SERIKALI KUVUNJA NYUMBA ZOTE ZILIZOJENGWA BILA KIBALI

SERIKALI KUVUNJA NYUMBA ZOTE ZILIZOJENGWA BILA KIBALI

October 22, 2017
1
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji na kuwaagiza kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati za kumiliki ardhi kwa dhuruma.
2
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.
3
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi
4
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wakati walipoenda kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, ambapo ameagiza eneo hilo lirejeshwe serikalini.
…………………………………………………………………………
Na. Hassan Mabuye
Serikali imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki zao za ardhi kwa dhuruma.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameyasema hayo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipoenda kutatua mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza eneo ya lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa, na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.
Waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela lianaanza pale ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wanawaacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.
“Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza Wakurugenzi, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuweka x katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa dhuruma” amesema Lukuvi.
Lukuvi amesema atapambana na viongozi hao pale ambapo atakuta majengo yamekithiri katika miji yao na hayana vibali vya ujenzi na baya zaidi majengo hayo yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika kiwanja cha mtu mwingine na viongozi hao wameshindwa kufuatilia kwa kuyavunja au kuyaweka alama ya x majengo hayo, kwa kuwa huu ni uzembe unaotokea nchi nzima.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemhakikishia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa atayafanyia kazi mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
Aidha, katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.
Waziri Lukuvi ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, dubai na kwingine duniani.
Lukuvi amesema Haiwezekani mtu atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu fedha hizo azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.
“Kwa hiyo Wizara yangu imekusudia mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 24 ya mwaka 1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana” amesema Waziri Lukuvi.
Marekebisho haya tunalenga kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo katika mabenki. Kwa kuwa Tathmini iliyopo inaonesha, baada ya wekezaji hao kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana fedha hizo hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote hapa nchini.
Lukuvi amesema, kuanzia mwezi Novemba tatizo hilo litakwisha kabisa kwa kuwa jukumu hili yatapewa mabenki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika Benki husika.
“na kama Benki husika haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi Serikali itamyang’anya mkopeshwaji huyo shamba hilo kwa kuwa atakua amekiuka sheria halafu Benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleza shamba lile itakuwa imekula hasara yenyewe” amesema Waziri Lukuvi.

NIHF ARUSHA YAANZA KUTOA ELIMU YA BIMA YA AFYA MTAA KWA MTAA

October 22, 2017

 Afisa Metekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Arusha,Miraji Kisile akiwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo ili kuweza kunufaika na huduma zinazotolewa ikiwemo za matibabu
  Afisa Metekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Arusha,Miraji Kisile akiwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko huo ili kuweza kunufaika na huduma zinazotolewa ikiwemo za matibabu
 ELIMU ikiendelea kwenye moja ya masoko Jijini Arusha kuhusu umuhimu wa wajasiriamali kujiunga na mfuko huo ili kuweza kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo za matibabu
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Arusha (NHIF) umeanza kutoa elimu ya bima ya afya mtaa kwa mtaa kwa wakazi wa mkoa huo ili waweze kujiunga nao ili kuweza kunufaika na huduma mbalimbali ikiwemo za matibabu.
 
Hayo yalibainishwa na Afisa Matekelezo wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Mkoani Arusha ,Miraji Kisile  ambapo alisema lengo ni kuhamasisha wazazi na walezi kuwaandikisha watoto wao na mpango wa toto afya kadi kwa chini ya miaka 18.

Alisema mfuko huo umeamua kushiriki katika zoezi hilo kikamilifu kwa kupita katika masoko na magulio ambayo asilimia kubwa ya wananchi wamekuwa wakipatikana huko.

Aidha alisema sambamba na hilo lakini pia uongozi wa mfuko huo wamedhamiria kuwahamasisha wajasiriamali mbalimbali kujiunga na mfuko huo kupitia mpango wa kikoa ili kulinda mitaji yao kwa kuwa na uhakika wa huduma za afya na matibabu kupitia NHIF kwa gharama nafuu.

“Zoezi hilo limeanza Octoba 18 mwaka huu na litafanyika kikamilifu kwa muda wa miezi miwili lengo ni kuwafikia wakazi wengi wa mkoa wa Arusha na viunga vyake “Alisema.

Alisema kwa sasa mfuko huo unatoa kipaumbele kusajili watoto kupitia mpango wa Toto Afya Kadi kwa gharama za kitanzania 50400 kwa mwaka  ambapo ataweza kuhudumiwa kwa vituo 7000 vilivyosajiliwa na bima ya afya vikiwemo hospitali zote za serikali,Hospitali zinazomilikiwa na Madhehebu ya dini,Hospitali za watu binafsi, maduka ya dawa pamoja na vituo maalumu vya uchunguzi.

Zoezi hilo limefanyika na kutarajiwa kuendelea kufanyika kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo soko la Tengeru,Soko la Ngaramtoni,Soko Kuu,Soko la Kilombero,Soko la Mbauda,Soko la Namanga, Mnadani Monduli,Loliondo,Digodigo Ngorongoro na Waso Ngorongoro.

BODI YA LIGI KUU KUKETI OCTOBA 26 MWAKA HUU

October 22, 2017
Kamati mpya ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) inafanya kikao chake cha kwanza Alhamisi, Oktoba 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Moja ya ajenda katika kikao hicho ni kuteua Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, na kamati nyingine mbalimbali.

TPLB ilifanya uchaguzi Jumapili, Oktoba 15 mwaka huu na kupata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti wake Clement Sanga.

Viongozi wengine waliochanguliwa ni Shani Mlingo (Makamu Mwenyekiti) na wajumbe Hamisi Madaki, Ramadhani Mahano, Almasi Kasongo na Egdar Chibura.

Boniface Wambura
Ofisa Mtendaji Mkuu
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)