WATENDAJI WA UBORESHAJI WA DAFTARI WATAKIWA KUWEPO VITUONI MUDA WOTE

August 27, 2024
Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifunga  mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza   jana Agosti 26 na kumalizika leo Agosti 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara.
Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele, akizungumza wakati akifunga  mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza   jana Agosti 26 na kumalizika leo Agosti 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Bw. Kailima Ramadhani, akizungumza wakati wa  mafunzo ya siku mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza   jana Agosti 26 na kumalizika leo Agosti 27, 2024 Mkoani Mkoani Mara.
***************
Na Mwandishi wetu
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wametakiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura muda wote hata kama hakuna waombaji wa kujiandikisha vituoni.
 
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele wakati akifunga mafunzo kwa watendaji wa uboreshaji ngazi ya mkoa wa Mara na halmashauri za mkoa huo.

Amesema watendaji wa vituo wanapaswa kuwepo vituoni muda wote kuanzia saa mbili kamili asubuhi hadi saa 12 kamili jioni kila siku katika siku saba za kujiandikisha zilizowekwa na Tume.
 
“Muda wa kufungua na kufunga kituo uwe ni ule uliopangwa ili waombaji wanapohitaji kuja kituoni kujiandikisha watukute kituoni,” amesisitiza Mhe. Mwambegele.
 
Tukio kama hilo la kufunga mafunzo limefanyika pia mkoani Simiyu ambako Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Magdalena Rwebangwira amewataka watendaji hao kufuatilia kwa karibu zoezi hilo ili lifanikiwe, kutoa kipaumbele kwa makundi mbalimbali na kuwa makini katika usambazaji na utunzaji wa vifaa.
 
Akifunga mafunzo ya watendaji Mkoani Manyara, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari kwa upande wake amehimiza uhamasishaji wa wapiga kura na kuwa Tume inatarajia wapiga kura halali tu ndio wapatiwe kadi za mpiga kura.
 
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki kuwachagua viongozi wao. Aidha ni matarajio ya Tume kuwa baada ya zoezi hili kukamilika watu watakaopatiwa kadi watakuwa ni wapiga kura halali,” amesema Jaji Asina.
 
Mafunzo haya yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mzunguko wa nne unaojumuisha mkoa wa Mara, Simiyu na baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Manyara ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Babati na Halmashauri za Wilaya za Babati, Hanang na Mbulu ambapo uboreshaji utaanza tarehe 04 Septemba, 2024 hadi 10 Septemba, 2024 na vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu Asina Omari akizungumza wakati akifunga mafunzo hayo mkoani Manyara. 
Sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka mkoa wa Manyara. 
Meza Kuu wakiwa katika picha wakati wa kufunga mafunzo kwa mkoa wa Manyara.
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Magdalena Rwebangira akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo kwa upande wa Mkoa wa Simiyu. 
Washiriki wakisikiliza kwa makini hotuba ya kufunga mafunzo.

Washiriki kutoka Mkoa wa Simiyu wakishiriki mafunzo kwa vitendo 
-- Mroki Mroki Online Reporter/Blogger Mob: +255 755 373999 Email: mrokim@gmail.com. Blog: https://mrokim.blogspot.com/ DODOMA, TANZANIA

RAIS SAMIA AWASILI KWENYE UWANJA WA KIA, TAYARI KWA KUELEKEA MKOANI ARUSHA

August 27, 2024

 





Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) mkoani Kilimanjaro tayari kwa kuelekea mkoani Arusha ambapo ni Mgeni Rasmi kwenye Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kitakachofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) tarehe 28 Agosti, 2024.

Mhe. Dkt. Samia amewasili uwanjani hapo akitokea nchini Kenya ambapo alihudhuria hafla ya Uzinduzi wa Kampeni ya Mhe. Raila Amolo Odinga, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya anayewania nafasi ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), tarehe 27 Agosti, 2024

RIADHA TANGA KUMPA USHIRIKIANO MUANDAAJI WA MASHINDANO YA TANGA CITY MARATHON

August 27, 2024



Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Mkoa wa Tanga Sophia Wakati akizungumza 



Na Oscar Assenga, Tanga.

CHAMA cha Riadhaa Mkoa wa Tanga (RT) kimesema kwamba kitampa ushirikiano wa kutosha muandaaji wa Mashindano ya Riadhaa ya Tanga City Marathon ili kuweza kuondoa changamoto zilizojitokeza msimu uliopita na yaweza kuwa na tija na mafanikio makubwa.

Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti wa Chama cha Riadha (RT) Mkoa wa Tanga Sophia Wakati alipokuwa akizungumza na vyombo bya habari kuhusu namna walivyojipanga kuhakikisha wanampa ushirikiano wa kutosha muadaaji huyo ili mashindano hayo yaweze kufanyika kwa ufanisi.

Alisema pia kuweza kufanyika vizuri kwa kufuata taratibu zote za Mashindano hayo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga kupitia Afisa Michezo Mkoa

“Mbio hizi za Tanga City Marathon ni mashindano muhimu kwa mchezo wa Riadha mkoani hapa na kwa sasa tumeyaingiza kwenye kalenda ya Mkoa na sasa yatakuwa yakifanyika kila mwaka na sisi RT kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga tutatoa ushirikiano wa kutosha kwa waandaaji”Alisema Sophia Wakati.

Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 22 mwaka huu ambapo yataanzia kwenye Hotel ya Tanga Beach Resort na kuzunguka maeneo mbalimbali Jijini Tanga na kuishia hapo huku yakishirikisha wakimbiaji katika makundi matatu ya Kilomita 21,10 na 5 za kujifurahisha.