Gambo Cup kuanza Machi 16 Korogwe.

Gambo Cup kuanza Machi 16 Korogwe.

March 12, 2013
Na Oscar Assenga,Korogwe.
LIGI ya Gambo Cup inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Machi 16 mwaka katika vituo nane na itashirikisha timu 75 kutoka maeneo mbalimbali wilayani humo.

Ligi hiyo imedhaminiwa na Mkuu wa wilaya ya Korogwe,Mrisho Gambo yenye lengo la kuibua vipaji vya wachezaji wachanga wilayani humo na kuhamasisha vijana kupenda michezo.

Akizungumza jana,Mratibu wa Ligi hiyo,Zaina Hassani alisema maandalizi yake yanaendelea vizuri na itachezwa katika vituo
Kumi vilivyochaguliwa ili kuweza kumpata bingwa wa ligi hiyo.

Hassani ambaye pia ni katibu wa chama cha soka wilaya ya Korogwe (KDFA) alisema kutokana na kuanzishwa ligi hiyo ni dhahiri kuwa vijana nao watapata fuksa ya kushiriki katika michezo mara kwa mara na kuipongeza hatua ya Mkuu huyo wa wilaya.

Alivitaja vituo ambavyo ligi hiyo itachezwa kuwa ni 10 ambapo Korogwe mjini kutakuwa na timu 12,Kerenge kutakuwa na timu 13,Mombo timu 8,Mswaha timu 8,Makuyuni timu 9,Old Korogwe timu 8,Bungu timu 10,Kwamndolwa timu 5,Kwamsisi timu 5 na Hale timu 2.

Katibu huyo alizitaka timu ambazo zinashiriki ligi hiyo kufanya maandalizi kabla ya kuanza ili ziweze kuleta ushindani wa hali ya juu na kuleta hamasa kwa mashabiki pamoja na upinzani kwa timu pinzani.

Mwisho.

“Lushoto Shooting waanza vema Ligi ya Mkoa”

Na Oscar Assenga,Lushoto.

TIMU ya Lushoto Shooting juzi ilianza vema mzunguko wa pili wa Ligi ya Mkoa wa Tanga baada ya kuibamiza Korogwe United mabao 2-1,katika mchezo uliochezwa uwanja wa soka Halmashauri uliopo wilayani hapa.

Katika mchezo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani wa hali ya juu kutokana na timu zote kucheza kwa kujipanga na kushambuliana kwa zamu ambapo Korogwe United ndio walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za Lushoto Shooting kwenye dakika ya 5 bao lilolofungwa na Abdallah Ramadhani baada ya kutokea piga ni kupiga lengoni mwa Lushoto Shooting.

Baada ya kuingia bao hilo,Lushoto Shooting wakiwa na wachezaji wao makini ambao waliwasajili wakati wa dirisha dogo waliweza kujipanga na kuanza kulishambulia lango la Korogwe United kwa dakika kadhaa na hatimaye kuweza kuwasadhisha bao hilo kwenye dakika ya 35 kupitia Philipo Kabonda ambaye alitumia uzembe wa mabeki wa timu hiyo kupachika wavuni bao hilo.

Mpaka timu zote zikienda mapumziko zilikuwa nguvu sawa ambapo kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa kwa kila timu kuonekana kufanya mabadiliko kwenye kikosi chake.

Wakicheza kwa kujipanga na kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika kipindi cha kwanza,Lushoto Shooting waliweza kutawala kipindi hicho kwa asilimia kubwa huku wachezaji wake wakicheza pasi fupi fupi na ndefu kitendo ambacho kiliwafurahisha umati wa mkubwa wa mashabiki waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.

Kutokana na uchezaji huo,Lushoto Shooting waliweza kuandika bao la pili na la ushindani katika dakika ya 70 ambalo liliwekwa kimiyani na Philipo Kabondo ambaye aliweza kuwakonga nyoyo mashabiki wa timu hiyo kwa kuifungia mabao yote mawili.

Akizungumza baada ya kumalizika mchezo huo,Kocha Mkuu wa timu ya Lushoto Shooting,Alanus Fransis alisema sasa hivi nguvu zao zote wanazielekeza kwenye mechi yao na Makorora Star itakayochezwa kwenye uwanja huo huo ili kuweza kuchukua pointi tatu muhimu.

Mwisho.