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufungua mkutano wa wadau wa Anga na kusherekea miaka 20 ya TCAA na wadau wa anga kwa kutathimini mafanikio tuliyopata na changamoto zinazotukabili, “amesema Johari.

Amesema jukumu lao ni kuhakikisha wadau wa anga wanafanya shughuli kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

Amesema watu walikuwa wanakimbia vizuri na walijiaanda na mbio hizo katika kuweka mwili vizuri na afya njema.

Ametoa wito kwa watanzania wote kujali sana afya zao kwa kula vizuri na kufanya mazoezi kwa sababu ni tiba na yawe sehemu ya maisha yetu.

“Tukiendelea kufanya mazoezi mara kwa mara tutaepukana na magonjwa nyemelezi ambayo yanaweza kuhatarisha afya zetu,” amesema .

Aidha amewashukuru wana TCAA na wadau wengine ambao wamewaunga mkono katika mbio hizo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amesema kuwa miaka 20 ya TCAA ni mageuzi ya Sekta ya anga.

“Leo tulikuwa tunasherekea miaka 20 ya TCAA kwa kukimbia mbio za TCAA Fun Run 2023 kufanya mazoezi ni kuimarisha afya ya akili zetu, “amesema Komba.

Amesema TCAA inatoa huduma kwenye viwanja vya ndege 15 nchi nzima na amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha viwanja vya ndege.   

LAKE MANYARA MARATHON 2023 FURSA MPYA YA UTALII HIFADHI YA TAIFA ZIWA MANYARA

October 29, 2023

 Na. Jacob Kasiri - Manyara.


Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe.Joshua Nassari ameshiriki mbio za Lake Manyara Marathon 2023 na kusema kuwa ni fursa mpya ya utalii ndani ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, hifadhi inayosifika kwa kuwa na Simba wengi wanaoparamia miti.

Mhe. Nassari alisema "kwa mara ya kwanza Wilaya ya Monduli imeandaa Marathon hii kwa lengo la kufungua fursa mpya ya utalii katika hifadhi yetu na kuongeza mzunguko wa fedha katika wilaya yetu".

"Kwakuwa eneo la Mto wa Mbu liko kimkakati wa kiutalii ndio imekuwa sababu kubwa ya kuvuta watu wengi kiasi hiki. Na tumeona kuanzia tarehe 27.10.2023 wakimbiaji walianza kuwasili hii yote imeongeza pato kwa taifa na mtu mmoja mmoja", aliongeza Mhe. Nassari.

Mbio hizi ndefu (Marathon) licha ya kuongeza fursa za kifedha kwa jamii pia, huimarisha afya na kuondoa magonjwa nyemelezi na kutoa mwanya kwa makampuni makubwa ikiwemo TANAPA kujitangaza na kupata wateja wanaowahitaji.

Afisa Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Maendeleo ya Biashara Makao Makuu - TANAPA, Augustine Massesa alisema utalii huu wa michezo umeanza kushika kasi kwa miaka ya hivi karibuni. "Hivyo, niwaase na kuwashauri watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki, licha ya kuimarisha afya pia inakuza utalii".

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Eva Mallya alisema mbio hizi ni fursa kwetu kwa sababu baadhi ya washiriki wamehamasika kuingia hifadhini na kuliingizia Taifa mapato.

"Kwa niaba ya hifadhi tunamshukuru Mkuu wa Wilaya yetu Mhe. Joshua Nassari na waandaaji wa Marathon hii, kwa kipindi chote cha uamasishaji kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imeleta tija kwa hifadhi yetu.

Mbio hizo zenye lengo la kuhamasisha utalii zilizobeba kaulimbiu "Tukimbie Tukitalii" zimefanyika leo tarehe 29.10.2023 zikianzia katika Lango la Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara iliyopo Mto wa Mbu mkoani Manyara.








WAZIRI KAIRUKI AMUAPISHA CC MPYA WA NCAA NA KUSISITIZA USIMAMIZI WA SHERIA ZA UHIFADHI.

