NYOTA CITY ‘WAPATA SOMO’ KUTOKA NHIF

NYOTA CITY ‘WAPATA SOMO’ KUTOKA NHIF

October 27, 2015


MCC NHIF
Kocha Mkuu wa City Meja Mstaafu Abdul Mingange, leo jioni aliungana na kikosi chake kupata darasa maalumu kutoka kwa wataalamu wa shirika la bima ya taifa ya afya waliotembelea kambi ya timu yake maalumu kabisa kwa shughuli hiyo.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kumalizika kwa darasa hilo maalumu lililofanyika kwenye kambi ya City iliyopo katikati ya jiji la Mbeya, Kocha Mingange alisema kuwa limekuwa ni jambo nzuri kwa madaktari na wataalamu kutoka NHIF kufika kambini hapo kwa ajili ya kutoa elimu kwa wachezaji na viongozi kuhusu umuhimu wa bima ya afya hasa ukizingatia uwepo wa matukio mengi ya bahati mbaya kwenye soka.
“Dunia nzima inafahamu kuwa soka sasa ni kazi,tofauti na zamani ambapo mchezo huu ulichukuliwa kama burudani, kwa hiyo ndani ya kazi yapo matukio ambayo hutokea ya kigusa afya, hayo yanahitaji matibabu, sasa somo la leo limekuwa muhimu kwetu kwa sababu tumejuwa umuhimu wa bima ya afya, njinsi gani inaweza kutusaidia tukipata matatizo kwenye kazi yetu,binafsi nimefurahi na nimejaza fomu hii ya NHIF” alisema.
Akiendelea zaidi kocha Mingange ambaye msimu uliopita aliifundisha timu ya Ndanda Fc ya Mtwara aliweka wazi kuwa mpango huu wa shirika la bima ya taifa ya afya litawasaidia wachezaji wengi kupata matibabu ya uhakika pale wanapokuwa wamepata matatizo makubwa ambayo pengine yangaweza kuwaweka kando na soka mapema kwa kushindwa kumudu gharama.
“Nchi yetu inao wachezaji wengi ambao wamelazimika kustaafu soka kutokana majeraha makubwa waliyoyapata viwanjani,licha ya jitihada zao kubwa lakini ikashindika kurudi kucheza kutokana na gharama kubwa za matibabu,sasa hii NHIF imekuja kuondoa hilo,naomba vijana waiunge mkono kwa kujaza fomu zao kwa sababu sasa uhakika wa matibabu upo iwe ndani au nje ya nchi hawa jamaa watafanya kazi kwa ajili yao” alimaliza.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni shirika la bima ya taifa ya afya nchini limeingia mkataba na shirikisho la soka Tanzania TFF  kwa lengo la kutoa  huduma za matibabu na bima  kwa afya za wachezaji wa vilabu vyote vinavyoshiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.