MAKAMU WA PILI WA RAIS MH ABDULLA AFIKA NYUMBANI KWA MH OTHUMAN MASOUD KUMPA POLE KUFUATIA KIFO CHA DADA YAKE

May 23, 2023

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefika Chukwani nyumbani kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman kumpa pole kufuatia kifo cha Dada yake Bi Mkali Masoud Othman aliefariki jana Jumatatu 22 Mei, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja,Innaa Lillaahi wainnaa Ilaihi Raajiun 

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefika Chukwani nyumbani kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman kumpa pole kufuatia kifo cha Dada yake Bi Mkali Masoud Othman aliefariki jana Jumatatu 22 Mei, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.


Innaa Lillaahi wainnaa Ilaihi Raajiun 


Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

23 Mei, 2023

SERIKALI KUJENGA MELI TATU MPYA NYINGINE ZIKIKARABATIWA

May 23, 2023


Katika kuhakikisha Sekta ya Usafiri kwa njia ya maji unaimarika Serikali Kupitia Kampuni ya huduma za Meli imedhamiria kujenga meli tatu mpya katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika baada ya kukamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba.

Meli hizo mpya ambazo zitajumuisha ujenzi wa meli moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 na meli moja ya abiria na mizigo yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Tanganyika pamoja na meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mabehewa ya mizigo katika Ziwa Tanganyika.

Hayo yamesemwa leo Mei 22,2023 Bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka 2023/2024.

Mbali na ujenzi wa meli hizo mpya Prof. Mbarawa aliongeza kuwa MSCL tayari imeshakamilisha taratibu za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa ukarabati wa meli ya MV. Liemba tarehe 5 Machi, 2023.

“Kwa sasa, majadiliano na Mkandarasi kabla yakusaini mkataba yanaendelea. Mkataba huo unatarajiwa kusainiwa Julai, 2023. Aidha, MSCL inakamilisha taratibu za kumwajiri Mhandisi Mshauri kwa ajili kufanya tathmini ya kina na kuishauri Serikali kuhusu ukarabati wa meli ya MV. Mwongozo ambayo ilisimamishwa kutokana na changamoto ya msawazo (stability). Kazi hii inatarajia kuanza mwezi Juni, 2023 na kukamilika mwezi Novemba, 2023.” Alisema.



Aidha, Prof. Mbarawa alielezea hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa ya ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo ya MV Mwanza Hapa kazi Tu na ukarabati mkubwa wa Meli ya mizigo ya MV Umoja za Ziwa Victoria pamoja na ukarabati wa meli ya kubeba mafuta ya MT. Sangara ya Ziwa Tanganyika.



“Ujenzi wa Meli ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo umekamilika kwa asilimia 83, Meli ya MV Umoja yenye uwezo wa kubeba tani 1,200 za mizigo umekamilika kwa asilimia 75.8 na meli ya MT. Sangara yenye uwezo wa kubeba lita 400,000 umekamilika kwa asilimia 90.7.”



Katika mapendekezo hayo Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imeomba kiasi ya Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa meli mpya na Ukarabati.




Imetolewa na

Kitengo cha Masoko na Uhusiano Kwa Umma

Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL).





WAAJIRI WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUJISAJILI NA KUWASILISHA MICHANGO WCF

May 23, 2023

 


NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MWANZA

MKUU wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ametoa wito kwa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa manufaa ya wafanyakazi pindi watakapopata changamoto za kuumia au kuugua kutokana na kazi.

Ameyasema hayo Mei 22, 2023 katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu uliosababishwa na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa madaktari wa mikoa ya kanda ya Ziwa ikijumuisha Mwanza, Kagera, Mara, Simiyu, Geita na Shinyanga katika ukumbi wa chuo cha BoT jijini Mwnaza.

“Ili uweze kunufaika na huduma au mafao yanayotolewa na WCF, ni lazima waajiri wajisajili na kuwasilisha michango ya wafanyakazi waliowaajiri.” Alifafanua.

