WAWILI WAPANDISHWA KUZIMBANI KWA KUTAKA KUMPA RUSHWA DC KILINDI.

November 16, 2013

 


Na Oscar Assenga, Kilindi.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Tanga (Takukuru) imewafikisha mahakama ya wilaya ya Handeni wakazi wawili wa wilaya ya Kilindi kwa tuhuma za kutaka kutoa rushwa ya sh.1,100,000kwa mkuu wa wilaya ya Kilindi Suleima Liwowa ili atamke eneo la Elerai liwe kijiji halali na kimeundwa baada ya kupitia taratibu zote za kisheria jambo ambalo halikuwa la kweli.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga,Edson Makala alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 12 mwaka huu mara baada ya taasisi hiyo kuweka mtego ambao uliwekwa na ofisi ya mkuu huyo wa wilaya na kufanikiwa kuwakamata wahusika hao.

Makala alisema watuhumiwa hao  walitenda kosa la kujihusisha na vitendo vya kushawishi na kutoa hongo ya kiasi cha sh.milioni moja na laki moja kwa mkuu wa wilaya hiyo ili kulifanya jambo la eneo hilo lifanikiwe kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Kamanda Makalo aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Sharrif Lemanda Lemteka mkazi wa Lesoit Kiteto na Emanuel Ole Kileli mkazi wa Elerai kata ya Kibirashi  wilayani Kilindi na kufunguliwa kesi  ya jinai Na CC 228/2013 ambapo washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na kifungu  cha 15(b) cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa Na 11/2007.

Alisema washtakiwa wote wawili walisomewa mashtaka na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa George Magoti mbele ya hakimu wa wilaya ya Handeni Patrick Maligana ambapo washtakiwa wote wawili walipata dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyotolewa na mahakama wakati kesi hiyo ikipangwa kutajwa tena mahakamani hapo Novemba 28 mwaka huu.

Aliongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kuzingatia maadili na kutojikujihusisha na vitendo vya rushwa kwani kufanya hivyo watakuwa wameingia matatani.

TAARIFA KUTOKA SHIRIKISHO LA SOKA NCHINI TFF

November 16, 2013
Release No. 196
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Novemba 16, 2013

MALINZI KUFUNGUA MICHUANO YA UHAI 2013
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi atafungua rasmi michuano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 (U20) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom mwaka huu.

Uzinduzi wa mashindano hayo utafanyika LEO (Novemba 17 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam saa 2 kamili asubuhi. Mechi ya ufunguzi itakuwa ya kundi A kati ya Azam na Coastal Union.

Mechi nyingine za kesho ni kundi; Yanga na Mbeya City (saa 8 mchana- Uwanja wa Karume), kundi B ni Ruvu Shooting na Ashanti United (saa 4 asubuhi- Uwanja wa Karume), Oljoro JKT na Simba (saa 10 jioni- Uwanja wa Karume).

Kundi C kutakuwa na mechi kati ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar itakayochezwa saa 2 kamili asubuhi kwenye Uwanja wa Azam Complex, na kwenye uwanja huo huo saa 10 jioni ni Rhino Rangers dhidi ya Tanzania Prisons.
RAMBIRAMBI MSIBA WA NYOTA COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha mchezaji wa Sayari, Fatuma Bahau ‘Crouch’ kilichotokea jana (Novemba 15 mwaka huu) kwenye Hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika mpira wa miguu kwani Fatuma ndiyo kwanza alikuwa anachipukia katika mpira wa miguu wa wanawake ambapo alikuwa mfungaji bora wa michuano ya U15 Copa Coca-Cola ya mwaka huu akichezea timu ya Ilala, hivyo mchango wake katika mchezo huu tutaukumbuka daima.

Kwa mujibu wa mlezi wa mchezaji huyo, Stephania Kabumba, marehemu anasafirishwa kesho kwenda kwao Mwanza kwa ajili ya maziko ambapo kifo chake kimesababishwa na ugonjwa wa malaria.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Bahau, klabu ya Sayari, Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondoni (KIFA) na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Fatuma mahali pema peponi. Amina

Boniface Wambura Mgoyo
Kaimu Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)