October 29, 2023

 Kassim Nyaki, Karatu.


Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Angellah Kairuki (Mb) leo tarehe 29 Oktoba, 2023 amemuapisha Bw. Richard Rwanyakaato Kiiza kuwa kamishna wa Uhifadhi wa mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) baada ya Uteuzi uliofanywa na mhe. Rais hivi karibuni.


Katika tukio hilo Mhe. Waziri amebainisha kuwa Uteuzi wa Kamishna huyo ni sehemu ya kuimarisha majukumu ya Uhifadhi, utalii na maendeleo ya Jamii na kuongeza kasi ya kutangaza utalii kwa njia mbalimbali za kisasa ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi yetu kama ilivyo adhima ya Mheshiwa Rais wetu.

Waziri Kairuki ameilekeza bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kusimamia sheria za uhifadhi ikiwemo kutoa mifugo yote iliyoingiza kinyemela katika maeneo yaliyohifadhiwa ikiwemo Pori tengefu la Loliondo.

“Pamoja na majukumu mengine mliyonayo nawaelekeza wahifadhi kusimamia sheria zilizopo na kuhakikisha mifugo iliyoangizwa kinyemelea katika maeneo ya Hifadhi iondolewe” amesisitiza mhe. Kairuki

Aidha Mhe. Kairuki amempongeza Kamishna wa Uhifadhi aliyemaliza muda wake, Dkt. Freddy Manongi kwa juhudi ambazo wamezifanya katika kutangaza Vivutio vya utalii tulivyonavyo ambapo juhudi hizo zimeiwezesha Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kuchaguliwa na mtandao wa “Word Travel Awards” kama kivutio bora cha Utalii barani Afrika “Africa Leading tourist Attractions” na mafanikio ya kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia wageni zaidi ya 752,000, kuongeza mapato hadi kufikia Bilioni 171 mwaka wa fedha 2022/2023

Vilevile Mhe. Kairuki amemuelekeza Kamishna wa Uhifadhi NCAA na wadau wengine wanaohusika na zoezi la zoezi la uelimishaji, uandikishaji, uthaminishaji na uhamishaji wa wananchi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wanaojiandikisha kuhama kwa hiari kuendelea kusimamia eneo hilo kwa kufuata sheria na misingi ya haki za binadamu.

“Serikali inaendelea kuwahakikishia Wadau mbalimbali, Wananchi wa Ngorongoro na Jumuiya za Kimataifa kuwa zoezi hili ni la hiari, shirikishi na linazingatia misingi ya haki za kibinadamu na utawala bora na kila mwananchi aliejiandikisha kuhama kwa hiari Serikali itampa fidia na gharama zote za kumhamisha hadi alipochagua kwenda zinabebwa na Serikali kwa asilimia 100” amesisitiza mhe Kairuki. 



JUMUIYA YA WAZAZI (CCM) WILAYA YA TANGA WAMPONGEZA DKT TULIA

October 29, 2023

 



Na Oscar Assenga, TANGA

 

JUMUIYA ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tanga imepongeza Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) huku wakihaidi kuendelea kumuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu katika majukumu yake hayo.

 

Pongezi hizo zilitolewa leo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wilaya ya Tanga Hamza Bwanga wakati akizungumza na mtandao huo ambapo alisema kwamba wanaamini kwamba kuchaguliwa kwake kumekuja wakati muafaka kutokana na utendaji wake mahiri katika kuongoza Bunge la Tanzania.

 

Alisema kuchaguliwa kwake ni kutokana na jitihada zake katika utendaji wake ambao umejengwa na uchapakazi, uzoefu, uaminifu na uadilifu ambao umekuwa ni chachu kubwa kufikia mafanikio hayo.

