|
Kocha
wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm akimpongeza kipa Ally Mustafa
'Barthez' baada ya mechi jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam |
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MLINDA
mlango Ally Mustafa ‘Barthez’ amepangua penalti mbili na kuiwezesha
Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Azam FC kwa penalti 8-7
kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 jioni ya leo Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Barthez
alipangua penalti za beki raia wa Ivory Coast, Serge Wawa Pascal na
mshambuliaji Ame Ali ‘Zungu’, wakati kipa wa Azam FC, Aishi Manula naye
alicheza penalti ya Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’
ikapanguliwa.
Penalti
za Yanga SC zilifungwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amissi Tambwe,
Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na
Kelvin Yondan aliyepiga ya mwisho.
|
Wachezaji wa Yanga SC wakishangilia na Ngao yao baada ya mechi |
Penalti
za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Nahodha John Raphael
Bocco, Himid Mao Mkami, Aggrey Morris, Jean Baptiste Mugiraneza, Erasto
Nyoni na Shomary Kapombe.
Ushindi
huo ni sawa na kisasi baada ya Yanga SC kufungwa kwa penalti 5-3 katika
Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
Julai 29, mwaka huu Uwanja wa Taifa, baada ya sare ya 0-0.
Katika
dakika 90 za mchezo wa leo, timu zote zilishambuliana kwa zamu na
kosakosa zilikuwa za pande zote mbili, lakini dakika za mwishoni, Yanga
SC walikuwa wakali zaidi.
Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alionekana kabisa akijiangusha kupoteza muda ili kupunguza kasi ya Yanga SC dakika za mwishoni.
Kevin
Yondan alicheza kwa kiwango kikubwa leo na dakika ya 37 aliitokea
vizuri pasi ndefu ya Mzimbabwe Thabani Kamusoko na kumchambua vizuri
kipa Aishi Manula, lakini beki Shomary Kapombe akabinuka ‘tik tak’
kuuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
|
Nahodha wa Azam FC, John Bocco (kushoto) akimuacha chini beki wa Yanga SC, Kevin Yondan |
Almanusra
Bocco aifungie Azam FC dakika ya 86 baada ya pasi nzuri ya Mugiraneza,
lakini shuti lake likaokolewa na kipa Barthez aliyekuwa katika ubora
wake siku ya leo.
Hii
inakuwa mara ya tano Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii ikiwa ni rekodi,
baada ya kuifunga Simba SC mara mbili, mwaka 2001 mabao 2-1 na 2010 kwa
penalti 3-1 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90, kabla ya
kuifunga Azam FC miaka mitatu mfululizo, 2013 bao 1-0 na 2014 mabao 3-0.
Inafuatia
Simba SC iliyotwaa Ngao mara mbili, mwaka 2011 wakiifunga Yanga SC 2-0
na 2012 wakiifunga Azam FC 3-2, wakati Mtibwa Sugar ni timu nyingine
iliyowahi kutwaa Ngao mwaka 2009 ikiifunga 1-0 Yanga SC.
Kikosi
cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi
Mngwali, Kevin Yondani, Nadir Haroub, Said Juma/Haruna Miyonzima dk57,
Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma/Deus Kaseke dk85, Amisi
Tambwe na Godfrey Mwashiuya.
Azam
FC: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Agrey Morris, Paschal
Wawa, Mudathir Yahya/Jean Mugiraneza dk68, Himid Mao, Frank Domayo/Ame
Ally dk82, Farid Mussa, John Bocco na Kipre Tchetche.