Alisema hivi sasa wafanyakazi wanao uhakika wa kinga na kipato kutokana na majanga yanayosababishwa na ajali, magonjwa na vifo kutokana na kazi kufuatia uwepo wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF).

“Waajiri nao wanapata muda zaidi wa kushughulikia uzalishaji na uendelevu wa biashara zao na hivyo kuongeza tija inayopelekea kuongezeka kwa pato la taifa.” Alisema.

Aliwaasa washiriki kuwa waadilifu wanapotekeleza jukumu hilo la kufanya tathmini ya ulemavu utokanao na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi ili WCF iweze kutoa fidia stahiki na kwa wakati.

Alisema uwepo wa Mfuko wa Fidia ni hatua muafaka katika mazingira ya sasa ambapo serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na kazi ikiwemo ya kujenga uchumi na hivyo kuwa na ongezeko kubwa la maeneo ya uzalishaji.

“Katika hali ya kawaida ongezeko litakwenda sambamba na ongezeko la matukio na athari zinazotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hivyo jukumu la WCF sio kulipa fidia pekee bali pia kushirikiana na wadau katika kubuni na kuendeleza mbinu za kupunguza au kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.” Alisisitiza.

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema mafunzo hayo ni sehemu ya hatua muhimu ya kuuwezesha Mfuko kutekeleza vyema jukumu la kufanya tathmini sahihi na hatimaye kutoa fidia stahiki pindi mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.

“Katika mwaka huu wa fedha tayari tumetoa mafunzo kwa madaktari 85 na leo tunawafundisha madaktari 100 na hivyo watafanya idadi ya madaktari ambao tayari wamepatiwa mafunzo na WCF, ya kufanya tathmini za ulemavu uliotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kufikia 1,585 nchi nzima.”Alifafanua Dkt. Omar.

Akielezea zaidi umuhimu wa mafunzo hayo, Dkt. Omar alidokeza kuwa Madaktari ni kiungo muhimu, ni daraja baina ya Mfuko na wahanga wanaopata magonjwa au ajali zinazotokana na kazi.

“Madaktari hawa wakijengewa uelewa wa kuweza kujua na kubaini magonjwa yanayotokana na kazi, vilevile wakaweza kufanya tathmini za ulemavu, itawawezesha hawa wahanga kupata haki zao za fidia kwa wakati lakini kupata stahiki zao.” Alisisitiza.

Kwa upande wa madaktari wameishukuru Serikali kwa kuuwezwesha Mfuko kusimamia majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo.

“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo haya yatatuwezesha kufanya majukumu yetu ya kuwahudumia wafanyakazi watakaopata changamoto za kuumia na au ulemavu kutokana na ajali na magonwja yatokanayo na kazi kwa usahihi zaidi>” Alsiema Dkt. Pasclates Ijumba kutoka Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Geita.

Aidha Dkt.Julieth Nkovabi kutopka Hospitali ya Bugando, alisema mbali na kupatiwa mafunzo hayo ya tathmini za ulemavu na magonwja yatokanayo na kazi, lakini pia wamepatiwa elimu ya uelewa wa namna ya kuwasilisha taarifa endapo mfanyakazi ataumia au kuugua.

“Na sisi watumishi wa afya tunakumbana na shida mbalimbali, magonjwa ya kuambukiza wakati tunapowatibu wagonjwa wetu, kwa hivyo ni fursa nzuri ya kuelewa hatua kwa hatua jinsi ya kuwasilisha taarifa.” Alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masalla
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter akiwasilisha mada ya mchakato wa madai ya fidia
Mkuu wa Huduma za Sheria WCF, Bw. Abraham Siyovelwa akiwasilisha mada ya Sheria iliyoanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Sehemu ya madaktari wanaoshiriki mafunzo hayo
Sehemu ya madaktari wanaoshiriki mafunzo hayo
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano WCF, Bi. Laura Kunenge akizungumzia utaratibu wa uendeshaji mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar (kulia) akizungumza jambo na Meneja Tathmini Dkt. Ali Mtulia