 

“Sisi kama Wazazi wilaya ya Tanga tunakupongeza sana Spika wa Bunge kuwa kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa umoja huo na tunahaidi kumuunga mkono na nafasi hii imekuja wakati muafaka kabisa kwa kuwa yeye ni spika na mchakapazi,mwerevu msikivu “Alisema

 

Hata hivyo alisema kwamba wao wataendelea kumuunga mkono na kumuombe kwa mwenyezi mungu ili kutenda vema majukumu yake kwa waledi mkubwa .


Kijani Bond ya Benki ya CRDB yaorodheshwa DSE baada ya kufanikiwa kukusanya Sh. 171.82 bilioni kufadhili miradi inayotunza mazingira

October 29, 2023

 

Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt Charles Mwamaja (katikati) akiwasili katika hafla ya kutangaza matokeo ya hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB ‘Kijani Bond” iliyofanyika hoteli ya Johari Rotana ambapo Benki ya CRDB imetangaza kukusanya Shilingi bilioni 171.82 sawa na asilimia 429.57 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 40 ambazo zitaelekezwa katika kufadhili biashara na miradi inayozingatia utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kamishna alipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia), na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (kulia).

========   =======  ========

Benki ya CRDB imetangaza matokeo ya mauzo ya hatifungani yake ya kijani ‘Kijani Bond’ iliyoweka historia ya kuwa hatifungani ya kwanza ya kijani nchini na kubwa zaidi kusini mwa Jangwa la Sahara katika hafla iliyofanyika kwenye hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

Kijani Bond iliyozinduliwa Septemba 1, 2023 na kufungwa Oktoba 6, 2023, imekuwa na mwitikio mkubwa na hivyo kupelekea kufikia lengo kwa asilimia 429.57 ambapo jumla ya Shilingi 171.82 bilioni zimekusanywa ikilinganishwa na lengo la awali la TZS 40 bilioni. Kati ya wawekezaji 1,754 waliowekeza kwenye hatifungani hii, asilimia 99 ni Watanzania. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna wa Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Dkt Charles Mwamaja aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba ameiopongeza Benki ya CRDB kwa ubunifu na juhudi ilizochukua kuitoa na kuiuza hatifungani hiyo.
Dkt Mwamaja amesema idadi kubwa ya wawekezaji waliojitokeza kuwekeza kwenye hatifungani hii inadhihirisha juhudi kubwa zilizofanywa na Benki ya CRDB na fedha zilizopatikana zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea utekelezaji wa ajenda za maendeleo na juhudi za kulinda mazingira.

Kamishna Mwamaja pia amesisitiza umuhimu wa kulinda mazingira katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi sio tu unahitajika, bali haukwepeki kwani mahitaji ni makubwa.
"Tanzania inahitaji takriban dola bilioni 19.2 za Marekani mpaka mwaka 2030 ili kutoa mchango wake unaohitajika katika vita dhidi ya uharibifu wa mazingira. Sehemu kubwa ya fedha hizi inatakiwa itolewe na sekta binafsi. Kwa niaba ya Serikali, napenda nawapongeza kwa juhudi mnazozifanya ikiwamo Hatifungani hii ya Kijani na nyinginezo kama vile Programu ya Matumizi ya Teknolojia Endelevu za Kilimo Tanzania (TACADTP) mnayoshirikiana na Mfuko wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNGCF),” amesema Dkt. Mwamaja.

Akiwashukuru wawekezaji waliojitokeza kwa imani waliyonayo na ushirikiano walioutoa hata kuwezesha mauzo hayo kuvuka malengo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kiasi kilichokusanywa kimeongeza mtaji mpya ndani ya taasisi hiyo kwa Shilingi bilioni 140 zitachochea utoaji wa mikopo kwenye miradi inayolenga kulinda mazingira nchini.

Mikopo hiyo sio tu itaongeza upatikanaji wa ajira hasa kwa vijana na kukuza uchumi, Nsekela amesema zitadhihirisha utayari na umakini wa Tanzania kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na cha baadaye. 

“Ongezeko hili la mtaji wa Benki yetu ya CRDB litatuwezesha kutoa fedha zinazohitajika kwenye miradi tofauti inayojihusisha na kutunza mazingira kama vile viwanda endelevu, nishati safi, ujenzi na usafirishaji, maji, afya na elimu. Nawaomba wawekezaji wa ndani na kimataifa muendelee kushirikiana na benki yetu kufanikisha miradi hii,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, ameipongeza Benki ya CRDB kwa mafanikio iliyoyapata na kusema hatifungani hii ya kijani imetolewa kwa muda muafaka kukidhi mahitaji yaliyopo.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa, Kijani Bond iliorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ili kuuzwa katika soko la upili. Akizungumza wakati wa uorodheshaji wa hatifungani hiyo sokoni, Kaimu Afisa Mtendaji wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Mary Mnisawa amesema mauzo ya hatifungani ya Benki ya CRDB sio tuimeinufaisha taasisi hiyo bali soko zima la fedha nchini.

“Kuorodheshwa kwa Kijani Bond kutakwenda kuongeza uuzaji na ununuaji wa dhamana katika soko hilo mara dufu kutoka wasatani wa sasa wa Shilingi bilioni 150 hadi zaidi ya Shilingi bilioni 300,” alisema Mniwasa.
Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Ubalozi wa Uingereza nchini, Euan Davidson amesema Uingereza inayo furaha kubwa kufanikisha kutolewa hata kuuzwa kwa Hatifungani ya Kijani ya Benki ya CRDB. Mchango wa taifa hilo umetolewa kupitia taasisi ya FSD Africa iliyokuwa mshauri huru katika mchakato mzima wa kutoa mpaka kuuzwa kwa Hatifungani ya Kijani. Hayo yote yalifanyika yakiwezeshwa na Shirika la Maendeleo la Uingereza (UK Development).

“Historia iliyoandikwa katika mauzo ya hatifungani hii kwa wingi wa wawekezaji binafsi hata mashirika yanadhihirisha kukubalika kwa sekta ya fedha ya Tanzania na kuonyesha kwamba kuna uhitaji mkubwa wa fedha za kufanikisha miradi ya mazingira mwongoni mwa wawekezaji tofauti, wa ndani na kimataifa,” amesema Davidson. 

Shirika la IFC lililo chini ya Benki ya Dunia ni miongoni mwa wawekezaji waliotoa kiasi kikubwa kwenye mauzo ya hatifungani hii. Shirika hilo pekee limewekeza Shilingi ambazo ni sawa na dola milioni 20 sawa na asilimia 29.3 ya uwekezaji wote uliofanyika.

Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki IFC, Jes Chonzi amesema: “Upatikanaji wa fedha za kufanikisha miradi inayolinda mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni fursa iliyo wazi kwa Tanzania na fedha nyingi zinahitajika hasa kutoka sekta binafsi. Hatinfungani hii itaongeza upatikanaji wa mikopo kwenye miradi ya mazingira na kuongeza ujumuishaji wa wananchikatika uchumi.”

Katika mchakato wa kutolewa na kuorodheshwa kwa Kijani Bond, Benki ya Stanbic Tanzania imeshiriki kama msimamizi mkuu, huku kampuni ya Denton Tanzania Law Chamber ikitoa huduma za ushauri wa kisheria. Kampuni ya Orbit Securities Tanzania ilikuwa wakala mfadhili, huku KPMG ikikabidhiwa majukumu ya kutoa taarifa za kihasibu.

Kijani Bond ni awamu ya kwanza ya mpango wa dhamana ya uwekezaji ya Benki ya CRDB wenye thamani ya dola za marekani milioni 300 unaolenga kukusanya fedha kwa ajili ya ufadhili miradi ya kijani, kijamii na endelevu. Benki ya CRDB imejitolea kuendeleza ukuaji wa uchumi wa kijani na shirikishi nchini kupitia ufadhili bunifu na rafiki kwa mazingira.